
Nukta Habari
February 14, 2025 at 10:01 AM
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajia kufanya ziara ya kikazi jijini Addis Ababa, Ethiopia, kuanzia leo hadi Februari 16, 2025 kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).
Taarifa ya Sharifa Nyanga, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu iliyotolewa Februari 13, 2025 inabainisha kuwa mkutano huo utahusisha uchaguzi wa mwenyekiti mpya wa umoja huo kwa mwaka 2025.
Uchaguzi huo unafanyika ili kumpata mrithi wa Rais wa umoja huo Mohamed Ould Cheikh El Ghazouani kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania anayemaliza muda wake.
Kwa mujibu wa Katiba ya AU, kila mwaka wakuu hao wa nchi wanatakiwa kufanya uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti wa wa umoja huo ambaye huchaguliwa kutoka miongoni mwa viongozi wa nchi wanachama, kwa msingi wa mzunguko wa kanda za Afrika.
