
MAJIVU YA FASIHI 📖🪶
February 5, 2025 at 08:44 PM
*`SHAMBA LA HELA`*
Yake; *Godlove Kabati*
WhatsApp; 0763204351
--------------------------------
SEHEMU YA KUMI NA NANE
*ANAITWA FRANKO DARIO*
----------------------------
Kuduwaa ni msamiati wa Kiswahili.
Na hapakuhitajika msaada wa kamusi kwa mtu asiyefahamu maana ya msamiati huu kwa wakati kama huu.
Kama tu mtu angetaka kufahamu maana halisi ya kuduwaa tena kwa vitendo, basi asogee hapa barabarani na kumtazama Abednego.
Alikuwa ameduwaa!
Mkono mmoja kiunoni, mwingine ukishikilia simu ile ndogo mbayo aliitazama bila kupata majibu yoyote yale. Ilikuwa ni kama anaiuliza maswali magumu na yenyewe ikakosa majibu ya kumpatia.
Ubaridi uliosukumwa kwa pepo nyepesi kutoka katika vilindi vya ziwa Viktoria, vikamkumbusha kuwa amepoteza dakika kadhaa akiwa ameduwaa. Akazinduka ghafla, na kugundua kuwa amefanya makosa mawili makubwa bila kujua.
Kwanza amefanya uzembe wa kumruhusu Feruzi aingie kwenye gari la watu wasiojulikana.
Na kosa la pili, ameikata simu ya mtu anayefanana na neno 'hatari' mpaka amelizidi neno hatari lenyewe.
Akakurupuka na kuipigia namba ile lakini sauti nyepesi ya mwanadada ambaye siku zote huwakumbusha wateja wa mtandao huo wa simu kuwa hawana salio la kutosha, ikamkasirisha. Akajipekua upesi na kutoa simu yake kubwa...akazinakiri nambari zile kwa umakini na kuzipigia.
Aliyepokea hakumtarajia,
"Namba unayoipigia haipatikani kwa sasa, tafadhari jaribu tena baadae.
The number you're calling...isn't reachable at the moment, please try again later..."
Ni yuleyule mwanadada...ambaye safari hii alitumia lugha mbili ili aeleweke vizuri endapo tu lugha ya Kiswahili isingeeleweka.
Abednego akapiga tena na tena, akiwa mwingi wa hofu na mashaka. Majibu yakabaki kuwa yaleyale, mepesi lakini yanayokera.
Na kama angeendelea kupiga zaidi huenda yangebadilika na kuwa,
"Aisee we mteja! Huu ni usiku aisee, tusisumbuane... Huyo mtu si ushaambiwa hapatikani? Kulikoni tena?"
Akashusha simu kutoka sikioni na kufuta jasho usoni mwake kwa kiganja cha mkono.
"Nimeyakanyaga!" Akatamka akiwa na uhakika kuwa amejiingiza kwenye mchezo ambao amefika na kusukuma kete bila kujua kanuni za mchezo.
Akatazama kulia na kushoto, hakukuwa na kiumbe hai chochote kile kilichokuwa barabarani pale.
Kwa mbali akaona magari ya askari wa doria yakisogea taratibu kuja upande ule alikokuwa. Daima hakuwapenda polisi na damu yake na polisi havikuwahi kupikika chungu kimoja. Ni kweli kuwa kwa desturi watu wengi hawawapendi polisi. Lakini kwake hadithi ni tofauti kidogo.
Tayari ameshapitia masaibu ya kutosha kujaza vitabu vya uhalifu kwenye maisha yake, uhalifu uliomfanya ajenge tabia ya kukaa nyuma ya nondo za rumande mara kwa mara kiasi kwamba akakaririka na polisi wa mji huu.
Biashara zake za magendo na matukio kadhaa ya wizi na uhalifu vililifanya jicho la polisi likae kwake daima.
Wengine kila alipokutana nao walimkamata pasi na sababu wakiamini kuwa huenda ana makosa fulani, halafu watamuachia wakijiridhisha kuwa hana hatia.
Uhalifu ulimzoea, ukawa tabia yake.
Mara hii akiwa amevaa nguo zisizoeleweka tena katika viwanja hivi karibu na ziwa, hakutaka kukamatwa kwa mara nyingine hata kama angekuwa na makosa, halafu alazwe rumande mpaka asubuhi tena kwenye wakati huu ambao amevuruga kazi aliyopewa na mtu mwenye sauti iliyomchachafya na kumfanya atii, sauti ya mtu ambaye ameambiwa kuwa ni zaidi ya hatari.
