
KitaaCtics: Where the Elite Meets The Streets
257 subscribers
About KitaaCtics: Where the Elite Meets The Streets
Tunaongea maisha,matukio mbali mbali,saikolojia,falsafa,mahusiano,na habari zote za walimwengu na ulimwengu. The Home of Knowledge Elimu na Kitaa!Ishi na Jifunze Lugha:Swahili na English! Host :*Yours Truly* *BantuKwanza*
Similar Channels
Swipe to see more
Posts

Wale wapenzi wa NBA. Tyrese Haliburton ambaye ni mlinzi katika timu ya Indiana Pacers ana rekodi ya aina yake ya kuwa mmoja ya wachezaji wanne tu katika historia ya NBA waliozaliwa February 29.. Alizaliwa February 29, 2000…


*HAKUNA ‘FREELUNCH’ IKULU YA MAREKANI* *Maisha ya Rais wa Taifa Tajiri Zaidi Duniani Hayana Mtelezo Unavyodhani* Ilikuwa ni mwaka 2009, Michelle Obama akiwa bado mgeni kabisa ndani ya White House. Wiki chache tu baada ya kuhamia, alipokea kile alichodhani ni bahasha ya taarifa kutoka kwa wahudumu wa jumba hilo. Lakini alipofungua, akakutana na bill iliyoshiba, ndefu, tena iliyochambua hadi vipande vya peanut butter vilivyotumika kwenye mkate wa binti yake Sasha. Bila maelezo mengi, alichopewa ilikuwa ni orodha ya gharama za chakula na matumizi mengine walizotumia kama familia, akiwa na wajibu wa kulipa kutoka kwenye mshahara wa mumewe, na bill hii ilikuwa ni ya kwanz kati ya nyingi ambazo angeendelea kupata kila mwezi.. Michelle alishtuka, hakujua kabisa kwamba hata ukiwa mke wa Rais wa Marekani, nchi tajiri zaidi duniani hakuna mtelezo. Kwa haraka unaweza kuimagine jinsi alivyoenda kuwaambia wanae kuishi kwa bajeti. Rais wa Marekani analipwa kama *dola 400,000 (sawa na pesa za kitanzania billioni 1)* kwa mwaka kiasi ambacho kwa hapa nchini kwetu kinaonekana kuwa kikubwa sana. Lakini ukishajua namna ambavyo analazimika kutumia fedha hiyo, utaanza kuelewa kwamba kuwa rais siyo tiketi ya kuishi kama mfalme, hasa hasa nchi za wenzetu. Kwa maadili ya kisiasa na uongozi ya Marekani, serikali inagharamia yale tu yanayohusiana na majukumu rasmi ya rais kwa taifa (official government business). Mengine yote hasa ya familia na matumizi binafsi yanaachwa kwa rais mwenyewe, si analipwa mshahara bwana. Chakula mkuu jilipie, hii sio kazi ya kodi za wananchi, ingawa ndani ya White House, kuna wapishi wa kimataifa (ambao mshahara wao huwa inalipa serikali), meza za kifalme, na huduma ya hali ya juu ambayo ni classic kweli kweli, lakini ukila lasagna au fleur burger ujiandae kulipa bill. Rais analipia kila kitu kinachohusu mlo wa familia yake. Kuanzia kifungua kinywa cha mtoto wake hadi dessert ya usiku, anawajibika. Bila kujali hadhi, serikali ya Marekani haitumii senti ya kodi ya raia kwa mambo binafsi ya mtu anayeshikilia ofisi ya juu zaidi. Kwa watanzania wengi waliokulia kwenye dhana ya “mheshimiwa akifika, kila kitu ni bure,” hili ni jambo linalotia mshangao. Lakini huko, ndiyo msingi wa utawala madaraka si leseni ya kutumia pesa ya wananchi hovyo. Unaweza kuwa interested kutaka kujua kuhusu ishu za ada za watoto maana ni jambo ambalo kawaida huwapa wazazi kijipresha cha hapa na pale. Labda nikuambie tu kama Rais wa Marekani akiamua mwanae asome shule ya kifahari kama *Sidwell Friends School* moja ya shule bora zaidi Marekani au labda IST ( yenye hadhi hizo hapa bongo), ambapo ada inavuka *dola 50,000* kwa mwaka, mzazi wake ambaye ni Rais hulipa kama mzazi mwingine yeyote. Hakuna habari ya serikali italipa.. Hakuna posho za elimu wala “voucher” kutoka Ikulu. Hii ni sehemu ya kudumisha kanuni kwamba cheo cha baba yako hakiwezi kuwa mzigo kwa umma. Na hii si hadithi ya rais mmoja tu; kuanzia *Clinton, Obama hadi Biden*, jambo hili limekuwa ni kanuni isikiukwa. Vipi mambo yake binafsi inakuwaje analipiwa au? Nchini Marekani Rais na familia yake hujiendesha kama raia mwingine wa kawaida. Matumizi kwenye vitu kama: 1. Nguo anazovaa au gharama za dry cleaning analipia mwenyewe. 2. Huduma za saluni, kukatwa nywele, au kufanyiwa makeup pia ni gharama zake. 3. Safari binafsi (kama vacation au matembezi ya kifamilia) familia yake hulipa sehemu inayolingana na gharama za usafiri kwenye ndege za commercial (first class equivalent), hata kama wamesafiri kwa Air Force One (ambayo kwa sababu za usalama ni lazima atumie). Ingawa wengi hudhani kuishi White House ni kama kushinda bahati nasibu ya maisha, ukweli ni kwamba baadhi ya marais wameondoka Ikulu wakiwa wameelemewa na madeni si kwa sababu ya ufujaji, bali kwa sababu ya mfumo unaowatwika mzigo wa gharama binafsi huku wakiumizwa na mtazamo wa hadhi yao. Kwa mfano, familia ya Ronald Reagan iliondoka White House mwaka 