
Tumainimedia
February 1, 2025 at 04:48 PM
[01/02, 15:12] Fr. Henry Rimisho: SAUTI YA MTU ALIAYE NYIKANI…ITENGEZENI njia ya BWANA yanyoosheni Mapito yake… ( Math 3:3)
JUMAPILI YA 4 MWAKA -C-
(2.02.2025)
“Jubilee 2025, Mahujaji wa MATUMAINI”
MASOMO:
Somo la I: . Yer 1:4-5,17-19
Somo la II: 1Kor 12:31; 13:1-13
Somo injili: .Lk 4:21-30
UTANGULIZI:
Masomo haya yanatufundisha kwamba Mungu anatuita kwa kazi yake na anatupa nguvu. Tunapaswa kuishi kwa upendo wa kweli, na tusimfungie Mungu ndani ya matarajio yetu binafsi.
Tuombe neema ya kumtambua na kumpokea Mungu katika maisha yetu ya kila siku, hata pale tunaposhawishika kumsukumia mbali kama watu wa Nazareti walivyofanya.
SOMO la KWANZA:
Yeremia 1:4-5, 17-19
Katika SOMO hili, Mungu anamwita nabii Yeremia na kumhakikishia kuwa alimteua kabla hajazaliwa. Pia anamwambia asihofu, kwani atampa nguvu za kusimama imara mbele ya watu, hata kama watampinga.
Katika SOMO la KWANZA tunajifunza Jambo (1) lifuatalo:
1.WİTO wa MTUMISHI WA MUNGU:
Huu ni ujumbe wa faraja kwa yeyote anayejisikia mdogo au hafai kwa kazi ya Mungu. Yeremia katika umri wake mdogo anaitwa na Mungu kuwa NABII, wito huu unajawa na changamoto nyingi kutokana na umri. Lakini Mungu anampigania hili kufikia lengo lake.
Hivyo, Kila mmoja wetu ana mwito wa pekee, na Mungu hatuachi peke yetu tunapokabiliana na changamoto za utume wetu.
SOMO la PILI:
1 Wakorintho 12:31 – 13:1-13
Katika SOMO la PILI tunajifunza Jambo (1) lifuatalo:
1.UPENDO wa KWELI na ŞIFA ZAKE:
Mtume Paulo anatufundisha kuwa kipaji kikuu kuliko vyote ni upendo. Bila upendo, hata matendo makubwa ya imani hayana maana. Anabainisha sifa za upendo wa kweli: hustahimili, hauna wivu, haujisifu, haukasiriki kwa urahisi, na hufurahia ukweli.
Hili ni somo muhimu kwa jamii zetu leo.
SWALI: Tunawezaje kuwa mashahidi wa upendo huu katika familia, jumuiya, na mahali pa kazi?
SOMO la INJILI TAKATIFU:
Injili: Luka 4:21-30
Yesu anahubiri kwa watu wa Nazareti, lakini badala ya kumpokea kwa furaha, wanamkataa kwa sababu walimjua tangu utoto wake. Anawaambia kuwa hakuna nabii anayekubalika katika nchi yake, jambo linalowakera hadi wanataka kumuua. Hii ni changamoto kwetu pia.
SWALI: Je, tunapuuza ukweli kwa sababu ya ubaguzi au mazoea?
SWALI: Je, tunakataa ukweli wa Mungu unapokuja kupitia watu au hali tusizozitarajia?
Katika SOMO la INJILI TAKATIFU İnatufundisha mambo Makuu (4) yafuatayo:
1. YESU ATANGAZA KWA UJASIRI: “LEO MAANDIKO HAYA YAMETIMIA”
Hii ni kauli nzito sana kwa watu waliomsikiliza.
Wanashangazwa na hekima yake lakini bado wanabaki na mashaka. Wanashindwa kumwelewa kwa sababu wanamwona kama kijana wa kawaida waliyekua naye.
Wapendwa,hii ni changamoto kubwa kwa kila mmoja wetu: je, tunamruhusu Mungu atufikie kwa njia zisizotarajiwa? Watu wa Nazareti walimchukulia Yesu kwa mtazamo wa kibinadamu pekee, kuwa ni mwana wa Yusufu.
Hivyo wakashindwa kutambua utukufu wake. Hata sisi tunaweza kumpuuza Mungu anapotuongea kupitia watu tunaodharau au hali tunazoziona kuwa za kawaida.
2. “DOKTA, JIPONYEE MWENYEWE” – WATU WANAMASHAKA NA YESU
Baada ya Yesu kusema kuwa maandiko yametimia, watu wanamwelekea kwa mashaka na Yesu.
Hii ni aina ya imani inayotaka kuona kwanza ndipo iamini. Watu wa Nazareti wanataka uthibitisho wa macho badala ya kuwa na imani ya kweli. Lakini Yesu anawakataa kwa sababu imani ya kweli haihitaji uthibitisho wa ishara tu, bali unyenyekevu wa moyo unaopokea ukweli wa Mungu.
