Tumainimedia
Tumainimedia
February 14, 2025 at 05:14 AM
LEO PIA FEBRUARI 14 MAMA KANISA ANAMKUMBUKA MTAKATIFU VALENTINO, PADRIE Februari 14 ni Siku ya "Valentine Day" asili yake ni kutoka Dola ya Warumi. Ni siku ya kumbukumbu (Memoria day) na sehemu nyingine ni (festum) maana yake Sikukuu ya Daraja la kwanza kwa kumkumbuka Padre Valentino aliyeuawa na utawala wa Kirumi. Mtakatifu Valentini alizaliwa mwaka 226 AD huko Terni, Nchini Italia na aliuawa Februari 14, 269 AD huko Roma, Italia. Aliuawa kwa sababu ya kutetea Waamini wake kufunga ndoa badala ya kuishi na vimada tu. Lakini sikukuu hiyo imeenea sana katika nchi za Magharibi na baadaye karibu sehemu kubwa ya Ulimwengu huisherehekea kama siku ya Mapenzi kinyume cha dhamira ya Mtakatifu Valentine. Watawala wa dola ya kirumi walikuwa na fikra za kueneza Dola ya Kirumi duniani kote na hivyo Vijana hawakutakiwa kuoa ili wawe huru muda wote kwenda vitani kupigania nchi. Hii ilimaanisha kuwa kama wangeoa wasingekuwa na uhuru wa kwenda Vitani bali kuwa na familia zao. Vijana wengi wakawa na mtindo wa kuwa na vimada tu kitu ambacho Kanisa lilikuwa linapinga. Padre Valentino ambaye alikuwa Roma, akawa anawahimiza vijana kufunga ndoa badala ya kufanya ngono bila ndoa, kwani ni dhambi na kitu kisichokubalika mbele za macho ya MUNGU. Akawa anafungisha ndoa kwa siri kubwa kwenye Makatakombe yaani Mahandaki chini ya Kanisa ambako kuna sehemu za Ibada kwa watu wachache na alifanya hivyo kwa vile kufunga ndoa hadharani ilikuwa ni kukiuka Amri ya Wakuu wa Dola ya Kirumi. Baadhi ya watu walifichua siri hiyo hivyo Padre Valentino alishikwa na uongozi wa Dola ya Warumi na kuuawa kama Shahidi Mfiadini kwa ajili ya kutetea Waamini wake wafunge ndoa badala ya maisha ya ngono zembe bila ndoa. Kanisa Takatifu Katoliki la Mitume kote Ulimwenguni, likatenga tarehe maalum ya kumkumbuka Padre Valentino kama mfiadini sababu ya kutetea maisha ya Wanakanisa kuwa wanandoa. Ni tarehe14, Februari kila mwaka. Baadaye ikapokeleka na watu hata wasio na imani ya Kikristo kama ni siku ya kufanya kumbukumbu kwa Mtakatifu Valentino kama mtetezi wa Ndoa. Maudhui ya siku hiyo kwa wasio Wanakanisa imechukua maana nyingine ya kwamba ni siku ya wapendanao hata kwa wasio wanandoa ilimradi wanapendana, kitu ambacho ni kinyume cha malengo ya Mfia Dini Mtakatifu Padre Valentino aliyetaka vijana wafunge ndoa badala ya kuwa na hawara tu (vimada). Wenye hofu ya MUNGU tunaalikwa kuiheshimu Siku hii kama ni Siku Takatifu ya kumpendeza MUNGU kwa watu tuwapendao na sio kuifanya kama siku ya kutenda machukizo mbele ya MUNGU. Tumuombe Mtakatifu Valentino, Padre atuombee kwa MUNGU tuwe na upendo wa kweli kwa watu tuwapendao ili hatimaye tutimize mapenzi ya MUNGU wetu. "PENDANENI KAMA NILIVYOWAPENDA NINYI" MTAKATIFU VALENTINE. UTUOMBEE #tumainimedia
🙏 1

Comments