Nukta Habari
February 3, 2025 at 03:40 PM
Rais Samia Suluhu Hassan amesema Mahakama ya Tanzania itakuwa na mchango katika kuiwezesha nchi kufikia malengo ya maendeleo kama yalivyobainishwa kwenye Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kwa kuweka mifumo bora ya kisheria na inayoendana na wakati.
Dira hiyo inayotoa mwongozo wa malengo na mwelekeo wa maendeleo ya nchi kwa miaka 25 ijayo itaanza kutekelezwa mwaka huu hadi mwaka 2050 baada ya ile ya awali kuisha muda wake.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika mkoani Dodoma leo Februari 3, 2025 amesema kuwa dira hiyo itavutia ongezeko la mitaji ya uwezekezaji nchini hivyo mahakama na sekta zote za haki madai zijiandae vyema.
“Utekelezaji wa dira utavutia mitaji ya uwekezaji jambo litakalohitaji kuingia mikataba mbalimbali baina ya Serikali na sekta binafsi. Hivyo, natoa rai kwa sekta zote zinazohusika na haki madai kujiandaa vyema katika kutoa huduma za haki,” amesea Rais Samia.