
MAJIVU YA FASIHI 📖🪶
1.4K subscribers
About MAJIVU YA FASIHI 📖🪶
MAJIVU YA FASIHI ✍🏿 Ni kituo kinachokuletea burudani na elimu kupitia fasihi andishi. Karibu tufurahie; 1. Visa na hadithi 📖 2.Riwaya📚 3.Uchambuzi wa filamu🎬🎞 4.Makala mbalimbali (Michezo, Sayansi na maisha)📃 Vyote katika lugha adhimu ya kiswahili... @Kalamu_ya_kabati @Chivihi's son
Similar Channels
Swipe to see more
Posts

RIWAYA; *KIBIRITINGOMA* MTUNZI; *GODLOVE KABATI* KWENDA KWA; *MAJIVU YA FASIHI channel* WhatsApp; 0763204351 ----------------- *Sikia,* *Tafsiri sahihi ya wewe kuwa na umaarufu, ni kujulikana na watu wengi ambao wewe huwajui.* *Haijalishi wanakujua kwa mema ama mabaya. Lakini daima tambua kuwa, kwenye wengi kuna mengi.* *Zichunge sana nyendo zako ewe supastaa mwenzangu.* *Ni kosa moja tu linaweza kuyafuta mema tisini na tisa uliyoyafanya.* *Nakuandikia haya katika sehemu hii ya kumi na nne.* Siku zilitembea kwa kasi sana kama mshale hewani. Ndani ya wiki moja baada ya makubaliano ya ana kwa ana baina ya Bebe na msanii Kenzy, hatimaye mtandaoni lilitupwa jiwe jipya lenye mshindo mkuu, ulioyatikisa masikio ya watanzania. FROLA ATAKUWEPO KWENYE NGOMA MPYA YA KENZY FLAVOUR! Hii haikuwa taarifa rasmi, bali zilikuwa tetesi tu. Tetesi hizi zikatambaa kwa kasi kama moto mkubwa nyikani. Macho na masikio ya watanzania wote wapenzi wa Bongo fleva vikakaa chonjo kusubiri. "Acha utani bwana!! Kwamba Frola huyuhuyu, atakuwa video queen kwenye ngoma mpya ya Kenzy?" "Sa' hapo unabisha nini mzee? Unaambiwa Kenzy flavour amemwaga mpunga wa kutosha kaka. Majuzi tu kamera zimewanasa pale Sheraton wanashoot! We unacheza na media nini?" Yalikuwa ni maongezi ya vijana wawili wa rika moja, wakipata mlo wa mchana kwenye moja kati ya migahawa, uliokuwa karibu na chuo chao. Wanakula chakula, vidole vya mikono yao ya kuume vikikamata vijiko kupambana na punje tamu za wali mweupe. Huku vile vya mikono yao ya kushoto vikipapasa vioo vya simu zao. Macho yao yanazidi kupepesa wakikagua kinachojiri kwenye kurasa mbalimbali za mitandao. "Kama ni kweli, basi hili dude litakuwa na bonge moja la video aisee!" "Ooh ooh, Bro! Hii *Me and you* itakuwa ni dunia nyingine." Wakamaliza kupashana habari na kuendelea kuufaidi uhondo wa kile kilichoko kwenye sahani mbele yao. Dunia ya muziki, ikaisubiri kwa hamu kubwa ile tarehe ya kuachiwa kwa video ya wimbo huu mpya wa msanii Kenzy Flavour. Kuhusu ubora wa uimbaji wake, hilo halikuwa suala la kushangaza. Tayari alishafanikiwa kuziteka nyoyo za mashabiki wake wengi tangu walipompa masikio yake. Suala kubwa muda huu lilikuwa ni kuitazama video ya wimbo huu ambao ilisemekana kuwa yule mrembo maarufu nchini Tanzania, yumo ndani. Mrembo ambaye anajulikana mpaka na watoto wadogo kila wanapoyaona makopo ya *icecream* yaliyopambwa na sura yake. Siku ya siku ikawadia. Lile jiwe la kimondo cha *Me and you* lililohaidiwa, likatupwa mitandaoni. Safari hii haikuwa tetesi tena na hakuna aliyetaka kusimuliwa. Mitandao ya kijamii ikafurika. Watu wakateketeza masalio ya vifurushi vyao vya intaneti ili tu kutazama kunani? Maajabu, Ndani ya lisaa limoja tu, takribani watu milioni moja na ushee walikuwa wamezipepesa mboni za macho yao kwenye ukurasa wa msanii Kenzy. Rekodi mpya ikaandikwa nchini Tanzania katika mtandao wa *Youtube* . Msanii wa kwanza Afrika mashariki, kupata watazamaji wengi ndani ya muda mfupi. Mafanikio! "Bro siamini macho yangu aisee!" Kenzy flavour alikuwa wima, mikono yake inamtetemeka viganja vyake vinamiliki simu yake. Anachokiona haamini kama ni kweli kinatokea. Amewahi kupandisha video za kutosha, tena zenye mawe ya maana kwelikweli. Lakini hii ilikuwa ni kubwa kuliko. Haelewi afanye nini. Ni kama anayetaka kupaa na kukimbia kwa wakati mmoja. Anazunguka huku na kule kwenye sebule yake ya kifahari. Mara anaitupa simu ile na kumrukia rafiki yake aliyekuwa karibu kwa shangwe. Ni furaha tupu! Haya ni mafanikio makubwa kwake katika tasnia hii. Yupo kwenye kilele cha furaha yake. Upesi anawasiliana na Bebe, na kumshirikisha juu ya hili. Ni furaha na burudani mara mbili kwa wale wanaosimuliana hadithi za urembo na madaha ya Bebe kwenye video ya wimbo huu. Wimbo wenye mashairi matamu ya mapenzi yenye mchanganyiko wa kiingereza na kiswahili. Anga la nchi ya Tanzania, likahanikizwa kwa mrindimo wa sauti za wimbo huu. Umaarufu wake ukatishia kuuweka kwenye daraja moja na wimbo wa taifa. LE CLUB GRANDE, ukapigwa usiku na mchana. Ukamfikia mpaka Madam Sally na mabinti zake ambao waliufurahia japo kwa matamanio makubwa ya kuipata nafasi kama ile aliyo nayo Bebe. Mitandao haifichi kitu, wimbo ukapigwa mpaka kwenye vipindi mbalimbali vya runinga. Ukaifikia familia ya Bwana Didas. Watoto wake wakaufurahia, wakajitahidi kuyakariri mashairi yake, mke wake akayatumia mashairi haya kumliwaza mmewe. Lakini yeye bwana Didas aliutazama wimbo huu kwa uchungu, roho yake imechafuka kwa kisirani, wivu na hasira. * * * * * * Jukumu la mashabiki siku zote ni moja tu. Ama ni mawili kwa hakika. Kusifia na kupiga makofi pale panapostahili pongezi vilevile kukosoa na kukemea pale panapohitaji kukosolewa. Baada ya makofi mengi kupigwa na sifa kedekede kujazwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii kuhusu wimbo huu mpya wa msanii Kenzy Flavour, ghafla likaibuka kundi la wale mashabiki wenye macho ya mwewe yanayotazama na kufanya uchambuzi wa umakini zaidi. Hawa wakayafuatilia kwa umakini zaidi yale makumbato, ile mipapaso na miguso kwenye video hii...kisha wakarejea na mawazo mapya ambayo abadani hayakutegemewa. Mawazo haya yaliyobeba hoja mbalimbali, yakaibua mijadala kwenye makundi mbalimbali ya udaku kwenye mitandao ya kijamii. Wimbi kubwa la wale wanaokesha kujadili maisha ya wasanii, wakaipenda mada iliyosogezwa mezani. Vikao visivyo rasmi vikaanzishwa. :Sanaa imeingiliwa! :Kenzy hakufanya makosa kabisa, alihakikisha hela yake haiendi burebure. :Alimkamatilia kwelikweli aisee. :Duh! Kwa namna alivyokuwa anampiga tachi, sidhani kama yule manzi alitoka salama. Mijadala hii ikaibua hoja ambazo ni kama zilikuwa zinasubiriwa kwa hamu na kiumbe fulani aliyekuwa nyuma ya kioo cha kompyuta yake, ndani ya chumba chake chenye giza la wastani. Kiumbe huyu akatabasamu kisha kwa utulivu mkubwa, akaendelea kunukuu machache kwenye kitabu chake kidogo chakavu kilichokuwa kando. Akaendelea kusoma yanayoendelea huko mitandaoni. :Aaaah wasanii hawa kawaida yao hawa! Tumeshawazoea! :Kwanza huyo Frola si inasemekana aliwahi kufanya kazi pale LE CLUB GRANDE? Au kumbukumbu zangu haziko sawa? :Uko sawa mkuu, miaka ya nyuma aliwahi kufanya kazi pale. :Kwa hio flavour kapita naye? Ila wabongo, hampoi :Naipenda nchi yangu, kila siku skendo mpya. :Huenda hii nchi ni chaneli ya vichekesho huko mbinguni. Maoni haya lukuki yakazidi kuipeleka mada hii kwenye uelekeo ule ule, aliokuwa anautaka. Kiumbe huyu alikuwa mtandaoni muda huu pia, japo kwa akaunti isiyo rasmi. Kwa maana hiyo, isingekuwa rahisi kujulikana na vyombo vya usalama. Kwa kujiamini akavielekeza vidole vyake juu ya kompyuta ile na kuzicharaza herufi, :Kwani bado tu hamjaona koneksheni yao? Akauliza swali lililozua kizaazaa. Neno koneksheni, kama lilivyotumika mitandaoni kumaanisha video chafu za ngono zinazorekodiwa kwa makusudi ama kimakosa. Watu waliomuelewa wakamshukia kwa maombi na vingi viulizo, ikiwa ni kweli kitu kama hicho kipo. :Mnadhani natania? Haya huyu nani? Akatuma picha, ambayo iliwashangaza wengi. Ni Bebe akiwa na Kenzy, miili yao ikiwa ndani ya mavazi mepesi ya kulalia. Wamekumbatiana na tabasamu zito la huba likitalii nyusoni mwao. Picha hii inaelezea kila dalili ya wawili hawa kuwa ndani ya chumba kimoja, hotelini. Baada ya sekunde sitini akaifuta picha hii. Ilikuwa picha ya kipekee, picha ambayo kila aliyejaribu kuipakua alishindwa. Waliofanikiwa kuiona upesi wakawaka kwa shauku ya kutaka kuiona tena. Lakini isivyo bahati, ilionwa na wachache. Wakamlalamikia kwa kitendo chake cha kikatili kwa kutundika picha na kuifuta upesi. :Mnadhani ni nini kiliendelea baada ya hapo? Akatupa swali jingine. Watu wakazidi kumshambulia kwa maswali na kudai udhibitisho wa ziada ambao hakuutoa. Wengine wakaifatilia akaunti yake kumchunguza. Mtu huyu ni nani? Hakuwa wafuasi wengi mtandaoni. Lakini kitendo chake alichokifanya dakika kadhaa nyuma, kikampatia umaarufu wa ghafla. Naam, jina la ukurasa wake aliouita kwa jina la MUTU MWEUSI ukawa gumzo kwenye mtandao huu. Mafuriko ya jumbe nyingi kutoka kwa watu mbalimbali yakammiminikia, wakimsihi awatumie picha na video hizo kwenye akaunti zao binafsi, kama ikiwa ni kweli anazo. Kiumbe huyu, akatabasamu baada ya kuiona fursa. Namna ambavyo wanadamu wanalalamika kutaka kuziona tupu za wanadamu wenzao wakifanya zinaa. Wana nini watu hawa? Tamaa! Tamaa ya ngono. Macho yao yenye tamaa yanang'aa kwa uchu yakidai shibe kwa kuangalia video hizi chafu zinazojulikana kama *koneksheni* huko mitandaoni. Watu hawa wanaabudu fedheha kuliko utu. Kiumbe huyu, J4 akashusha pumzi na kuchepuka kutoka mtandao ule, akaunti yake feki ikayeyuka na kusinzia ghafla. Akaifunga kompyuta yake na yeye akakisogelea kitanda kuutafuta usingizi wake. Mtego wake umenasa tayari. Mwanzo wa usingizi wake mtamu, ukawa ndio kengele ya kuwaamsha wale wanaokesha mitandaoni usiku kucha. Linalotafutwa ni jina moja, ama mawili hakika lakini ya mtu mmoja. Mtu mwenye *koneksheni* ya Kenzy na mrembo Frola. Kampuni za mitandao zikapata wateja lukuki mida hii. Wateja wanaomtafuta mtu mmoja tu. *MUTU MWEUSI* !!! ******* Baada ya kazi ngumu ya kurekodi na mahangaiko ya uandaaji wa video ya wimbo huu, kila mtu alikuwa tepetepe kwa uchovu. Bajeti iliyotengwa kando na Kenzy, ilitosha kabisa kukodi vyumba kadhaa vya hoteli kubwa kwa ajili ya mapumziko ya kundi lote linalohusika na uandaaji wa kazi hii. Ni katika namna ambayo hakuelewa ilikuwaje, na wala hakukumbuka alifanya nini. Lakini alijikuta yeye na Bebe, wameamua kupumzika kwenye chumba kimoja. Achana na chumba, hebu tuongeze ukali wa maneno kidogo. Walipumzika kwenye kitanda kimoja. Yumkini kwa Bebe hili lilikuwa ni pumziko la kawaida. Lakini kwa Kenzy hii ilikuwa ni kama nafasi moja ya kipekee inayojitokeza kila baada ya miaka elfu. Nafasi ya dhahabu! Nafasi ambayo hakutaka kuipoteza kabisa. Kulala na mrembo kama huyu kwenye kitanda kimoja? Maajabu! Pumziko hili likaanza kupata uhai baada ya ngozi za miili yao kugusana. Kila mmoja akalihisi joto la mwenzie. Wakabadilishana joto hili na damu kwenye mishipa yao ikaanza kuchemka. Hisia kali ikasafiri kwenye mishipa hii kwa kasi. Yule Frola, akabadilika ghafla na kuwa Bebe tuanyemfahamu sisi. Bebe aliyehitimu chuo cha Profesa madam Sally. Na sasa huyu hapa yuko kazini. Masomo kwa vitendo bwana! Ghafla wakachangamkiana. Wakausahau ule uchovu wa siku nzima uliowafanya wapumzike. Haoooo, kukurukakara, vuta n'kuvute, wakatapatapa huku na kule. Dakika thelathini za mahangaiko zikahitimishwa kwa usingizi mzito wa Kenzy Flavour, msanii wa kizazi kipya anayetegemea kuachia ngoma yake hivi karibuni. Huku Bebe akiwa nd'o kwanza amechangamka. Hii michezo ana uzoefu nayo. Na hapa alikuwa uwanja wa nyumbani. Mashahidi wa tukio hili walikuwa na ahadi moja tu. Kubaki kimya milele. Japo sio wote ambao wangeitimiza ahadi hii. Wapo waliokataa katakata kubaki kimya. Na ni hawa ambao walimfanya Bebe asipate usingizi. Binti akasimama baada ya kuhakikisha kuwa Kenzy amelala usingizi wa pono. Akanyata taratibu mpaka kwenye pembe kadhaa za chumba kile na kunasua vipande vidogo vya kamera kwa uangalifu. Akavitunza mahali salama na kisha akaikota simu yake kufanya mawasiliano na namba ambayo alijua tu kuwa iko hewani kusubiria majibu. DEAL DONE, akaandika. BRAVO, akajibiwa. Akazima simu yake na kurejea kitandani kuubembeleza usingizi. Roho yake ina amani na anauona ushindi mkubwa mbele yake. Mtego umenasa! _____________________ Aiseeee 😀, Mitego imenasa! Mitandao imechafuka. Ngoma ya *ME AND YOU* inazua taharuki ambayo sidhani kama itamuacha mtu salama. Ni hekaheka! Tumekuwa familia kubwa sasa, watu Alfu si haba. Haya sasa raection zenu zimwagike hapa. Nahitaji thelathini tu, tuendelee Alhamisi hii. Riwaya ya bure hii jama... 30 kati ya 1000. Na hapa mshindwe kweli? 🥱


