
Nuru Ya Imani
February 24, 2025 at 07:59 AM
Shalom wana wa Mungu!
Tunashukuru Mungu wetu kwa wema wake na fadhili zake nyingi juu ya maisha yetu.
Leo hii tunaangalia uwezo wa Mungu katika kufunua yaliyo siri. Ningependa nianze swali hapa
"Je, umewahi kupitia wakati ambapo hukuelewa nini kinaendelea maisha yako? Labda ulikuwa na swali lisilo na jibu, au ulichanganyikiwa kuhusu hatua inayofuata?. Je ulichukua hatua gani kupata majibu ya maswali yako?
Tunapojaribu kutafuta majibu kwa akili zetu wenyewe, tunagundua kuwa hatuwezi kuona mbele wala kupata mwafaka. Lakini Leo hii tu najifunza kuna mmoja anayejua kila kitu, hata yale yaliyofichwa.
Danieli 2:22 inasema: ‘Yeye huufunua yaliyo mazito na ya siri; hujua yaliyomo gizani, na nuru hukaa pamoja naye.’ BHN
Hii inatufundisha kuwa Mungu ndiye chanzo cha ufunuo na hekima. Hakuna kitu kinachoweza kufichika kwake. Ikiwa kuna jambo linalokutatiza leo, usijaribu kutegemea nguvu zako mwenyewe. Mgeukie Mungu, mwombe akuonyeshe njia, naye atakufunulia."
Mungu ana uwezo wa kufunua mambo yaliyofichika na kuyafanya yajulikane. Anajua kila siri kwa sababu hakuna giza mbele yake yeye ni nuru yenyewe.
Mwenye uwezo wa kutuonyesha mambo tunayohitaji kujua, kutupa hekima, na kutuongoza katika maamuzi yetu ni Mungu pekee.
Tukisoma sura nzima, tunaona jinsi ambavyo Danieli aliomba kwa Mungu na kupokea ufunuo wa ndoto ya Mfalme Nebukadneza,jambo lililowezekana kwa sababu Mungu ndiye mfunuaji wa siri. Hapa tunajifunza kutozitegemea akili zetu bali kumwomba Mungu atupe hekima na ufunuo katika maisha yetu ya kila siku.
Tuombe:
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu. Mungu wa nuru na ufunuo, tunakushukuru kwa kuwa hakuna kilichofichika machoni pako. Tunakuomba utufunulie mapenzi yako maishani mwetu, utupe hekima na kuelewa yale tunayopaswa kufanya.
Tunaomba nuru yako ing'ae na kuangaza katika kila hali ngumu tunayopitia na utuonyeshe njia sahihi ya kuiendea.
Kama ulivyomfunulia Danieli, tunaomba utufunulie mambo mazito na ya siri yanayohusu maisha yetu, huduma zetu, na hatima yetu(ongeza hitaji lako) .
Katika jina la Yesu, Amina.
❤️
1