
Mwigulu Nchemba
January 24, 2025 at 09:38 AM
*ASANTENI WALIPAKODI*
Awali ya yote, nichukue fursa hii kumshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya utoaji Tuzo kwa Walipakodi Bora wa mwaka 2023/24.
Tunathamini sana heshima hii na uongozi wako wa kuhamasisha ulipaji kodi kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Rais, tunapokea kwa uzito mkubwa mwelekeo, maelekezo na maagizo uliyotupa. Napenda kukuhakikishia kuwa tayari tumeanza kuyafanyia kazi kwa haraka na kwa weledi, tukiweka msisitizo katika ukusanyaji wa mapato kwa haki—bila dhuluma kwa walipakodi na bila kuruhusu mianya ya ukwepaji kodi kutoka kwa wasio waaminifu.
Kwa heshima kubwa, tunashukuru sana kwa kukubali kuzibeba Tuzo hizi kwa Jina lako, ambapo sasa zitajulikana kama TUZO ZA RAIS kwa Walipakodi Bora. Hatua hii ni ya kihistoria na inatoa msukumo mkubwa kwa walipakodi wote nchini, huku ikihamasisha uwajibikaji na uwazi katika kulipa kodi. Tunaamini kuwa hatua hii itaongeza hadhi ya Tuzo hizi hadi ngazi ya kimataifa.
Pia, nawapongeza kwa dhati Kamishna Mkuu wa TRA na watumishi wote wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa maandalizi mazuri na mafanikio ya hafla hii. Kazi haijaisha—sasa ni wakati wa kutekeleza maelekezo na matarajio ya Mheshimiwa Rais kwa bidii na umakini mkubwa.
Kwa Walipakodi wote mlioibuka washindi wa tuzo hizi siku ya jana, hongereni sana! Mmeonesha mfano bora wa uzalendo kwa kulipa kodi kwa uaminifu. Ni rai yangu kwenu kuendelea na moyo huo huo, kwani kupitia kodi zenu, Taifa letu linaweza kujitegemea kiuchumi na kusonga mbele kimaendeleo, kama ambavyo Mheshimiwa Rais ameazimia.
Natoa wito kwa Walipakodi wote nchini kuhakikisha wanalipa kodi stahiki kwa hiari, ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima na kusaidia kukuza uchumi wetu kwa manufaa ya wote.
*ASANTENI WALIPAKODI, ASANTE MHESHIMIWA RAIS.*
❤️
👍
🙏
😂
21