Tanzanian Catholics Online
Tanzanian Catholics Online
February 17, 2025 at 06:10 AM
https://youtu.be/hMuaVVEmN3U?si=xvzbFvcd1n4nt56M Usiahau ku-SUBSCRIBE kupitia link hii https://youtube.com/@asalimubashara?si=x-OFlyZwW6PI8G4z watumie pia wengine waweze kulisikia neno la Mungu na kulishika. MASOMO YA MISA, FEBRUARI 17, 2025 JUMATATU, JUMA LA 6 LA MWAKA Mwa 4: 1-15, 25; Adamu alimjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana. Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi. Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyma dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye, twende uwandani. Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua. Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoto na mtu asiye na kikao duniani. Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki. Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami niakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua. Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo yeyote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pia Habili; kwa sababu Kaini alimwua. Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu. WIMBO WA KATIKATI Zab. 50:1, 8, 16 – 17, 20 – 21 (K) 14 (K) Umtolee Mungu dhabihu za kushukuru. Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi, Toka maawio ya jua hata machweo yake. Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako, Na kafara zako ziko mbele zangu daima. (K) Bali mtu asiye haki, Mungu amwambia, Una nini wewe kuitangaza sheria yangu, Na kuliweka agano langu kinywani mwako? Maana wewe umechukia maonyo, Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. (K) Umekaa na kumsengenya ndugu yako, Na mwana wa mama yako umemsingizia. Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza, Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe. Walakini nitakukemea; Nitayapanga hayo mbele ya macho yako. (K) SHANGILIO 1Sam. 3:9 Aleluya, aleluya, Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia: Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Aleluya. INJILI Mk. 8:11 – 13 Walitokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana na Yesu; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu. Akaugua rohoni mwake, akasema, Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni, Hakitapewa ishara kizazi hiki. Akawaacha akapanda tena chomboni, akaenda zake hata ng’ambo. Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo. *ASALI MUBASHARA-Jumatatu 17/02/2025* Karibuni ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana linaanza kwa kuiangalia Zaburi yetu ya Wimbo wa katikati toka zaburi ya 50. Hapa tunakutana na Zaburi isemayo: umtolee Mungu dhabihu za kushukuru. Hii ni amri, zaburi hii inasisitiza pia tena kwamba kila tujapo kwa Bwana kwa ajili ya hii dhabihu, lazima moyo wetu uwe safi. Na hapa Bwana huipokea na kuibariki dhabihu hii. Leo katika masomo yetu, anayetimiza hili ni Abeli. Yeye anakuja mbele ya Bwana na dhabihu ya kushukuru, na anakwenda na moyo safi, na dhabihu yake inakubaliwa. Kaini anakwenda na moyo mkaidi, na mara moja inakataliwa. Moyo wa uchoyo na hasira na chuki ndio unaofanya dhabihu nyingi zisikubalike. Yawezekana Kaini alikwenda mbele za Bwana na moyo kama huu. Bwana hakupokea dhabihu yake. Sisi tutambue kwamba ni wajibu wetu kutoa dhabihu mbele ya Bwana. Sisi tuje mbele ya Bwana, tuondoe chuki, na hasira na uchoyo. Uchoyo unaotukumba wengi ni kukataa kutoa muda Wetu kwa Bwana. Kuna wakati kweli tunanogewa na kazi, kazi inanoga tunamtupa Bwana pembeni. Pia tunakuja na chuki sana na wengine-mbele ya Yesu hakuna haja ya kuhifadhi chuki kabisa. Huu ndio udhaifu wetu, lakini inatupasa kuuleza mbele ya Bwana, tuukubali udhaifu huu. Tumuombe atusaidie. Kwenye somo la Injili, Yesu anakataa kuwapatia ishara Wafarisayo. Yesu anakataa kuwapa ishara kwani hii ilikuwa ni ishara kwa wasio na Imani, walitaka kumjaribu. Kati ya vitu anavyovichukia Yesu ni kutaka kujaribiwa. Yeye anatenda muujiza kwa aliye na imani. Hata siku moja hatendi muujiza kwa asiye na imani. Hiki kilichowapata mafarisayo ndicho kinachotutokea na sisi kila siku ndugu zangu. Wengi wetu hatujibiwi kwa sababu tunakwenda mbele ya Yesu bila imani. Ukosefu wa unyofu unatukosesha mengi, tukiwa mbele ya Yesu ni lazima tuoneshe unyofu. Yesu alisema heri walio wanyofu wa moyo, maana watamuona Mungu. Unyofu wa moyo ni kuishi kiapo chako bila kuonesha ufarisayo, bila kuwa ndumila kuwili, kama ni watu wa ndoa tunaishi kama watu wa ndoa kweli. Sisi tukazane kuwa wanyofu. Unyofu ni ufunguo wa baraka maishani mwetu. ©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.
Image from Tanzanian Catholics Online: https://youtu.be/hMuaVVEmN3U?si=xvzbFvcd1n4nt56M  Usiahau ku-SUBSCRIBE...

Comments