1989 ikiwa kwenye hali ngumu kifedha, baada ya kutumia mamilioni katika mapambo ya nyumba, hafla zisizo rasmi, na maisha ya heshima yaliyowalazimu kuchukua mikopo na kufanya mikataba ya hotuba mara tu walipotoka madarakani ili kujiokoa kifedha. Kiasi kwamba, licha ya Reagan kuwa Rais wa taifa lenye nguvu zaidi duniani, alihitaji kufanya matangazo ya umma na kuuza haki za hotuba zake ili kufidia gharama za kuishi Ikulu. Upande mwingine familia ya Bill Clinton, baada ya drama nzito ya Monica Lewinsky, waliondoka madarakani wakiwa na deni la zaidi ya dola milioni 16! Yap, kesi za kisheria, fidia kwa akina Paula Jones, na mawakili waliomsaidia kupambana na impeachment vilimkosesha usingizi. Maana yake ni kwamba matatizo yako binafsi utasolve wewe na familia yako. Kwa kifupi, jamaa alitoka White House akiwa na suti nadhifu lakini wallet imechakaa.. Hata wakati wa kampeni za mwaka 2020 Trump alipotumia ndege ile ya serikali kwa sababu alikuwa bado Rais alilipia karibu *dola milioni 4.7* kama gharama za safari hizo. Uzuri huyu jamaa ni milionea hivyo haikuwa tabu sana! Kuonyesha kuwa wenzetu wanaheshimu hela ya mlipa kodi ikitokea mmoja wa wanafamilia amepiga simu binafsi kwa kutumia line ya serikali, bili hutolewa, na kulipwa. Unashangaa eeh, ndio maanake simu zako binafsi tumia smartphone. *Kwa Nini Wenzetu Wanazingatia Haya?* Kwa Wamarekani, hoja kuu ni uwajibikaji wa matumizi ya fedha ya umma. Wanatambua kwamba kodi zinazokusanywa kutoka kwa madereva wa malori, wauguzi, walimu, wakulima na watu wengine wa hali za kawaida kabisa si kwa ajili ya maisha binafsi ya kiongozi even if ni Rais. Hii ndiyo sababu Marekani imejenga mfumo wa kiutawala unaotenganisha mamlaka na starehe. Ni dhana muhimu kwamba madaraka ya juu yanapaswa kuwa mfano wa nidhamu, si kivuli cha anasa. Hii ni tofauti kabisa na kwetu Afrika ambapo kiongozi ni kama mwana wa mfalme kama sio mfalme kabisa.. Katika mataifa mengi ya Afrika, picha ni tofauti sana. Mara nyingi, tunashuhudia viongozi wakitumia magari ya kifahari kwa shughuli binafsi, wakisafiri na misafara ya magari zaidi ya 15 kwa hafla isiyo ya kitaifa, au hata familia zao kusomea nje ya nchi kwa kodi za wananchi bila aibu. Kiongozi anapofiwa, serikali inalipa. Mtoto wake anapofunga ndoa, kampuni za umma zinatoa michango ya kifahari. Kuna wengine hata mtoto wa kiongozi anapojifungua, msafara unapelekwa kutoa hongera. Huko Marekani na nchi nyingi za Ulaya hakuna hizo habari. Kifo cha ndugu wa rais? Serikali inaweza kutoa rambirambi ya kidiplomasia, lakini gharama ni zake binafsi. Ndoa ya mtoto wa Rais huwa ni jambo la kifamilia na halihusishi kodi ya mlipa ushuru. Moja ya kitu cha kujifunza hapa ni kwamba uongozi ni heshima ya kutumikia, si fursa ya kula. Kwa viongozi wetu barani Afrika, watendaji wa serikali, kwa mashirika ya umma hili si somo la kuangalia kwa kejeli, bali la kuiga. Mataifa yanayoendelea hayawezi kujinasua kiuchumi kama viongozi wake wataendelea kuishi kama wafalme, huku raia wakihangaika na bei za unga na mafuta ya kula. So kila unapomuona POTUS akiwa White House, usidanganyike na uzuri wa mjumba ule. Ndiyo jumba ni zuri na lina historia ya aina yake na lina ulinzi wa hali ya juu lakini ukivuka mlangoni, na kuingia maisha ya ndani, utagundua kwamba hata rais wa taifa lenye nguvu zaidi duniani lazima awe na bajeti.. Hakuna mlo wa bure, wala suti za bure au sijui vacation ya bure. Kwa wenzetu Ikulu siyo kasri la kifalme bali ni ofisi ya taifa. Na pengine, kwa kujifunza kutoka kwao, sisi pia tunaweza kujenga nchi ambayo viongozi wake hawakai juu ya kodi, bali upande wa wananchi. Kwa mfumo huu wa Marekani, hata ukiwa Rais, ukisahau wallet unaweza kukosa lunch Ikulu… tofauti na huku ambapo ukivaa tai tu, unaweza kula mpaka posho ya chai ya watumishi wengine. 😌 *Mjombaako* *©️BantuKwanza*


*HATIMA YA KIMUNGU* *Hadithi ya Unabii na Kifo Cha Mfalme Ahabu* _”Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.“_ Moja ya sehemu muhimu sana katika ‘Sala Ya Bwana’.. Hatima ya mwanadamu inategemea sana mapenzi ya Mungu ‘God’s Will’, na ingawa mara nyingi sisi wanadamu huangalia ulimwengu na yaliyomo katika macho yetu ya kianadamu, nachelea kusema kuwa kuna mengi nyuma ya hatima zetu.. Leo kuna stori moja huwa naipenda sana inamhusu moja wa wafalme wakorofi na watukutu kuwahi kutokea katika falme ya Israel.. Hapo zamani za kale, katika ufalme wa Israeli, kulikuwa na mfalme aitwaye *Ahabu mtoto wa Omri*. Ahabu alikuwa ni mfalme mtukutu ambaye alipenda kufanya mambo mengi kwa njia zake mwenyewe. Aliitawala nchi kwa mkono wa chuma na huku akiwapa heka heka za hapa na pale manabii wa Mungu akiwemo Eliya. Siku moja, *Ahabu akiwa na mkwe wake Jehoshaphat aliyekuwa mfalme wa Juda* katika porojo zao kifalme akamwambia mkwewe “ Poti nataka nikampige *Ben Hadadi niichukue Ramoth-Gileadi unasemaje?.