Yule paka mweusi niliyempiga mawe na kumuua ndotoni, amezua kamzozo. Nimeamka asubuhi ajuza wa mtaa wa pili amekuja kwa baba mwenye nyumba akihitaji kuniona 🥺. Nilisikia koridoni wakizungumza _"Huyu kijana wako amemuua paka wangu usiku wa jana"_ ajuza akiongea kwa ukali. _"Ni nani kati ya hawa?"_ mwenye nyumba aliuliza. _"Ni huyu, chumba cha kwanza hapa"_ Huyu chumba cha kwanza hakuwa mwingine ni mimi tu! Moyo ulianza kutweta kama gari moshi ya wakoloni... Hofu ilinitawala, muda huo sikusikia chochote zaidi ya mazunguzo hayo. Akili ilinishauri kuufikia mlango wangu. Nilijishusha taratibu kutoka juu ya kitanda, nikaenda kushindilia komeo mbili za juu... maana alfajiri nilitoka kwenda maliwato mlango niliegesha tu, sikuufunga... ile nafika tu mlangoni nakutana uso kwa uso na sauti za kubishwa hodi... ndii ndii ndii. 🥶 Shoti iliburuza pande nne za moyo [woga..] Nilijituliza huku nikitetemeka miguu kama mbuzi mcheza kiduku... kimya, nikitafakari ni nini cha kufanya. Nilijikausha sikuruhusu kupumua hata kidogo. Niliwaza pengine watajua kama nimeamka.. mgonga mlango hakuchoka aligonga moja takatifu kama mabomu ya gongo la mboto `Paa!! Paa!!..` huku akitingisha kitasa... aii!! Niliruhusu milango ya fahamu kufanya kazi yake waaah!!!! Mavumbi yalinitoka... hapa nilijua tu mlango ni lazima ufunguke..🥺 [balaa]... _"Huu mlango ukifunguka na hii hali niliyonayo itakuwaje?"_ Nilijiuliza sikupata majibu ya maana. Hapa nilikuwa na kiboxa, pembeni askari wangu alisimama imara kushambulia yeyote atakaye thubutu kufungua... _"Huyu kijana anadharau sana, unadhani hasikii kelele hizi?, ila anajikausha tu!"_ ajuza yalimtoka ya moyoni. Hapa ndipo nikajua kuwa anayegonga huu mlango ni baba mwenye nyumba.. nilirudisha shingo pembeni nikapaza sauti nikijifanya natoka kwenye usingizi mzito. _"Nakujaaa"_ _"Ndo kinajifanya kujibu saa hivi, yani huyu paka atamlipa tu!"_ Nilisikia kauli za kibabe zikimporomoka ajuza wa watu.. Hapa nilijitutumua liwalo na liwe nikiwaza cha kujibu hii kesi maana haikuwa kesi ya kawaida. Nilivaa traki yangu nyeusi pana na koti la mlinzi, miwani na kofia, pembeni kulikuwa na rungu nikalibeba. Yani nilijiandaa kukiwasha kama kitanuka.. nilisogea mlangoni na kuufungua, nilifungua huku nikiogopa... nikachomoza kichwa tu koridoni kama mjusi kenge... 🌚 nilimuona ajuza akiwa ametuli ananitazama kwa macho ya ushakunaku.... _"Lione kwanza baya, embu jitokeze huko muuaji mkubwa wewe"_ kauli ya kuchukiza kinywani mwa ajuza ilinipandisha morari. Nikatoka chapu, nikipandisha mori kama masai wa njiro. Hapa sasa nilitoka na vile vifaa vya kazi yani nilibeba rungu na ile traki niliyovaa ni wazi niliwahi kukimbia mgambo. Ajuza alianza kigugumizi cha woga kilimjaa kinywani.. _"Ah... a.. babu.. sio wewe bana.. iii..ta ..kuwa tumekosea chumba"_ 😹💔 nilikaza macho nikiwatazama.. _"Kwani vipi?"_ mwenye nyumba alitoa kauli ya mwisho _"Basi hakuna kitu, si umesikia hapa kumbe sio wewe bwana"_ nikazama ndani huku nikichekea tumboni. _Kwi!! kwi!! kwi!! kwi!! kwi!!_ __________________ `HAPA NDIO NIKAJUA UKIWA JASIRI HAKUNA KITAKACHO KUZINGUA. YANI HATA UKALI WA SIMBA MWITUNI UNATOKANA NA ULE UJASIRI WAKE.` Wewe ni shujaa ukizidisha ukali fulani. 🖊️📖 [It ends where it all began]. _@chivihi's_son writer._ #ŰNOWAY Author. 📖🖊️ 💕 🫰 Call: 0621885257


*PAZIA LA FILAMU* 📽🎬 *`IO CAPITANO`* (2023) Ni kweli kuwa njia ya kuyafikia malengo na kuzitimiza ndoto zetu imejaa miiba, suluba na mateso ambayo hatuna budi kuyavumilia. Pia ingawa ni mara chache sana njia za mkato hujitokeza, sio salama kuzitumia ili kufikia kile tunachokilenga. Haya yote yalizingatiwa kwa moyo na vijana wawili, Seydou na Moussa. Vijana waliokulia katika familia zilizoendelea kusota na kuwa mateka wa umasikini wa kudumu. Walikuwa masikini lakini walikuwa na furaha. Furaha ambayo ilidumisha upendo na amani kwenye maskani yao. Walijiona matajiri kila walipokaa pamoja, kula, kunywa na kucheza ngoma za kiasili pamoja. Umoja wao ukaipiga teke fikra ya umaskini kwenye bongo zao. Wengine wote waliridhika...wote, isipokuwa Seydou na Moussa binamu yake. Kutoridhika kwao, ndiko kunaifanya filamu hii iwe moja kati ya zile *bora za muda wote*. Kulikoni? Songa nami 👇🏼. Ni ubora wao tu, katika kutunga na kuimba mashairi ya nyimbo mbalimbali. Ama kwa lugha rahisi waweza kuwasifu kuwa walikuwa na kipaji. Naam, walikuwa na talanta ya kuimba. Kipaji chao kikawaaminisha kuwa, wanaweza kuyaandika majina yao kwa wino wa dhahabu kwenye mioyo ya kila sikio la shabiki atakayesikiliza nyimbo zao. Sio hapa Afrika tu...hata Ulaya! Eeh hata Ulaya! Wakaamini kuwa hata wazungu watapanga foleni kuzililia saini zao. Vipaji vyao vikawaaminisha hivyo. Wakaendelea kuvinoa. Kwa desturi, kipaji humtesa sana mwenye nacho. Huwaka na kuteketea nafsini mwake kama moto mkali. Humfanya mtu ajihisi kama mwenye deni kubwa maishani mwake. Naam, Talanta yao, ikawafanya Seydou na Moussa wasilale usiku na mchana. Ikawafanya wasote na kupitia suluba, kufanya kazi na kutunza fedha kwa muda wa miezi sita. Lengo lao? Wapate fedha itakayowatosheleza kwa safari yao kutoka Senegal mpaka Ulaya. Wakiwa chini ya ule umri wenye ruksa ya kutumia vileo, wakaweka nia ya kusafiri kwenda Ulaya kwa njia haramu. Hawakutaka kumuaga yeyote maana kwa hakika wasingeruhusiwa na wazazi wao. Na hawakutaka kitu chochote kiwazuie. Wakakwepa baraka za wazazi na walezi wao na badala yake wakazikimbilia baraka za Sangoma. Mganga ambaye alipeperusha usinga wake huku na huko, akinena maneno ya kilugha yasiyoeleweka. Kisha akaibariki safari yao. Seydou na Moussa wakatoroka nyumbani kwao wakiwa na matumaini na heri nyingi ya kule waendako. Taratibu, wakaanza kuipasua ramani kutoka Dakar, Senegal kuelekea Kaskazini. Njia za magendo na usafirishaji haramu wenye unafuu wa nauli na uhakika wa kufika kule wanakoelekea, vikazidi kuwaaminisha kuwa safari yao bado ni salama. Ni noti kadhaa tu zilizotosha kuvifunga vinywa vya askari wa mipakani waliodai rushwa. Ama la uende kuozea jela. Nani anataka jela? Wanatoa noti kadhaa na kubaki salama kuendelea na safari yao. Usalama huu mpya, katika nchi za kigeni ukaungana na shetani kama abiria mpya kwenye safari yao. Barabara kwa barabara, mipaka kwa mipaka, kituo kwa kituo. Hatimaye wakapata usafiri wa bei cheee, utakaowafikisha Tripoli, mji mkuu wa Libya. Usafiri ambao utawaepusha na manyanyaso ya jangwa la Sahara. Ni hapa mambo yalipoanza kubadilika. Shetani akachanua makucha yake, na matumaini yao yakaanza kuyeyushwa na lile joto kali na jua lililokasirika la jangwa la Sahara. Askari jeshi, walinzi wa jangwa wakauvamia msafara wao haramu. Wakadai fedha na mali zao, huku wakiitanguliza sheria mbele kama kitisho cha kuwasweka jela. Seydou akapona..lakini Moussa akakamatwa kupelekwa jela. Dhuluma hii iliyofanana na haki, ikawatenganisha ndugu hawa wawili waliokuwa safarini. Yumkini Seydou aliwahi kusoma kuhusu historia na hadithi za enzi za utumwa darasani. Yale yalikuwa ni nadharia tu, na sasa alikuwa kwenye mafunzo kwa vitendo. Alianza kama msafiri jangwani, ghafla shilingi ikageuka, akawa mtumwa. Macho yake yakashuhudia hatua zote anazopitia mtu, anapoelekea kukata roho. Ukatili unaofanywa na mwanadamu juu ya ngozi yenye madonda ya mwanadamu mwenzake. Aliona, aliogopa, alitishika! Ali-ililia chai na sasa ilikuwa inamchoma kwa joto lake. Seydou kwenye gereza la siri, katikati ya jangwa la Sahara Libya. Aliyafumba macho yake, akaikumbuka amani aliyokuwa nayo kwenye udongo wa nyumbani kwao. Ni kama malaika mtoa roho alikuwa anarandaranda karibu yake, kumsubiri amalize mkataba wake wa maisha na dunia. Akatamani walau aombe msamaha kwa mama yake, kabla hajaiaga dunia. Labda ndotoni pekee, huko ndiko angewasiliana na mamaye. Kijana wa miaka kumi na sita tu kwenye uso wa dunia, akakomazwa na maisha. Akautafuta ukombozi katika nchi za kigeni. Baada ya kubahatika kuukwepa moto wa mchanga jangwani...anakutana na mawimbi ya mauti yanayoelea kwenye mdomo mpana wa bahari ya Mediterranean. Ni filamu ambayo itakupa kila sababu ya kukijali ulicho nacho, na kukuasa kuepuka tamaa mbaya. Huku, ukipata ufahamu juu ya ukatili wa usafirishaji haramu wa binadamu. Inaitwa *Io Capitano* ya mwaka 2023. Hii nd'o maana halisi ya bonge la filamu. Imeandikwa na Godlove Kabati ✍🏼


Hayawi hayawi, Sasa yamekuwa! Baada ya kusubiri kwa muda mrefu, sasa rasmi nakala ya riwaya yetu ya *SHAMBA LA HELA* iko sokoni. Ni kitabu kilichosheheni taharuki, mapigano na nukta kadhaa za upelelezi na hekaheka ndani ya kurasa zaidi ya 350. Ni kisa cha kusisimua kilichosukwa na kalamu ya yuleyule fanani wenu, GODLOVE KABATI. Inapatikana katika mfumo wa nakala laini kwa bei ya Tsh. 2000/= tu. Nambari ya malipo: 0678204350 (MIXX BY YAS) Jina, GODLOVE KABATI SELESTINE Ukilipia tu, niarifu. Nami sitosita kukutumia kazi hii bora ya fasihi 🙏. Kwa maelekezo zaidi, wasiliana nami kwa njia ya WhatsApp kupitia 0763204351. *`FASIHI NDIO ZETU`* 📚📚


Jama mnamkumbuka Ferouz?... Eeh yule Ferouz Adam kinyozi... Aliyeenda kutafuta pesa, akakutana na mabazazi... Kutoka hapo...tukapata riwaya bora ya hiki kizazi... 🤭 E bwana eeh! Riwaya ya *SHAMBA LA HELA* itakamilika Ijumaa hii. Itakuwa kwenye mfumo wa nakala laini yaani PDF. Ni riwaya ya hekaheka, mapigano na mavarangati... Ni msitu wa maneno zaidi ya *Elfu hamsini na moja* kwenye kurasa zaidi ya 350. Ni kalamu ya yuleyule fanani wenu Godlove Kabati. Kwa nini uikose kazi hii adhimu?


