Vice President Tanzania

Vice President Tanzania

112.9K subscribers

Verified Channel
Vice President Tanzania
Vice President Tanzania
January 21, 2025 at 03:44 AM
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Watanzania wote kuibua taarifa zinazohusu vitendo vya ukatili ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika. Makamu wa Rais ametoa wito huo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Miaka 25 ya Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) leo tarehe 20 Januari 2025. Amesema wapo wanawake, watoto na wanaume wanaopitia vitendo vya ukatili wa kijinsia au kimwili lakini hawatoi taarifa kwenye vyombo vya sheria, vilevile baadhi ya mila na desturi zimekuwa zikitumika kuwakandamiza waathirika. Amesema pamoja na dhamira njema ya Serikali ya kuhakikisha usawa wa kijinsia hapa nchini, bado wanawake ambao idadi yao ni zaidi ya nusu ya watu hapa nchini, wanapewa nafasi ndogo katika umiliki wa mali na wanabaguliwa kwa msingi wa jinsia. Ameongeza kwamba kwa mujibu wa Mpango wa Kitaifa wa Kupinga vitendo vya Kikatili dhidi ya Wanawake wa mwaka 2016, kati ya wanawake kumi, 4 wamepitia ukatili wa kimwili, na mmoja kati ya watano wamepitia ukatili wa kingono miongoni mwao wakiwa na umri mdogo (chini ya miaka 15). Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema kulingana na Ripoti ya UN Women Social Institution and Gender Index (SIGI) 2022, ukatili wa kijinsia nchini Tanzania unabainishwa zaidi kupitia ndoa za utotoni, ubaguzi ndani ya familia, ukatili dhidi ya wanawake, ukosefu wa uhuru katika kupanga uzazi, upatikanaji na umiliki wa ardhi. Pia kulingana na Taarifa ya Tathmini ya Ukatili wa Kijinsia Tanzania iliyoandaliwa na Benki ya Dunia mwaka 2022, 40% ya wanawake wote wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili na 17% wamepitia ukatili wa kingono. Aidha Makamu wa Rais amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imejizatiti kuimarisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake hapa nchini kwa kuanzisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambayo inasimamia masuala ya usawa wa kijinsia. Amesema dhamira hiyo ya Serikali inaonekana zaidi kupitia mikakati, mipango na sera za kitaifa kama vile Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mipango ya Maendeleo ya Taifa ya Miaka Mitano, Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (NSGR) na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya 2000. Ameongeza kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhihirisha kwa vitendo dhamira yake ya kuboresha utendaji katika utoaji haki, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usawa wa kijinsia katika ngazi mbalimbali za uongozi wa Mahakama ambapo kwa takwimu, Mahakama ya Rufani, 33% ya Majaji ni wanawake, Mahakama Kuu, ni 38%. Kwa Wasajili wa Mahakama ,wanawake ni 33% na Naibu wasajili ni 48.72%. Aidha, wanawake ni 50% ya Mahakimu wa Mahakama za Mahakimu Wakazi na 41% ya Mahakimu wa Mahakama za mwanzo. Makamu wa Rais ametoa wito wa kujenga tabia ya kutambua na kusheherekea mafanikio ya wanawake katika jamii ili kutoa hamasa kwa wasichana na wanawake wengine kujifunza na kuiga mifano hiyo. Amesema ipo mifano ya wanawake hapa nchini waliofanya vizuri katika fani mbalimbali kwa kuanza na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa kwanza mwanamke; Bibi Titi Mohamed, mwanamke aliyekuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru wa nchi pamoja na wengine wengi.
🙏 ❤️ 👍 😢 😂 😮 27

Comments