
KitaaCtics: Where the Elite Meets The Streets
February 28, 2025 at 02:31 AM
SIX TRIPLE EIGHT
Wanawake Walioshinda Vita Bila Risasi, Lakini Wakapigwa na Ukimya wa Historia
Historia tunayoifahamu imeandikwa kwa jasho, machozi, na damu. Ni hazina isiyochoka kutufundisha, kutufumbua macho, na kutuweka sehemu sahihi ya mnyororo mrefu wa wale waliotangulia kabla yetu. Katika kila ukurasa wa historia, kuna majina yaliyosahaulika, mashujaa waliojitoa bila kutarajia heshima, na watu waliovunja kuta za dhuluma ili kufungua njia kwa waliokuja baada yao.
Historia si hadithi tu za kifahari zinazosherehekewa kwa fataki na gwaride, bali pia ni simulizi za wale waliopigana kimya kimya, waliotumikia jamii bila kusubiria sifa, na waliovumilia mateso ili wengine waonje ladha ya uhuru na heshima.
Kuna mashujaa wengi waliosahaulika kwa sababu hawakuwa sehemu ya simulizi rasmi za taifa, au kwa sababu walikuwa na ngozi yenye rangi isiyokubalika katika mfumo uliotawala.
Historia yao haikuandikwa kwenye vitabu vya shule, haikufundishwa katika vyumba vya mihadhara, na kwa miaka mingi, majina yao yalizikwa kwenye vumbi la ukimya wa kihistoria.
Lakini ukweli ni kwamba, ushujaa wao haukupotea uliendelea kuishi ndani ya kazi waliyofanya, ndani ya watu waliowagusa, na ndani ya mabadiliko waliyosababisha, hata kama hawakupokea medali au shukrani.
Katika historia ya Marekani — Battalion Six Triple Eight, kikosi cha wanawake weusi wa Jeshi la Marekani waliopambana siyo tu na vita vya dunia, bali pia na mfumo wa kibaguzi uliowadharau kabla hata hawajaonyesha thamani yao ni moja ya mashujaa wa aina hii.
Nyakati ambazo Marekani yenyewe ilikuwa na sheria kali za ubaguzi wa rangi, wanawake hawa walivaa sare za jeshi la taifa lililowachukulia kama raia wa daraja la pili. Walipewa kazi ngumu, waliwekewa vikwazo vyote vinavyowezekana, lakini mara zote walijibu kwa ujasiri wa ajabu.
Simulizi hii siyo hadithi ya ushindi wa bunduki au mabomu, bali ni hadithi ya ushindi wa dhamira dhidi ya unyonge uliolazimishwa, ya juhudi dhidi ya mazingira yaliyotaka kuwadidimiza, na ya heshima dhidi ya dharau iliyokuwa imeota mizizi.
Ni hadithi ya damu, jasho, na machozi lakini zaidi ya yote, ni hadithi ya ushindi dhidi ya mifumo kandamizi, ubaguzi wa rangi, na vita vilivyotishia kuweka dunia nzima kwenye giza la kutokuaminiana.
Katika zama hizo, mwanamke mweusi hakuwa na sauti katika jamii, sembuse ndani ya jeshi. Katika taifa ambalo lilijinasibu kuwa linapigana dhidi ya udikteta na dhuluma duniani, lilikuwa bado linawadharau baadhi ya raia wake kwa sababu ya rangi ya ngozi yao. Hata hivyo, wanawake wa Six Triple Eight walijua jambo moja: Hawakuwa wanapigania kutambuliwa, walikuwa wanapigania kutimiza wajibu wao. Walijua kuwa vita siyo tu kwenye uwanja wa mapambano vita vilikuwa kwenye haki ya kila mwanadamu kuheshimiwa, hata kama dunia haikuwa tayari kuwakubali.
Hii ni hadithi yao. Hadithi ya wale waliothubutu kusimama katika ulimwengu uliotaka kuwaweka chini. Hadithi ya wale waliokataa kuanguka.
