Vice President Tanzania

Vice President Tanzania

112.0K subscribers

Verified Channel
Vice President Tanzania
Vice President Tanzania
February 11, 2025 at 01:33 PM
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kukamilisha mchakato wa kusanifu na kujenga Mfumo Mkuu wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini na kuhakikisha Taasisi zote za umma zinajumuishwa katika mfumo huo. Makamu wa Rais ametoa rai hiyo wakati wa Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Tano cha Mamlaka ya Serikali Mtandao kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC). Amesema Jambo hilo ni muhimu ili kurahisisha utendaji kazi katika taasisi na kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Taasisi za Umma kuhakikisha kuwa mifumo yao inasomana na kubadilishana taarifa. Aidha Makamu wa Rais amesema Taasisi zote za umma zinapaswa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao katika hatua zote za ujenzi au ununuzi, usimamizi na uendeshaji wa Miradi ya TEHAMA pamoja na kuwataka kuwaelekeza Wakuu wote wa taasisi za umma kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo inayotolewa na Mamlaka husika katika utekelezaji wa shughuli za Serikali Mtandao. Hali kadhalika, Makamu wa Rais ameagiza mikoa ambayo bado haijaanza kutumia utaratibu wa Ofisi ya Kielektroniki (e-office) kuhakikisha wanaaanza kutumia mfumo huo ifikapo tarehe 30 mwezi juni. Aidha ameagiza kituo cha utafiti kiweze kuimarishwa pamoja na kuongezewa eneo la ufanyaji kazi. Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA na kada nyingine, kwa kuweka mazingira wezeshi ya ufundishaji katika Vyuo Vikuu na Taasisi za elimu ya juu ili viendelee kuzalisha wataalam wa kutosha. Makamu wa Rais amewasihi washiriki wa kikao kazi hicho pamoja na Watanzania wote kwa ujumla, ambao wana sifa za kupiga kura kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kuhakikisha wanajiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki kupiga kura ili kuchagua viongozi wenye sifa na uwezo stahiki wa kusimamia na kuratibu shughuli za maendeleo katika ngazi husika.
🙏 ❤️ 3

Comments