RIWAYA; *KIBIRITINGOMA* MTUNZI; *GODLOVE KABATI* KWENDA KWA; *MAJIVU YA FASIHI channel* WhatsApp; 0763204351 ----------------- SEHEMU YA KUMI NA MBILI *Kwa kuwa bado tunaishi ndani ya hii dunia..* *Hakika ipo siku moja isiyo jina, utakutana na mtu ama atakuja mtu mpya maishani mwako.* *Huyu ataubadilisha mwelekeo wa maisha yako...atakupa elimu mpya na changamoto ambazo hukuwahi kamwe kukutana nazo.* *Omba sana, mtu huyu mpya asilipeleke motoni jahazi la maisha yako...* *Hii ni sehemu ya kumi na mbili!* Zilipotea takribani dakika thelathini na tano, mpaka walipoukamilisha mlo wao katika hoteli hio kubwa waliokutana. Wakaziteketeza dakika nyingine ishirini kwenye mazungumzo ya hapa na pale huku wakiyasindikiza maongezi haya kwa vinywaji laini. Matumbo na nafsi zao zilipotosheka, ukawadia muda maalumu ambao uliwaweka katika hoteli hii mpaka muda huu. Bebe akaangaza macho yake huku na kule kuhakikisha usalama ambao tayari ulikuwepo. Kisha taratibu bila papara akainama na kuibuka na begi dogo mfano wa briefcase kutoka chini ya meza hii. Sanduku lililoonekana kuwa na uzito baada ya kujazwa vitu fulani fulani, akalitua juu ya meza ile, na meza ikaitika kwa kutoa mlio *TIIII!!* Naam, lilikuwa na uzito usiokuwa wa kawaida. Ni uzito ambao unahitaji dakika moja tu ya maajabu kumbadilisha mtu anayeonekana kama mwehu, aanze kuitwa chifu. Uzito wa fedha! Akalisukuma katika namna ya kuteleza kuelekea kwa J4. J4 ambaye alikuwa na mshawasha wa kuziona hizo milioni mia zilizomo. Akajisogeza karibu zaidi, uso wake ukiwa na shauku. "Mzigo huu hapo, ufungue!" J4 akasita na kumtazama Bebe usoni kwa macho ambayo ni kama yanamuuliza, "Una uhakika kuwa humu ndani kuna milioni mia?" Bila kutamka neno lolote, akayerejesha tena macho yake juu ya sanduku lile. Huenda huu nd'o muda pekee ambao J4 alihitaji kuwa mtulivu. Milango yake yote mitano ya fahamu ikaanza kufanya kazi sawasawa. Akainyoosha mikono yake tayari kwa ajili ya kulifungua. Akili yake ilikuwa tayari imelifungua sanduku hili na kukisia juu ya wingi wa mabunda makubwa ya fedha uliomo ndani yake. Na sasa alikuwa akienda kuyahakiki yale aliyokuwa akiyadhahania akilini mwake mubashara kabisa. Milioni mia! Alaaa, hii ilikuwa fedha ambayo hakika asingewahi kuimiliki mpaka atakapozama futi sita ardhini. Mikono inamtetemeka, J4 akavibetua vyuma vilivyolikaza sanduku lile. Kisha kama anayefungua mlango hivi, akalifungua sanduku. Hamadi! Pua zake zikapokelewa na harufu ya kipekee. Harufu halisi ya fedha kutoka sandukuni. Mboni za macho yake zikapanuka, macho yake yakaona, Safu za mabunda ya noti mpya nyekundu zilizonyooka zilijipanga vyema kama zimepigwa pasi. Bado haamini, mkono wake hakukutaka kubaki nyuma. Akaamua kuzigusa. Mkono wake ukatambaa na kuteleza juu ya noti hizi. Vidole vikakana kuwa havijawahi katu kuzigusa milioni mia moja. Akafanya kama anayechimba, akaibuka na bunda moja la noti zilizoviringwa ndani ya mpira mdogo. Akalitikisatikisa kama anayepima uzito wake. Akazichezesha noti kwenye ncha za vidole vyake kama anayezihesabu hivi. Ni noti mpya kabisa ambazo hazijapita kwenye mikono ya watu wengi. Uso wake ukawa wa mwisho kudhibitisha kuwa amefurahishwa sana na kile alichokikamilisha. Tabasamu likawaka usoni mwake, akamtazama Bebe usoni. Akaufungua mpira ule uliozidhibiti noti za bunda lile, zikawa huru. Akazitupa juu ya meza kumwelekea Bebe. Noti zikateleza mezani katika mfumo wa kusambaa. "Unajua tunaziitaje hizo?" J4 akauliza akiwa wima. "Zinaitwa hela!" Bene akamjibu kwa bashasha. "Lipe neno uzito...sema fedha! Kama wasemavyo wao." J4 akarejea kwenye kiti. Akauinua mguu wake wa kulia na kuubebanisha juu ya paja la ule wa kushoto, akakaa kwa kuchonga namba nne. "Ni burudani sana kutazamana na utajiri uso kwa uso. Na leo nimepata bahati ya kuipata burudani hii bure kabisa. Kwa nini nisiburudike?" J4 akatamka huku akilifunga upya briefcase lile. Bebe akacheka kidogo huku akiuziba mdomo wake kwa aibu. "Haya nd'o maisha tunayotakiwa kuyaishi Bebe!" J4 amemaliza kulifunga sanduku lile na sasa anafanya jitihada ya kuzikusanya fedha zile alizozitawanya mezani pale kwa mbwembwe. "Hii ndio namna tutakavyo-yanyanyasa maisha. Mpaka yapige magoti yakisota na kuomboleza chini ya nyayo zetu. Hivi hivi...mimi na wewe!" Sauti yake imejaa unabii, J4 anatamka akiwa ametazamana na Bebe uso kwa uso. Wote wakatabasamu wakitazamana. Tabasamu lao lilinena lugha moja. Lugha ambayo waliielewa wao tu. Sio lugha ya mapenzi asilani. Ilikuwa lugha ya ajabu ambayo Bebe aliitafuta kwa muda mrefu sana bila mafanikio. Lugha ya ukombozi! Ni lugha hii hii iliomfanya akutane na J4 na kumkabidhi uaminifu wake wote. Hakuwahi kumuamini mwanaume yeyote yule lakini kwa J4 ilikuwa tofauti. "Tutakuwa huru...tutakuwa matajiri! Ni haya haya maisha yaliyotufikisha hapa tulipo. Mimi na wewe tunajua ni nini tunakihitaji." Ni maneno ya J4 yaliyogeuka kuwa asali masikioni mwa Bebe. Maneno ambayo baadae yalimfikisha Bebe kwenye anga ambazo hakuwahi kutarajia kufika. Anga zinazoifanya simulizi hii iwe hii. ******* Ilikuwaje mpaka wawili hawa wakakutana? Ni swali ambalo hakika linakufanya unishutumu mimi ninayekusimulia. Ilikuwa hivi... Jumanne Maliki, ama J4 kama mlivomzoea ndiye alikuwa mchoraji wa hii ramani yote. Mpango wake aliusuka kwa ustadi na hakutaka kupoteza muda kabisa. Hapo awali, Akiwa katika harakati za ujana maji ya baridi na swahibu yake Dotto, alipagawa alipoitia sura ya Bebe kwa mara ya kwanza kwenye mboni za macho yake. "Hii pisi kwelikweli aisee, imenyooka sana hii!" Dotto aliinadi picha ile kwenyw simu yake. "Anaishi wapi huyu? Mbona sijawahi kumuona hapa mtaani." J4 akahoji. "Aaa wewe...unadhani hiki kiwango ni cha kucheza kwenye viwanja vya chandimu? Hiki ni kiwango cha kimataifa kaka. Class A kabisa! Wa watu wazito hawa!" D akaanza mbwembwe zake zilezile za udalali. J4 akampokonya simu yake na kuitazama picha ile kwa umakini zaidi. Akakitikisa kichwa chake kukubaliana na alichokiona. "Mali iko Sinza hii mzee baba. Inapiga ukaunta pale GRANDE!" Dotto akaendelea kuipamba picha yake. "Ni baamedi eh?" "Itakuwa...lakini ninasikia, japo sina uhakika...kuwa ni dada poa!" D akanong'ona. Hili la mrembo huyu kuitwa dada poa, likazitia doa kubwa jeusi sifa zote nyeupe zilizokuwa zikipepea kwenye akili ya J4. "Kwamba anajiuza au?" "Nasikia hivyo...maana yule bimdashi mmiliki wa klabu, nasikia nd'o mishe zake hizi pande zile." "Duh anaitwa nani aisee?!" "Nani? Huyo bimkubwa au-" "Huyu demu" "Be-Bebe! Anaitwa Bebe!" Anaitwa Bebe! Nd'o ikawa sentensi ya kwanza kukisumbua kichwa chake. Akamhimiza rafiki yake himahima ampeleke pale kwenye klabu ambayo mrembo huyu anafanya kazi. Siku ya kwanza, wakafukuzwa na walinzi baada ya mavazi yao kuwatambulisha kama vijana mabarobaro waliokuja kutalii na kuondoka tu. Hawakujipanga, bali walikurupuka tu. LE CLUB GRANDE sio mahala pa wanaoulizia bei. Wakajipanga vyema siku ya pili, lakini haikuwa bahati yao. Hawakumkuta! Baada ya J4 kubembeleza sanaa, Wakajaribu tena siku nyingine. Safari hii wakaenda usiku. Na kweli, akamuona Bebe kwa mara ya kwanza. Moyo wake ukamuuma sana! Ni heri asingemuona kabisa labda angeweza kujiepusha na yote. Kwamba hii sanaa bora ya uumbaji inayopumua ni kahaba? Alikataa kuamini. Moyo wake ukataka kufanya kosa la kumfumba macho na kumtupa kwenye shimo la huba. Lakini akili yake ikawahi upesi na kuikamata miguu yake, ikamrudisha kwenye njia sahihi. Kwamba azame penzini na kahaba? Akili yake ikamshutumu na kumfanya ajidharau. Lakini moyo uliougua gonjwa la mapenzi unatibika kwa namna ya kipekee sana. Na tiba yake ya kweli ni muda! Naam, kama ambavyo alimpenda taratibu. Ni hivyo hivyo alijifunza kumsahau taratibu. Na katika darasa hilo la kujifunza kumsahau, akadurusu somo ambalo alitaka limpe sababu zenye mashiko, ni kwa nini asimpende kahaba. Hapa akaiacha nadharia, akajifunza kwa vitendo. Akaanza kumfuatilia Bebe nyendo zake zote alizotegemea ziwe chafu machoni mwake. Yeye alikuwa na lengo moja tu. Kujifunza kumsahau. Hilo tu. Lakini macho yake kijana huyu mhitimu wa uhandisi wa umeme na masomo ya kompyuta, yakaiona fursa! Fursa ambayo labda aliwahi kuiona na kuipuuza. Lakini sasa anapata kila sababu ya ni kwa nini anahitaji sana fursa hii. Akazidi kuzama darasani! Aliyaona macho ya wanaume wenye tamaa, yanavyolitazama umbo la Bebe na kummezea mate. Aliyaona macho yao yanavyoweweseka baada ya kutazamana na ile sura yake jamali. Tazama wanaume hawa wanavyomwaga fulusi za kutosha ili tu wampate Bebe kwa ajili ya kuiridhisha miili yao. Tazama namna wanavyoteketeza fedha ambazo labda zingetosha kabisa kubadilisha maisha ya J4 na wazazi wake kule Ushirombo. Wanaume hawa ndimi zao zinaning'inia nje wakitokwa na mate kwa uchu wa ngono. Macho yao yanawaka tamaa wakimtazama Bebe. Tazama! J4 akafumba macho yake na kuzikumbuka nyakati na maisha yote magumu, yaliyogubikwa na umasikini aliyoyapitia tangu akiwa chuoni hasa baada ya kukosa mkopo wa serikali. Akalazimika kukitumia kipaji chake akidukua vyanzo mbalimbali vya mitandao na kuuza intaneti kwa wanafunzi wenzake ambao nao walimlipa kwa rasharasha. Mara kadhaa akakoswakoswa kudakwa na vyombo vya usalama kama mhaini na tapeli wa mitandao. Yote