Bwana mwenye kovu usoni.
Upesi akakata kona kuelekea kwenye barabara iliofunikwa kwa vivuli vya miti mikubwa ya mikaritusi. Vivuli ambavyo daima viliifanya barabara hii iwe ya kutisha hasa wakati wa usiku. Weusi wa giza la mahali hapa ulikoza sana na kutengeneza mseto wa giza na kivuli.
Kulikuwa na kasumba miongoni mwa wakazi wa mji huu kuwa barabara hii hutembelewa na majini hasa wakati wa usiku. Kasumba ambayo haikuwahi kuhalalishwa kuwa kweli, mpaka pale kulipokuwa na taarifa za baadhi ya watoto na watu kupotea ghafla na wengine kulalamika kuwa wameona viumbe vya ajabu ajabu vikifanya riadha kutokea ziwani na kuja kwenye barabara hii kwenda na kurudi. Na ni hapo watu wakachukua tahadhari kutembea eneo hili wakati wa usiku.
Ni kasumba hizi hizi za imani juu ya majini na kupotea kwa watu zikalifanya jeshi la polisi kuongeza ulinzi maeneo haya hasa wakati wa usiku.
Mchanganyiko wa imani ya fununu hizi na hofu iliyomkumba juu ya mambo yaliyotokea dakika kadhaa nyuma vikamfanya aongeze mwendo. Akatembea upesi kwa hatua ndefu ndefu na hakutaka kusimama.
Akatazama juu kwenye matawi ya miti ile iliyoweka mifano ya maumbo ya watu walio tayari kumrukia, akameza mate kwa woga na kuongeza kasi.
Akaufikia mti mmoja upesi na kujibanza kupisha mwanga wa taa za gari lile la askari waliokuwa doria akajificha na kwa bahati gari lile halikuchukua uelekeo wa barabara hii ndogo, likanyoosha mbele.
Akapumua pumzi nzito iliyompa ahueni, kisha macho yake yakarejea kulikabili giza na kivuli kizito cha miti hii mikongwe.
Akaendelea kutembea kwa kasi aondoke mahali hapa, ghafla akasikia sauti za vicheko vya viumbe wasioelewekawaliokuwa kwenye matawi. Tumbili sio tumbili, ndege sio ndege, popo sio popo. Akasimama na kuangaza bila mafanikio.
Alikuwa amepunguza hatari ya kukamatwa na polisi bila makosa, na sasa amebakiwa na hatari ya kukumbana na majini katili, majini wala watu!
Bundi akalia!
Matawi yakatikisika!
Popo kadhaa wakarukaruka wakipepea karibu zaidi na uso wake!
Mchanganyiko wa matukio haya yote ndani ya sekunde chache vikamkumbusha juu ya hadithi za majini wa viwanja hivi. Akaamua aanze mbio.
Ghafla kiumbe kikubwa chenye uzani wa uzito wa juu kikatua mbele yake kwa namna ya kutisha,
TIII!!!
Akakurupuka kwa woga na kujikuta amemuita mama yake mzazi na tayari makalio yake yako ardhini, mikono yake ikifanya kazi ya kutambaa kinyume kinyume kwa woga.
Mbele yake alisimama mtu mwenye umbo kubwa, ambaye licha ya kwamba hakuweza kumuona vizuri bado angeweza kuukadiria ukubwa wa misuli yake na tambo la mwili wake wa kutisha.
Tobaaa! Alitamka kimoyomoyo, macho yake yaliyokuwa kwenye nusu wa utimamu na upofu yakamuaminisha kuwa sasa amekutana na jini lenyewe mubashara.
Jini lililodondoka kutoka kwenye matawi ya mikaritusi mirefu ya viwanja hivi vya Gymkana! Akapigia mstari kuwa ule ndio mwisho wa maisha yake.
"Wewe ni nani?..." Sauti nzito ya kukoroma ikatoka kinywani mwa yule jini-mtu.
Kilichofuata ni ndondi na hekaheka kati ya kigugumizi na ulimi wa Abednego Kagoye. Akashindwa kutamka neno lolote lile.
"Wewe ni Abednego Kagoye?...".
Hili halikuwa swali tena masikioni mwa Abednego. Likageuka upanga wa moto unaokitwa kwenye moyo wake wa nyama.
