
WIZARA YA MAMBO YA NJE
160.1K subscribers
Verified ChannelAbout WIZARA YA MAMBO YA NJE
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tanzania _______________________________________________ Tanzania Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation
Similar Channels
Swipe to see more
Posts

TAARIFA KWA UMMA


WAZIRI KOMBO AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA WARATIBU WA UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO YA FOCAC Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Waratibu wa Utekelezaji wa Maazimio ya Jukwaa la Ushirikiano baina ya China na Afrika (FOCAC), unaofanyika tarehe 11-12 Juni 2025 jijini Changsha, China. Mkutano huo umejadili utekelezaji wa Mpango Kazi wa FOCAC wa mwaka 2024 na kuidhinisha maeneo manne mapya ya matokeo, yakiwemo: kuimarisha biashara kati ya China na Afrika, utekelezaji wa miradi ya iliyochaguliwa katika ngazi ya majimbo, kuutangaza mwaka 2026 kuwa wa ushirikiano wa watu kwa watu, na azimio la mshikamano dhidi ya vita vya ushuru wa kibiashara vinavyoathiri mataifa yanayoendelea. Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. Wang Yi, ametangaza kuondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa kutoka nchi zote 53 za Afrika zenye uhusiano wa kibalozi na China. Hatua hiyo inalenga kuongeza uingizaji wa bidhaa za Afrika katika soko la China na kuchochea ukuaji wa biashara. Akiwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping, Mhe. Wang Yi amesisitiza kuwa China inaupa kipaumbele cha juu ushirikiano wa kimkakati kati yake na Afrika, hasa katika kipindi hiki ambacho FOCAC inaadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Awali, katika Mkutano wa Kilele wa FOCAC wa mwaka 2024, China ilitangaza hatua 10 za ushirikiano zitakazopewa kipaumbele kwa kipindi cha 2025 hadi 2027, zikiwemo: kujifunza baina ya mataifa, ustawi wa biashara, ushirikiano wa viwanda, maendeleo ya miundombinu, afya, kilimo, ulinzi, maendeleo ya kijani, na ushirikiano wa watu kwa watu. Ili kuendeleza utekelezaji wa malengo hayo, China iliahidi kutoa dola za Kimarekani bilioni 50, ambapo bilioni 29 ni kwa mikopo, bilioni 11 kwa misaada, na bilioni 10 kwa uwekezaji kutoka sekta za umma na binafsi. Tanzania imenufaika na FOCAC kupitia miradi ya maendeleo katika sekta za afya, miundombinu, elimu, teknolojia, mifugo na utalii. Ushiriki wake unaimarisha nafasi ya nchi katika kukuza diplomasia ya kiuchumi na maendeleo jumuishi.


RAIS MSTAAFU WA AFRIKA YA KUSINI MHE. THABO MBEKI AWASILI NCHINI KUSHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA AFRIKA Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini Mhe. Thabo Mbeki amewasili nchini Tanzania Mei 20, 2025, kushiriki Mhadhara wa Siku ya Afrika (Africa Day Lecture) ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao utafanyika jijini Dar es Salaam tarehe 24 Mei, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Thabo Mbeki amepokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato David Chumi (Mb.). Mhadhara huo ambao ni wa 15 kuandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki, unatarajiwa kujadili kuhusu mustakabali wa Bara la Afrika na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wanataaluma, wadau kutoka Serikalini, viongozi wastaafu, vijana, na wawakilishi wa sekta binafsi. Sambamba na Mhadhara huo, Mhe. Rais Mstaafu Mbeki anatarajiwa kushiriki katika mijadala mbalimbali ikiwemo; mjadala kuhusu Uchumi wa Buluu na Utalii, mjadala wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu, halikadhalika majadiliano kuhusu Fursa ya Urais wa Afrika ya Kusini wa kundi la Nchi zenye Uchumi Mkubwa Duniani (G20) kwa ustawi na maendeleo ya Afrika. Mhadhara wa Siku ya Afrika unafanyika nchini baada ya Taasisi ya Thabo Mbeki kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji kwa ukanda wa Afrika Mashariki.


Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah amewasili nchini Mei 20, 2025 kwa ajili ya kuanza ziara rasmi ya siku mbili kuanzia tarehe 20 hadi 21 Mei, 2025. Ziara hiyo ya kwanza kwa Mhe. Nandi-Ndaitwah kufanyika hapa nchini tangu kuingia kwake madarakani mwezi Machi 2025, inafuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Nandi-Ndaitwah amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo. Akiwa nchini pamoja na mambo mengine, Mhe. Dkt. Nandi-Ndaitwah atafanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi ya kujadili namna ya kukuza ushirikiano baina ya nchi hizi mbili. Kadhalika Viongozi hao kwa pamoja watazungumza na Waandishi wa Habari kuelezea makubaliano waliyofikia katika mazungumzo yao kabla ya kushiriki dhifa ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa heshima ya Mhe. Dkt. Nandi-Ndaitwah. Akiendelea na ziara yake nchini, Mhe. Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah, Mei 21, 2025 anatarajiwa kutoa Mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na kutembelea Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika kilichopo Dar es Salaam. Tanzania na Namibia zimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria ulioasisiwa na Waasisi wa mataifa haya mawili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sam Nujoma kupitia mikataba mbalimbali ya uwili na masuala yote yanayohusu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amempokea Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mheshimiwa Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah Ikulu, jijini Dar es Salaam, Mei 20, 2025.


TANZANIA NA FINLAND KUSHIRIKIANA KATIKA DIPLOMASIA YA UCHUMI Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Finland zimeazimia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kupitia sekta za kimkakati kama vile nishati, biashara na uwekezaji, ili kukuza diplomasia ya uchumi. Azma hiyo imefikiwa katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika Ofisi Ndogo ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam, kikihusisha viongozi waandamizi kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Naibu Waziri wa Biashara za Kimataifa wa Finland, Mhe. Jarno Syrjรคlรค. Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, amesema Tanzania inaendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kushirikiana na mataifa rafiki kama Finland, kwa lengo la kufungua fursa zaidi za maendeleo. Amesisitiza kuwa ushirikiano huo una mchango mkubwa katika kuleta teknolojia, mitaji, na ujuzi unaoweza kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa. Kwa upande wake, Mhe. Syrjรคlรค amepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia wawekezaji wa kimataifa. Amesema Finland iko tayari kushirikiana na Tanzania katika maeneo yenye maslahi kwa pande zote, hususan nishati jadidifu, teknolojia ya kisasa na elimu ya ufundi stadi. Katika kikao hicho, ujumbe wa Tanzania uliwasilisha vipaumbele vya Serikali katika kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda, kilimo, nishati na utalii. Pia, ujumbe huo umetoa wito kwa wawekezaji kutoka Finland kutumia fursa zilizopo kuwekeza nchini. Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho ulijumuisha viongozi na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).


Matukio mbalimbali ya Uzinduzi wa Baraza jipya la Wafanyakazi la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Uzinduzi huo umefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa JNICC, uliopo jijini Dar es Salaam. Tukio hilo limefanyika tarehe 11 Mei, 2025.

Leo tarehe 20 Mei, 2025, Mhe. Cosato Chumi (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Giuseppe Coppola. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam. Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Coppola ameeleza kuhusu nia ya Serikali ya Italia kuendelea kuunga mkono jitihada za kuleta maendeleo zinazofanywa na Serikali chini ya uongozi mahiri wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kuthibitisha hilo, Balozi Coppola amejulisha kuwa Italia iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mkopo wa gharama nafuu wa Dola milioni 281 kusaidia utekelezaji wa Awamu ya nne ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa. Vilevile, alijulisha kuhusu kurejeshwa kwa Tanzania katika orodha ya nchi zinazonufaika na mitaji inayowezesha kuboresha elimu ya ufundi stadi, ambapo kupitia mpango huo Tanzania itanufaika na ufadhili wa hadi Euro milioni 20. Katika hatua nyingine, Tanzania na Italia zilikubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta ya uchumi wa buluu, uchukuzi na usafirishaji, mawasiliano na teknolojia ya habari, kilimo na ufugaji, ulinzi na usalama pamoja na biashara na uwekezaji.