
Wizara ya Ardhi
February 16, 2025 at 06:21 AM
PINDA KUUNDA TIMU KUBAINI WAMILIKI WA MASHAMBA KITETO
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amesema ataunda timu ya wataalamu kufanya utafiti kuwabaini wamiliki wa mashamba ikiwa ni jitihada za kutatua migogoro ya ardhi wilayani Kiteto pamoja na mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya hiyo na Wilaya ya Chemba.
Naibu Waziri Pinda amesema hayo Februari 15, 2024 wakati akizungumza na umati wa wananchi wa wilaya hizo mbili katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji Ndareta na kuhudhuriwa na kamati ya Usalama ya Wilaya ya Kiteto ikiongozwa na Mkuu wa wilaya Mhe. Remidius Mwema.
Vilevile Mhe. Pinda amesema kuwa timu hiyo itakuwa suluhu ya migogoro ya mpaka kati ya Kiteto na Chemba kwa kufanya zoezi la upimaji ili kubaini mipaka halisi ya maeneo hayo.
Mhe. Pinda amebainisha timu hiyo itaongozwa na na Mkugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Viongozi mbalimbali kutoka pande zote mbili zenye mgogoro huo.
Kadhalika Naibu Waziri amewaasa wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa timu hiyo ili kupata taarifa sahihi na kutafta majawabu ya migogoro ya ardhi wilayani Kiteto na Chemba.
Aidha, Mhe. Pinda amewataka wananchi hao kuwa watulivu wakati timu hiyo ikitekeleza kazi yake kwani Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inataka kila mtanzania aishi kwa furaha.
Ziara hiyo ya Naibu Waziri Pinda ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa Januari 29, 2025 akiwa Bungeni Jijini Dodoma ya kufika wilayani hapo kusikiliza malalamiko ya wananchi juu ya mpaka wa wilaya za Chemba na Kiteto.