MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
January 31, 2025 at 08:19 PM
*`SHAMBA LA HELA`* Yake; *Godlove Kabati* WhatsApp; 0763204351 -------------------------------- SEHEMU YA KUMI NA SABA *MOTOKAA NYEUSI* ----------------------------- "Oyah! Ulimwambia huyu jamaa yako kuwa uko hapa au?" Kagoye akamuuliza Feruzi huku akihema kwa hofu na jasho jembamba likimvuja, pumzi zikimtoka kwa kasi. "Hapana bro!" "Sasa amejuaje kuwa uko hapa...kwanza amenijuaje?" Maswali mfululizo yakanyesha kutoka kinywani kwake. Lakini kitu pekee alichokiambulia ni kutazamana na Feruzi ambaye hata naye alionekana kuchanganyikiwa. Jambo hili likawajumuisha watu wawili ndani ya chumba ambao wote wamechanganyikiwa. "Katumia simu yako bwana...na nilipopokea hata sikutamka sentensi zaidi ya mbili. Tayari kashanifahamu!" Akazidi kulalamika lakini muda huu alilalamika kwa namna ya kufoka akiwa amesimama. Feruzi akamtuliza na kumrudisha juu ya kiti, akaketi. "Tayari ameshakufahamu kaka. Na ameshatambua kuwa nimekueleza mengi kunihusu na kumuhusu yeye pia. Hapa kilichopo ni kukubaliana na matokeo. Lakini chondechonde usije ukakosea step." Akiwa amelishika bega la Abednego akamueleza kwa upole na sauti yake ndogo ikatangaza waziwazi kuwa wamezidiwa ujanja. "Lakini mi simjui aisee....mi simfahamu hata kidogo. Sijawahi kuua mimi!" Sauti ya Abednego ikaanza kubadilika na kuvaa kilio ambacho kilimfanya achekeshe badala ya kutia huruma. Ni dakika moja tu iliyopita alitangaza vita na huyu bwana mwenye kovu. Akataka kukutana naye na waongee kiume na kama muda ukitosha wamalizane kiume. Lakini muda huu ametishika na sauti tu, tena ya kwenye simu. Hakika alichekesha kwelikweli. Abednego akazidisha kulalamika na kumlaumu sana Feruzi kwa kumuingiza kwenye balaa kama lile. Yeye akitumia sauti kubwa dhidi ya Feruzi anayetaka jambo hili lichukuliwe kwenye hali ya utulivu na umakini mkubwa. Ni katika mzozano huo, uvumilivu wa Feruzi ukashindwa na lawama za Abednego. Akafumba macho yake na hasira ikamchemka kama mvuke kwenye kifua chake...hakujali umbo kubwa la Abednego, hakujali kuhusu uswahiba wao, hakujali kuhusu umri wala kitambi chake kidogo kilichompa heshima mtaani, akavurumisha kofi kali lililotua usoni kwa Abednego. Abednegi akapepesuka na kuanguka kando akiwa haelewi amepigwa na kitu gani, zaidi aliona mwanga mweupe unaowakawaka kama nyota. Na kweli matarajio ya Feruzi yakaenda sawasawa. Kofi lile kali lilimtuliza Abednego. "Utanisaidia au utataka mimi nikusaidie?!" Feruzi akafoka! Abednego akiwa bado amejishika paji la uso haieleweki kama anaona au haoni, akatikisa kichwa kukubali. "Lakini huyu jamaa mi simjui!" Akatamka kwa upole. "Humjui lakini yeye anakujua tayari. Na kwa maana hio huna budi kuingia kwenye circle yangu bro.!" Feruzi akatamka akiwa mwenye jazba kiasi. Akasogelea jagi la maji mezani na kumimina ya kutosha kwenye glasi, akayabugia yote kwa pupa. Kisha akamsogelea Abednego pale sakafuni na kumnyanyua mpaka juu ya kiti, akatulia mbele yake na kumtazama. "Mtu wa mwisho kumueleza kuhusu huyu jamaa alikuwa Mtemi. Na baada ya siku mbili tu nilipewa taarifa za vipande vya mwili wa Mtemi. Jamaa likaniambia kuwa limeupiga mguu wake mpaka likausagasaga. Halafu likanishauri kuwa ni heri limuue tu ili limpuguzie mateso ya maumivu