haya aliyafanya ili tu apate fedha ya kujikimu. Leo hii yupo mtaani, anatumia kipaji chake kama silaha ya kuiwinda fedha. Lakini hapa anaona fedha ile inamwagwa na matajiri kwenye uasherati. Ajabu! Vita yake ya kuitafuta fedha ikamdai silaha ya ziada. Hapa akamtazama Bebe kama silaha yake mpya ya maangamizi. Alikuwa amemfatilia kwa muda mrefu. Mpaka Bebe anapata umaarufu, J4 alikuwa kimya nyuma ya skrini za kompyuta akiandaa mitego yake ambayo aliiamini sana. Na alihitaji nyakati moja pekee ya kuitega mitego hii. Ndipo ikafika hii siku ambayo aliwafuata Bebe na Didas hotelini kwa usiri. Akalazimisha kumpiga Bebe kikumbo mpaka vitu vyake vilivyokuwa ndani ya mkoba legevu vikaanguka chini. Katika kumsaidia kuviokota, mikono yake ikafanya kazi kwa kasi ya ajabu na kubandika vinasa sauti na kamera ndogo ndogo kwenye baadhi ya vitu vyake. Akiwa na uhakika kuwa ni lazima tu atanasa. Na kweli akanasa! Ilikuwa bahati mbaya sana kwa bwana Didas Kilonzo Ambrozi. Ndani ya muda mchache, tayari J4 alikuwa na vipande vya video kadhaa ambavyo aliviunganisha. Usiku wa siku ile akakutana na Bebe baada ya kumpigia na kumueleza kuwa upo ujumbe wa siri anaotaka kuzungumza na yeye peke yake. Akamuondoa hofu kuwa kwa usalama zaidi, Bebe yeye mwenyewe apange mahala ambapo angependa wakutane. Bebe alipojaribu kuleta maringo, akashtuliwa kwa kipande cha video ile kilichotumwa katika simu yake. Hapo akakurupuka na kukutana na J4. Saa nne usiku, LE CLUB GRANDE! Ni hapa ambapo Bebe alipaona kuwa mahala salama zaidi kutokana na kujulikana kwake mahala pale. Hapo akakutana na J4 kwa mara ya kwanza, wakazungumza. "Wewe ni nani? Hiyo video umeitoa wapi?" Bebe aliuliza akiwa mwingi wa hofu. Licha ya uzoefu wake wa kuwahudumia wanaume kingono, hakuwahi katu kujirekodi au kuruhusu hilo litokee akiwa kazini. "Jina langu utalifahamu mara tu baada ya mimi kukamilisha kile nilichokusudia kukifanya ili wote tufaidike. Namaanisha, nikusaidie wewe na wewe unisaidie mimi." J4 akiwa ndani ya kofia pana na mavazi yaliyojaribu kumfanya aonekane kama jasusi wa kimataifa, akatamka kwa kujiamini. "Unisaidie? Nikusaidie?...wewe unanisaidiaje mimi? Unaweza kunisaidia kwa lipi?" Bebe akaruhusu kiburi kimfanye ajihisi yeye ni jitu la miraba minne na huyu anayeongea naye ni mbilikimo tu. J4 akatabasamu kidogo kisha akaketi vyema. "Sikia Frola!" Kutajwa kwa jina hili kukamfanya Bebe aubadili mkao wake na kukaa chonjo. "Mimi nafahamu fika wewe ni mwanamke wa aina gani. Nafahamu fika kuwa unapenda kuwa huru, ulitoka hapa GRANDE ili uwe huru. Hata huko ulikoenda, unautafuta uhuru! Lakini bado maisha yako, yako ndani ya minyororo ya utumwa. Haujapata kile unachokitafuta." Akatulia na kuyapa nafasi maneno yale yazame kwa Bebe. "Uhuru? Unadhani mi ni mtumwa?" Jazba inaanza kumpanda Bebe. "Hii video hii...inaweza kukupa fedha mara ishirini ya huo mshahara wako wa milioni mbili na nusu unaopata kwa ajili ya tangazo moja unaloigiza! Huwezi kuamini." J4 akatema cheche huku akitikisatikisa simu yake ya kupangusa, iliopasuka kioo chake na kuacha nyufa kadhaa zikitambaa. Bebe akapagawa. Huyu jamaa anajua mpaka mshahara wake! "We..ume..umejuaje mshahara wangu?" Akababaika. "Nataka nifanye kazi na wewe Frola! Kazi yetu tukiwa huru, mimi na wewe. Nakuhaidi tutapata hela nyingi sana! Tutakuwa matajiri." Utajiri? Utajiri gani hasa ambao Bebe alikuwa akihuitaji kutoka kwa huyu kijana mpya machoni mwake? Tayari anao umaarufu mkubwa nchini japokuwa huu haukumfanya awe tajiri moja kwa moja. Hata kama angepata ofa yenye malipo makubwa, bado isingeweza kuzidishwa mara ishirini ya mshahara wake. Akaketi vizuri na kuiegemea meza yake, akajisogeza karibu, tayari kumsikiliza J4. J4 akaachiwa umiliki wa dimba la maongezi. Akauweka mezani mchoro wake mzima wa namna atakavyoikamilisha mipango yake yeye na Bebe. Maneno yake yakawa sumu kali ambayo iliulegeza moyo wa Bebe, supastaa. Bebe akalainika na kukubaliana moja kwa moja na mpango ule wa J4. Mpango ambao ulimhakikishia kuwa siku inayofuata, atakuwa na zaidi ya milioni hamsini kibindoni. Ulikuwa mchezo rahisi sana kwake...ugumu wote uliachwa kwa J4. Ni ndani ya siku mbili tu. Muda huu wanatazamana na kisanduku kilichosheheni fedha. Milioni mia! "Huu ni mwanzo tu! Bado kuna mtu fulani huko ametutunzia hela zetu. Inatakiwa anase kwenye mtego wetu upesi." J4 anayasema haya baada ya mgawo kufanyika kama walivyokubaliana. Na sasa kila mmoja amekifutika kiasi chake anapopafahamu. Wako ndani ya gari la Bebe alilopewa na kampuni ya Bwana Didas. Muda mchache tu ujao, anafahamu kuwa ataachana nalo. "Kituo kinachofuata?" Bebe akamuuliza mikono yake ikiwa kwenye usukani. "Hakuna oda yoyote ile ya mtu binafsi ambayo umeipokea?" J4 akamuuliza. "Ooh yupo, Yule msanii Kenzy. Aliniomba niwe naye kwenye rekodi ya moja kati ya nyimbo zake za hivi karibuni." Bebe akachangamka. "Basi nadhani unajua ni nini unatakiwa kufanya." J4 akanong'ona kisha akatoa cheko la kibabe. Cheko la fedha! Akafungua mlango wa gari hili na kuanza kutoka nje. "Wapi sasa, si ninakupeleka mpaka kwako au?" "Hapana, ukifika wakati wa wewe kupajua kwangu. Nitakuleta mwenyewe. Mahusiano yetu hapa ni ya kibiashara tu na si vinginevyo..." J4 akatamka kwa kujiamini tayari yuko nje ya gari. "Mawasiliano yako ni yalayale ama?" Bebe akapaza sauti. "Hapana hayo yameshapotea, hayapo tena hewani....nitakutafuta kwa namba mpya." J4 akamjibu akitokomea. Hakumng'ang'ania Bebe kwa lolote na wala hakuonesha kumjali. Hili ndilo lililomuacha Bebe njia panda. "Ni mwanaume wa aina gani huyu?" Akajiuliza. Amekutana naye jana usiku tu...lakini tayari amemzoea kama ndugu mapacha wa tumbo moja. Na hajaweza kubabaishwa na urembo wake. Bebe akaliondoa gari lake eneo lile huku akilitafakari ombi la kijana huyu mwenye uelekeo wa hirimu moja na yeye. *Alitaka wawe na mahusiano ya kibiashara!* hivyo tu. Akazikagua noti zile mpya ndani ya mkoba wake, akazikuta bado zinapumua. Akatabasamu. Ama hakika, alikuwa kwenye biashara. ------------------------ Milioni mia kutoka kwenye vibubu vya bwana Didas, imepasuliwa na kutulizwa kwenye mifuko ya Jeifoo na Bebe. Pacha ambayo imetuhaidi kuhusiana kibiashara katika namna ya kushangaza. Wamemtaja Kenzy, msanii wa kizazi kipya ambaye ni maarufu pia nchini. Ni bomu gani limeandaliwa na pacha hii matata? Share link ya chaneli, acha reaction na toa maoni yako kwenye 0763204351. Mtunzi anapokea yote! Riwaya hii inaendelea...


RIWAYA; *KIBIRITINGOMA* MTUNZI; *GODLOVE KABATI* KWENDA KWA; *MAJIVU YA FASIHI channel* WhatsApp; 0763204351 ----------------- SEHEMU YA KUMI NA MOJA *Mwanaume mnyime ugali...atakula hata viazi.* *Mnyime kanzu, atavaa hata kaniki mbovu ama gunia* *Mnyime salamu, hii ataipata popote pale kwingineko kama sio kwako.* *Lakini chondechonde, katu usimnyime heshima yake.* *Na hii ni sehemu ya kumi na moja.* Siku yake iliyoanza kwa bashasha sasa ilikuwa imegeuka siku mbaya. "Siku ya shetani hii!" Nafsi yake ilimshtakia, kila alipolinganisha vibwanga na vibweka vyote vilivyomuandama siku hii. Didas Ambrozi alikuwa njiani kuelekea asikokujua. Alikuwa amechanganyikiwa haswaa. Mikono yake ilioshikilia usukani ilikuwa bado inamtetemeka kwa hasira. Kila mara jina la Bebe likimjia kichwani ana sonya na kutukana kimoyomoyo. Mara nyingine anapiga honi hovyohovyo kwa kuupiga kwa nguvu usukani. "Nimeyaona macho yake yule mnafiki. Changudoa mkubwa na tapeli kutoka kuzimu. Nimeyaona macho yake, yalikuwa makavu kabisaaa. Malaya yule!" Hatimaye akatamka kwa sauti akilalamika. Sentensi zake zikafuatiwa na honi iliyomkurupua mwendesha baiskeli ambaye aliponea chupuchupu kupitiwa na gari lile lililokuwa kasi. Didas amechachamaa! "Machozi yake ni ya kinafiki! Machozi ya wizi kabisa. Nimemuona usoni! Msaliti...mpumbavu." Didas akazidi kulalamika, akatema mate kwa hasira, amesahau kuwa yu ndani ya gari lake zuri la kifahari. "Yaani jitu pumbavu pumbavu litoke huko kusikojulikana, lile magimbi na ugali lisishibe...halafu liniamrishe eti ooh, nipe milioni mia halafu sitisha mkataba! Mimi huyooo?! Yeye kama nani kwanza." Didas yu peke yake garini, bado analalamika. Safari hii ghafla akashika breki zake kwa nguvu almanusura amgonge mlemavu aliyekuwa anavuka barabara kwenye alama za pundamilia. Nje ya gari, aliweza kuwatazama watembea kwa miguu waliokuwa wamecharuka kwa hasira, ndita zimechoreka kwenye nyuso zao, midomo na vinywa vyao vikionekana kumnenea maneno ya hasira kwa kuaalamika. Vidole vyao vya shahada vikilinyookea gari lake la kifahari lililomficha kwa vioo vyeusi vyenye sifa ya 'Wa ndani anamuona wa nje, lakini huyu wa nje katu, hawezi kuona kilicho ndani.' Yeye hakuwasikia na akamshukuru sana yule mtu mwerevu aliyebuni vioo vya namna ile. Mzee yule mlemavu alipovuka salama, akachochea upya gari lake na kufyatuka eneo lile. Baada ya kilomita chache akagundua kuwa anakosa umakini kwenye kuendesha gari. Akaliegesha gari lake kando ya barabara na kutulia akijipa dakika chache ili afanye tafakuri. Bado mawazo yake yanashindwa kuamini kuwa huenda Bebe amemzunguka na kumchezea shere tena katika namna ya kitapeli. "Au namsingizia?" Akajihoji. "Hapana simsingizii!" Akajijibu. "Hawa malaya wana mambo mengi sana ya ovyo! Wana