* “Mimi sina tatizo mkwe, si unajua tena watu wangu watu wako na farasi wangu farasi wako. Imeisha hiyo poti.” akajibu Jehoshafati Lakini sababu mfalme huyu wa Juda alikuwa ni mtu mwenye tahadhari sana, akaona itakuwa wazo zuri kuuliza manabii kwanza, wawape ubashiri kabla ya kwenda vitani. Kwa ufahamu tu, tabia ya kuomba ubashiri wa kiroho/kupiga ramli kutoka kwa manabii, mizimu, wasoma nyota, au wabashiri kabla ya kwenda vitani imekuwa ikitumika kwa muda mrefu na kuna mifano mingi kuhusu tamaduni hiyo kuanzia enzi za kale hadi miaka ya karibuni. Hivyo Jehoshafati akamwambia Ahabu _“lakini nilikuwa nawaza hapa tungepata unabii kuhusu jambo letu kabla tujaenda ingekuwa vyema zaidi”_ Ahabu akaafiki. Ndipo Ahabu aliwaita manabii wake karibu 400 ambao walipenda kumsifu kuliko kusema ukweli, sijajua aina hiyo ya watu enzi hizo waliitwaje ila kizazi chetu wanaitwa machawa. Akawauliza _“je niende kushambulia Ramoth-Gileadi au lah?”_ Manabii wale waliopenda kumjaza mfalme ujinga aliotaka kusikia bila kuwaza mara mbili, walipiga kelele kwa pamoja, _“Nenda vitani, Ee Mfalme! Ushindi utakuwa wako!”_ Yehoshafati, mfalme wa Yuda kutokana ule umakini wake hakuwa ameridhishwa kabisa. _“Poti, hakuna nabii wa Bwana ambaye tunaweza kumwuliza, hawa jamaa sijawaamini sana?”_ aliuliza, akiwa na shaka kidogo. Ahabu aliminya macho kidogo na kutoa pumzi ndefu kisha akajibu _“Yupo Mikaia mwana wa Imla, lakini namchukia huyu jamaa. Yaani siku zote hanitolei unabii mwema, ila ubaya ubwela tu.”_ Licha ya kusitasita kwake, Ahabu aliamua kumwita Mikaia. Yule Mjumbe aliyemchukua Mikaia wakiwa njiani alijaribu kumwelekeza aseme nini, lakini Mikaia, akiwa nabii makini, aliahidi kusema tu kile Bwana atakachomwambia. Mikaia alipowasili, mfalme akampokea kwa kijembe _“ umekuja eeh mwana wa Imla usiyependa mazuri juu yangu”_ Mikaya akajibu kwa utani _“ hapana mkuu mi nipo kwa ajili yako, nini shida?”_ Ndipo mfalme akauliza _“Mikaya nilikuwa na mpango wa kwenda kuvamia Ramoth-Gilead kurudisha ardhi ambayo Ben Hadadi mkubwa alichukua huko nyuma, vipi tuende vitani au tutulie?”_ Awali nabii huyu kutokana na upepo aliokuwa kauona hapo alimpa Ahabu ujumbe wa matumaini kama manabii wengine, lakini alisema kwa kuipamba na kuzidisha mno kitu ambacho hata Ahabu akahisi ni kejeli. Alimwambia _“enenda ukashinde,”_ Mikaia alisema kwa tabasamu pana, _“kwa maana Bwana ataitia mikononi Ramoth-Gileadi mikononi mwako mfalme.”_ Ahabu akakunja uso akimfokea kwa ghadhabu _“Hivi we Mikaya ni mara ngapi nimekufanya uape ili uniambie ukweli kwa jina la Bwana?”_ Tabasamu la Mikaia likafifia, basi akaamua kutoa unabii wa kweli. Akasema _“niliona Israeli wote wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Bwana akasema, ‘Watu hawa hawana Kiongozi. Kila mmoja na aende nyumbani kwa amani.’”_ Ahabu akamgeukia Yehoshafati huku akisikitika na ghadhabu _“sikukuambia! huyu jamaa hajawahi kunitolea unabii mwema hata siku moja?”_ Hayo ndio yaliyokuwa yakiendelea pale Israel katika hekalu la mfalme. Lakini shughuli nzima ilifanyika katika viunga vya mbinguni. Muda huo Mungu alikuwa akifanya baraza mahsusi na jeshi lake la mbinguni. Lusifa, akiwa katika ‘mood’ yake ya utani, aliingia katika mkutano huo kwa mikogo huku akijiimbisha nyimbo zake za hapa na pale. Mwenye Enzi akajiegemeza kwenye kiti chake cha enzi na kuhutubia mkutano akasema _“Ahabu ameshakuwa pasua kichwa mno. Nilimsamehe wakati ule wa Naboth kuhusu kuangamiza nyumba yake yote ila naona ni muda muafaka apumzishwe”._ _“Mpango wangu ni akafie katika uwanja wa vita, nani ataweza kumrubuni Ahabu ili akapigane Ramoth-Gileadi na afie huko?”_ alimalizia Mungu Mwenye enzi kwa sauti ya kutetemesha iriyorindima ukumbi mzima. Malaika wa majeshi mbalimbali wakatoa maoni yao ya hapa na pale, lakini hakuna aliyekuja na plan nzuri iliyonyooka. Ndipo Lusifa, mjanja wa mjini akaona asipitwe na nafasi hii adhimu kabisa, akasogea kwa mbele akiwa na tabasamu lake la hila. _“Mwenye enzi mimi nina mbinu moja uhakika mno, jamaa hawezi toboa”_ alisema kwa kujiamini sana …_”ni rahisi sana nitakwenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote, sababu ninamjua Ahabu ana aleji kali na ukweli”_ alijibu, huku akifurahia ishu nzima ilivyokuwa inaenda . _“Si unakumbuka hata wakati wa Eliya, huyu jamaa huwa anapenda kuambiwa vitu anavyopenda kusikia tu, hivyo hapo hapo ndio mimi nitakapomwangusha”_ Mungu akainuka na kusema. _“Vizuri sana, natumai utafanikiwa kumdanganya. Nenda ukafanye hivyo.”