anayoyapitia!" Akaweka pumziko na kuendelea. "Mtemi alifanya makosa na akakosea step, jambo lililomfanya aikamilishe safari yake hapa duniani. Sasa naona na wewe una roho nyepesi bro, haukuwa kama nilivyokudhania. Nisikilize bro, hili jamaa lenye kovu linapenda kuua. Na linaua vibaya sana. Kuna wanafunzi wake wale ambao amewatunuku shahada ya kufanya ukatili. Wao ni wakubwa wa miili, misuli yao imevimba sana na nyuso zao zina uadui mkubwa sana na vitu kama kutabasamu na kucheka. Sijui kama waliwahi kutabasamu wale viumbe, kwanza wana majina ya ajabu ajabu. Sijui Dubu na Duba! Oa bro...!" Akaweka pumziko na kulishuhudia jasho jembamba linalomtoka Abednego aliyekuwa anatetemeka zaidi. "Ni kwa..ni kwa nini unaniambia haya?" Akauliza. "Nakwambia haya ili ujue ni viumbe wa aina gani unaenda kukutana navyo. Sitaki unisaidie kupigana vita na mimi ubavu kwa ubavu ukiwa haumjui adui yetu bro! Ni hao watu watatu...hao tu! Wamemuua yule mzee aliyekuwa abiria wangu. Wamemuua Mtemi, na kama mimi na wewe tutazubaa na kuleta uzembe hawatakawia kutuwahisha futi sita ardhini!" Maneno yake yakazidi kupigilia misumari ya kuogopesha kwenye nyama za moyo wa Abednego. Akakaa vizuri na kuvuta pumzi ndefu. Akasogezewa maji ya kunywa na akayafakamia kwa pupa. Mara akasita na kumtazama Feruzi kwa ghafla, "Em subiri...ni kwa nini tusiwafahamishe polisi?" Akatamka. Feruzi akaonyesha kukata tamaa upya, "Sikia mzee...kama huyu mwamba amejua nilipo. Na akajua kuwa niko na wewe na akakutaja kwa jina bila kuambiwa na yeyote. Mpaka hapa unajua kuwa tunadili na mtu mwenye ubora kiasi gani Unadhani atasababisha maafa kiasi gani kama tukijidai kukimbilia msaada wa polisi?" "Aah sikia, sio polisi wote ni wa kuaminika hilo nalifahamu fika. Lakini wapo ambao ninaweza kuwaamini. Hao sina mashaka nao hata kidogo mdogo wangu niamini mimi!" Akatamka kwa sauti yenye msisitizo zaidi. "Enhe ni kina nani hao!" "Sikia mdogo wangu...misala ambayo mie nimepitia imenikutanisha na mamwela kibao sana. Na wote wakawa marafiki zangu kila niliposovu hio misala!" Akatamka kwa bashasha akimtazama Feruzi usoni akitarajia kuwa huenda atashtuka au kufurahia zaidi. Lakini Feruzi akabaki mkavu, amekauka kabisa. Tayari ameshakata tamaa. "Oa bro! Hii vita ni ya kwangu mimi mwenyewe, niachie mimi nitaimaliza. Polisi haohao walikuwa wananiwinda mtaani, unadhani ni kitu gani kitatokea kama nikijisalimisha kifalafala. Na wana ushahidi wa leso yenye damu! Oyah aisee. Achana naye huyo askari wako. Muhimu leo saa nne usiku niende pale Gymkana basi! Nikifikiria maisha ya jela naogopa sana mzeebaba." Feruzi akajibu kwa kirefu. Abednego hakuwa na jinsi badala yake akashusha pumzi ndefu na kuegama kwenye mgongo wa kiti. Wote wakabaki kimya kuisubiri saa nne usiku. Watimize agizo la kutisha. Agizo kutoka kwa jamaa mwenye kovu usoni! ********* Viwiliwili vya watu wawili vikaonekana kupishana na watu barabarani kwa kasi. Ikiwa ni usiku, walikuwa wamejivika mavazi yaliyowafunika barabara. Bila kusemeshana kwa muda mrefu, hatimaye mmoja wao akavunja ukimya ule.. "Oyah Feri eh!" Akamuita kwa sauti ya kunong'ona akihakikisha kuwa ni yeye na aliyeitwa pekee wanaweza kuisikia. "Niambie..." "Muda ule jamaa alikuita majina ambayo hata mi siyajui, yale ni majina yako kweli?" "Aa unamaanisha yale ya Adam?" Akauliza "Enhe hayohayo...ni yako kweli au alikubambikizia tu." "Yale ni yangu kweli kaka....ni majina yangu ya kuzaliwa kabisa!" "Kulikoni sasa mpaka huyo jambazi ayajue halafu sie wanao huku kitaa eti hatuyajui?" Akamswalika huku akihakikisha kuwa kasi ya miguu yake na ile ya Feruzi iko sawa, hawaachani kwa hatua kubwa. "Kwani kuna siku mshikaji yangu yeyote alitaka kuyajua majina yangu matatu?" Feruzi akamjibu kwa swali. Na Abednego akaguna kukataa "Nadhani mpaka hapo jibu unalo...jamaa alitaka kuyajua yote kabla hajaniua na nikamwambia." Wakiwa katika maongezi yao, wakamulikwa na mwanga mkali wa gari jeusi ambalo halikufahamika kama linadai kupishwa njia au la! Maana mwanga wake uliongezeka kwa ghafla na dereva wake wala hakujishughulisha na kupiga honi. Ni heri basi kama angepiga honi ili wafahamu kama wanahitajika kumpisha au la. Hata hivyo licha ya barabara ile kiwa ndogo kiasi, vijana hawa walitembea pembezoni na kuacha uwazi mkubwa ambao bila shaka ungetosha kabisa kwa gari lile lipite. Mwanga ule ulikuwa ni adui namba moja kwao, wakaukwepa na kujisogeza pembezoni zaidi ili kulinda utambulisho wao ambao, hawakutaka kuonekana ovyo. "Alaa huyu fala naye vipi aisee?!" Abednego akang'aka kwa sauti ya chini. "Mtu akiwa na gari anaweza kukufanyia kila aina ya manyanyaso bro. Unaweza dhani anaingiaga chooni na gari..." Feruzi akanong'ona kisha akasonya, akataka kutamka sentensi kisha ghafla akayqmeza maneo yake. Sentensi ile ilimkumbusha namna alivyoingia majaribuni. Alitaka kusema, "Tutafute hela aisee..." Gari lile jeusi likawapita kwa kasi na kutangulia mbele yao kisha likapunguza mwendo ghafla na kusimama. Likapindisha matairi yake na taa za nyuma zikawaka rangi nyekundu, likageuka kwa madaa na kuanza kutambaa likirudi nyuma kiupandeupande. Kisha likageukia upande lilikotoka likiwatazama na kuwamulika upya Feruzi na Abednego ambao walifanana karibu na mtu na mdogo wake kimaumbo. Wakafunika nyuso zao na kusimama. "Oa bro...nd'o wenyewe hawa au vipi?" Feruzi akauliza. "Mmh hata sijui, lakini we shusha hio kepu yako ikufiche. Halafu naanza kunusa hatari hebu tembea tutoke hapa haraka!" Abednego akamjibu na wakaongeza mwendo kulielekea gari. Safari hii wakakaa pembezoni mwa barabara mbali kabisa na upande wa gari lile. Gari lilisimama lakini lilisikika likiunguruma taratibu likiwa limewasha taa zake full light! "Mmh labda ni wenyewe bro." Feruzi akazidi kutangaza makisio yake. "Maelekezo ni kukutana Gymkana. Na sio hapa mjini kati. Usiwe mbishi!" Abednego akabadilika. Wakaongeza mwendo. Lakini Abednego hakuyaondoa macho yake kwenye namba za gari lile, akazitazama na kuzikariri kwa umakini. Ikiwa ni saa tatu na dakika hamsini na mbili usiku. Wakiwa hatua chache kabla hawajafika eneo la Gymkana, simu ya Feruzi ikaita. Akaitazama na akasoma jina la mtu aliyempigia, alikuwa Alinda. Akapata kigugumizi cha kupokea au kutoipokea simu ile. "Nani huyo?!" Abednego akauliza. "Ni mpenzi wangu..." Akajibu kwa wasiwasi kisha akaongezea, "Vipi nipokeee? Make itakuwa mara ya mwisho kama sita-" akakatishwa. "Mm dogo sikia...hatuna muda wa kupoteza muda kabisa. Yaani nikupe mda wa kubebika na demu wako na ukiangalia hakuna jipya ambalo mtazungumza zaidi ya kuahidiana mambo yasiyokuwa na msingi." Akamnyakua Feruzi simu ile na akaikata