Tume Ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC)
                                
                                    
                                        
                                    
                                
                            
                            
                    
                                
                                
                                February 8, 2025 at 06:45 PM
                               
                            
                        
                            Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa amefunga maadhimisho ya wiki ya anwani za makazi nchini na amezindua matumizi ya progaramu tumizi ya anuani za makazi (NAPA) itakayotumika kupitia simu ya kiganjani na itakayowawezesha wananchi kutambua kwa urahisi maeneo ya karibu ya kupata huduma.
Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 08/02/2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya anwani za makazi iliyoandaliwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Akizungumza katika ufungaji ya wiki ya anwani ya makazi na uzinduzi wa programu ya NAPA, Mhe. Majaliwa amewataka wananchi kutumia programu ya NAPA ili iwaongoze katika kupata huduma mbalimbali. 
“Mfumo wa anuani za makazi ni daftari la kidijitali la wakazi pamoja na makazi linalolenga kuharakisha na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii kwenye maeneo yetu, kuimarisha maswala yote ya ulinzi na usalama nchini, kuchochea uchumi na ukuaji wake, kuwezesha biashara za mtandaoni kufanyika wakati wote na kwa ufanisi, na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na majanga mbalimbali kwa urahisi. Huu mfumo upo nchini, kila mmoja aanze kuutumia” amesema Mhe. Majaliwa.
Mhe. Majaliwa pia amezindua huduma ya kuomba, kutoa na kupokea barua ya utambulisho wa makazi kidijitali kupitia mfumo wa anuani za makazi (NAPA) itakayowawezesha wananchi kuomba na kupata barua ya utambulisho bila kufika kwenye ofisi zinazohusika kutoa barua hizo.
‘Ili kuweza kupata huduma hii ya barua ya utambulisho kupitia programu ya NAPA, mwananchi anatakiwa awe na anuani ya makazi iliyosajiliwa kwenye mfumo wa NAPA. Hii itamrahisishia mwananchi kupunguza muda wa kutumia kusafiri kufuata huduma hii kwenye ofisi zinazohusika’ amesema Mhe. Majaliwa.
Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) pia imeshiriki kwenye maadhimisho hayo ya wiki ya anuani za makazi yamefanyika kwa mara ya kwanza nchini kuanzia tarehe 06 hadi 08/2025 yenye kauli mbiu ‘Tambua na tumia anwani za makazi, kuimarisha utoaji na upokeaji wa huduma’ ambapo kulikuwa na banda maalum la kuonyesha shughuli zinazotekelezwa na PDPC na kuelimisha umma kuhusu dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi.
                        
                    
                    
                    
                    
                    
                                    
                                        
                                            👍
                                        
                                    
                                    
                                        2