
WIZARA YA FEDHA - TANZANIA
June 19, 2025 at 07:39 PM
*WANANCHI WATAKIWA KUFAHAMU GHARAMA ZA MKOPO KABLA YA KUKOPA*
Afisa Mkuu wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, amewataka wakazi wa Dodoma na maeneo mengine nchini kufahamu gharama za mkopo na kuziafiki kabla ya kuchukua mkopo wowote.
Bw. Kimaro aliyasema hayo wakati akitoa elimu ya fedha kwa watu waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha, wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.
Alisema kuwa gharama zinazotakiwa kuangaliwa ni pamoja na riba na ada nyingine zilizoainishwa katika mkataba wa mkopo.
Bw. Kimaro alisema kuwa kabla ya kuchukua mkopo ni vema kumuuliza mkopeshaji kuhusu jumla ya kiasi kinachopaswa kulipwa katika kipindi chote cha mkopo na ni wajibu wa mkopeshaji kumfahamisha mkopaji jumla ya gharama zote zinazohusiana na mkopo husika.
Alisema kuwa riba inaweza kuwa inabadilika au isiyobadilika (Flat interest Rate) ambapo riba inayobadilika hutolewa kulingana na kiasi cha mkopo ambacho hakijarejeshwa na riba isiyobadilika kiwango chake huwa hakibadiliki wakati wote wa kurejesha mkopo
“Kutambua aina za riba kunakuwezesha kupanga kwa usahihi namna ya kurejesha mkopo”, alisema Bw. Kimaro.
Akizungumza baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Wiki ya Utumishi wa Umma, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF, Bw. Paul Kijazi, alisema kuwa elimu ya fedha ni muhimu kwa watanzania na akaipongeza Wizara ya Fedha kwa kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa watanzania wote.
Wiki ya Maadhimisho ya Utumishi wa Umma imeanza Juni 16 na inatarajiwa kuhitimishwa Juni 23 mwaka huu ikiwa na kauli mbiu ya “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidigiti ili kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchangia Uwajibikaji”.
❤️
1