Wapendwa,Imani yetu haipaswi kutegemea tu kuona miujiza. Watu wengi leo wanakimbilia unabii na ishara badala ya kujenga uhusiano wa kweli na Mungu. Yesu anatufundisha kuwa imani ya kweli ni kumwamini Mungu hata pale tunapokosa kuona ishara za haraka.
3. YESU AWAKUMBUSHA ISRAELI JINSI WAGENI WALIVYOPOKELEWA NA MUNGU
Yesu anawapa mifano miwili kutoka Agano la Kale:
1. Eliya na mjane wa Sarepta (1Fal 17:8-16) – Kulikuwa na njaa Israel, lakini Mungu hakumtuma Eliya kwa wajane wa Israeli, bali kwa mwanamke Mpagani huko Sarepta.
2. Elisha na Naamani (2Fal 5:1-14) – Ingawa Israeli walikuwa na watu wengi wenye ukoma, nabii Elisha alimponya Naamani, jemadari wa kigeni kutoka Aramu.
Kwa mifano hii, Yesu anaonyesha kuwa mara nyingi wale waliodhaniwa kuwa “wa mbali” na Mungu ndio waliopokea neema kwa sababu walifungua mioyo yao kwa imani.
Wapendwa,Mungu hatabiriki wala hajifungi kwa taifa moja au kundi fulani. Wana wa Israeli walijiona kuwa watu wa Mungu pekee, lakini Yesu anaonyesha kuwa hata watu wa mataifa walihitaji wokovu na waliupokea kwa imani.
SWALI: Je, sisi tunajiona kuwa tuko karibu sana na Mungu kiasi cha kuwadharau wengine? Mungu anaweza kutumia mtu yeyote, hata yule tunayemdharau, kutuletea ujumbe wake wa wokovu.
4. WATU WAMKATAA YESU NA WANATAKA KUMUUA
Baada ya Yesu kusema haya, watu wa Nazareti wanachukia sana. Wanasukumwa na hasira, wanamsukuma hadi kwenye mwinuko wa mlima ili wamtose chini na kumuua. Kwao, Yesu amevuka mipaka kwa kuwalinganisha na wale waliomkataa Mungu katika historia.
Lakini maandiko yanasema:
“Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake.”
Hili linaonyesha kuwa hawakuwa na mamlaka juu yake. Wakati wake wa kufa haukuwa umefika, na maisha yake yalikuwa mikononi mwa Mungu.
Wapendwa, Yesu anakataliwa kwa sababu alisema ukweli ambao watu hawakutaka kuusikia. Hii inatufundisha kuwa mara nyingi, ukweli wa Mungu unaweza kupingwa, na wale wanaousimamia wanaweza kupata upinzani mkali. Kama wafuasi wa Kristo, hatupaswi kuogopa kusimamia ukweli hata kama tunapingwa.
HITIMISHO:
UNABII HAUKUBALIKI KWA WAO WENYEWE
Yesu anatoa somo kuu: “Hakuna nabii anayekubalika kwao wenyewe.”
Hili linatufundisha kuwa mara nyingi tunashindwa kutambua na kuthamini kazi ya Mungu ndani ya watu tuliowazoea. Watu wa Nazareti walimjua Yesu kama mwana wa seremala, wakadhani hawawezi kupokea wokovu kupitia kwake.
MASWALI YA KUJIHOJI:
1. Je, ninamruhusu Mungu kuniongelesha kupitia watu au njia nisizotarajia?
2. Je, ninamwamini Mungu hata pale ambapo sioni ishara za haraka?
3. Je, nina moyo wa unyenyekevu wa kupokea ukweli wa Mungu hata kama unaniweka kwenye changamoto?
4. Je, naweza kuendelea kushuhudia imani yangu hata nikipata upinzani?
SALA:
Ee Bwana Yesu, unayetufundisha kuwa nabii hapokelewi katika nchi yake, tusaidie tusiwe na mioyo migumu kama watu wa Nazareti. Utufungue macho tuweze kukutambua katika maisha yetu ya kila siku na tukupokee kwa imani ya kweli. Amina.
TUMSIFU YESU KRISTU🙏🏾
Tafakari hii imeandaliwa nami,
Rev. Fr. Henry Rimisho AJ
(Kwa msaada wa Roho Mtakatifu)
[01/02, 17:30] Fr. Henry Rimisho: SAUTI YA MTU ALIAYE NYIKANI…ITENGEZENI njia ya BWANA yanyoosheni Mapito yake… ( Math 3:3)
DOMINIKA YA SIKUKUU YA KUTOLEWA BWANA HEKALUNI.