mitandao yao ya siri ya kufanya uhalifu na dhambi zote zimchukizazo muumba." Sasa Didas akaikumbuka kofia yake ya uzee wa kanisa. "Yaani afanye uzinifu na uasherati huko halafu nimpe-" Mawazo yake yakavurugwa na mlio wa simu yake iliyoita kwa ghafla. Akaitazama kwa hofu, nambari iliyokuwa imempigia wakati huu ilionyesha kuwa ya tofauti kidogo. Akaitazama kwa sekunde chache. Kumbukumbu zake zikamkumbusha kuwa aliwahi kuziona mahali. Namba za namna hii hutumiwa na watu wachache sana hasa wale walio kwenye sekta nyeti za kiserikali kama mawaziri au usalama wa taifa. "Atakuwa nani huyu ambaye sijamsevu?" Didas akaingiwa na hofu akiinua simu yake tayari kwa kuipokea. Alikuwa akifahamiana na viongozi wengi tu wakubwa wa kiserikali, lakini wote alikuwa na mawasiliano nao. Ni kwa namna gani simu hii mpya imjie tena kwenye nyakati kama hizi ambazo anaandamwa na hofu? "Video zimewafikia!!" Kengele ya hatari ikalia kwenye ubongo wake. Akaketi vizuri na kujikohoza ili kuweka sawa sauti yake kisha akaipokea simu ile kwa nidhamu na unyenyekevu mkubwa. "Ha...haloo!" "Naongea na Didas Kilonzo Ambrozi!" Sauti nzito changamfu iliyoonekana kuwa na haraka ilipepea kutoka kwa mpigaji. Didas akagutuka. Kutajwa kwa majina yake matatu kama yalivyo kwenye vyeti vyake vya elimu, kukamshtua. Tena wakati huu hakuitwa bwana au muheshimiwa. Hakika alikuwa anaongea na mtu mkubwa. "Naam ni..ni mimi!" Akajibu kwa kigugumizi. "Unaongea na Special agent YW536 kutoka kitengo cha kiintelijensia na usalama wa mitandao Tanzania." Utambulisho huu ukamfanya Didas apate tumbo la kuhara. Akajishikilia kwa nguvu ili kujizuia. Mfano wa vitu kama vipepeo, vinapepea tumboni mwake. "Kwa nini unafanya mambo ya aibu ndugu yangu?" Swali jepesi la kiungwana lakini linalotatanisha likaachika kutoka kwa mpigaji yule. Mfumo wa upumuaji wa Didas ukabadilika. Pumzi zikaanza kupishana kwa kasi puani mwake, hakujua ajibu nini. Maadamu anayeongea naye ni mtu wa ndani ya mfumo, basi kuna uhakika wa asilimia zote kuwa ameziona video zake. Hakuwa na sababu yoyote ya kupoteza muda kuuliza mambo gani ya aibu aliyoyafanya. Aulize ili atumbuliwe? "Nisaidie ndugu yangu!" Kauli hii ikamtoka kwa uchungu huku akiikumbatia simu ile kwa mikono yote miwili sikioni mwake. Alikuwa anazungumza na masihi wake. "Hapa nakusaidiaje Didas? Enhe? Yaani ungejua namna unavyoheshimika huku lkulu, sidhani kama ungefanya huu upuuzi wa kujirekodi ukifanya uchafu. Huu ni upuuzi aisee! Akiona mheshimiwa Raisi itakuweje? Kwenye mitambo hapa inaonesha bado nusu saa, video zote ishirini zitakuwa mitandaoni! Na mtandao wa kwanza kufikiwa na huu upuuzi ni ule unaotumiwa na serikali." Sauti ya mpigaji ikapandwa na jazba, bado kasi yake ni ya haraka na haina mahusiano na utani wa aina yoyote ile. Yalipotajwa maneno kama *Raisi* na *serikali* , ushuzi ulimponyoka Didas kwa mafungu. "Bwana mkubwa! Bwana mkubwa! Naomba unisaidie kaka. Ni wahuni tu wamenifanyia mchezo mchafu. Nimeangushiwa jumba bovu ndugu yangu!" Ni Didas kwenyw harakati za kuutafuta wokovu wake. "Mimi sio ndugu yako! Na wala usiniite kaka. Sina undugu na wazee wazinifu wasio na uaminifu kwa wake zao. Wewe mzee hauna maadili kabisa!" Sauti ile inaonekana kama haitaki kupoteza muda, ni nzito, sauti ya mamlaka. "Kesi za maudhui ya namna hii hutufikia siye kabla ya kuingia mitandaoni. Yapo yanayofutika na yapo maudhui kama haya tusiyoweza kuyafuta kutokana na umahiri na ujanja wa mdukuzi anayeyapakia kwenye system. Na mimi siko tayari kuona huu uchafu unaingia kwenye rada za serikali yetu tukufu ya Jamhuri. Kwanza ni bahati sana nimeipata namba yako na nikakupigia. Nimekuheshimu sana kwa vile mimi ni mpenzi wa bidhaa za kampuni yako. Kimsingi sina cha kukusaidia, Lakini kama kuna mtu unayedaiana naye kwa namna yoyote ile, mlipe kabla ya nusu saa... Ama sivyo, Mzee wangu...jiandae kisaikolojia! Adui yako anaijua teknolojia vyema kuliko kitu chochote kile!" Simu ikakatwa. Upesi! Didas hakuwa na muda wa kujiuliza mara mbili. Akaliwasha gari lake na kuugeuza usukani. Gari likachomoka kwa kasi kuelekea eneo lolote lile ambalo alifahamu kuwa kuna jengo linaloitwa benki. Kiburi na majivuno yake yote akaamua avitie mfukoni kwa muda. Shilingi yake ya ukombozi ilikuwa ikinesanesa kiganjani mwake karibu na tundu la choo, hakutaka kuipoteza! Potelea mbali kama Bebe ni msaliti, mnafiki ama malaika mtoa roho. Akampigia simu mara moja kutaka kukutana naye ofisini mwake. Alikuwa ni kama aliyepewa mzani achague ni kipi chenye uzito kati ya utajiri na heshima yake alivyovihangaikia tangu zamani akiwa kijana, ama msichana changudoa aliyekutana naye ukubwani na kuamua kumsaidia. Wakati huu akaipa heshima yake uzito wa jiwe la fatuma mbele ya Bebe mwenye uzito wa unyoya. ******** "Saini hapa na hapa!" Didas anaitazama saa yake, upara wake unavuja jasho. Anamtazama Bebe ambaye naye ni kama haelewi ni nini kinachoendelea. "Nisaini nini tena mbona sielewi?" Bebe anauliza. "Usinichanganye! We saini hapa... sina muda wa kupoteza. Mengine utayajua mbele ya safari." Didas anabwata, matone kadhaa ya mate yakimtoka kinywani. Tai yake shingoni imegeuka nyuma. Ina maana kifua chake kimehamia mgongoni?Hatujui. Anajua yeye. Bebe akakamata kalamu ile ya wino na kuanza kusoma karatasi ile kabla hajasaini. "Come on! Unasoma nini tena?" "Unataka nisaini kitu ambacho sikijui? Kama unataka kuniuza?" Bebe akauliza kwa kujiamini. Didas akashusha pumzi kwa nguvu. "Sikia Frola!" Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu akamtaja kwa jina lake halisi. "Hapa tunaongelea uhai na kifo! Heshima yangu na familia yangu niliyo nayo ni maisha yangu Frola. Huu ni mkataba wa kusitisha kazi yako wewe na kampuni yetu kama anavyohitaji huyo mwenzio...Ahhh (Anabadili) huyo jamaa aliyeturekodi. Umenielewa?!" Uso wake umetota kwa jasho anamtazama Bebe. "Ina maana naacha kazi?" "Yeah! Haya saini hapa." "Kwa nini lakini?" "Bebe...hayo masuala mengine tutajua baadae. Tazama! Tuna dakika kumi na moja tu hapa." Bebe akaiinamia karatasi ile na kuanza kuchonga herufi zake. Didas anamtazama kwa shauku, bado anaona Bebe kama anaandika taratibu. Bebe akamaliza kutia saini yake. Didas akaikwapua bahasha kubwa ya kaki iliyosheni fedha kutoka kwenye begi dogo na kumkabidhi Bebe. "Haya mama! Mpelekee huyu jamaa hivi vitu haraka kwenye eneo nililokuelekeza. Fanya upesi." Didas akamsurutisha Bebe. "Lakini-" "We nenda, hili likiisha hayo mengine tutayaongea!" Didas akamkatisha. Bebe akaondoka kishingo upande kutoka ofisini mwa Didas na kutoka nje. Huku nyuma akamuacha Didas aliyechanganyikiwa, anaitazama saa yake kila baada ya sekunde kadhaa. Baada ya takribani dakika ishirini simu yake ikaita. Akakurupuka kuipokea baada ya kugundua kuwa mpigaji ni huyu huyu aliyepelekewa mahitaji yake. Didas akapongezwa kwa juhudi zake alizozifanya kukamilisha kile alichoagizwa. "Makubaliano yetu ni kutoziachia video mitandaoni. Kwa hio ziko salama kabisa! Hutozikuta kwenye mtandao wowote ule kiongozi wala usiwe na wasiwasi. Na hakuna mtu awaye yote anayeweza kuzipata." Sauti ya kijana mchangamfu asiyejulikana ikamtoa hofu. "Naweza nikaongeza kiasi zaidi ili zifutwe kabisa kama inawezekana? Samahani lakini." Didas anauliza kwa saut ya nidhamu. "Ninayo furaha kukuambia kuwa hilo haliwezekani mzee wangu!" Sauti changamfu akamjibu. Anayo furaha? Kivipi? "Kwa nini haiwezekani?" Didas akauliza. "Siku yoyote ile utakapolitamka jina la Frola, ama kukutana naye, ama kumuhusisha kwenye mduara wa maisha yako, basi video hizi zitakuwa kama wa muhtasari wa taarifa za habari kwenye televisheni kubwa hapa nchini. Nina uhakika sishindwi kufanya hilo jambo!" Sauti changamfu akaweka kituo kisha akaendelea. "Kiufupi kuanzia muda huu, nataka uachane na Frola moja kwa moja. Huyu nd'o anguko lako! Muone kama ukoma. Kaa mbali naye kabisa. Hapo utakuwa salama." Akamaliza na simj ikakatwa. Didas akachoka. ******* "Kiufupi kuanzia muda huu, nataka uachane na Frola moja kwa moja. Huyu nd'o anguko lako! Muone kama ukoma. Kaa mbali naye kabisa. Hapo utakuwa salama." Yalikuwa ni maneno ya mwisho kutoka kinywani mwa J4 akiwasiliana na mtu kwenye simu. Kando yake ameketi Bebe akiburudika kwa kinywaji chepesi kulipasha tumbo lake kwa ajili ya maandalizi ya mlo mzito uliokuwa ukisubiri hukumu yake pale mezani. J4 akakata simu ile na kumtazama Bebe aliyekuwa anatabasamu kwa madaha. Cheko fupi likawavamia wote kisha wakahamia mezani pale na kuanza kula. "Unawezaje kuyafanya haya yote?" Bebe akamuuliza huku akitafuna paja nono la kuku wa kukaanga. "Ni njaa tu!" J4 akamjibu kwa kifupi. "Njaa? Kivipi." "Njaa amekuwa mwalimu wangu mzuri. Kama hujanielewa endelea kula, ukishiba utanielewa vizuri." J4 akatamka kwa mzaha akiwa na uso unaowaka tabasamu. ------------------- Mambo yamekuwa mambo! Bwana Didas Kilonzo Ambrozi anashambuliwa kutoka kila pande. Ile Utatoa sitoi, utatoa sitoi...Anajikuta anaachia tonge. Anapewa vitisho vikali kutoka kwa mtu asiyemfahamu. Je, huu ni mwisho wa Bebe kukutana na Didas? Ana lengo gani na Bebe huyu J4? Halafu ni kama wana jambo lao hawa...kulikoni? Kazi yetu sisi ni kushare link ya chaneli, kureact na kutoa maoni kwa mwandishi kupitia 0763205351. Riwaya hii tamu Inaendelea...