_ _“Imeisha hiyo, Mwenye Enzi”_ alisema huku akinesa na kutembea kwa madaha, Lusifa alitoweka kwenda kufanya kazi yake, na kuliacha baraza la mbinguni likiongea kwa kicheko kuhusu jinsi Ahabu anavyoenda kudanganywa na tamaa yake ya kusikia habari nzuri pekee. Lakini sababu haki ya kiungu huwa imenyooka na inatenda haki pasipo kupinda.. Kutokana na hili basi Mungu akasema sababu mimi ni mwenye haki na siku zote haki yangu ni nyoofu lazima nimpe Ahabu nafasi. Basi ili hilo kutimia, roho wa Mungu akashuka kwa Mikaya na kuhakikisha kuwa ingawa kulikuwa na manabii 400 ambao waliingiwa na roho wa uongo, bado kulikuwa na nafasi ya kuokolewa iwapo Ahabu ataamua kusikia sauti ya Mungu ndani ya nabii mmoja. Haya turudi duniani.. Sasa baada ya Mikaya kuwaambia kwa kina unabii huo, baadhi ya manabii wakawa wakali na hadi kuanza kumshambulia. Basi akiwa amechukizwa na unabii huo wa Mikaya, Ahabu akawaambia walinzi wake _“hebu mfungeni huyu jamaa na unabii wake wa ajabu ajabu hadi nitakaporudi. Hakikisheni mnamnyoosha, chakula na maji apewe kidogo akili imkae sawa.”_ Mikaya akisikiliza maelekezo hayo akadakia _“ukirudi mzima labda sio Bwana aliyeongea na mimi. Nimekaa palee, hutoboi wewe”_ Akiongozwa na ukaidi wake Ahabu, akaamua kuusikiliza unabii wa roho ya uongo, akapanga kwenda vitani. Huku akijaribu kuipiga chenga hatima kwa kujificha, na kubadilisha mavazi yake asionekane mfalme na kumwambia Jehoshaphat pekee avae kifalme bado haikutosha. Katikati ya mapambano makali mshale uliopigwa bahati mbaya ukampata, kuthibitisha kuwa huwezi kuikwepa hatima, hasa ikiwa imeamriwa na Mungu. Mshale huo ukampa jeraha kubwa Ahabu hivyo akamwamrisha dereva wa chariot yake kugeuza na kutoka kwenye uwanja wa mapambano ili akajiuguze lakini jioni ile ile kutokana na jeraha lile hali yake ikawa mbaya hatimaye umauti ukamkuta. Nilikuwa najaribu kuwaza muda ule Ahabu alipolala kuelekea kufa katika chariot yake, huenda alijiuliza jinsi mambo yote yalivyokwenda kombo na jinsi ukaidi wake ulivyomponza wakati Mikaia labda alicheka peke yake huko alipofungwa, akijua kuwa alikuwa amesema ukweli usio na doa. Huku nae Mungu akiwa anasema shughuli imeisha na Lusifa akitikisa mguu na kujipiga kifua kuhusu umahiri wake. Hivyo, hadithi ya Ahabu inamalizika kwa mtindo huo huku tukiona kuwa unabii wa Mungu huwa haukimbiwi. MAFUNZO Hadithi nyingi huwa na mafunzo, mengine ni ya wakati inatokea na nyingine ni kwa ajili ya kizazi cha mbele.. Tuseme tu waisraeli walikuwa vichwa ngumu hivyo mafunzo ya wakati wao sidhani kama walizingatia sana, lakini sisi wa kizazi hichi tuna la kujifunza.. 1. Hatima ya Kiungu haikimbiwi, ni wazi kuwa lile neno la mapenzi ya Mungu yatimizwe ni zito na lenye maana kubwa sana.Maisha ya mwanadamu yanahitaji sana hii God’s will. Hatima ya mwanadamu iko ndani ya mikono ya Mungu lakini amempa mwanadamu uwezo wa kusikiliza sauti ya ndani yenye kweli.. Ingawa mara nyingi inaonesha wengi huwa hawasikilizi sauti hii na kuipuuza. 2. Haki ya Kiungu ni ya ajabu ni iko fair mno, unaweza ona kuwa pamoja na kwamba roho wa uongo aliingia kati ya manabii 400 , bado mwenyezi Mungu aliruhusu mtu mmoja kuwa na ukweli ili kama Ahabu angefungua sikio lake la kiroho basi angesikia. Hii inaweza pigilia msumari kuwa huwezi pewa jaribu pasipo mlango wa kutokea. 3. Kumbe uchawa upo muda mrefu, na kuna viongozi wana asili ya kupenda kuambiwa vitu wanavyotaka kusikia tu hata kama vina madhara. Hii imesababisha watu wote wasio na ujasiri wa kusema ukweli kukaa kimya na kuitikia kile ambacho kiongozi anataka. Na kibaya zaidi ni kwamba wale wachache wenye ujasiri wa kuwaambia viongozi ukweli jinsi ulivyo wamekutana na madhila makubwa kuanzia kutengwa,kuteswa hadi kuuwawa. Hivyo ni vyema viongozi wetu kujenga tamaduni ya kuwapa nafasi akina Mikaya ili wawaambie ukweli hata kama unauma vipi maana inawezekana ukweli ndio ukombozi wao na inaweza kuwaepusha maanguko makubwa.. Nini kingine umejifunza!? Cogito, ergo sum *Mjombaako* *©️BantuKwanza*


Si Mbaya kujua? Jiji la Copenhagen nchini Denmark lina baiskeli nyingi kuliko magari, ikiwa na zaidi ya kilomita 400 za njia za baiskeli na madaraja ya kisasa kama Bicycle Snake. Zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wake husafiri kwa baiskeli kila siku, na kuifanya kuwa moja ya miji ya kijani kibichi zaidi duniani.