Amenijuaje?
Hapa akagundua kuwa anaongea na jini, na yeye ni kitoweo kijacho cha huyu jini.
"Ee...eheeee ni ni mimi!"
Yule jini-mtu akamsogelea kwa ukaribu na yeye akazidi kutambaa kwa mikono na makalio yake kinyumenyume.
"Tulia hapo!" Akaamrishwa kwa sauti nzito ya kutisha na mwili wake ukakamaa ghafla kwa woga, akatulia.
Macho yake yakaanza kulizoea giza na akaweza kukiona kiumbe hiki kadri kilivyomsogelea taratibu.
Ebooo! Sasa mbona hana mapembe? Akajiuliza maswali yeye mwenyewe akijijengea taswira ya maumbo ya majini ya kutisha aliyozoea kuyaona kwenye filamu na picha.
Akajifariji kuwa huenda mtu yule akawa jini aliyemjia kwenye umbile la mtu wa miraba minne...huenda, huenda.
Yule jini-mtu akamkaribia kisha kwa kubonyea chini akachuchumaa na kutazamana na Abednego. Alikuwa anapumua kwa hasira, pumzi zikipishana kwa fujo kwenye tundu za pua yake.
Katikati ya usiku wa saa tano, viumbe hai wawili wanatazamana, mmoja akiwa mwingi wa hofu na mashaka mwingine akiwa amevimbiwa kwa hasira na jazba.
Ilitisha sana kuwatazama.
"Sogea karibu!" Ikawa amri nyingine ambayo haikuhitaji mjadala.
Vilevile kwa kutambaa makalio na mikono, Abednego akajivuta na kusogea karibu kidogo na yule jini-mtu.
Akiwa bado hajajiandaa kutulia ili aendelee kujiuliza juu ya masuala ya maumbile na uumbaji wa kiumbe hiki cha ajabu mbele yake, akakutana na kofi kali ambalo hakulitegemea asilani.
Aliona mchanganyiko wa vimulimuli vya rangi nyeupe na bluu kisha kichwa kikawa kizito. Na hakutambua kinachoendelea.
********
Gari lilitembezwa kwa kasi barabarani na masaa kadhaa yakapotea wakiwa palepale barabarani.
Wakati huu wote vijana wale watatu wageni waliodai kuagizwa kumfuata Feruzi walichagua kukaa kimya bila kumsemesha Feruzi neno lolote lile.
Na ukimya huu ukawa kidonda kinachowasha kwa Feruzi. Akaamua kukikuna.
"Wajomba eh...kwani huyu bosi wenu kawaambia mnipeleke wapi wajomba? Ma'ke ni muda mrefu sana tangu tumeanza safari..."
Swali lake halikujibiwa.
Feruzi akaguna na hakutaka kuongeza swali jingine.
Haya ni majambazi sugu yanayoweza kuua kama yakitaka na tena mkuu wao ndio moto wa kuotea mbali! Yeye ni mwalimu wao wa kozi ya mauaji na wao ni wanafunzi makini sana kwenye darasa lake. Wazo hili likatembea kwenye ubongo wake na akaufyata ulimi wake.
Akajipapasa kutafuta simu yake ili afahamu muda na hakuipata, hapo akagundua kuwa ipo kwenye miliki ya Abednego.
Akaamua kuwa mpole mpaka atakapofikishwa eneo maalumu lililokusudiwa na bwana mwenye kovu usoni.
Gari likakata kona na kuingia kwenye ujia ambao ulikuwa wa siri sana kisha likaibuka kwenye barabara iliyojitenga kwenye muinuko na kwa mbali ukaonekana uzio uliozunguka jumba kubwa la kifahari.
Wakiwa bado mbali, walinzi wakachangamka na kufungua geti la uzio ule. Ilionekana kuwa gari lao lilifahamika hata kwa mbali na lilifunguliwa kutokana na taarifa maalumu.
Gari likamiminika mpaka ndani ya uzio ule na mbele yao lilisimama jumba kubwa ambalo lingehusishwa moja kwa moja kwenye orodha ya majumba ya kifahari.
Liliwaka na kumetameta likipendezeshwa kwa taa na mazingira mazuri ya eneo lile, yaliyogubikwa kwa ukimya na utulivu.
