SAHIHI TV
SAHIHI TV
February 12, 2025 at 06:07 AM
Kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda limevishambulia vikosi vya serikali ya Congo katika jimbo la Kivu kusini katika mapigano ya baada ya ukimya wa siku mbili. Mashambulizi yalianza Jumanne asubuhi ikiwa ni siku tatu baada ya mkutano wa viongozi wa jumuiya ya Afrika mashariki na ile ya kusini mwa Afrika SADC kutoa wito wa mapigano kusitishwa mara moja pasi na masharti. Waasi hao wamedhibiti sehemu kubwa ya ardhi katika eneo la mashariki ikiwemo mji mkubwa wa Goma. Sasa wanashinikiza udhibiti kuelekea Bukavu, mji mkubwa wa jimbo la kusini – ambao ni mji mwingine muhimu katika eneo hilo. Takriban watu 2,900 wameuawa tangu mapema January kutokana na uhasama, kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Umoja wa mataifa. Wengine takriban 700,000 wanakadiriwa kulazimishwa kuyatoroka makazi yao na melfu wengine wamejeruhiwa. Mapigano ya Jumanne yalizuka karibu na Ihusi, eneo lililopo 70km kutoka Bukavu na 40km kutoka uwanja wa ndege jimboni Kivu kusini, duru za usalama zimelieleza shirika la habari la AFP. Msemaji wa Congo River Alliance (AFC), muungano wa makundi ya waasi likiwemo M23 linaashiria kuwa wapiganaji wake huenda wakafikisha vita Bukavu. Lawrence Kanyuka amejibu hatua ya serikali ya Congo kuwakamata maafisa 84 wa jeshi kwa uhalifu kama vile mauaji karibu na Kivu, akisema: "Iwapo uhalifu huu utaendelea, tutawajibika kulimaliza tishio kutoka kwenye chanzo chake na kuwalinda raia wetu". Wakati huo huo, ripoti zinasema kuwa mamia kwa maelfu ya wakimbizi waliotoroka mapigano ya sasa wanalazimishwa na M23 kurudi nyumbani. M23 limekana madai hayo lakini shirika la utangazaji la Ufaransa RFI limeripoti kuwa kambi kadhaa kubwa za watu walioachwa bila makazi zimevunjwa na watu wamelazimishwa kutembea kurudi vijijini wanakotoka katika maeneo ya mizozo. Shirika la Umoja wa mataifa linaloratibu misaada Ocha linasema kuwa M23 liliwapa watu walioachwa bila makazi Goma makataa ya saa 72 kurudi nyumbani. #habarisahihi

Comments