
WIZARA YA MAMBO YA NJE
February 15, 2025 at 04:02 PM
AFRIKA YASISITIZA AMANI NA USALAMA WA KUDUMU KWA MAENDELEO
Mkutano wa 38 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 15 hadi 16 Februari, 2025 umesisitiza juu ya umuhimu wa kuweka jitihada za maksudi za kupatikana kwa amani na usalama wa kudumu barani Afrika.
Hayo yameelezwa wakati wa sherehe za ufunguzi wa mkutano huo kupitia hotuba zilizowasilishwa na Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mhe. Abiy Ahmed, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika aliyemaliza muda, Mhe. Moussa Faki Mahatma, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Antonio Guterres, Rais wa Taifa la Palestina, Mhe. Mahmoud Abbas, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika aliyemaliza muda wake na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania, Mhe. Mohamed Ould Cheikh El Ghazouani na Mwenyekiti mpya aliyekabidhiwa madaraka wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Angola Mhe. João Lourenço.
Viongozi hao wameeleza kuwa hivi karibuni suala la amani na usalama limeendelea kuwa changamoto katika bara la Afrika hivyo, ni muhimu jitahada za pamoja za kidiplomasia zikachukuliwa kwa kuruhusu mazungumzo yatakayowezesha kusitisha migogoro na kumaliza vita.
Pamoja na masuala mengine suala la vita inayoendelea kati ya Israel na Palestina ni miongozi mwa masuala ambayo nchi za Afrika zimesisitiza kutokuunga mkono na kwamba zitaendelea na msimamo wake wa kupatikana kwa amani kwa Taifa la Palestina na watu wake. Aidha, imesisitizwa kufanyika kwa majadiliano ya kumaliza migogoro inayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Jamhuri ya Sudan ili kunyamazisha silaha na kuzuia watu wake kuendelea kupoteza maisha na makazi.
Kuhusu kufikiwa kwa maendeleo endelevu kupitia agenda 2030 ya Umoja wa Mataifa na agenda 2063 ya Umoja wa Afrika viongozi hao wameeleza kuwa rasilimali za Afrika zinatakiwa kuwanufaisha waafrika wenyewe ambapo wameeleza asilimia 40 ya madini ya thamani kubwa yanapatikana barani Afrika lakini sehemu kubwa yamekuwa yakiwanufaisha mataifa mengine huku yakiacha migogoro na madeni. Hivyo ni vema kukawepo na mfumo bora wa usimamizi wa utajiri wa rasilimali zilizopo.
Kadhalika, wamesisitiza usawa wa kidunia katika maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano hususan matumizi ya akili mnemba (AI) na upatikanaji wa mtandao kwa gharama nafuu. Fursa zilizopo katika teknolojia ni vema zikanufaisha watu wote ambapo bara la Afrika linahitaji kujengewa uwezo ili kuendana na kasi ya ubunifu na uvumbuzi ulimwenguni.
Suala la nishati ya uhakika ni moja ya masuala yaliyopewa kipaumbele katika hotuba hizo ambapo imeelezwa kuwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Barani Afrika kuhusu Nishati uliofanyika Dar es Salaam, Tanzania umeonesha njia, umeweka mikakati na maazimio ya ifikapo 2030 waafrika milioni 300 wawe wamefikiwa na nishati safi na ya uhakika. Hivyo, ni jukumu linalotakiwa kuchukuliwa na kila nchi kwakuwa nishati ya umeme ni muhimu katika kuwezesha sekta ya viwanda, afya, kilimo, umwagiliaji na sekta nyingine kukua na kupelekea maendeleo kwa bara hilo.
Ujenzi wa miundombinu pia umeelezwa kuwa utarahisisha mawasiliano na kuruhusu usafirishaji wa bidhaa na kukuza biashara kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) ambapo, imeelezwa kuwa ushoroba wa Lobito na bandari ya Dar es Salaam ni kiungo muhimu katika kukuza biashara na usafirishaji.
Maeneo mengine yaliyosisitizwa na viongozi hao ni pamoja na ajira kwa vijana na ushirikishwaji wao katika shughuli za maendeleo, elimu na uelewa kwenye masuala ya kidigitali, jinsia na uwezeshaji kwa wanawake, demokrasia, utawala bora, na umuhimu wa kuzingatia utu na utamaduni wa mwafrika hususan kwa vijana na diaspora.
Uwakilishi wa kudumu wa Bara la Afrika katika Umoja wa Mataifa umelezwa ni jambo linatakiwa kupiganiwa ili kuleta usawa wa uwakilishi wa kikanda na uwasilishwaji wa taarifa za hali halisi na changamoto za Bara hilo ili zipate suluhisho sahihi la mahitaji yake. Hata hivyo, katika hotuba yake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Antonio Guterres amesisitiza kuendelea kusimama na Afrika katika kuhakikisha uwakilishi wa nafasi mbili (2) unapatikana katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
👍
🙏
11