*SI MBAYA KUJUA* *Mfalme Aliyeomba Msamaha kwa Kuendesha Gari kwa Mwendo Mkali* Unaweza kudhani ni utani,lakini ilitokea.. Mwaka 2000, Mfalme Carl XVI Gustaf wa Uswidi alikamatwa akiendesha gari kwa mwendo mkali nchini Denmark. Alikiri kosa lake na hakukimbia, hakukanusha, hakutumia cheo chake kufanya ubabe. Badala yake, akaomba msamaha wa hadhara kwa wananchi. Alisema: _“Samahani, tulikuwa tuna haraka kwenda kuwapokea watoto uwanja wa ndege.”_ Mfalme huyo akaomba msamaha, kwa kosa la barabarani. Na si kwa shinikizo bali kwa utu na heshima. Sasa geuza kamera upande wa Afrika…Wangapi wa viongozi wetu wangeweza hata kufikiria kusema “pole” sembuse kuomba msamaha kwa kosa dogo tu kama hilo? 🤣🤣


*THE CREDIT CARD STORY* *Historia ya Kadi ya Mkopo Iliyotokana na Aibu Mezani* Inawezekana huku kwetu Bongo, kadi ya mkopo isiwe maarufu sana hasa kwa sisi watu wa chini. Lakini huko kwa wenzetu, hii kitu ni life saver ni mkombozi wa aibu ndogo ndogo, pressure za ghafla, na kuepusha mambo ya kudekishwa au kuosha vyombo yasikukute kabisa. _Hebu imagine…_ Uko kwenye ki-date pale Samaki Samaki mambo ni bam bam, pembeni mtoto wa 2000s amejaa tabasamu mwanana kama filter za TikTok, vibes zipo kama zote, mnaagiza chakula na vinywaji mpaka waiter anapata *‘leg fatigue’.* Mara ule muda unawadia, bili inaletwa… unajinyayua kidogo ili utoe wallet yako mfuko wa nyuma ghafla moyo unashtuka. _Shit!!_ unakutana na risiti ya parking tu ila wallet umeisahau home. _Kijasho!_ Unamwangalia mtoto wa 2000s ambaye amekaa akisubiri uonyeshe uanaume wako na waiter anakutazama kama vile unamcheleweshea promotion yake ya mwezi. Ni muda huo unahisi kama mkanda umebana sana na kuna dalili zote za kupata tumbo la kuharisha, mdomo unakauka, na kicheko kinakata ghafla, huku ulimi unakuwa mgumu kutoa maelezo kama ATM yenye network error. Sasa, ngoja nikwambie… Hali kama hiyo iliwahi kumtokea jamaa mmoja *mwaka 1949 kule New York.* Jina lake alikuwa anaitwa *Frank McNamara.* Siku hiyo akiwa kwenye dinner ya heshima na clients wake pamoja na mkewe katika moja ya mgahawa maarufu jijini humo, muda wa kulipa bill ulipowadia akagundua kasahau wallet nyumbani. Hapo ukumbuke nyakati hizo hakukuwa na simu ya kutolea hela. Hakuna M-Pesa, swipe machine wala benki za mtandaoni. Frank ikabidi kumstua mke wake chap aokoe jahazi. Bahati yake ni kuwa mke akalipa bill ile. Tukio hilo haikuwa aibu tu but ilikuwa bonge la _“lightbulb moment.”_ Hivyo badala ya kuishia kujiumauma tu, Frank akamwita meneja na kufanya kitu ambacho kingesaidia watu wengine kutokumbwa na aibu kama ile na kubadilisha ulimwengu wa malipo kwa ujumla. Akamwambia; _“Hii si mara ya kwanza kusahau wallet, na nadhani si mimi peke yangu imenikuta. Kuna watu wengi lazima imeshawatokea. Kwa nini tusitengeneze kitu ambacho kinaweza kuwa mbadala wa kubeba pesa kila wakati?”_ Ni siku hiyo ndipo lilipozaliwa wazo la kadi ya mkopo (credit card) ya kwanza kabisa duniani. Kitu ambacho leo hii kinafanya watu wasiwe na stress hata kama hawana cash mkononi. Swipe tu malipo yafuate mwisho wa mwezi. Mwaka mmoja baadaye, 1950, Frank McNamara kwa kushirikiana na rafiki yake *Ralph Schneider,* wakazindua kitu kipya duniani walikiita *“Diners Club Card.”* Hii ndiyo ilikuja kuwa kadi ya kwanza ya mkopo (credit card) duniani inayokubalika kwenye maeneo mengi ya biashara. Ilianza kama mpango wa wanachama wachache waliokuwa wakienda kula kwenye migahawa ya jijini New York badala ya kulipa papo hapo, walipata bili baadaye mostly mwisho wa mwezi . Credit, kwa mara ya kwanza, ikawa ya watu wa kawaida not just mabilionea. Unaweza tamani kujua ilifanyaje kazi? *Rahisi sana:* * Unatumia kadi yako kula au kufanya manunuzi * Mwishoni mwa mwezi, unapokea bili ya jumla * Unalipa kwa mkupuo au kidogo kidogo Kwa mwanzo ilikuwa kwa ajili ya chakula tu migahawani. Lakini watu wakaona faida yake ni kubwa sana. Hivyo, benki na kampuni nyingine zikaanza kuiga mfumo huo na hapo ndipo makampuni kama *American Express (1958)* na baadaye *Visa & Mastercard* zilipoingia sokoni. Labda nikufahamishe tu, hii kadi aliyobuni Frank ile ya kuokoa aibu migahawani ndiyo chimbuko la kadi zote za kisasa tunazotumia leo, iwe ni za kutoa hela ATM, kuswipe kwenye supermarket, au hata za kufanyia manunuzi kwenye apps. Kadi ile ya kwanza ya Diners Club haikutolewa na benki, ilikuwa ni kama kadi ya uanachama wa mgahawa (membership card) una kula leo, unalipa mwisho wa mwezi. Hata usipokuwa na pesa mkononi, huduma utapata. Lakini ubunifu ule ulivuta macho ya mabenki duniani. Miaka michache baadaye, benki kubwa kama Bank of America zikaanza kutoa kadi zao za mkopo (credit cards) rasmi, na hapo Visa na MasterCard zikazaliwa. Na kadri teknolojia ilivyokua, tukaziona: * ATM cards za kutolea hela benki bila foleni za ndani * Bank Debit cards kutumia hela yako moja kwa moja dukani au mtandaoni * Bank Credit cards kutumia hela ya benki, halafu unalipa baadaye * Halafu sasa tuko kwenye era ya tap-to-pay, Apple Pay, na mobile wallets Kwa hiyo ile kadi ya mkopo ya Frank, ndiyo babu wa kila swipe tunayofanya leo. Kitu kilichozaliwa kwenye aibu ya kusahau wallet, leo ndio backbone ya mfumo wa kimataifa wa malipo unaobeba mabilioni ya miamala kila siku. Takwimu zinaonyesha kuwa hadi sasa kuna zaidi ya *kadi bilioni 2.8 zinazotumika duniani.