KitaaCtics: Where the Elite Meets The Streets
KitaaCtics: Where the Elite Meets The Streets
February 10, 2025 at 11:41 PM
*KISASI CHA ADEBAYOR* *SHANGILIO LA GOLI LISILOSAHAULIKA NA WASHABIKI WA ARSENAL* *Ni Septemba 12, 2009.* Mashabiki wa Arsenal wamejazana kwenye Uwanja wa Etihad jijini Manchester. Wengi wao wanamshangilia Arsene Wenger na kikosi chake, lakini kuna jina moja wanaloimba kwa dharau, *Emmanuel Adebayor.* Nyota huyu wa Togo ambaye kutokana na ustadi wake wa kufumania nyavu washabiki wa Arsenal nchini Tanzania waliwahi mtungia jina la kumsifia wakimwita *Ade-mabao.* Lakini tokea ahame mambo yalikuwa tofauti sana. Ilikuwa wazi, hawakumsamehe kwa kuhamia Manchester City kwa dau la *pauni milioni 25 (kama bilioni 79 za TZS).* Adebayor ambaye alikuwa na sababu zake za kuondoka, akiwa Arsenal, alihisi hakuheshimiwa vya kutosha. Alitaka mkataba mpya na kuthaminiwa zaidi, lakini badala yake, Wenger akampa mlango wa kutokea na hadi kumfungia kuingia kwenye viunga vya mazoezi. Hivyo tangu alipoondoka, matusi na kejeli kutoka kwa mashabiki wa Arsenal yalikuwa sehemu ya maisha yake. Hata hivyo, kwa Adebayor, haya yote yalikuwa kidogo ukilinganisha na kilichotokea siku ya mechi hiyo pale Etihad Stadium . Siku hiyo, alipokuwa anaingia uwanjani, mashabiki wa Arsenal walikuwa wakimrushia maneno ya kejeli na nyimbo za dharau. Kati ya mambo yaliyomuumiza zaidi, walikuwa wakiimba: _“Baba yako anaosha tembo, mama yako ni malaya!”_ Katika mila za Kiafrika, kutukanwa wewe ni jambo moja, lakini familia yako ni suala lingine kabisa. Kwa Adebayor, hili lilikuwa dharau kubwa sana. Alikaza uso, lakini moyoni, moto ulianza kuwaka. Mechi ile ilianza ikichezwa kwa kasi na mashambulizi ya hapa na pale kati ya timu hizo mbili. Hadi kipindi cha pili Arsenal walikuwa wakihangaika kupata bao la kusawazisha baada ya City kuongoza. Ndipo dakika ya 80 ikawadia wenyeji wakiwa wanaongoza goli 2-1, Shaun Wright-Phillips alipiga krosi safi langoni mwa Arsenal, na Adebayor akaruka juu na kupiga kichwa maridadi kabisa na kuipatia Man City goli la tatu. Kwa kawaida nyakati kama hii mfungaji wa goli huwa hapendi kushangilia kuifunga timu yake ya zamani kama ishara ya heshima na mahusiano waliyojenga wakati anachezea timu hiyo, lakini kitu tofauti sana kilitokea siku hiyo. Mashabiki wa City wakalipuka kwa furaha, lakini kwa Adebayor, bao hilo lilikuwa zaidi ya ushindi wa mpira ilikuwa haki yake ya kujibu matusi!Na moyoni mwake hakukuwa na tone hata moja la heshima kwa Arsenal. Akiwa hana muda wa kushangilia kawaida, alikimbia moja kwa moja takribani mita 100 kuelekea upande wa mashabiki wa Arsenal. Alifika mbele yao, akapiga magoti, akapanua mikono, na akawaangalia kwa dharau! Mashabiki wa Arsenal walilipuka kwa hasira! Walirusha chupa, wakapiga kelele, wengine wakajaribu kuvamia uwanja. Lakini Adebayor alibaki pale pale, akiwatazama kwa macho ya mtu aliyeshinda vita yake binafsi. Kiko wapi?!Tukaneni tena. Baada ya mechi, magazeti yote yaliandika kuhusu ushangiliaji ule wa Adebayor. Wengine walisema amekosa heshima, wengine walisema alitaka tu kuchokoza. Lakini ukweli uliojificha haukuwa umewekwa wazi. Nawafahamu washabiki wa Arsenal ambao walisema hawatomsamehe kamwe. Adebayor baadaye alifunguka kuwa moja ya sababu kubwa za kushangilia vile ni jinsi mashabiki wa Arsenal walivyomtusi na familia yake. Katika mahojiano na Goal.com, alisema: _“Ubaguzi wa rangi ulikuwa mkubwa kupita kiasi. Walimtukana mama yangu, walimtukana baba yangu, sababu sikuwa na uwezo wa kupambana na umati ule ilinibidi nijibu kwa njia yangu niliyoona inafaa.”_ Mbali na hayo, Adebayor pia alikuwa amepokea vitisho vya kifo kutoka kwa mashabiki wa Arsenal, kiasi cha kuhitaji ulinzi wa ziada. Mashabiki wa Arsenal walionekana kuapa kutomruhusu tena kuwa huru. Kwa Adebayor, siku hiyo haikuwa tu mechi. Ilikuwa ni fursa ya kujibu matusi na dharau kwa njia pekee aliyoweza kufunga bao na kuwaonyesha kuwa hawezi kufungwa na maneno yao. Hata hivyo, shangwe ile haikupita bila adhabu FA ilimfungia mechi mbili na kumpiga faini ya *pauni 25,000* kwa kushangilia kwa uchochezi mbele ya mashabiki wa Arsenal. Lakini kwa Adebayor, haikuwa hasara maana kwake ilikuwa haki imepatikana na moyo wake ulikuwa na amani. Akinukuliwa miaka mingi baadae nguli huyu wa kutoka Togo anasema hana majuto na tukio lile hata punje. Na hata leo, ushangiliaji ule unasalia kuwa moja ya ushangiliaji mabao wenye utata mkubwa zaidi katika historia ya soka. *Mjombaako* *©️BantuKwanza*
👍 😂 2

Comments