
Aviation Media Tanzania
February 27, 2025 at 01:09 PM
Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania imetia saini mkataba na Kampuni ya Saba Engineering Private Company Limited kwa ajili ya huduma za ushauri na ubunifu wa kina wa ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha kimataifa cha Serengeti.
Hafla hiyo ya utiaji saini imefanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu huku ikishuhudiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Serengeti Dkt. Maulid Madeni, Menejimenti ya TAA na Mwenyekiti wa kamati ya Serengeti ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Serengeti Dkt. Rhimo Nyansaho.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Abdul Mambokaleo alielezea kuwa mradi utatekelezwa na Mhandisi Mshauri, Saba Engineering Private Company ltd kwa ushirikiano na Intairplan GMBH na Projectplus Consult (T) LTD ambapo gharama za mradi huu ni kiasi cha Shilingi Bilioni 1.3 huku muda wa utekelezaji wa mkataba utakuwa ni wa Miezi sita (6) mara baada ya kusainiwa kwa mkataba huu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Serengeti Dkt. Maulid Madeni amesema, kuja kukamilika kwa mradi wa kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Serengeti kitawezesha watalii kuongezeka kutemebelea mbuga ya Serengeti kutokana na urahisi wa kufika mbugani moja kwa moja pia na kuwezesha kuongezeka kwa huduma mbalimbali Wilayani Serengeti ikiwemo kodi jambo ambalo litasababisha kuongeza uchumi na ajira katika eneo hilo.
Naye Mwenyekiti wa Kamati Serengeti na Mjumbe wa Bodi ya TANAPA Dkt. Rhimo Nyansaho amesema ukamilikaji wa Kiwanja cha Serengeti utawezesha urahisi wa mtalii kufika katika eneo hilo na kupunguza vikwazo vitakavyo mfanya aishie nchi jirani bila kufika nchini.
