
RADIO NUUR FM
May 19, 2025 at 04:11 PM
Sheikh wa mkoa wa Tanga Juma Luwuchu amewataka walimu kuwajenga wanafunzi katika malezi mema ya kiimani na maadili kwa kuwapa elimu yenye msingi imara ambayo inatarajiwa kuganda katika akili ya mtoto.
Akizungumza kwenye semina ya walimu walezi shule za msingi na sekondari za jijini Tanga, iliyoandaliwa na jumuiya ya TAMSYA Tanga, Sheikh Luwuchu amesema kuwalingania vijana katika malezi ni msingi imara utakaosaidia.
“Kazi ya kwanza ni kuwalingania wanafunzi na vijana kwa kuwapa malezi thabiti ya kielimu kwani elimu kwa mtoto ni nakshi kwenye jabali” amesema Sheikh Luwuchu.
Sheikh Luwuchu amesema walimu wanafanya kazi kubwa inayowasaidia kukua kimaarifa kutokana na kusoma mara kwa mara maisha ya watoto.
Naye Katibu wa TAMPRO Tanga Mwl. Kombo Ramadhan amewataka walimu kutambua majukumu yao na kuyasimamia, kwani wanafunzi wanaiga mengi kutoka kwa walimu.
“Mwalimu atakapojitambua atajua kuwa ana wajibu wa kutekeleza majukumu yake” amesema Mwl. Kombo Ramadhani.
Mwl. Mwajuma Akiti ni mmoja wa walimu waliohudhuria katika semina hiyo, ambapo amesema amejifunza kuwa, kuna umuhimu wa walimu kumjenga mtoto kiroho kisha taaluma ili mtoto awe mwema kwa jamii na familia.
Abdallah Ngereza | Radio Nuur Habari
