
TAKUKURU
June 15, 2025 at 01:19 PM
*NW DEUS SANGU: TAKUKURU IMEJIPANGA VYEMA KUDHIBITI RUSHWA UCHAGUZI MKUU*
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imejipanga vyema kudhibiti vitendo vya rushwa kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu, huku akiwaonya watakaogombea kujiepusha na rushwa kwani TAKUKURU ipo kazini.
Ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la TAKUKURU Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, lililogharimu shilingi milioni 314.2. Ameeleza kuwa uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kutoa magari 195 kwa TAKUKURU ni ishara ya dhamira yake ya dhati kupambana na rushwa nchini.
Sangu amesema TAKUKURU itachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayehusika na rushwa ya aina yoyote kwa lengo la kuwarubuni wapiga kura, na kuwasihi wananchi kutokubali kununuliwa bali kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Aidha, amepongeza uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Samia kwa taasisi hiyo, ikiwemo ujenzi wa ofisi 25 na ajira mpya 1,900 kwa watumishi wa TAKUKURU, hatua inayolenga kuongeza ufanisi kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai, amesema hakuna nafasi kwa wagombea wa rushwa katika wilaya hiyo, na kwamba wamejizatiti kuhakikisha viongozi wanachaguliwa kwa misingi ya haki na uwazi.

❤️
👍
📌
🤝
7