* Kila sekunde, maelfu ya watu wanalipia vitu kwa swipe, tap, au online kwa sababu ya mtu mmoja aliyesahau wallet mwaka 1949. Mfumo wa kifedha umebadilika kabisa na umeweka msingi wa huduma za kifedha za kisasa kama buy now, pay later, credit scores, na hata Fintech apps. Story hii ni mfano mzuri kwamba wazo kubwa linaweza kuzaliwa kutoka sehemu usiyoweza idhania kabisa. Frank McNamara hakuwa genius wa teknolojia wala hakuwa mjasiriamali maarufu. Alikuwa tu mtu wa kawaida aliyesahau wallet na kuamua: “Sitataka hii hali ijirudie.” Huu ni ushuhuda tosha kuwa akili ya mwanaume si huwa tu haikubali kuaibika pia hutafuta njia ya kulinda heshima, na kunufaisha jamii nzima. Cheers kwa walipa bill za migahawani wote duniani.. *Mjombaako* *©️BantuKwanza*


_“If no one is dying because you took your time to do it right, then don’t betray your process most urgency is just noise pretending to be necessity.”_ *— Mjombaako’s Razor*

*SI MBAYA KUJUA* *Nanasi Pambo La Kitajiri* Wakati leo hii ukifika msimu wake tunanunua hadi kwa shillingi mia tano, na kama ukienda Stereo pale Temeke unaweza shangazwa na urahisi wa bei za tunda hili, mambo hayakuwa hivi miaka kama 300 tu iliyopita barani ulaya. Katika *miaka ya 1700*, mananasi yanayojulikana kwa jina lake la kitaalamu *Ananas comosus* hayakuwa tu matunda yaliyopatikana kirahisi kama sasa, yalikuwa ni kilele cha anasa na upekee barani Ulaya. Uadimu wake na asili yake ya kigeni yaliyafanya kuwa na thamani kubwa sana miongoni mwa matajiri. Tofauti na leo, ambapo mananasi yanapatikana kwa urahisi kwenye supermarkets na masoko mengine, safari ya nanasi moja kutoka shambani hadi Ulaya ilikuwa ni ndefu na yenye gharama kubwa. Mananasi kwa asili yalitoka Amerika Kusini na Carribean na yalilimwa kwa mara ya kwanza na jamii wazawa kama Tupi-Guarani waliokuwa wakikaa kusini mwa Brazili na Paraguay wenyeji hawa waliliita tunda hilo kwa jina la *“nana,” likimaanisha “tunda bora.”* Mananasi yalikutana na wapelelezi (explorers ultimately have wasoma kwenye historia) wa kutoka Ulaya mwishoni mwa karne ya 15. Ni nyakati hizi hitaji kubwa ya mananasi ilianza baada ya exploration ya wazungu barani Amerika. Tunda hili kwa mara ya kwanza liliripotiwa katika visiwa vya Carribean na kisha baadae Amerika Kusini, na ukisoma barua pamoja na shajara zao zilizoelezea tunda hilo zilijaa sifa za kupindukia kama za kijana aliyepagawa na mapenzi. Chukua, kwa mfano, maelezo yaliyoandikwa na Gonzalo Fernández de Oviedo y Valdés mwaka 1535. Aliandika kwamba nanasi lilikuwa halijawahi kushuhudiwa kwa “uzuri wa mwonekano, harufu mwanana, ladha isiyosemeka,” na kwamba, “kati ya hisia tano za mwili, zile tatu zinazoweza kutumika kwa matunda na hata ya nne, ile ya kugusa, linazidi matunda yote Upo!? Jitihada za mwanzo za kubeba mbegu na kupanda ziligonga mwamba na hivyo njia pekee ya kulipata tunda hilo ilikuwa ni kulisafirisha. Hata hivyo kusafirisha tunda hilo kuvuka bahari ya Atlantiki bila kuharibika ilikuwa mchakato mahsusi na wenye wa gharama kubwa. Ili kuhifadhi ubichi wake, mananasi yalikuwa yakisafirishwa katika ‘conditions’ zilizotengenezwa kwa uangalifu mkubwa, na mara nyingi maandalizi hayo yalisababisha tunda hilo kugharimu kiasi kikubwa cha pesa—wakati mwingine sawa na maelfu ya dola za leo. Inasemwa nanasi enzi hizo lilifika hadi dola 8000 (takribani Tsh 20m) kwa pesa ya leo. Kwa sababu hizo, mananasi yakawa zaidi ya chakula; yalikuwa alama ya hadhi. Familia tajiri zilionyesha mananasi kwenye karamu za kifahari au hata kukodisha mananasi kuonyesha kwenye sherehe. Ndiyo, umesoma sawa—kukodisha nanasi ilikuwa ilikuwa ni big deal nyakati hizo! Wamiliki walihakikisha tunda hilo halijaguswa ili liweze kurudishwa na kutumika tena kwa maonyesho ya baadaye. Mananasi pia yaliathiri usanifu na sanaa. Muonekano wake wa kipekee uliashiria ukarimu na utajiri, na kuathiri miundo kama vile “Pineapple Finial” maarufu juu ya Kanisa Kuu la St. Paul huko London na sanamu mbalimbali za mananasi. Upekee wa nanasi ulipungua katika karne ya 19 kutokana na maendeleo ya mifumo ya usafirishaji,ugunduzi wa friji na mbinu za kilimo, na kufanya tunda hilo liweze kupatikana kwa urahisi zaidi. Leo hii matumizi ya nanasi kama alama ya anasa na ufahari inabaki kuwa kipande cha kuvutia cha historia!Na kama hukujua basi leo nimekusanua. So wakati unapanga kwenye New Year hii kupata Pinacolada, hebu waza kwanza miaka 300 iliyopita ingakuwaje. *Mjombaako* *©️BantuKwanza*


