OFISI YA RAIS - TAMISEMI
February 11, 2025 at 07:23 PM
SERIKALI YATOA SABABU UCHELEWESHAJI WA UJENZI WA STENDI YA KISASA JIJINI ARUSHA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema ucheleweshaji wa ujenzi wa stendi ya kisasa ya Jiji la Arusha umetokana na changamoto ndogo ndani ya taratibu za Serikali, lakini akasisitiza kuwa mradi huo utaanza hivi karibuni.
Mhe. Mchengerwa amebainisha hilo leo Jumanne Februari 11, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, aliyekuwa akitaka maelezo juu ya kuchelewa kumpata mkandarasi wa mradi huo licha ya ahadi zilizotolewa bungeni.
“Miradi yote chini ya Mpango wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTIC) unaendelea, ikiwemo mradi wa stendi ya Arusha. Makandarasi wote waliopo kwenye mpango huu wataanza kupokea fedha za ujenzi kuanzia wiki ijayo,” amesema Waziri Mchengerwa.
Ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa stendi hiyo ni sehemu ya mpango mkubwa wa Serikali wa kuboresha miundombinu ya miji mikubwa nchini kwa lengo la kurahisisha usafiri na kuchochea uchumi wa wananchi.
“Serikali imejipanga kuhakikisha miradi yote iliyopangwa inatekelezwa kwa wakati. Tunatambua umuhimu wa stendi hiyo kwa wakazi wa Arusha na tunaomba uvumilivu wakati taratibu za mwisho za kumpata mkandarasi zikikamilishwa,” aliongeza.
Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa Serikali ina dhamira ya dhati kutekeleza mradi huo kwa wakati na kuwahakikishia wananchi wa Arusha kuwa hatua zote zinazoendelea zinalenga kuhakikisha ujenzi huo unaanza haraka iwezekanavyo.
🙏
👍
❤️
👏
😂
🍅
😢
🤝
🥹
25