
Tanzania National Parks
February 7, 2025 at 08:25 PM
*TANAPA YAPONGEZWA KWA MAFANIKIO KATIKA UHIFADHI MALIASILI NA KUKUZA UTALII NCHINI.*
*Na: Happiness Sam - Arusha*
Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wameipongeza menejimenti ya shirika hilo kwa juhudi kubwa zinazofanywa katika kuimarisha uhifadhi wa maliasili na kukuza utalii nchini, hatua ambazo zimeendelea kulifanya taifa letu kuwa na maliasili bora Afrika na dunia kwa ujumla.
Pongezi hizo zimetolewa leo, Februari 07, 2025, na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini -TANAPA na Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi, CPA. Khadija Ramadhani, alipokuwa akitoa muhtasari wa ziara ya wajumbe wa Bodi hiyo katika Ofisi za Makao Makuu ya TANAPA yaliyopo mtaa wa Majengo jijini Arusha.
CPA. Khadija alisema “Natoa pongezi kwa menejimenti ya shirika kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuimarisha uhifadhi na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, kama vile ujenzi wa barabara, vyoo, ofisi, malango ya kuingilia wageni, sehemu za kupumzika wageni pamoja na madaraja, hatua ambayo imeendelea kuchagiza ongezeko la watalii katika hifadhi zetu”.
Aidha, CPA. Khadija aliongeza, “Hifadhi hizi zipo kwa ajili ya faida ya watanzania wote kwani mapato yanayotokana na utalii hutumika kati kukuza uchumi na ujenzi wa miundombinu kama vile barabara, mashule na huduma za afya hivyo jukumu la kuzilinda ni letu sote.”
Akizungumza baada ya kupokea maagizo ya Wajumbe wa Bodi hiyo, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA Musa Nassoro Kuji, aliwashukuru Wajumbe hao kwa kutenga muda wao na kuja kufanya ziara hiyo, kwani vile walivyoviona na kuvitolea maelekezo vitatoa mwanga kwetu kama TANAPA wa kuvifanyia kazi ili tuendelee kuimarisha ulinzi wa maliasili, kukuza utalii na kuvutia wawekezaji.
Sambamba na hayo pia, Kamishna Kuji aliongeza, “Tunaahidi kuendelea kuchukua hatua madhubuti na za haraka ili kuhakikisha Hifadhi zetu zinabaki kuwa sehemu salama kwa wanyama, huku vivutio vyetu vya utalii vikiongezeka na kuwa na manufaa makubwa kwa Taifa letu”
Naye, Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga - Mkuu wa Kanda ya Kaskazini alisema kuwa ziara ya Wajumbe hao wa Bodi ya Wadhamini imekuwa na mafanikio makubwa kwani imewarahisishia kuelezea changamoto zinazoikumba Hifadhi ya Taifa Tarangire na Kanda ya Kaskazini kwa ujumla sambamba na Wajumbe hao kupata fursa ya kutembelea uwandani kujionea uwekezaji mkubwa ulifanywa na Serikali chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Ziara ya Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini TANAPA ilianza Februari 03, 2025, ikiwa na lengo la kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya shirika hilo, pamoja na kutathmini hali ya uhifadhi na utalii katika Hifadhi za Taifa, ikiwemo Hifadhi ya Taifa Saanane, Serengeti, Manyara na Tarangire.
👍
🙏
😮
11