*ELIMU ILIYOTUKIMBIZA NYUMBANI* _Kizazi Kilichodharau Shamba, Kikakimbilia Ajira Isiyolipa Kodi_ _“Wanangu, someni muajiriwe… msije mkaishia kuwa kama mimi na baba yenu… Kulima ni kugumu mno, si unaona leo? Tokea asubuhi tuko shambani hadi sasa hivi ndo tunarudi.”_ Maneno haya yaliingia na kuandikwa kwenye mioyo ya watoto wake *Amani, Roja, na Milembe* kama alama ya udhalili isiyoonekana. *Bi Nuru, mama yao,* aliwaambia akiwa amejifunga khanga kiunoni, miguu na mikono vikiwa vimejaa mavumbi ya Mkalaini, kijiji kidogo kilichojificha chini ya jua la Kwimba, mkoani Mwanza. Siku hiyo walikuwa wanarudi kutoka shambani, majani ya viazi (malando) yakiwa bado yananing’inia kwenye matoroli ya miti waliyokuwa nayo. Wakati huo huo, mamia ya kilomita kusini, huko *Njombe, kijiji cha Ukalawa, Bi Ndelwa* naye alikuwa anabeba mapipa ya pombe ya kienyeji na kuwapakia watoto wake: *Luhuvilo, Penensia, Daudi, na Faraja.* Waliibeba hadi kilabu cha pombe cha karibu ambako ndio walipopatikana wateja waliokuwa wanafurahia na kushikilia glasi zilizojaa pombe hizo. Bi Ndelwa alinyanyua uso, akawatazama wanawe kwa simanzi na kuwaambia: _“Wanangu chonde chonde msome kwa bidii mkaajiriwe., msije mkaishia kuwa kama mimi. Hii kazi ya kuuza pombe imeniletea fedheha nyingi, msije ishi haya maisha.”_ Familia mbili tofauti, kazi mbili tofauti, kulima na kutengeneza pombe za kienyeji. Lakini sauti zao zilifanana, ujumbe wao ulikuwa mmoja: elimu ndio njia pekee ya kutoroka fedheha ya maisha waliyoyapitia. Na kweli, kwa juhudi na jasho la hizo kazi walizoziona kama adhabu, waliwasomesha watoto wao. Amani alisomea Kilimo na Mifugo, Roja na Milembe walichukua masomo ya Masoko. Kwa upande wa Bi Ndelwa: Luhuvilo na Penensia walihitimu digrii ya sheria. Daudi akajikita kwenye Chemical Processing, Faraja akamaliza Business Administration na Masoko. Wazazi wakafurahi, watoto ni wasomi na wanajua kuongea kiingereza na hadi walitambiana na wazazi wengine kule kijijini. Vijana wakatunukiwa vyeti, wakavaa nadhifu, wakabeba CV zao na kuanza matembezi kupita maofisini kutoka Wizara moja hadi kampuni binafsi nyingine. Wengine walifanikiwa, Amani alipata ajira Kigoma kama Bwana Shamba, Daudi akaajiriwa Tanzania Breweries, akihusika na kutengeneza pombe kiwandani pale. Faraja akaingia Vodacom; kama afisa masoko akitangaza na kusambaza vifurushi. Huku Roja, Milembe, Penensia na Luhuvilo wakitembea na bahasha bila mafanikio hadi miguu ikaanza kuota sugu. Miaka ikazidi kukatika, huzuni na simanzi zikatawala kwa vijana wale na wakati mwingine walishindwa kuwaambia wazazi wao uhalisia kwa kuogopa kuwavunja moyo. Maana hebu fikiria matarajio ni kuwa ukisoma kuna kazi, ila leo hii msomi anamwambiaje mama yake wa kijijini kuwa kakosa hela ya kula? Wapi tulipokosea ? Kwa macho ya kawaida, tunaweza kusema: “Elimu ni njia ya kutoka kwenye umasikini.” Lakini hebu tujiulize… je, elimu yetu ilitufundisha namna ya KUONA thamani ya tulikotoka? Au ilitutenganisha kabisa na mzizi wa mafanikio yetu halisi? Wazazi hawa wawili, Bi Nuru na Bi Ndelwa walikuwa na _‘micro-enterprises’_ za maana tu. Kilimo na utengenezaji wa pombe vilisomesha watoto hadi chuo kikuu! Hii ni proof of concept kwamba walichokuwa nacho kilikuwa sustainable, shida haikuwa kwenye aina ya shughuli, bali tatizo lilikuwa ni *scale na structure.* Shida ilianzia pale walipoanza kuichukia kazi yao mbele ya watoto wao. Kilio cha _“msije mkaishia kuwa kama mimi”_ kilipandikiza mbegu ya aibu na kujikataa ndani ya watoto hawa. Badala ya kuona kazi za wazazi wao kama urithi, waliiona kama adhabu. Waliamini maisha mazuri yapo ofisini, si shambani au kwenye chupa za pombe ya kienyeji. Roja na Milembe walienda chuoni kusoma elimu ya masoko, wakitazamia mbeleni kuwa maofisa masoko na matangazo, wakikaa kwenye ofisi zenye kiyoyozi, huku wakinywa kahawa za bure. Hawakuwahi kufikiria kwamba walizaliwa nyumbani penye chakula tele kilichotoka shambani, na mama yao alikuwa na viazi na mahindi ya kutosha kula na kuuza. Kama elimu yao ya masoko ingeunganishwa na uzalishaji wa Bi Nuru, pengine leo wangekuwa na organic farm brand yenye label: “RoMi Organics – Mazao Bora kutoka Mkalaini.” Faraja alisoma masoko na biashara. Alitamani kuajiriwa Vodacom na ofcoz aliweza. Lakini je, aliwahi kujiuliza: kama mama yangu aliweza kutengeneza pombe ya kienyeji hadi akanisomesha, kwanini nisitafute kibali, nifanye branding ya hiyo pombe, nipate nembo ya TBS, niuze katika mahoteli ya kitalii kama authentic Tanzanian spirit na kila mtu akaonja ufundi wa Bi Ndelwa katika ubora wa kisasa. Daudi, kwa kejeli ya circle ya ulimwengu, now anafanya kazi TBL akitengeneza pombe kwa teknolojia ya kisasa; wakati alikua akibeba pombe ya mama yake kwenye ndoo, leo hii anatumia elimu yake kuendeleza kile alichokikataa. Ni kama historia imejirudia kutoka Ukalawa hadi Dar es Salaam, akiwa amerudi katika wimbo ule ule wa Bi Ndelwa, lakini kwa jina tofauti: