MwinyiApp
February 20, 2025 at 12:03 PM
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), itaendelea kuweka mazingira wezeshi katika soko la bima ili kuongeza pato la taifa. Akipokea taarifa ya soko la bima kwa mwaka 2023, Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa sekta ya bima kuendana na kasi ya serikali kwa kutumia ubunifu na teknolojia, pamoja na kuimarisha elimu ya bima kwa wananchi. Aidha, alihimiza kufanyika kwa utafiti wa vihatarishi vya mali za serikali, kupitia sheria na kanuni za bima ili ziendane na mazingira ya sasa. Pia, aliwasisitiza wananchi na wadau kutumia huduma za bima, akipongeza uanzishwaji wa ofisi za TIRA kanda ya Unguja na Pemba kwa lengo la kuimarisha huduma hizo.