
KitaaCtics: Where the Elite Meets The Streets
March 1, 2025 at 05:26 PM
*HADITHI YA CLIFF YOUNG*
*Mkulima Aliyetikisa Ulimwengu wa Mbio za Masafa Marefu*
Wakati wanariadha waliovalia viatu maalumu vya kukimbilia na vifaa vya kisasa wakijiandaa kwa mbio ndefu zaidi duniani, mwanaume mzee kutoka kwenye shamba la viazi alijitokeza akiwa amevaa buti za shambani (gumboots)na suruali ya kazi. Huku wakicheka, baadhi ya washiriki waliulizana kwa kejeli’ _‘hivi huyu mzee anajua kuwa tunaenda umbali wa kilomita 875?’._
Mzee yule aliwaangalia kwa mbali huku akitabasamu, hakuna aliyejua kuwa ndani ya siku tano tu zilizofuata, tabasamu lake lililoonekana la kichovu lingewanyamazisha wote, historia ingeandikwa na kuuacha ulimwengu wa mbio za masafa marefu ukisimama kwa mshangao mkubwa.
Ni Australia, nchi inayofahamika kwa kuwa na nyika za kupendeza na nyumbani kwa kangaroo wanaorukaruka kwa majivuno. Katika ardhi hii iliyojaa hadithi za ushindi na majabali, jina moja lilizaliwa upya kwenye midomo ya watu: Cliff Young. Mkulima wa viazi mwenye umri wa miaka 61 kutoka kijiji kidogo cha Beech Forest, aliikabili moja ya changamoto kubwa zaidi ya maisha yake.
Lakini ilikuwaje mtu huyu asiyekuwa na uajabu wa aina yoyote akawashangaza wanariadha vijana, wenye nguvu, na wenye uzoefu? Hii ndiyo hadithi mjombaako naenda kukusimulia leo.
*Cliff Young*
Cliff aliyetokea katika maisha ya kawaida kabisa, alizaliwa mwaka 1922, katika familia maskini ya wakulima huko Beech Forest, Victoria. Familia yake ilimiliki shamba la viazi lenye ukubwa wa ekari 2,000 na kondoo. Katika maisha ya kawaida ya shambani, Cliff alikua akiwachunga kondoo na kukimbia nyuma yao kwa siku nzima, mara nyingi akiwatafuta waliopotea kwenye nyika za upepo mkali na mvua.
Mazoea haya yasiyo rasmi yalikuwa msingi wa stamina yake, ingawa hakuwahi kufikiri kwamba siku moja angeingia kwenye mashindano ya kimataifa ya mbio.
_"Mara nyingi, nilikimbia kilomita nyingi kwa siku bila kujua kwamba nilikuwa najitayarisha kwa ajili ya kitu kikubwa,"_ alisimulia baadaye.
Cliff alikuwa mnyenyekevu sana, hakuna siku aliwahi kuwa na mipango ya kuwa maarufu kitu alichofahamu kwa undani ni jinsi ya kufanya kazi kwa bidii.
*Mbio za Sydney hadi Melbourne*
Mwaka wa 1983, shirika la Westfield lilizindua mashindano ya ultramarathon ya kilometa 875 kutoka Sydney hadi Melbourne. Mashindano hayo yalilenga wakimbiaji walio bora duniani—wenye uwezo na wenye uzoefu wa kukimbia kwa siku nyingi bila kupumzika. Dau la ushindi likatajwa kuwa ni pesa *taslimu za AUD 10,000 (takriban milioni 2.5 za Shilingi za Tanzania leo)* ila hii ni mwaka 1983 usisahau..
Kilomita hizo 875 zilipita kwenye barabara za milimani na mabondeni, nyikani na katika joto la jua kali la Australia. Washiriki karibu wote walikuwa wanariadha professional, wakiandaliwa na makocha, wakiwa na vifaa vya kisasa kwa ajili msaada wa kukimbia na vyakula maalumu vya kuongeza nguvu. Hili lilikuwa shindano la watu waliokuwa wamejipanga ili kupata ushindi.
Katika hali ya kustaajabisha mtu mmoja mwenye muonekano wa kizee na asiye na dalili za kuwa ni mwanariadha alionekana akiwa katika harakati za kujiandikisha katika shindano hilo. Bila hili wala lile mzee yule alifika akiwa amevaa buti za kazi za shambani na suruali ndefu iliyochakaa.
Watu walidhani kwamba alikuwa amekosea njia—maana hakuwa na mwili wa mwanariadha, wala chochote kuonyesha kuwa alipanga kushiriki marathon ile.
_"Mzee una uhakika unachofanya?"_ aliuliza mwenyeji wa mashindano kwa nyuso ya kustaajabu. Cliff alitabasamu na kusema, _"Ndio, nimekimbiza kondoo kwa miaka takribani 50. Nitafanya hivyo tena kwenye hii marathon."_
Asubuhi ya Mei 27, 1983, watu takribani elfu mbili walikusanyika Sydney kushuhudia wakimbiaji 150 waliojiandaa kwa mbio. Wakiwa na mbwembwe zote huku kila mmoja akiwa na timu yake ya wataalamu, wakihakikisha kila kitu kiko sawa. Kati yao, Cliff alisimama akiwa amevaa kofia ya jua, koti la mvua, na viatu vya kawaida (ingawa kabla ya mbio kuanza moja ya washiriki alimpatia viatu maalumu vya kukimbilia). Kwa haraka ungeweza kuhisi ni mgeni kutoka zama za mawe.