RIWAYA; *KIBIRITINGOMA* MTUNZI; *GODLOVE KABATI* KWENDA KWA; *MAJIVU YA FASIHI channel* WhatsApp; 0763204351 ----------------- SEHEMU YA KUMI NA TATU *Katu usijidharau na wala usiwadharau wengine.* *Huenda wewe ni daraja la mafanikio ya mtu mwingine, yupo mahala fulani na mtakutana katika namna ya kushangaza.* *Ama neema ya mafanikio yako imebebwa na mtu fulani aliye mbali ama huyuhuyu aliye karibu yako.* *Ulimwengu wetu umeumbwa kwa kanuni ya ajabu sana...* *Tunaishi kwa kutegemeana.* *Karibu kwenye sehemu ya kumi na tatu.* Kila kitu kilikuwa kama mchezo wa sinema. Ndani ya siku moja tu...kila mtu alikuwa amebadilisha historia ya maisha yake. Sio Bebe, sio J4 na pia sahau kuhusu Chief Didas, kama alivyozoea kuitwa na Bebe. Kila mtu kwa nafasi yake, aliyapokea mabadiliko japokuwa katika namna tofauti. Haswaa, Bwana Didas, alilazimishwa kulivujisha pakacha lake. Bebe na J4, wakafurahia nafuu hii ya kuwa wachukuzi. Bwana Didas alikuwa bado haamini kama ameokoka kwenye hatari kama hii. Hatari ya jina lake kupakwa matope mbele ya Watanzania wanaomheshimu. Na zaidi ya yote, wanazipenda bidhaa za kampuni yake. Akashusha pumzi ndefu kujiweka sawa. Ni kama punguani aliyeiokoa kete yake ya mwisho kwenye mchezo wa kamari ambao alikuwa na kila dalili ya kupoteza. Hofu ya kuaibika bado ilizidi kuutafuna ujasiri wake. "Hivi huyu jamaa hajapost kweli?!" Ni swali pekee alilozidi kujiuliza akiwa anaendesha gari lake kuelekea nyumbani. Ameshapiga simu mara kadhaa kwa mkewe, akimuuliza endapo kuna taarifa yoyote ile mpya iliyogonga hodi. "Mh Baba Junior, umekuwaje mme wangu? Hii ni mara ya nne. Mara ya nne unaniuliza kama kuna jipya. Vipi, kwema huko? Ama kuna msiba?" Sauti bembelezi ya kujali, lakini yenye kujiamini ikahitaji majibu. "Aaam...hapana laazizi. Nakujulia tu hali mke wangu. Hehehe wala hamna shida." Didas anamjibu huku akijichekesha kwa aibu. Siku hii anamuita mkewe kwa jina *Laazizi* , haikuzoeleka hivi. Hatulii anabadili upepo angani, atapiga simu kwa baadhi ya vigogo na viongozi wakubwa wa serikali anaofahamiana nao. Hawa atawauliza juu ya kile kinachoendelea Ikulu. Didas atasimamisha gari lake kando kidogo. Anapoongea na watu wenye nyadhifa kama hizi, kelele hazihitajiki. Badala yake ataiinamia simu yake na kulitega sikio lake kwa adabu zote, kusikia litakalosemwa. Hataambulia kitu zaidi ya malalamiko ya viongozi hawa juu ya kero za wananchi na ugumu wa majukumu yao. Ni saa tatu na robo usiku, Didas Kilonzo Ambrozi anarudi nyumbani baada ya siku ndefu sana. Ama siku hii gari la *faza hausi* limerudi nyumbani mapema kuliko siku za nyuma. Tazama, hii ni siku ya tofauti kabisa kwa familia hii tangu asubuhi. Labda ni siku nzuri kwa mama Junior na wanae, lakini kwa Didas ni ya kipekee. Anakuja kupokelewa na bintiye mdogo wa kike katika namna ya *Baba huyo*...anaigiza tabasamu, nalo linamgomea kuigizwa. Anamkwapua na kumuinua juu kiasi lakini hambebi, anamrejesha upya sakafuni baada ya kugundua kuwa amechafuka! Suti yake nyeusi nadhifu aliyoandaliwa na mkewe asubuhi ya siku hii, imepakwa rangi mpya ya vumbi. Tai yenye nembo ya bendera ya taifa, haipo tena shingoni mwake. Ukosi wa shati lake nao ni kama umepata muundo mpya shingoni mwake. Didas anaiburuza miguu yake na kuingia nyumbani mwake akiwa amechoka mwili na akili. Hataki usumbufu wala mazozano na mkewe, ambaye anamshushia mvua ya maswali juu ya muonekano wake. Huyooo Didas anajisogeza bafuni ili akakoge. Lakini hapigi hatua zaidi ya tano kabla hajahisi kuongezeka kwa gramu kadhaa za uzito wa kichwa ni chake. Anayumba na kuisalimia ardhi kwa kuanguka chini kama mzigo. Hii nayo ina maswali ya kumuuliza. Hana majibu...anakoroma tu, anaona giza! Giza linamfumba macho yake. Kinachofuata ni hekaheka za mama Junior na wanae kumpepea kabla hawajaomba msaada wa wafanyakazi wa nyumba ile. ******* "Mic check, mic check...one two, one two!" Sauti nzito changamfu iliendelea kurindima ndani ya Studio kubwa. Ilikuwa sauti ya bwana mmoja mnene wa umbo, aliyeyafunika masikio yake yote mawili kwa kifaa cha kidigitali, maalumu kwa ajili ya kusikiliza muziki, headphones! Fulana yake pana ya kijivu, imelowa jasho na kuchora mfano wa ramani kwenye kifua na mgongo wake. Mbele yake ni meza iliyochafuka kwa vifaa lukuki vya kieletroniki. Vifaa vinavyomweka kwa rangi mchanganyiko. Rangi zinazompa mzuka wa kufanya hiki anachokifanya. Atagusa hapa na pale, atabonyeza kitufe hiki na kile, huku atasugua sugua kisha kile atakizungusha. Ili mradi tu, aukoroge mchanganyiko wa sauti na azalishe mziki bora. Hii nd'o kazi yake.Yeye ni producer (mzalishaji) wa muziki. Pia ni mkufunzi wa wasanii wa muziki wa kizazi kipya. Na siku hii alikuwa akimpika kijana mpya pale pale kwenye studio yake. Kichwa chake kinapanda juu na chini, kikifuatisha miondoko ya mdundo wa muziki anaousikia yeye peke yake. Kisha anatoa ishara ya kidole gumba kwa kijana nyuma ya kinasa sauti, aliye ndani ya chumba maalumu kilichomtenganisha naye kwa kioo kipana kinachoruhusu waonane. Kijana yule anaiweka sawa sauti yake, anayafumba macho yake kiasi kwa hisia kali na kuanza kuimba yale anayoyasoma kwenye karatasi mbele yake, japo kwa kuibiaibia. Hamalizi hata mshororo mmoja wa beti lake, "Hajwaa! Hajwaaa!" Sauti inapazwa, haisikiki. "Dogo achaa! Acha nakwambia! Hii mbovu, mbovu sana!" Bwana yule mnene amechachamaa, anasimama kwa hasira na kufoka. Kitambi chake kinatikisika, ndita zimeweka kambi usoni mwake. "Nimeshakwambia, usiimbie kooni my boy! Sauti itoke kwenye tumbo! Tumboni nimesema! Haya shime..." Anarejea kwenye kiti chake, uso wake mnene bado una ramani za ndita. Ni kama aliyekunywa dawa chungu. Kijana ndani ya chumba, anajiweka sawa kwa mara nyingine. Naye, anavaa kifaa kilekile masikioni. Safari hii anajitahidi kuimba kama alivyoelekezwa. Anaibia mashairi kwenye karatasi mbele yake, kisha anapepesa macho kumsanifu bwana yule mnene, ambaye bado amemkazia macho kwa hasira. Mara ghafla, bwana yule mnene anakitoa kifaa kile masikioni. Anasimama kwa pupa, akimtazama kijana yule. Pumzi zinapishana kwa kasi puani mwake, ni kama mbogo mwenye hasira. "Dogo! Hivi nikueleze mara ngapi? Umekuja kuimba au kunipotezea muda?Mh? Sema!" Akiwa kwenye mahojiano haya na kijana huyu ambaye anaonekana kuipoteza hali yake ya kujiamini. Mara unafunguliwa mlango wa studio hii na kinaingia kikundi cha wanaume watano, kikiongozwa na kijana mmoja aliyevalia mavazi ya kisasa. Nyuma yake ni wenzie wawili wanaoonekana kufanana naye kimavazi, pamoja na watu wawili wa miraba minne, waliovimba kwa mazoezi. Ujio huu unabadilisha hali ya hewa ndani ya studio hii na kusababisha uchangamfu wa ghafla. "Alaaaa! Kenzy kama Kenzy! Finally, you are here my boy!" Bwana mnene anakurupuka na kumkumbatia kijana huyu. "Eeeeh BIG kama BIG!" Kijana yule akamchangamkia. Wanakumbatiana kwa furaha huku kicheko cha ushindi kikikatiza baina yao. "Aiseee...kitambo sana ticha!" Kenzy akatamka kwa bashasha. "Haswaa naona umenitupa mwanangu...mara ya mwisho, lini ilikuwa?...show yako ya pale Mbeya! Tangu hapo!" Bwana mnene, aliyetambulishwa kwa jina la BIG akatamka huku anakielekea kiti chake. "Nimeimiss sana hii studio ticha!" Kenzy anagundua kuwa kuna kijana ndani ya chumba cha mazoezi. "Nani huyu? Chipukizi eeh?" "Yeah...niko namchonga kijana. Sema huyu boga sana aisee...doh!" BIG akatamka huku akilipangusa jasho lake kwa kitambaa kipana. Kenzy akamfanyia ishara kijana yule asogee pale walipokuwa wao. Kijana anasogea akiwa anatetemeka. Haamini kama ni yeye leo hii anaonana na mwanamuziki mashuhuri nchini uso kwa uso. Msanii nyota, ambaye anatamani siku moja aje kuwa kama yeye. "Mambo vipi?!" Kenzy akamuuliza kwa uchangamfu. "Sa..sa-lama bro! Ke- Kenzy. Shkamoo!" Anajiumauma. "N'do nakwambia boy! Mimi nimewaandaa wasanii wakubwa! Huyu hapa Kenzy, nimemchonga mimi. Alikuwa anafuata maelekezo. Anatoa sauti! Kutoka tumboni...haibanii. Wewe sasa!" BIG akatamka kwa kisirani huku akisonya. Wale wapambe waliokuja na Kenzy wakacheka kwa sauti baada ya kuyasikia maneno ya BIG. Kijana akatazama chini kwa aibu. "Unaitwa nani mdogo wangu?" Kenzy amemshika begani kijana huyu, katika namna ya kumfariji. "Jackson" "Hili ni jina lako la kisanii?" "J-la...J-love nd'o jina langu la kisanii" "Safi sana...haya sasa nenda katuoneshe ulichonacho. Jiamini!" Kenzy anampiga begani, kijana anarejea ndani ya chumba. Anavaa kifaa kile masikioni, anashusha pumzi kwa nguvu. BIG anamtazama kwa pembe za macho yake katika namna ya *ole wako na hii uharibu*. Unawashwa muziki na kijana anaanza kutembea na mapigo yake akiimba. Ama! Ni kama mashetani yake yalikuwa yanasubiri ujio wa Kenzy, ndipo yampande kichwani. Sauti yake ikapita kwa adabu kwenye vifaa hivi vya kielektroniki. Ikawa sasa, ni kama mapigo ya muziki ule yanamtii yeye na kuifuata sauti yake badala ya yeye kuyafuata mapigo. Jackson, J-love akamaliza ubeti wake wa mwisho kwa kufumbua macho yake. Akakuta watu wote ndani ya studio hii, vinywa wazi. Makofi! Wote wakampigia makofi! Wote isipokuwa BIG. "Hebuu kwanza!" Bado haamini kama kweli Jackson ameimba namna ile. "Nipe stanza ya mwisho..." Akamsihi huku akicheza na vifaa vyake. J-love akaiimba beti ile kwa ubora zaidi ya mara ya kwanza. Aliyepiga makofi safari hii alikuwa ni BIG peke yake. "Unaishi wapi aisee!" Kenzy akamuuliza akiwa na shauku. "Msasani bro." Akajibu kwa adabu. "Unaimba vizuri sana mdogo wangu. Ukiendelea hivi, nitatoa ngoma moja na wewe siku si nyingi!" Kauli hii ikafufua tabasamu usoni mwa Jackson. "Sauti yako ina kitu mdogo wangu...ina raw energy ambayo wasanii wengi wanaikosa. Usiache, push harder! Na ukiweza kupata mentor kama BIG hapa, usimuachie." Kenzy akaongeza. Wakabadilishana nambari za mawasiliano na kupiga picha ya pamoja. Hili likawa kama kombe la ushindi kwa Jackson. Achana na kupiga picha na staa, hilo si suala. Suala kubwa ni kumiliki namba zake za mawasiliano. "Karibuni aisee wanangu! Sie tupo." BIG akarejea kuutambua ugeni wa Kenzy na wenzie. Ni yeye aliyemtengeneza Kenzy tangu alipokuwa chipukizi mpaka hivi sasa alivyo. Nyota wa muziki wa kizazi kipya. "Naam faza! Nilikuwa nakatiza, nikaona si vyema nipite kwenye mtaa ulionilea halafu nisipite hapa mgodini pasi na kutoa hata salamu!" "Oooh safi sana...walau hata umelikumbuka hilo. Nyie mkitoka huwa mnatusahau. Tumeshawazoea, na wala sishangai!" Producer BIG anajibu kwa kujiamini bado kitambaa chake kipana cha jasho kipo mkononi mwake, kinafanya kazi yake kwa uaminifu. "Walaa mimi siwezi kukusahau anko wangu, BIG mzazi! Tena..." Kenzy anasita kisha mkono wake unazama mfukoni na kuibuka na noti nyekundu kadhaa. "Nadhani hii ya maji itakufaa!" Anampatia BIG kiasi kile. BIG haonekani kushtuka. Anaipokea na kuisweka kwenye mfuko wa suruali lake bila hata kuihesabu. "Mafao yetu ya uzeeni haya!" Anatoa kijembe. Wote wanacheka kidogo. Anamkazia macho Jackson kisha na yeye anazama mfukoni na kumpatia noti ya rangi tofauti na zile alizopewa. "Haya dogo! Changanya mbaliga zako, kaniletee maji makubwa. Chenji inayobaki chukua!" Jackson anaipokea noti ile na kuondoka ndani mule kwa bashasha. "Enhe vipi umefikia wapi na ile project yako mpya? " BIG anamuuliza Kenzy. "Ipi hiyo?" "Video ya lile jiwe lako, ME AND YOU!" Anaweka wazi swali lake. Kenzy anachangamka, "Aaaah ME AND YOU....naelekea kushoot wiki ijayo mzazi. Kila kitu kipo tayari so far! Na