Tanzania National Parks
February 2, 2025 at 04:54 PM
*MKOMAZI SASA KUINGIA*
*“B-CLUBS”*
Na. Edmund Salaho ~ Mkomazi
Hifadhi ya Taifa Mkomazi imejidhatiti kuingia katika orodha ya Hifadhi za Taifa zinazoingiza mabillioni ya fedha (B-Clubs) kupitia shughuli za Utaliii zinazofanyika katika Hifadhi hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Emanuel Moirana katika Kikao Kazi kati ya Maafisa na Askari Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA kilichofanyika leo tarehe 02, Februari 2025 katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi iliyopo Same Mkoani Kilimanjaro.
“Hifadhi ya Taifa Mkomazi inaenda kuingia kwenye hifadhi zinazojiendesha zenyewe kwa kuzalisha mapato makubwa na sasa tunaenda kuingia katika orodha hiyo ya “B- Clubs” mpaka leo tumekusanya millioni 939 ikiwa ni miezi saba ya makusanyo tangu mwaka wa fedha kuanza na tumesalia kiasi cha milioni 239 kufika malengo bilioni 1.2 kwa mwaka mzima”.
“Tumeshuhudia idadi kubwa ya wageni, na kwa mafanikio katika Hifadhi yetu ya Mkomazi, kipekee nitoe shukrani zetu zimfikie Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake ambapo Hifadhi ya Taifa Mkomazi tumeona matunda ya Filamu yake maarufu ya Tanzania: The Royal Tour” alisema Kamishna Moirana.
Naye, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Juma Kuji aliwapongeza Hifadhi ya Mkomazi kwa mafanikio makubwa waliyoyapata kupitia Uhifadhi na Utalii na kusisitiza kuzitunza rasilimali za wanyamapori kwa faida ya kizazi cha sasa na kile cha baadaye.
“Niwapongeze kwa mafanikio mliyonayo na nimefurahi kusikia kuwa mmekaribia kufikia malengo na sasa mnaingia Club ya Hifadhi zinazoingiza mabilioni, hivyo basi, nimepita kuangalia mipangilio mliyonayo na namna mnavyoitekeleza. Lengo la TANAPA ni kuhifadhi Maliasili hizi lakini pia tushiriki kujenga uchumi wa Taifa letu kwa ujumla wetu na kwa hakika malengo yetu ni kutoka kwenye kukusanya mabilioni na kwenda kuingiza Trillioni na ili tuingize fedha hizo inahitaji mchango wa kila mmoja wetu katika kutekeleza majukumu yake”, alisema Kamishna Kuji.
Aidha, Kamishna Kuji katika Kikao kazi hicho alisisitiza utendaji kazi imara kwa Maafisa na Askari wa Hifadhi hiyo ili kutimiza malengo ya Serikali.
“Suala la kuchapa kazi liwe namba moja, sifa ya jeshi ni kuchapa kazi na matokeo yanayoonekana na hivyo nisisitize kuchapa kazi ili kufikia adhma ya Serikali”
Hifadhi ya Taifa Mkomazi iliyopo Kaskazini mwa Tanzania ni maarufu zaidi kwa wanyama adimu aina ya faru weusi (The home of black Rhino) ambao huonekana kwa urahisi zaidi unapotembelea hifadhi hiyo.
👍
🙏
❤️
😂
9