Tanzania National Parks
February 17, 2025 at 06:02 PM
*KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YAKOSHWA NA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA KUDHIBITI WANYAMAPORI WAHARIBIFU - KOROGWE*
Philipo Hassan - Korogwe
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii leo Februari 17, 2025 imekagua na kuridhishwa na matumizi ya teknolojiia katika kituo kipya cha askari kitakachotumika kudhibiti wanyamapori waharibifu, kituo hicho kipo katika kijiji cha Goha Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) , Mbunge wa Korogwe Vijijini ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutumia teknologia ya ndege nyuki (drones) katika kufukuza wanyamapori waharibifu wakiwemo tembo ambapo kamati ilishuhudia zoezi la namna ya ufukuzaji wa tembo kwa kutumia ndege nyuki iliyorushwa kwa umbali wa takribani kilomita 10 huku vipaza sauti vyake vikipiga kelele kuashiria namna ya kufukuza wanyamapori waharibifu.
“Tunaipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake ambazo ni Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana katika kuhakikisha udhibiti wa wanyamapori waharibifu katika Wilaya ya Korogwe unaimarika” alisema Mhe. Mnzava.
Aidha, Askari Uhifadhi Daraja la Tatu, Isaack Daudi kutoka Hifadhi ya Taifa Mkomazi ambaye ni miongoni mwa wataalam wa urushaji wa ndege nyuki katika Shirika (TANAPA) alieleza kuwa ndege nyuki hiyo ni aina ya DJI Matrice 30 (M30) toleo la mwaka 2024 na ina uwezo wa kwenda umbali wa kilomita 10 na juu mita 300, na pia ina teknolojia ya kipaza sauti kwa ajili ya kupiga kelele wakati wa kufukuza tembo jambo linaloongeza ufanisi wa zoezi hilo.
Kituo hicho kilijengwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na kukabidhiwa kwa Hifadhi ya Taifa Mkomazi kwa ajili ya usimamizi ambapo kituo pia kina askari sita (6), gari moja (1) pamoja na ndege nyuki (Drone) 1. Vitendea kazi hivyo ni maalum kwa ajili ya kufukuzia wanyamapori waharibifu wakiwemo tembo wanapovamia makazi ya Wananchi. Wananchi watanufaika na kituo hicho ambapo kitahudumia jumla ya vijiji sita (6) ambavyo ni kijiji cha Manga, Mtitiro, Masira, Kwenangu, Mkomazi na Mikoche.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imekagua kituo hicho katika mwendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii. Kamati hiyo iliambatana na Mhe. Dunstan Kitandula (Mb), Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba, Naibu Katibu Mkuu (Maliasili) na watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.
👍
🙏
3