
Aviation Tanzania 🇹🇿
February 19, 2025 at 07:24 AM
https://www.instagram.com/p/DGPvEHcN6Xl/?igsh=ajZqajltZndqYXds
*Ifahamu East African Airways, Chimbuko la Mashirika Makubwa Matatu Afrika Mashariki.*
Shirika la Ndege la East African Airways (EAA) lina nafasi ya kipekee katika historia ya usafiri wa anga Afrika Mashariki.Kuanzishwa kwake kulitokana na mapendekezo ya kamati ya usafiri wa anga,Afrika Mashariki, mwaka 1943 kisha shirika hilo likasajiliwa rasmi jijini London tarehe 30 Oktoba 1945.
EAA ilikuwa na Mamlaka ya pamoja ya usafiri wa anga katika nchi za Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar, ambazo wakati huo zilikuwa chini ya utawala wa Uingereza.
Shirika hilo lilijengwa katika misingi ya Wilson Airways, shirika la ndege lililoanzishwa mwaka 1929 na Bi. Florence Wilson, raia wa Uingereza. Kufuatia maono yake, EAA ilianzishwa ili kushughulikia mahitaji ya usafiri wa anga Afrika Mashariki.
Makao makuu ya EAA yalikuwa Nairobi, Kenya, na shirika hili lilihudumia si tu Afrika Mashariki bali pia maeneo ya mbali kama London, Cape Town, Bombay, Zurich, Rome, Athens, New York, na Frankfurt.
Hadi wakati Shirika hilo linasitisha huduma zake,lilikuwa na jumla ya ndege 20 na zilizotoa huduma ya usafiri katika maeneo zaidi ya 60 duniani.
Katika miaka yake ya awali, EAA ilianza shughuli zake na ndege sita aina ya DH89A Dominies zilizokodishwa kutoka BOAC, ambapo zilifanya safari 21 kwa wiki ndani ya Afrika Mashariki, zikipitia miji kama Nairobi, Mombasa, Zanzibar, Dar es Salaam, Lindi, Moshi, Kisumu na Entebbe. Katika mwaka wake wa kwanza, shirika lilisafirisha abiria 9,404 kwa jumla ya maili 587,073, ingawa lilipata hasara ya £25,483.
Pamoja na mafanikio yake, EAA ilikumbana na changamoto nyingi ikiwemo ile iliyojitikeza Juni 28, 1945, ambapo ndege yake aina ya Rapide VP-KCU ililazimika kutua kwa dharura karibu na Garsen kutokana na rubani kuchukua mwelekeo usio sahihi. Abiria watano na mtoto mchanga walikuwa miongoni mwa walionusurika katika tukio hilo ambapo walikaa porini kwa siku tatu kabla ya kuokolewa.
Kadri miaka ilivyopita, EAA ilikumbana na changamoto za kifedha, ushindani mkali, na muingiliano wa kisiasa ndipo Januari 1977, shirika hili lilisitisha safari zake rasmi, na hivyo kupelekea Kenya, Uganda, na Tanzania kuanzisha mashirika yao ya ndege ya kitaifa.
Hadi hivi leo, EAA inabaki kuwa sehemu muhimu ya historia ya anga Afrika Mashariki. Ingawa haipo tena, mchango wake uliweka msingi wa mashirika ya ndege ya kitaifa kama Kenya Airways, Uganda Airlines, na Air Tanzania ambayo kwa sasa yana mtandao mkubwa barani Afrika na duniani.
Watu wengi wa Afrika Mashariki bado wanajiuliza, "Je, ingekuwaje kama EAA ingedumu hadi sasa?"