
Samawati Safari
June 11, 2025 at 06:36 AM
MATATIZO YA UGANDA
Mara baada ya Mapambano ya Vita vya Kagera, Mwanzoni mwa mwaka 1979 Vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania vilifanikiwa kumng'oa Madarakani Dikteta Amin wa Uganda na kumpachika Ndugu Yusufu Lule kama Rais wa Muda wa Taifa hilo Jirani. Lule hakudumu sana madarakani kwa kuwa mwezi Juni, 1979 naye aling'olewa madarakani kwa kutofautiana na Baraza la Ushauri la Taifa la Nchi hiyo juu ya uteuzi wa nafasi za Mawaziri, na nafasi yake kuchukuliwa na Ngudu Godfrey Binaisa.
Miezi kadhaa baada ya kuchukua madaraka kwa Binaisa katika Serikali ya Uganda bado mambo ya kuendesha nchi hiyo hayakuonekana kwenda vizuri, Changamoto za kujenga upya nchi hiyo iliyoharibiwa na vita zilikuwa kubwa, huku Jeshi jipya la nchi hiyo likiwa na kashfa ya kufanya ukatili kwa wananchi na pia kushiriki kwenye uhalifu na uporaji. Ili kuimarisha mambo ya Kiutawala ya Nchi hiyo ilimbidi Rais Nyerere ambaye bado vikosi vya Jeshi lake vilikuwa havijaondoka Uganda, ampeleke Waziri Hussein Ramadhani Shekilango kwenda kusaidia mambo ya Kiutawala ya Nchi hiyo.
Mwezi Mei, 1980 ilizuka sintofahamu kubwa katika Utawala wa Uganda, Rais Godfrey Binaisa alimuondoa Jeshini Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Nchi hiyo (zamani akiitwa Chief of Staff) Ndugu David Oyite Ojok na kumteua kuwa Balozi wa Uganda Nchini Algeria, sababu kubwa ikitajwa kuwa ni nidhamu mbaya ya Jeshi la nchi hiyo hasa kwenye masuala ya Ukatili kwa wananchi na Uporaji.
Uamuzi huo wa Rais Binaisa haukumfurahisha Kiongozi huyo Namba 2 wa Jeshi la Nchi hiyo, hivyo alikataa Uteuzi mpya, na wanajeshi waliokuwa Watiifu kwake wakatangaza kumuondoa Madarakani Rais Binaisa aliyekuwa akilindwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika Hekalu la Rais la Entebbe. Misururu mirefu ya Magari ikaonekana katika Jiji la Kamapala, ambapo Wanajeshi watiifu kwa David Ojok walikuwa wakiyapekuwa magari yote yaliyokuwa yakitoka na kuingia ndani ya jiji hilo ili kuhakikisha hakuna silaha, huku pia wakikiteka Kituo cha Redio cha Taifa cha Nchi hiyo.