Watazamaji walimwangalia kwa mshangao na kucheka. _“Mzee huyu kweli anaweza kuhimili umbali huu?”_ wengi walijiuliza kwa dhihaka.
Dakika chache kabla ya mbio kuanza, mwandishi mmoja alimhoji Cliff. Swali lake lilikuwa la moja kwa moja, “Unadhani una nafasi ya kushinda?” Cliff, akitabasamu kwa upole, alisema, _“Nafikiri nina nafasi. Nilizoea kukimbiza kondoo kwa siku nyingi bila kupumzika. Nadhani naweza jaribu.”_
Mlio wa bunduki uliporindima, washiriki wote waliondoka kwa kasi ya ajabu. Cliff, kwa upande mwingine, alianza mbio zake kwa mwendo wa polepole, mithili ya mtu anayechechemea au kukokota miguu yake.
Style yake hii maarufu iliyokuja kufahamika baadae kama *“Cliff Young Shuffle”* – mwendo wa polepole lakini wenye ufanisi wa ajabu hasa katika kusave ‘energy’.
Katika mbio hizi, ratiba ya wakimbiaji wengi ilikuwa kama ifuatavyo: kukimbia kwa masaa 18 na kupumzika kwa masaa sita kila siku. Lakini Cliff, kwa bahati au kwa uzembe, hakujua kwamba kulikuwa na utaratibu wowote wa mapumziko. Aliendelea kukimbia, mchana na usiku, akijua kwamba sababu kondoo hawapumziki basi na yeye pia hapaswi kupumzika. Wakati wenzake walipokuwa wamelala, Cliff aliendelea kukimbia kwenye barabara za giza, akiongozwa na dhamira yake ya ushindi.
Hadi siku ya kwanza inaisha, Cliff alikuwa nyuma sana. Vyombo vya habari vilianza kumfuatilia kama mzaha wa mbio zile, lakini kadiri siku zilivyopita kitu cha ajabu kilitokea. Mkulima huyu mzee, aliyevaa mavazi ya kawaida na mwendo wake wa kushangaza, alianza kuwashinda washiriki wenzake. Kufikia siku ya mwisho ya mbio, Cliff Young alikuwa mbele kwa umbali wa kilomita nyingi mno!
*Ushindi wa Historia*
*Mnamo Mei 3, 1983,* baada ya kukimbia kwa siku tano, saa 15, na dakika nne bila kupumzika, Cliff Young aliingia Melbourne akiwa mshindi. Alivunja rekodi ya mbio hizo kwa masaa 9 na kuwa mshindi wa ajabu zaidi katika historia ya mbio za masafa marefu. Mashabiki walipiga kelele kwa mshangao na furaha. Mzee huyu kutoka kwenye shamba la viazi alikuwa amethibitisha kwamba dhamira na bidii vinaweza kushinda kila kitu.
Katika mahojiano baada ya mbio, Cliff alielezea maisha yake ya kila siku. Hakukuwa na vinywaji maalumu vya kuongeza nguvu, alitumia chakula cha kawaida kama maziwa, viazi, na mikate. Hii ilionyesha kuwa si lazima uwe na rasilimali nyingi au teknolojia ya hali ya juu kufanikisha mambo makubwa. Vitu vingi huusisha mtazamo wa akili na dhamira thabiti ya kushinda changamoto.
Jambo lingine ambalo liliwashangaza watu zaidi ni kwamba baada ya kushinda ile zawadi ya dola 10,000, Cliff aliamua kugawa pesa hizo kwa washiriki wengine wa mbio zile na kubakiza dola 3000 pekee kwa ajili yake. Alielezea kuwa hakuwa na uhitaji pesa hizo zote, kwani alikuwa na kila kitu alichohitaji katika maisha yake. Kitendo hiki cha ukarimu kilimfanya kuwa zaidi ya mshindi wa marathoni.
Cliff Young alifariki mwaka 2003 akiwa na umri wa miaka 81, lakini kumbukumbu yake inaendelea kuishi hadi leo. Mbio zake za ajabu zinakumbusha ulimwengu kwamba hakuna kinachoweza kuzuia dhamira ya kweli. *“Cliff Young Shuffle”* ile mbinu ya ukimbiaji yenye kuhifadhi energy vizuri hadi sasa bado inatumiwa na baadhi ya wanariadha wa masafa marefu kama tactic ya kuzuia kuchoka mapema.
Mitaa haitasahau jina la Cliff Young. Maana pale wengine walipohesabu umri wake kama udhaifu, Cliff aliuthibitisha umma kuwa ni silaha. Mahali wanariadha wengi walitegemea mafunzo ya hali ya juu na mbinu za kisasa, yeye alitegemea roho ya mkulima na ujasiri wa mtu aliyewahi kuswaga kondoo kwa siku nzima bila kupumzika. Alianza mbio kama mzaha, akamaliza kama shujaa. Na hata baada ya ushindi wake, hakujiona kama mtu wa tofauti, kwake ilikuwa tu siku nyingine ya kawaida ya kazi.
*The streets will never forget.*
*Mjombaako*
*©️BantuKwanza*