kisha akaitia mfukoni mwake. Feruzi akaachwa na sononeko kubwa. Kwa mbali kutokea nyuma wakamulikwa na mwanga wa gari lililokuja kasi na kutangulia mbele yao kisha likasimama kwa ghafla. Abednego akawahi kusoma namba zake na kugundua kuwa lilikuwa ni gari lilelile la mwanzo. Milango ya gari lile ikafunguliwa kabla hawajakatoka vijana wawili walioonekana kuwa na maelekezo fulani. Wakapiga hatua na kuwasogelea Feruzi na Abednego waliokuwa wamesimama kwa tahadhari. "Nadhani ni nyie tulioagizwa kuja kuwapokea!" Akatamka mmojawao. "Tuokoe muda , gari ni lile pale. Sio muda rafiki kukaa uraiani huu." Akaongezea. "Aliyewaagiza ni nani?" Abednego akawauliza. Vijana wale wakatazama kisha kwa kusita mmoja wao akajibu, "Jina lake hatulitaji ovyo ovyo! Ni nuksi sana kulitaja." Feruzi akamnong'oneza, "Ni wenyewe hawa nilikuambia tangu muda ule." Abednego hakujali akaendelea kuwashambulia kwa maswali, "Na kwa nini mlikuwa mnatuzonga zonga njiani tangu muda ule?" Swali lake lilikuwa jepesi na liligitaji jibu jepesi pia. "Tulitaka kudhibitisha kama ni nyinyi kweli.." wakajibiwa. Ukimya wa sekunde kadhaa ukapita. "Oyah tunachelewa wazee!" Akafoka mwingine aliyekuwa ndani ya gari lile kwenye siti ya dereva. Feruzi akapiga hatua moja mbele na kutazamana na Abednego akamshika begani kwa namna ya kumtuliza kisha akamwambia, "Bro...acha niende kujikomboa. Naahidi sitakuja kama nilivyoenda. Naenda kumaliza haya mabalaa niliyoyaanzisha mimi mwenyewe." Akasihi. "Mungu akutangulie.." akajibiwa kwa ufupi. Feruzi akapiga hatua na kulisogelea gari lile kisha akazana ndani akifuatiwa na vijana wale wawili. Milango ikafungwa na gari likaondoka kwa kasi likitimua vumbi nyuma yake. "Alisema ataagiza kijana wake...lakini hawa waliokuja ni vijana watatu." Abednego akajisemea akiwa na mzigo wa mashaka kwenye akili yake. Akatazama muda kwenye simu yake, ilikuwa saa nne na dakika kumi. Akavuta pumzi na kuendelea kutembea kama kawaida akirudi nyumbani kwake. Simu ikaita na akagundua kuwa alisahau kumpatia Feruzi simu yake, na namba iliyopiga muda huu ilikuwa ngeni. "Duh! Jamaa kaniachia kidogoli chake bwana!" Akaamua apokee ili amjulishe mpigaji kuwa mwenye simu yuko mbali. Kabla hata hajasalimia akapokelewa kwa sauti iliyokuwa inalalamika. "Bwana Kagoye! Mko wapi mpaka sasa hivi? Kijana wangu mmemfanya kitoweo cha mbu akiwasubiri nyie huko alipo kwa muda mrefu!" Ajabu! Ilikuwa ni sauti ileile nzito iliyowapa maelekezo asubuhi. "Vijana wako mbona wamemchukua muda sio mrefu? Nadhani wanapepea kwenye gari lao kukufikia huko ulipo kiongozi" Akajibu kwa kujichekesha chekesha akidhani kuwa amejiweka mbali na hatia ya kumchelewesha Feruzi eneo lile. "Vijana? Vijana wangu ni wangapi? Mimi sijaagiza gari wala watu wengi. Usitake kunifanya niamini kuwa umemuuza Adam kwa hawa watu!" Sauti ile ikakoroma. Hamadi! Hakuna maelezo ya ziada ambayo angeyatoa Abednego akaeleweka kwa muda huo. Akaishusha simu kutoka sikioni mwake na kuikata mara moja. Mwili umezizima na damu ikamchemka kwa kasi. Feruzi alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana. Makosa! ----------‐—‐---------- Pilau limeanza kuiva huku jamani... Tualikane kuja kulionja. Sambaza link watu waje kwenye chaneli yetu, Raha ya pilau, liliwe kwenye sinia. TUKUTANE JUMAPILI
👍 ❤️ 👏 🔥 5

Comments