JUMAPILI YA 4 MWAKA -C-
(2.02.2025)
“Jubilee 2025, Mahujaji wa MATUMAINI”
MASOMO:
Somo I: 3:1-4
Somo II: 2:14-15
Injili: Lk 2:22-40
UTANGULIZI:
Sikukuu ya Kutolewa kwa Bwana Yesu Hekaluni ni tukio lenye uzito wa pekee katika fumbo la ukombozi. Yesu, akiwa bado mchanga, anapelekwa Hekaluni kama inavyotakiwa na Torati, lakini kwa undani zaidi, tendo hili linaashiria kujitoa kwake kwa Mungu na kwa wanadamu. Tukio hili linatuonyesha jinsi Mungu anavyotimiza ahadi zake kwa njia ya Yesu Kristo.
SOMO LA KWANZA:
Somo la Kwanza: Malaki 3:1-4
Nabii Malaki anatabiri kuja kwa Mjumbe wa Agano, ambaye ataitakasa hekalu na watu wake. Yesu ndiye utimilifu wa unabii huu, kwani Yeye ni Mwanga wa Mataifa na utakaso wa waamini.
Katika SOMO la KWANZA linatufundisha Jambo (1) lifuatayo:
1.UTAKASO WA MUNGU
Somo linatufundisha kuwa Mungu hututakasa kupitia Kristo, hivyo tunaalikwa sote tujikabidhi kwa Mungu Baba kwa kuwa anatarajia nasi kujitoa kikamilifu kwake hili kutimiza Ahadi zake.
SOMO la PILI:
Waebrania 2:14-18
Katika SOMO la PILI tunajifunza Jambo (1) lifuatalo:
1.YESU AMEUVAA UBINADAMU WETU:
Mtume Paulo anasisitiza kuwa Yesu alishiriki hali yetu ya kibinadamu ili apate kutushinda na kutuokoa kutoka utumwa wa dhambi na mauti.
Kwa kujitoa kwake, anatufanya kuwa ndugu zake wa kweli, akituonyesha kuwa tunapaswa kuwa tayari kujitoa kwa Mungu na kwa wengine.
SOMO LA INJILI TAKATIFU:
Injili: Luka 2:22-40
Maria na Yosefu wanampeleka Yesu Hekaluni ili kumtolea kwa Mungu, wakitimiza sheria ya Kiyahudi.
Katika tukio hili, tunakutana na Simeoni na Ana, watu wa imani kubwa waliokuwa wakingoja kwa hamu wokovu wa Mungu. Simeoni anampongeza Mungu kwa sababu amemwona Masiya kabla ya kufa. Maneno yake yanaonyesha kuwa Yesu ni “Mwanga wa Mataifa” na “Utukufu wa Israeli.” Ana pia anamshuhudia Yesu kama ukombozi wa watu wa Mungu.
Katika SOMO la INJILI TAKATIFU tunajifunza mambo Makuu (4) yafuatayo:
1.YESU NI MWANGA WA MATAIFA.
Yesu alikuja kuwa nuru kwa ulimwengu mzima. Kama Wakristo, tunaitwa kuwa mwanga kwa wengine kwa maisha yetu ya imani, upendo, na haki. Tunapaswa kumruhusu Yesu kutakasa maisha yetu ili tuwe mashahidi wa nuru yake.
2.KUJITOA KWA MUNGU.
Yesu, pamoja na wazazi wake, anajitoa kwa Mungu Hekaluni. Hili linatufundisha umuhimu wa kujitoa kwa Mungu bila masharti. Hili linajidhihirisha kwa namna tunavyoishi maisha ya sala, unyenyekevu, na huduma kwa wengine.
3.IMANI NA SUBIRA YA SIMEONI NA ANNA.
Simeoni na Anna walimngoja Masiya kwa muda mrefu kwa imani thabiti. Subira yao ni mfano mzuri wa jinsi tunavyopaswa kuendelea kumtumainia Mungu hata tunapopitia changamoto. Mungu daima hutimiza ahadi zake kwa wakati wake.
4.KRISTO KAMA CHEMCHEM YA WOKOVU.
Yesu anapotolewa Hekaluni, anatufundisha kuwa wokovu wetu unapatikana kwa kumkabidhi Mungu maisha yetu kikamilifu. Tunapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha ya Kanisa, sakramenti, na matendo ya huruma.
HITIMISHO
Sikukuu hii ni mwaliko wa kujitoa kwa Mungu bila masharti kama Yesu alivyofanya. Tunapaswa kuwa mwanga kwa wengine kwa matendo yetu mema na kushikilia imani hata katika nyakati ngumu.
SWALI: Je, tuko tayari kumruhusu Yesu atakase maisha yetu na kutufanya vyombo vya nuru yake kwa ulimwengu?
Bwana atupe neema ya kujitoa kwake kikamilifu, ili nasi tuwe mwanga kwa wengine.
Amina.
Ninawatakia MAPADRE, WATAWA wa kike na wanaume wote katika KANISA, HERİ NA BARAKA ya Sikukuu ya kutolewa kwa BWANA HEKALUNI.
TUMSIFU YESU KRISTU🙏🏾
Tafakari hii imeand aliwa nami,
Rev. Fr. Henry Rimisho AJ
(Kwa msaada wa Roho Mtakatifu)
#tumaini Media
🙏
1