Gari likasimama na wakatoka wakimsindikiza Feruzi kwa ustaarabu bila bughudha yoyote ile. Ni ustaarabu huu uliomfariji Feruzi na kumuondolea hofu akajiona yuko kwenye mikono salama.
Akatupa macho yake kwenye mandhari ya eneo la jumba hili lililofanana na kasri, akaridhika kuwa kuna watu matajiri wanaoishi kwenye mazingira mazuri na hawa wanapumua na kuna watu wanaoishi kwa kuhema. Yeye akajiweka kwenye kundi la wale wanaohema.
Mguu kwa mguu wakasogea mpaka mlangoni. Ulikuwa mlango wa kisasa unaofunguliwa kwa utaratibu maalumu.
Ukafunguliwa na wakapita mpaka ndani.
Feruzi akategemea kukutana na sebule kubwa ya kifahari lakini ikawa sivyo.
Wakapita vyumba kadha wa kadha, wakiwa kimya. Wakashuka ngazi na kuelekea chini.
Hapa Feruzi akabaki kwenye mshangao wa namna jumba hili lilivyojengwa.
Kumbe kuna vyumba vya chini kwa chini? Akaendelea kutalii.
Huko akafikishwa mpaka kwenye chumba kimoja wapo kilichofanania na ukumbi mdogo kiasi. Akaonyeshwa mahala pa kuketi.
"Bosi wetu anakuja hapa kuonana na muda sio mrefu. Ukiwa unamasubiri tukupe kinywaji gani?" Mmoja kati ya vijana wale akamuuliza na wengine wakabaki kimya, wamekauka kama kuni.
"Pepsi!" Feruzi akatamka.
Wakatoweka na kumuacha ukumbini pale.
Akasimama na kuanza kushangaa baadhi ya picha na mapambo yaliyopambwa kwenye kuta za mahali hapa.
Zilikuwa picha za watu mbalimbali ambao wanaonesha kuwa na nguvu na utajiri mkubwa sana kutokana na suti za gharama walizovaa na mwonekano wa sura zao. Sura zilizotakata na kunawiri lakini zikakosa tabasamu.
Akiwa bado anashangaa picha hizi, binti mrembo akaingia ukumbini pale akiwa na kinywaji alichokihitaji.
Feruzi akamchangamkia na kumsalimia kwa utani kidogo, lakini binti yule naye akawa mkavu. Hakumjibu Feruzi na wala hakumchangamkia. Akaweka kinywaji mezani na kuondoka.
"Hivi hawa watu wa hapa wakoje? Yaani ina maana tabasamu limehitimu kukaa usoni kwao na maneno wameyapa likizo ya daima au?" Akajiuliza.
Akasogelea kinywaji kile na kukimimina kwenye glasi. Kabla hajaanza kukifaidi tu...akaona picha ambayo ilimshtua sana na katika mshtuko wake akajimwagia kiasi kidogo cha kinywaji kile.
Akaisogelea picha ile na kuigusa kwa udadisi zaidi.
Ilikuwa picha ya mtu anayemfahamu na bila shaka ndiye anayekuja kuonana naye.
Ni yule yule bwana mwenye kovu kwenye jicho lake la kulia.
Sura yake ni ileile yenye kila dalili ya kuchoshwa na dunia na inayotangaza kisasi muda wote.
Kwenye picha hii amevaa suti nzuri ya gharama na kofia nzuri ya wastani...hana lile koti lake kubwa, hana ile kofia yake pana ya kutisha na wala hana fimbo yake.
Feruzi akabaki kufanya hesabu za milinganyo kati ya mtu anayemjua na picha anayoiona.
Labda hapa alikuwa mdogo? Akajiuliza.
"Anaitwa Franko Dario!" Sauti kavu ikapasua anga kutokea kusikojulikana. Feruzi akageuka na kukutana uso kwa uso na mtu wa ajabu..mtu ambaye alifanya glasi yake imponyoke na kuanguka chini, ikapasuka na kuchafua marumaru ya sakafu ile.
"We Mtemi..wewe!" Akatamka kwa mshangao mkuu.
-------------------------------
Ayaaaaae 🙆♂️
Ni huyu huyu marehemu Mtemi Moringo, tunayemjua sisi au huu ni mzimu wake?
Hapa nd'o tunajua hatujui.
Kama kawaida share link ya chaneli. Acha reaction na toa maoni pale unapobidi.
Tutajua Ijumaa hii usiku!
❤️
👍
🔥
4