Sekretarieti ya Ajira
Sekretarieti ya Ajira
February 14, 2025 at 09:40 PM
Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Balozi Dkt. Asha Rose Migiro ametembelea Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma jijini Dodoma. Balozi Dkt.Migiro amepokelewa na Katibu wa Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Mick Kiliba pamoja na watumishi wengine wa ofisi hiyo na kupewa taarifa fupi ya mchakato wa ajira za ualimu unaoendelea nchini. Katika ziara hiyo, Kiongozi huyo mashuhuri ulimwenguni alikutana na watumishi wapya ambao wamefika katika ofisi hiyo kuchukua barua zao za kuitwa kazini baada ya kufaulu usaili wa kada za ualimu na kada zingine. Aidha,Balozi Dkt. Migiro alitembelea na kujionea jiwe la msingi aliloliweka wakati alipozindua majengo ya ofisi hiyo mwaka 2009 na alieleza kufurahishwa na namna majengo hayo yaliyopewa jina lake yanavyotumika. “Nawapongeza sana kwa kazi yenu kubwa na nzuri lakini zaidi nimefurahi kuona namna ambavyo majengo haya yanatumika kwa shughuli muhimu sana kwa mustakabali wa taifa letu” alisema. Majengo ya Dkt Asha Rose Migiro yalizinduliwa na kiongozi huyo mwaka 2009 na yamekuwa maarufu zaidi tangu Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilipoanza kuyatumia ambapo majengo hayo yamekuwa sehemu ya kuenzi mchango mkubwa wa mwanasiasa na kiongozi huyo mwenye historia kubwa duniani. Balozi Dkt. Asha -Rose Migiro aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani na nje ya nchi ambapo aliwahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto, Waziri wa Mambo ya Nje na vilevile Dkt. Migiro aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
🙏 2

Comments