
Ashraf JK 💚💙
February 27, 2025 at 05:24 AM
Malaria bado ni changamoto kubwa ya kiafya duniani, hasa barani Afrika ambako asilimia 97 ya maambukizi hutokea. Katika mjadala uliofanyika jana nchini kenya kupitia televisheni ya KTN kwenye kipindi cha "Your World", Dk. Willis S., mshauri maalum wa ALMA (African Leaders Malaria Alliance), anasisitiza lengo la kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo na maambukizi ifikapo 2025 na kutokomeza malaria kabisa ifikapo 2030.
Takwimu za 2023 zinaonyesha kuwa malaria inaendelea kuenea, ikiwa na kesi milioni 251 duniani, huku vifo vikifikia karibu 600,000. Ingawa kumekuwa na upungufu wa asilimia 4 katika maambukizi na asilimia 15 katika vifo tangu 2015, kasi ya kupambana na malaria imepungua kutokana na changamoto mbalimbali.
Dk. Willis anataja sababu za kusuasua kwa juhudi za kutokomeza malaria, zikiwemo uhaba wa ufadhili (asilimia 50 tu ya mahitaji yalifadhiliwa mnamo 2023), usugu wa vimelea vya malaria dhidi ya dawa, na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazosababisha mazingira bora kwa mbu waenezao ugonjwa huo.
Suluhisho zilizopendekezwa ni pamoja na matumizi ya neti zenye dawa za viua wadudu, chanjo ya RTS,S ambayo ina ufanisi wa asilimia 40, na mwitikio wa jamii kwa hatua za kujikinga. Ili kufanikisha lengo la kutokomeza malaria, ushirikiano wa serikali, sekta binafsi, na jamii unahitajika kwa dharura.
#kmt
#ashrafjk
#afyatamu