‘Lets go back’..kule ambapo yalianzia yote.
VITA YA DUNIA
Tuko mwaka 1945. Vita ya Pili vya Dunia inaelekea mwishoni kabisa, lakini bado kuna ukosefu wa amani na mapigano ya hapa na pale. Miji mingi ya Ulaya imebaki magofu, harufu ya moshi na vifo imetanda kila mahali. Wanajeshi wa Marekani na washirika wao wamepenya ndani ya ardhi ya Ujerumani, wakipambana na majeshi ya Hitler kwa kila kona.
Lakini mbali na milio ya mizinga na mapambano ya, kuna vita nyingine inaendelea vita isiyoonekana, vita ya kiutawala, mawasiliano na changamoto za kuhakikisha wanajeshi walioko mstari wa mbele wanapata huduma muhimu za kijamii na kisaikolojia hasa hasa mawasiliano kutoka kwa wapendwa wao.
Vita ilikuwa imechukua muda mrefu zaidi ya ilivyotarajiwa, na askari wengi walikuwa wamechoka, wakiwa mbali na familia zao, wakipigana katika mazingira magumu ya kivita.
Katika kipindi hicho, kulikuwa na wanajeshi zaidi ya milioni 7 wa Marekani waliokuwa wamesambazwa katika bara la Ulaya, wakihudumu katika vitengo mbalimbali pamoja na maelfu ya wafanyakazi wa Serikali ya Marekani na Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross). Hawa wote walihitaji kitu kimoja cha msingi: barua kutoka nyumbani.
Katika mazingira haya magumu, huduma za posta za jeshi la Marekani zilikuwa katika hali mbaya kuliko wakati wowote. Mamilioni ya barua kutoka kwa familia za wanajeshi zilikwama kwenye ghala kubwa huko Birmingham, England, na Rouen, Ufaransa baadhi kwa zaidi ya miaka miwili.
Jeshi lilikuwa limelemewa, mfumo wa posta ulikuwa umesambaratika, na mlundikano wa barua uliendelea kukua kila siku. Hili lilikuwa tatizo kubwa zaidi ya vile lilivyoonekana.
Kiwango cha barua ambazo zilihitaji kupangwa kilikuwa kikubwa mno.
Kulikuwa na mamilioni ya barua, picha za wapendwa wao, na zawadi kutoka kwa familia ambazo zilikuwa zimetupwa bila mpangilio ndani ya maghala hayo.
Barua nyingi zilikuwa na anwani zisizo sahihi, majina yaliyokosewa, au maandishi yasiyosomeka.
Zilikuwa zimepoteza maana ya muda wake — barua ambazo zilipaswa kuwafariji askari kabla ya Krismasi ya mwaka mmoja uliopita, zawadi ambazo zilipaswa kuwafikia wanajeshi waliokuwa tayari wamepoteza maisha vitani.
Barua hizi hazikuwa makaratasi tu kama inavyoweza fikiriwa, zilikuwa ni chachu ya matumaini kwa askari waliokuwa wanapigana msituni, kwenye vifaru, na kwenye miji iliyovamiwa na wanajeshi wa Nazi. Ndani ya bahasha hizo, kulikuwa na maneno ya upendo kutoka kwa wake na watoto wao, barua za faraja kutoka kwa mama zao, na wakati mwingine, habari za huzuni kutoka nyumbani au vitani.
Katika hali ya kawaida, wanajeshi wangeweza kuishi kwa siku kadhaa bila chakula kizuri, lakini kuishi bila matumaini, bila kujua kama familia zao bado zipo salama, lilikuwa jambo gumu zaidi hata kuliko adui aliyewakabili vitani.
Barua hizi zilikuwa kama silaha za kisaikolojia; zilitoa faraja, ziliwapa askari sababu ya kupambana, na zilikuwa ukumbusho wa kile wanachokipigania.
Inaendelea..
❤️
1