Tume Ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC)
Tume Ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC)
February 13, 2025 at 07:36 PM
UNWANTED WITNESS KUTOKA UGANDA WATEMBELEA PDPC Leo, Februari 13, 2025, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imepokea wageni kutoka asasi ya kiraia ya ‘Unwanted Witness’ kutoka Uganda, inayojishughulisha na kukuza uhuru mtandaoni na kulinda haki za kidijitali. Bi. Freda Nalumansi Mugambe, kiongozi wa Utafiti na Utetezi wa asasi hiyo, alitembelea ofisi za PDPC Njedegwa, Dodoma, kuomba ushirikiano katika kuandaa kongamano la ulinzi wa faragha litakalofanyika Septemba 2025. Katika mazungumzo yao, Bi. Mugambe alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika mashindano ya kuwapata washindi kati ya wanafunzi wa sheria kutoka vyuo vikuu vya nchi washiriki, ili kuimarisha uelewa wao juu ya dhana ya faragha. Alisema kuwa wanafunzi hao ni muhimu kwa mustakabali wa ulinzi wa taarifa binafsi, kwani watakuwa na jukumu kubwa katika kuhakikisha haki hizi zinapatikana kwa umma. Kwa upande wa PDPC, Wakili Humphrey Mtuy, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Dkt. Emmanuel Mkilia, alithibitisha kuwa tume itatoa ushirikiano kwa ‘Unwanted Witness’. Alieleza kuwa shughuli za asasi hiyo zinaendana na malengo ya PDPC ya kutoa elimu kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi, na kwamba ushirikiano huu utasaidia kuongeza uelewa katika jamii. Kongamano la mwaka huu litakuwa na kauli mbiu ‘Ulinzi wa taarifa na mfumo wa vitambulisho vya taifa’ (Data Protection and National Identification Systems). Washiriki kutoka vyuo 19 nchini Tanzania watashiriki katika kutafuta washindi watatu watakaopatiwa zawadi, ikiwemo fedha taslimu na makombe. Washindi hao pia watapata fursa ya kushiriki katika midahalo ya kitaaluma kuhusu ulinzi wa taarifa, hivyo kuchangia katika maendeleo ya sheria na haki za kidijitali nchini.
👍 2

Comments