Prime Minister Tanzania

Prime Minister Tanzania

259.0K subscribers

Verified Channel
Prime Minister Tanzania
Prime Minister Tanzania
June 16, 2025 at 02:50 PM
*MAJALIWA: WAKUU MIKOA HAMASISHENI WANANCHI KUTUMIA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA* WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuhakikisha wanaendelea kuhamasisha wananchi kutumia huduma ya kisheria ya Mama Samia ili iwasaidie kutatua changamoto zao za kisheria. Amesema kuwa juhudi za utoaji haki haziwezi kufikiwa na Serikali pekee bali zinahitaji ushirikiano wa dhati kutoka kwa kila mmoja ikiwemo viongozi, wazazi, jamii, taasisi za dini, mashirika ya kiraia na wananchi kwa ujumla. Amesema hayo leo Jumatatu (Juni 16, 2025) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika Mkoa wa Dar es Salaam iliyofanyika kwenye viwanja vya Maturubai Mbagala jijini Dar es Salaam. “Dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki kwa wakati bila ubaguzi, ili kujenga jamii yenye mshikamano na utawala wa sheria, Kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake, tunaweza kuwa Taifa linalojivunia mfumo wa haki ulio imara, unaoaminika, na unaowalinda raia wote kwa usawa.” Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuona Tanzania inaendelea kuwa Taifa linaloongozwa kwa kuzingatia haki, usawa na utawala wa sheria kwa kuwa ndiyo msingi wa amani ya kweli na maendeleo ya kudumu. Amesema kuwa wajibu wa kila mtanzania, taasisi za umma na binafsi, pamoja na wadau wa maendeleo kushirikiana na Serikali kuhakikisha juhudi hizo zinaungwa mkono na zinaendelea kuzaa matunda kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho. Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kutoa taarifa za uwepo wa vitendo vya ukatili katika jamii kwenye vyombo husika bila uoga. “Pale ambapo mwanajamii anaona, anasikia au anahisi kuna ukiukwaji wa haki, ni wajibu wake kuhakikisha suala hilo linaripotiwa mapema sehemu sahihi”.
👍 😂 3

Comments