Visit Ngorongoro - Tanzania
January 25, 2025 at 06:12 PM
*SERIKALI YAZITAKA MAMLAKA ZINAZOSIMAMIA KITUO CHA MAFUNZO YA JESHI LA UHIFADHI MLELE KUFANYA MABORESHO*
Na Hamis Dambaya, Mlele.
Serikali imeziagiza mamlaka na taasisi zinazosimamia na kutumia kituo cha mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi kilichopo Mlele mkoani Katavi kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazokikabili kituo hicho.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii mheshimiwa Dunstan Kitandula ametoa maelekezo hayo wakati akifunga mafunzo ya watumishi wa taasisi mbalimbali zinazotoa mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi ambapo mafunzo hayo yalikuwa ni mahsusi katika kuwabadilisha watumishi hao ili kupata mafunzo ya jeshi hilo.
Mheshimiwa Kitandula amesema ni muhimu taasisi hizo kuboresha miundo mbinu hiyo ikiwemo huduma za afya, barabara, maeneo ya kujifunzia, vifaa pamoja na kuhakikisha kituo hicho kinatumia nishati safi ya kupikia.
Katika risala yao wahitimu walimweleza mheshimiwa naibu waziri uwepo wa changamoto hizo ambapo walisema kwamba ikiwa maboresho hayo yatafanyika yataongeza tija kwa wanafunzi na wakufunzi kutumia muda wao vizuri.
Mheshimiwa Kitandula pia amewapongeza wahitimu wote na kuwataka kutumia mafunzo hayo katika kuhakikisha kuwa wanalinda rasilimali za umma kwa uadilifu, uzalendo, uaminifu na kufuata sheria na taratibu zote za serikali.
Akizungumza kwa niaba ya makamishna wa mamlaka na taasisi hizo Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dkt .Elirehema Doriye amesema maelekezo yote yaliyotolewa na serikali yatafanyiwa kazi kwa kushirikiana na mamlaka zinazotumia kituo hicho ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, TANAPA, TFS na TAWA.
Mratibu wa mafunzo hayo kutoka wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Msaidizi Mwandamizi Fidelis Kapalata amesema jumla ya wanafunzi 231 wamehitimu mafunzo ya mabadiliko ya utendaji kutoka muundo wa kiraia na kwenda katika muundo wa kijeshi.
👍
2