pia kuna surprise hapo!" Kenzy anatulia na kuiacha sentensi yake ielee hewani ili auvute usikivu wa BIG. "Surprise gani tena?" "Unajua ni video vixen gani nitakuwa naye?" Akauliza tena kwa bashasha. Lengo lake ni lilelile, amshangaze BIG. "Ni nani?" "Queen Frola!" Akatamka kwa kushtukiza, akitabasamu kwa shauku. Na kweli BIG akashangaa. "Unamaanisha? Huyu huyu mrembo ninayemuona kila siku kwenye matangazo au?" "Eeh huyu huyo. Na mimi nitakuwa msanii wa kwanza kufanya naye kazi hapa nchini!" "Duh hongera bwana. Lakini mbona ni kama ni wa bei ghali sana yule. Utamudu kum-" "Nitamlipa. Pesa sio tatizo. Uzuri ni kwamba nikifanya naye video moja. Itakimbiza sana mitandaoni, faida itakuja kwa kasi!" Kenzy akajipeperusha. "Mh sawa! Utakuwa umepiga hatua kubwa sana aisee. Maana industry haicheki na mtu sasa hivi." BIG akatamka bila kumuangalia Kenzy usoni. "Tena jioni hii nina appoitment naye, tutakutana tuongee." Kenzy akaweka nukta. Baada ya dakika kadhaa za maongezi mafupi hususani ya kisanaa, Kenzy na jopo lake waliondoka na kuacha ahadi nyingine lukuki za kurejea tena. Ahadi ambazo masikioni mwa BIG zilikuwa sawa na baba anayemuhaidi peremende mwanae mdogo ma asimletee. Alishawazoea hawa wasanii! Anawachonga mpaka wanafanikiwa na kupenya kwenye tasnia, wakishapata mafanikio wanamsahau. Ama kweli, Tenda wema nenda zako! Anakunywa mafunda makubwa ya maji na kurejea upya katika darasa lake na kijana Jackson J-love. "Sikiliza, mgema aliwahi kusifiwa sana kuwa anatengeneza pombe aina ya Tembo kwa ustadi wa hali ya juu pengine kupita wagema wote. Unajua ni nini alifanya baadae?" Akamtupia swali Jackson. "Alilitia maji!" Akajibu upesi kwa kujiamini. "Unajibu kwa kuwa umekaririshwa hivyo au unaelewa?" "Naelewa!" Jackson akamjibu. "Haya vaa Headphones tuendelee. Kanuni ni ileile, toa sauti tumboni...imba kwa kujiachia. Usibane sauti! Haya sasa...One! two! three!....twende!" ******* Kipande cha kitu mfano wa kalamu ya rangi kinapitishwa kwa adabu kwenye papi za midomo yake. Anaifumba na kuigusanisha katika namna ya kuikausha rangi ile. Lipstick! Hii ni baada ya uso wake kurembwa kwa vipodozi na kuufanya ung'ae na kumeremeta. Sijaongelea kope zake ndefu ambazo sio za bandia. Ni kope ambazo zikipepesa tu, zinatamfanya mtu anayetazamana naye aimbe pambio kumsifu Mungu. Alikuwa na silaha zote za maangamizi. Kama hatakuua kwa sura yake iliyovimbiwa urembo, basi umbo lake na ngozi yenye nuru havitakuacha salama. Basi tuseme wewe ni mgumu sana. Utapona kwenye haya, lakini chunga sana masikio yako. Labda yafunike kwa pamba usiisikie sauti yake inayoweza kuwatorosha malaika mbinguni. Basi tuseme wewe ni kiziwi japo kwa mkopo. Chunga sana, usimsogelee karibu. Huyu hapa! Anajipulizia manukato yake ya bei mbaya. Manukato yenye harufu tamu, inayodai kumbato zito la mtu atakayepishana naye karibu. Eeh unashangaa?! Inabidi uwe na mkusanyiko wa vilema vitatu mpaka vinne vinavyohusisha milango ya fahamu. Uwe kipofu, macho yako simuone Uwe kiziwi, masikio yako yasimsikie Uwe toinyo, harufu yake ikupite kando. Na katu, ngozi yako isimguse kumhisi...utapagawishwa na wororo wa ile ya kwake. Ulimi hauna mfupa! Hii dhambi sitaki kushiriki. Hamna namna yoyote ile utakayokwepa kukiri kuwa Bebe ni malikia wa uzuri. Hasa jioni hii anayojiandaa kwenda kukutana na Kenzy. Msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania. Bongo Fleva! Anasimama mbele ya kioo chake kipana. Anajitazama. Anajigeuza huku na huku, anajibinua kidogo. Kisha anazunguka nyuzi mia tatu sitini kwa madaha. Anafurahi namna nywele zake zinavyoufuatisha mzunguko ule. Ni huu urembo wake uliomtajirisha siku mbili zilizopita. Anatabasamu anapolifikiria hilo. Upesi anaitwaa simu yake, simu janja. Akachukua picha mbili tatu mbele ya kioo kile. Anamtazama yule Bebe mwingine wa ndani ya kioo. Ni kama anaweza kuzungumza naye, anampa uhai, "Enhe una nini sasa? Ulidhani nitakuwa mtumwa daima? Tazama! Mwili wangu unanilipa...tabia ile chafu, uliyokuwa ukinishutumu kwayo, inaeleka kunitajirisha. Upo hapo?!" Anatamka akitazamana na taswira ile. Safari hii huyu Bebe wa kwenye kioo hamjibu na wala habadiliki katika namna yoyote ile. Bali anafanya kile anachokifanya kwa kuigiza. Akicheka naye anacheka, akiruka anaruka. Bebe akatoka ndani ya chumba hiki akiwa na pochi yake ndogo. Anatoka nje akipewa salamu lukuki na vijakazi wake. Anazipokea kishingo upande kana kwamba hazistahili. Na kweli hazistahili! Anajua fika kuwa ima fa ima, muda wowote ule atanyang'anywa mji huu. Anaitazama nyumba hii kwa nje, kisha analigeukia gari lake na kulitazama kwa macho ya aibu. Dhamiri yake inamsuta kwa kutumia kisicho chake. Ilikuwa wazi sasa kuwa ameachana na kampuni ya Bwana Didas. Anaachana na mawazo haya baada ya kukumbuka kuwa hana muda wa kuwaza yaliyopita. Bado kitambo kidogo, atamiliki majumba makubwa hata kumi ya kifahari. Wasiwasi wa nini? Ofa mbalimbali za matangazo bado zimepanga foleni kuhitaji saini yake. Hata jioni hii anaenda kuongelea dili linalohusisha pesa. Ana shida gani sasa? Na zaidi ya yote, amefahamiana na J4. Ambaye ana madili ya maana zaidi yanayohusisha fedha nyingi chekwachekwa. Analiondoa gari lake taratibu na kuanza safari ya kuelekea walikopanga kukutana na msanii Kenzy. "Nipo njiani!" "Ooh okey, mi nimeshafika mama. Nakungoja wewe tu." Ni sauti ya Kenzy ndani ya simu ya Bebe. "Santeeee!" "Take care." Simu inakatwa. Kabla hajaitua chini, inaingia simu nyingine ambayo inaanza kuzungumza papo hapo bila yeye kuiruhusu. "Mlimbwende! Hakikisha anajaa kwenye mfumo huyo msanii. Naona ameshaanza kulainika." Bebe anashtuka. Ni sauti ya J4. "Wewe ina maana umeidukua simu yangu ama?" Anauliza akiwa na hamaniko. "Usiwe na hofu bibiye...mimi nimekutafuta tu kwa muda huu, na kwa bahati nikakuta unaongea na nyama mpya. Nilitaka kukusalimia tu." "Mh kwa nini lakini? Biashara gani hizo unaleta sasa? Masuala ya kudukuana mi staki." "Alaa basi sawa, nitakutafuta usiku." Simu ile ikakatwa. Kukatwa kwa simu hii, kukaambatana na Bebe kupokea ujumbe wa kutoka kwa namba hii ngeni. Ujumbe uliokuwa na ile picha yake nzuri aliyojipiga kwenye kioo chumbani mwake! Maneno chini yameandikwa, *What a beautiful lady!* Imemfikiaje huyu? Hajui. Na wala hata hajaitundika mitandaoni. Bebe akakosa la kufanya, akatabasamu na kuendelea na safari yake. J4 mdukuaji kwenye ubora wake. ---------------- Aisee 🥱, Tukiwa bado tunakitafuta kiini cha riwaya yetu ya *KIBIRITINGOMA*, Fanani wenu ninafurahishwa sana na juhudi zenu za kuisambaza link ya chaneli yetu. Hakika mnastahili kila kilicho bora! Msiache kushare link ya chaneli, acha reaction na toa maoni yako kwenye 0763204351. Mtunzi anapokea yote! Riwaya hii inaendelea...


*`PAZIA LA FILAMU`* 📽🎬 *FREDDY* (2022) Mungu alimbariki sana Freddy Ginwala, Akamuumbia moyo wa dhahabu, moyo wenye utajiri wa adili na ibada. Akamjaalia tabia njema zilizoambatana na adabu iliyotukuka. Mungu akamuongezea na mali za kumtosha alizoridhika nazo hakika. Unadhani Mungu wetu ana kikomo kwenye kumimina neema zake? La hasha! Freddy Ginwala, alikuwa na kazi nzuri ya udaktari wa vinywa na meno. Kazi hii ikampa umaarufu mkubwa kwenye jamii yake. Ikampa heshima na jina bora sana miongoni mwa vinywa vya watu. Freddy angedai nini kingine? Lakini hakika Mungu wetu hatupi vyote! Maadamu sio kila kitu kinatufaa. Na hata kikitufaa, huenda kina muda wake maalumu. Mungu hutupatia vitu hivi kwa muda wake, na muda wake daima ni sahihi! Naam, Freddy Ginwala hakuwa na mwenza wa maisha. Alitamani siku moja akutane na binti mrembo. Amuoneshe namna sahihi ya kulitumikia neno *Nakupenda*. Wapendane kwa damu na nyama, roho na mwili. Wafunge ndoa na wajenge familia bora. Hili kwake lilikuwa ni deni kubwa ambalo nafsi yake ilimdai usiku na mchana. Alikosa furaha na amani. Katika umri wake huu wa miaka takribani 30, hakuwahi kujihusisha na mahusiano katika namna yoyote ile. Sahau kuhusu mazoea na wasichana, Freddy alijawa na aibu kila linapofika suala la wasichana. Akajitahidi kutafuta wachumba wa mtandaoni lakini nao hakuwavutia kutokana na aibu yake na mtindo wake wa maisha. Akaamua kuisubiri bahati yake popote pale ambapo itamdondokea. Ni siku moja tu iliyotosha kumbadilisha Freddy. Naam, siku hii akiwa na bibi yake kwenye sherehe fulani, macho yake yakagota moja kwa moja kwa msichana mrembo wa kike aliyekuwa kwenye hafla ile. Angefanya nini sasa badala ya kumtazama tu? Huu nd'o ujasiri pekee aliokuwa nao dhidi ya wanawake. "Mjukuu wangu, ni lini utakuwa na mke?" Lilikuwa swali kutoka kinywani mwa bibi yake lililogeuka mkuki wa sumu masikioni mwa Freddy. Aibu imemjaa, anatetemeka, hajui amjibu nini bibi yake. Familia yake inamtazama kama mtu wa ajabu. "Haya kuna mrembo yule pale, na anaonekana yuko peke yake. Kamchangamkie upesi, huwezi jua. Nenda usiogope wanawake!" Bibi yake akamsurutisha. Freddy akaenda kuijaribu bahati yake. Huenda ni siku hii bahati imemwangukia, yeye alienda kujaribu tu. Akajikuta ameangukia kwa mke wa mtu. Mrembo Kainaaz! Na ni hapa alipokutana na binti Kainaaz kwa mara ya kwanza. Binti ambaye aliuteka moyo wake, nao ukatii bila shuruti. Akaufunga kwenye gereza la mapenzi. Freddy akawa mtumwa wa mapenzi kwa Kainaaz. Huyu ni msichana pekee aliyempokea na kumsikiliza kwa upole kuliko wale wengine wa mitandaoni. Kwa mara ya kwanza Freddy akajihisi amekamilika. Akabadili mtindo wa nywele zake, akanunua nguo mpya, akabadili mpaka mwondoko! Si amepata mpenzi bhana! Kwa nini asing'ae? Akapenda, akafa, akaoza! Zawadi kemkem hazikukatika kwa Kainaaz. Hakujali kuwa huyu ni mke wa mtu au la. E bwana eee, Freddy amependa tayari. Freedy akiwa anapambana kumfanya Kainaaz aifurahie kila dakika anayoiishi hapa duniani, akagundua kuwa binti huyu anapitia mateso makali. Vipigo na manyanyaso vya kila mara kutoka kwa mume wake vilikuwa kama wimbo wa taifa kwake. Alikuwa amevizoea. Freedy alipoligundua hili, akahaidi kumsaidia. "Niambie ukweli unampenda huyu mumeo?" Akamuuliza kwa moyo uliojaa wivu na kisasi. "Japokuwa ananitesa, bado nampenda. Yeye ni mtu mzuri na mwema sana!" Kainaaz akamtetea. "Namna gani anakupiga kila siku na bado unampenda huyu mtu katili? Haya sikia, ninao mpango hapa...em sogea!" Akamnong'oneza mpango wa siri ambao ungekuwa msaada wa moja kwa moja kwake. Msaada ambao ulipakwa rangi zote za dhambi ya mauti. Mapenzi yale yale yaliyosababisha Ngoswe apoteze nyaraka muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi, yakamfanya Freddy abadilike na kuwa kiumbe katili. Ama mapenzi yana nguvu sana jama. Akamvizia mume wa Kainaaz usiku usiku katika mida yake ya kufanya mazoezi ya viungo. Akamuua! Akapambana kuuficha na kuufuta ushahidi, akakamilisha uovu wake. Kwake hili lilikuwa ni jambo la kijasiri zaidi kulifanya tangu azaliwe. Alikuwa analipambania penzi lake kwa Kainaaz. Moyo wake ukiwa na ushindi uliosindikizwa na amani na salama, akarejea kwa Kainaaz akiwa na maua mkononi. Hamadi! Hakuamini kile ambacho macho yake yalikishuhudia. Kainaaz alikuwa na mwanaume mwingine. Mwanaume ambaye alitambulishwa kwa jina la mpenzi. Maajabu! Kainaaz alimtumia Freddy kufanya mauaji haya ili tu apate umiliki wa mali za mumewe na awe huru. Shoti ilitambaa kwenye mwili wa Freddy, hakuamini kile alichoambiwa. Akajaribu kumkumbusha Kainaaz ahadi zao na maneno yote matamu walizowahi kupeana. Jambo pekee aliloambulia ni kufukuzwa kama mbwa. Kitendo alichokifanya akikusudia kihesabike kama upendo, kikawa kama pingu za chuma kwake. "Ukiendelea kunifuatilia...nitakushtaki kuwa umemuua mume wangu!" Hakuamini. Ni mapenzi tu. Ni mapenzi ambayo yalimfanya amuuwe mtu asiye kuwa na hatia ili yule ampendaye aishi kwa amani mbali na mateso. Kumbe alikuwa amempenda nyoka mwenye sumu kali. Sumu ambayo inamtambaa kwenye mishipa ya damu yake na kuisuta nafsi yake juu ya dhambi aliyoifanya. Alipenda vibaya, na sasa upendo unampiga visu vya kifua. Freddy Ginwala, Akauzika ule upole na hulka yake ya utulivu. Akavaa kofia mpya ya ukatili. Sasa akawa muwindaji aliye tayari kulipa kisasi katika namna ya kisayansi zaidi. Daktari wa meno akapiga hatua moja kubwa. Simulizi ikageukia upande wa pili. Sasa sio mapenzi tena ni hekaheka na visasi. Ni filamu ya kusisimua yenye mseto mtamu wa hadithi kama asali. Ndani yake kuna mapenzi, visasi na upelelezi wa kisaikolojia. Hutabandua macho yako mara tu utakapoanza kuitazama. Inaitwa FREDDY imetoka mwaka 2022. Imeandikwa na Godlove Kabati ✍🏼