Industrial Alcohol Processing. Elimu Bila Mizizi ni Kiatu Bila Mguu Ukweli wa kusikitisha ni kwamba mfumo wetu wa elimu haukuwahi kutufundisha kuheshimu tulipotoka bali ulitutenganisha. Ukatufundisha kwamba maisha ya mashambani ni fedheha, kazi za mikono ni adhabu, na ustaarabu unapatikana tu unapokalia kiti cha matairi na kuvaa tai. Kwa bahati mbaya, kizazi kilichoamini hivyo leo kimegundua ukweli mchungu: ajira hazipo, mishahara ni midogo, maisha yamekuwa magumu na zaidi, zile “kazi za aibu” zilizowalisha na kuwasomesha ndizo zinazowapa watu uhuru wa kifedha leo. Mfumo huu uliasisiwa makusudi kwa ajili ya kutengeneza subordinates ambao ni rahisi kufuata amri na sio kufanya ‘ground breaking changes’ katika maisha yao ya kila siku au walipotokea. Kilichofanyika ni kana kwamba, vijana wetu walipewa jembe kisha waanze kuzunguka kwenye mashamba ya jirani kutafuta vibarua vya kulima, ilhali nyumbani kuna shamba lililohitaji tu kufyekwa na kupanuliwa. Elimu yao ingetumika kuboresha mfumo, kuongeza tija, kuongeza soko si kukimbia kabisa na kutafuta ajira kwa wengine. Tunaishi katika wakati ambapo vijana wanazunguka mjini na maofisini wakiwa na vyeti makini kabisa na wasifu mrefu kama soksi za wanafunzi wa unesi, lakini hawana pa kuvitumia. Wazazi wao walilima, wakafanya biashara, wakauza mkaa, pombe za kienyeji na walikuwa na mtaji wa maisha ambao walidhani ni “aibu.” Leo hii tuna shahada za biashara lakini hatuwezi hata kuuza vitumbua mtaani. *Suluhisho* Maisha ni zaidi ya ajira za ofisini tu wala kuajiriwa na kuvaa tai kwenye kiyoyozi sio ukombozi. Elimu ya kweli ni ile inayoweza kutafsiri tulichosomea ili iweze kuboresha kile kilichotulea. Kwa mfano: *Sheria:* Penensia na Luhuvilo wangeweza kusaidia mama yao kupata kibali halali cha kuuza pombe na kulinda biashara ndogo ndogo. *Biashara:* Faraja angeweza kutengeneza kampuni ya local brews na kuingia sokoni . *Kiwanda:* Daudi angeweza kuungana na ndugu zake kutengeneza kiwanda cha kuzaliwa pombe kwa kutumia mbinu za kisasa kabisa wanazotumia TBL. *Kilimo:* Amani angeweza kuanzisha shule ya wakulima vijijini na kuandika mwongozo wa agriculture for wealth. *Masoko:* Roja na Milembe wangeweza kufanyia rebranding bidhaa za kijijini chao na kuzipeleka sokoni kupitia mitandao. Ukweli mchungu ni kwamba Elimu isiyo na connection na maisha yako ya kila siku ni sawa tu na bomu linalosubiri kulipuka. Lazima unachosoma kiweze kutafsirika katika vile ambavyo walifanya wazazi wako hadi ukafika ulipofika. Moja ya sababu kubwa Wabantu kuwa na familia ambazo ni legelege (kulinganisha na waarabu na wahindi) ni kutoweka nguvu katika kuboresha legacy ya familia hizo. Sababu kila kizazi ni kama kinaanza upya na kuona shughuli iliyofanikisha mafanikio yake kama ushamba. Kuna mashujaa wengi wa maisha wanaojulikana kwa jina la wazazi. Ingawa walikosa vyeti lakini walihakikisha watoto wao wanahitimu elimu za juu. Waliuza mihogo, pombe, mkaa na walijinyima ili sisi tupate elimu. Iweje leo tumwone mama aliyelima mahindi ili usome kama mtu aliyeshindwa? Iweje tumwone baba aliyekuwa fundi seremala ukapata hela ya kujikimu kama aibu?Au iweje udharau shughuli hizo? Kujiendeleza haina maana ya kujikana, mafanikio halisi ni pale unapoweza kurudi kwenye chanzo, ukakitumia kama msingi wa ujenzi mpya. Sio kutupa kila kitu na kuanza upya ugenini bila mizizi. Usiione kazi ya mzazi wako kama aibu. Inawezekana ndicho kitu pekee kilichofanya uwe hapo ulipo leo. Badala ya kutafuta ajira tu, tafuta namna ya kufanya yale waliyoanza kuwa rasmi, kuwa ya kisasa na kuwa endelevu. Kwa sababu mwisho wa siku, ajira siyo ofisi. Ajira ni uwezo wa kutumia maarifa kujiletea kipato halali iwe ni kwa jembe, kwa mdomo, au kwa kichwa. Na pale ambapo historia yako imekupa mbegu usiikatae, ioteshe, ikuze, na itumike kuwainua wengine. Kama kuna kisasi kizuri tunachoweza kulipa kwa wazazi wetu basi ni hiki: Kuwafanya wajivunie kazi walizozifanya… kwa kuona kwamba kile walichodhani ni fedheha, kimetusaidia kujenga maisha yenye heshima na faida. _Mimi ni mjumbe tu..nisiuwawe._ *Mjombaako* *©️BantuKwanza.*

SI MBAYA KUJUA Singapore ni mojawapo ya miji ya kisasa zaidi duniani inayotumia teknolojia ya hali ya juu kama vile sensa na akili bandia (AI) kusimamia trafiki, kupunguza taka, na kuokoa nishati.  Kwa mfano, zaidi ya asilimia 80 ya makutano ya barabara nchini Singapore yanasimamiwa na mifumo ya AI inayoweza kurekebisha taa za trafiki kwa wakati halisi kulingana na hali ya barabara, hivyo kupunguza msongamano na muda wa kusafiri kwa wastani wa *asilimia 30.* Aidha, mifumo ya AI hutumika katika usimamizi wa taka kwa kutumia sensa katika mapipa ya taka ili kuonyesha ni lini yanapaswa kuondolewa, hivyo kupunguza gharama na matumizi ya mafuta . Katika sekta ya nishati, Singapore imewekeza katika gridi za umeme zinazotumia AI kusambaza nishati kwa ufanisi zaidi na kupunguza upotevu wa nishati . Upo?..
