Samawati Safari
Samawati Safari
June 21, 2025 at 08:14 AM
Kwa miaka mingi kabla ya uhuru wa Israel, kulikuwepo mvutano wa mara kwa mara kati ya wakazi wa Kiarabu na walowezi wa Kiyahudi, huku kila upande ukijihisi kutengwa na kuhujumiwa. Uingereza, kama msimamizi wa eneo hilo kwa mujibu wa mamlaka ya Umoja wa Mataifa, ilishindwa kuleta amani kati ya pande hizo mbili. Hatimaye Umoja wa Mataifa ulipendekeza mgawanyo wa ardhi hiyo mwaka 1947, ambapo Palestina ilipaswa kugawanywa katika mataifa mawili: moja la Kiyahudi na lingine la Kiarabu, huku jiji la Yerusalemu likiwa chini ya utawala wa kimataifa. Wapalestina na mataifa ya Kiarabu walikataa mpango huo wakiamini ulikuwa wa upendeleo na usiozingatia haki yao ya kihistoria. Tangazo la uhuru wa Israel lilifuatiwa mara moja na vita kati ya Israel na mataifa jirani ya Kiarabu. Vita hiyo ilisababisha maelfu ya Wapalestina kufukuzwa au kukimbia makazi yao, na hivyo kuanzisha kile kinachoitwa "Nakba", yaani maafa makubwa kwa Wapalestina. Hadi leo, suala la wakimbizi wa Kipalestina limeendelea kuwa sehemu ya mgogoro huo, kwani mamilioni ya Wapalestina bado wanaishi kama wakimbizi katika nchi za jirani, huku wakidai haki ya kurejea katika ardhi walikokimbia au walikofukuzwa.

Comments