RIWAYA; *KIBIRITINGOMA* MTUNZI; *GODLOVE KABATI* KWENDA KWA; *MAJIVU YA FASIHI channel* WhatsApp; 0763204351 ----------------- SEHEMU YA TISA *Usijidaganye...* *Siri ni ya mtu mmoja tu.* *Ikiwa ya wawili hiyo siyo siri tena, itatambaa kwa kasi ya ajabu...ikiwa na onyo lilelile la "Usimwambie mtu, hata mimi nimeambiwa nisiseme."* *Hii ni sehemu ya tisa.* TAHARUKI! Aliyafikicha macho yake kwa viganja vya mikono yake ili ajihakikishie kuwa ile sio ndoto. Kisha akaigeuza ile simu ili aone kama ni ya kwake au labda ni ya mtu mwingine. Nayo ikawa ni kama inamwonya kuwa chondechonde, asiikane. Akaitambua kuwa ni simu yake. Hayo hayakutosha. Akaitazama video ile kwa mara nyingine. Mara ya nne. Akajihakikishia kuwa hawa viumbe wanaopinduana kwenye video hii anawatambua. Huyu wa kiume hakumtambua kwa sura na majina tu, alimtambua mpaka kiroho na kimwili. Alikuwa ni yeye mwenyewe. Didas akajipapasa mfukoni mwake na kutoa leso. Huku akiitazama simu yake, akajipangusa matone ya jasho yaliyokuwa yameanza kuota kimafungu kwenye paji la uso wake. Yakatengeneza michirizi kwenye shingo lake. Simu ikamponyoka na kuanguka sakafuni. Hapa akagundua kuwa hata mwili wake ulimtetemeka sana, ni kama ulioshtushwa na video hii ya ajabu. Akainama na kuikota upesi akichelea kuonekana na mtu yeyote eneo lile licha ya kwamba alikuwa peke yake eneo hili. Asubuhi hii ya saa tatu kasoro, joto la mwili likamzidia. Koti la suti yake nadhifu akaliona kama mzigo mkubwa wa kilo hamsini juu ya mwili wake, akalivua. Tai yake shingoni akaiona kama kitanzi kilicho tayari kumpa mkataba wa kuiaga dunia, akailegeza katika namna ya haraka mpaka akaichomoa katika fundo lake. Didas alibabaika. Eneo lile ambalo dakika kadhaa nyuma aliliamini kama eneo lake bora kwa ajili ya mapumziko, akaliona sio salama tena. Simu yake akaiona kama bomu ambalo muda wowote linaweza kulipuka kama tu ikiwa mkononi mwa watu wengine. Akaitia kwenye mfuko wa suruali lake kwa umakini mkubwa kisha akapiga hatua kubwa kubwa kukitafuta chumba cha ofisi yake. Njia nzima kuelekea ofisini mwake, macho yake ni kama yametiwa kiwi. Hakuona wala kutambua mtu au kitu chochote. Wafanyakazi wakamshangaa, "Bosi amekuwaje tena?" Waliulizana na hakuna aliyekuwa na majibu. Siku hii Didas alionekana kuwa wa tofauti kwao kuanzia asubuhi. Aliwahi mapema kabla yao, alikuwa mwenye tabasamu na bashasha tele usoni na alikuwa mchangamfu mno kuliko walivyomzoea. Lakini ajabu ndani ya kipimo cha masaa mawili kama sio moja, Bosi wao Didas huyu hapa amebadilika. Miguu yake inapishana kwa kasi koridoni. Anahema juu juu, koti mkononi, tai imemlegea shingoni. Didas amepagawa! "Sipokei simu wala mtu yeyote kuanzia muda huu. Nina kazi ya maana sana naifanya ofisini, sitaki usumbufu!" Yalikuwa ni maagizo yaliyotolewa na sauti inayoamrisha kutoka kwa Didas kwenda kwa karani wake. "Sawa bo-" Hakusubiri jibu. Upesi akauvamia mlango wa ofisi yake na kuzama ndani, kisha akaubamiza mlango kwa nguvu na kitasa kikasikika kikitekenywa na ufunguo kwa ndani. "Kha! Kulikoni tena?" Karani huyu mrembo wa kike ,akapigwa na butwaa. Huko ndani, Didas akazima kila kifaa cha umeme alichokiona kwa hofu ya kuvujisha kile anachotaka kukifanya, safari hii hakutaka kufanya makosa. Akaikagua ofisi yake kwa umakini akihofia kuwa labda kuna vinasa sauti vilivyotegwa, visije vikamtia upya majaribuni. Aliogopa sana. Akamuogopa sana yule mtu aliyempigia simu na kumpa maelekezo kama haya yaliyoambatana na hii video ya aibu. "Ameturekodi muda gani huyu hayawani?" Akajiuliza yeye na nafsi yake. Kabla hajaanza kugawanya lawama, akajipa dakika chache za kukaa na kutafakari. Akiwa ameketi juu ya kiti chake kikubwa kinachonesa qmbacho muda huu kilikiwa kigumu kama chuma, akavua shati na kubaki na fulana. "Labda pale hotelini walitufanyia uhuni? Au...walitega kamera kwenye koti langu? Au Bebe...hebu ngoja!" Akaipekua orodha ya namba za mawasiliano kwenye simu yake, akitafuta namba ya Bebe. Akampigia, simu yake haikupokelewa. Akampigia mara ya pili, ya tatu na ya nne bila mafanikio. "Shit!" Akasonya na kupiga ngumi juu ya meza yake kwa nguvu. Akiwa kwenye taharuki, akajikuna kidevu chake kilichosheni ndevu nyingi. Fikra zake zikapaa na kumuonesha kila rangi ya hatari ambayo hakuwahi kuomba imkute maishani mwake. *"Hiki ni kipande kidogo tu cha keki nzima."* akausoma upya ule ujumbe ulioambatana na video ile. Safari hii aliuona ni kama umeandikwa kwa mwandiko wa kishetani, na aliyeuandika anamcheka kwa dharau. Didaa akatetemeka kwa hofu. "Ni kipande cha keki. Labda ipo au zipo ndefu zaidi ya hapa. Labda huyu jamaa video zangu za siku nyingi, hata kabla ya hii ya jana." Akatamka kwa huzuni. "Vipi...vipi kama akizitundika video zote mitandaoni na watu wa rika zote wazione. Nitaweka wapi sura yangu mimi Dida?!" Akahamishia mikono yake kichwani. Kumbukumbu zake zikamsulubu, zikimkumbusha matukio na matendo yake yote maovu aliyoyafanya na Bebe. Chozi likamdondoka! Akafikiria namna atakavyoaibika, namna atakavyoichafua sura ya kampuni. Akaona waziwazi atakavyoporomosha soko la bidhaa zao, atakavyouangusha ufalme wa biashara uliojengwa kwa muda mrefu tena kwa jasho, machozi na damu. "Eeh Mungu wangu!" Macho yake yakawa ya moto kwa machozi. Alikuwa na muda mrefu tangu ametoa machozi, lakini leo hii hofu ya matokeo ya kumbukumbu ya dhambi zake za nyuma, inamtoa machozi. Alipokumbuka kuwa hata mwanaye mkubwa Junior ana simu janja aliyompatia kama zawadi, Didas Ambrozi akahama kutoka kwenye kiti na kuchutama sakafuni. "Shenzi kabisa!" Akafoka kimyakimya. "Mtoto mdogo kama yule anamiliki vipi simu ya mkononi?" Haikujulikana kama anamlaumu mwanaye aua anajilaumu yeye mwenyewe aliyempatia. Mwanaye ambaye nd'o kwanza yuko elimu ya msingi, darasa la sita. Tena ni mjuvi na mtundu wa kuperuzi kwenye mitandao ya kijamii. Hakuna kurasa yoyote ya watu maarufu ambayo hakuijua. Didas siku zote alichekelea na kudai kuwa hiki ni kizazi kipya, kizazi cha teknolojia, hivyo haoni kosa la mtoto mdogo kuijua mitandao na kuitumia. Alichoka! Fikra hii ikaambatana moja kwa moja na matokeo baada ya mkewe kuiona video hii ambayo aliitafsiri kuwa ni video chafu. Kwa nini hakukifikiria kitendo kile alichokifanya kuwa kichafu na badala yake aichafue video? Alijua mwenyewe. Kwa mara nyingine akaona kuwa huenda hii ikawa hoja kubwa na yenye mashiko kwa mkewe anayelumbana naye kila uchwao. Akaifikiria heshima aliyojijengea katika kanisa lake la kiinjili analoabudia, heshima na busara zake vikampatia cheo cha kuitwa *mzee wa kanisa*. Hamadi! "Nitapoteza kila kitu!" Akatamka kwa sauti ya chini huku akipambana kulifuta jasho usoni mwake. "Kwamba magazeti yataaandika, SAKATA LA MREMBO FROLA NA BOSI WAKE LAITETEMESHA DAR." Akawaza. Hakutaka kusubiri mashambulizi haya ya kushtukiza yamfuate alipo... Akaamua kujihami kwa silaha alizo nazo. Na silaha yake kubwa aliyoitegemea muda huu ni pesa. "Anataka fedha huyu. Aseme kiasi chochotekile anachokitaka nitampatia! Ili mradi tu, aniondolee hii aibu!" Akaamua aipigie namba ya mtu yule asiyemfahamu. Ikapokelewa upesi. Akaanza kujitetea mara moja, "Nakusikiliza wewe. Niambie unataka nikulipe sh'ngapi? Nitajie kiasi unachokitaka tuyamalize." Akatamka kwa jazba iliyochanganyikana na woga. "Kunilipa? Kiasi? Sielewi unaongelea nini mzee wangu." Katika namna isiyotegemewa sauti ile ikajibu kwa utulivu. "Come on! Nisikilize kijana...usitake kushupaza shingo yako bwana. Ni matarajio yangu kuwa unaelewa ni nini namaanisha. Tafadhali, niambie unataka kiasi gani tuimalize hii kesi." Didas akirejea taratibu juu ya kiti chake akarusha karata yake nyingine. "Mzee...mimi nimebahatika kukufahamu japo kwa jina, lakini wewe hunijui. Nimefanya wema wa kukutumia kipande cha keki tufaidi pamoja. Na nikakueleza kuwa uniafute ili tujadiliane juu ya ladha yake, hivyo tu!" Akamalizia sentensi yake akiwa na cheko la dharau. Didas akazidi kuchanganyikiwa, akatoka kwenye kiti chake kwa mara nyingine, akaanza kutembea akizunguka zunguka mule ndani. Alitamani amjibu kwa kumrushia matusi mazito lakini wakati huu alihitajika awe mjinga na mnyonge, akachagua kubaki kimya. "Nisikilize mzee wangu..." sauti ile ikatangaza ubabe. "Maelekezo yote atakupatia huyo malaya wako. Ni maelekezo yanayohitaji utekelezaji wa haraka, mna siku moja tu. Ama sivyo vyombo vya habari na mitandao vitapata habari mpya inayovutia!" Sauti ile ya kukoroma ikaweka kituo na simu ikakatwa! Moyo wa Didas ukaruka mapigo kadhaa baada ya kusikia maneno yale. Kwa mara ya kwanza maishani mwake akamuweka Bebe katika orodha ya viumbe hatarishi wa kuogopwa. Akawa na asilimia zilizotosha kuvunja imani yake kwake. "Kumbe anahusika!" Donge kubwa la hasira likajiunda kifuani mwake. Akiwa harakati za kuvaa upya mavazi yake ili aondoke ofisini mule, simu yake ikaita. Mpigaji sio mwingine bali ni Bebe. Akashusha pumzi na kuitazama simu ile. Akaipokea akiwa anatukana matusi mengi kimoyomoyo. Lakini ajabu! Akapokelewa na sauti ya kilio na malalamiko. "Daddy...tuna siku moja tu Daddy!" Bee alikuwa analia na kuomboleza. Achana na kilio chake wala maombolezo yake. Kilichomzuzua Didas ni ile sauti nzuri na tamu ya Bebe, hasa akiwa kwenye kilio. Hata kama angekuwa anaigiza, kilio chake kingetosha kabisa kumpa msamaha na akauepuka moto wa milele. "Kuna nini Bebe? Mbo..mbona unalia eh?" Didas anazuga haelewi kinachoendelea, amevaa ujasiri bandia wa kiume. "Ametupa siku moja tu mpenzi wangu...siku moja tu!" Kitendo cha kuitwa *mpenzi* kikawa kama msumari wa moto kwenye kifua cha ujasiri wa Didas. Akasahau hasira yake yote aliyokuwa nayo dhidi ya Bebe. Akachukua jukumu la kumbembeleza na kumuondoloea hofu. "Usijali kipenzi...kila kitu kitakuwa sawa. Hili nitalimaliza mimi mwenyewe dear. Huyu nyang'au nitamtia adabu, hatatuchezea michezo yake tena! Uko wapi sasa hivi?" Didas akajitutumua na kuonyesha uanaume wake. Bebe akamueleza kuwa yuko nyumbani kwake. Wakapanga mahali pa kukutana ili wachore ramani ya kuokoa kwenye msitu huu mpya walioingia na kupotea ndani yake. Didas akiwa na huruma tani mia kwa Bebe. "Huyu dogo atanitambua mimi ni nani!" Akaweka nia yakumuangamiza huyo aliyewachezea mchezo huu. Hakujua! Hakujua! --------------------------- Itaendelea Jumamosi Tuendelee kusambaza link ya chaneli na kutoa maoni yetu kupitia 0763205351.