MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
February 7, 2025 at 08:37 PM
*`SHAMBA LA HELA`* Yake; *Godlove Kabati* WhatsApp; 0763204351 -------------------------------- SEHEMU YA KUMI NA TISA *MWANGA WA GIZA* ---------------‐------------- "Naam...ni mimi!" Mtu huyu mgeni aliyeingia ndani ya chumba pasi na kujulikana alikotokea akamjibu kwa sauti ileile iliyokauka. Feruzi akatamani kuparamia ukuta atafute upenyo na akimbie lakini akagundua kuwa akifanya hivyo ataishia kuchekesha tu. Akajua kuwa yuko mbele ya mzuka wa Mtemi, rafiki yake ambaye siku mbili au tatu nyuma aliambiwa kuwa ameagana na uso wa dunia. Lakini muda huu huyu hapa, anatazamana naye. Akamkagua kuanzia juu mpaka chini...akatambua mara moja kuwa mwili wa Mtemi ulimdhiaki kwa kupoteza gramu nyingi sana ndani ya siku hizo alizopotea na kumfanya aonekane kuwa amedhoofu. Alikuwa na michubuko kadhaa kwenye uso wake na mavazi yake yalikuwa machafu sana na ilionekana kuwa amejenga urafiki mpya na vumbi aidha kwa kugaragara mavumbini au kuoga mavumbi halafu akaanzisha uadui na maji. Kimsingi alifanana na mtu ambaye ameokotwa vitani kisha akatupwa uraiani na kutelekezwa aitafute amani yake yeye mwenyewe. "W-we..wewe ni nani aisee?" Kwa woga akauliza akijitahidi kukaa mbali iwezekanavyo kutoka kwa huyu Mtemi mpya aliyefufuka na kuja hapa mbele yake. Huyu hakuwa Mtemi aliyemfahamu. Huyu alifanana na chokoraa. Swali lake halikujibiwa. Akahamishia macho yake kwenye miguu yake, mguu mmoja ulikuwa peku na mwingine uliruhusu kidole gumba kichungulie nje baada ya kutobolewa kwenye namna isiyoeleweka. Hali yake ilitisha sana. "Umekuaje wewe? Nini kimekukuta mzee? Kwanza ulikuwa wapi..." Mvua ya maswali ikamnyeshea Mtemi. Mtemi hakumjibu moja kwa moja kwa matamshi. Badala yake akatikisa kichwa chake kwa huzuni kisha akatamka kwa sauti ya chini, sauti ya unyonge ... "Nisikilize Feri..." Akatulia kuvutia usikivu wa Feruzi kisha akaendelea huku akipiga hatua kumsogelea kwa ukaribu, akagundua kuwa naye Feruzi alijitahidi kusogea mbali naye kadri awezavyo kwa maana alimuogopa, "Mimi sio mzimu...na wala sikufa kama ulivyoambiwa na Franko Dario! Kwa hio usiniogope.Bado naishi kaka....Lakini maisha yangu ni kama nimeyalipia kuponi. Kila ninapoenda inanibidi niwe nayo ili nizidi kupumua!" Sentensi zake tata zikazua maswali lukuki kwenye kichwa cha Feruzi, ambaye naye hakusita kuyatapika muda huohuo, "Kuponi?! Mbona sikuelewi....na huyo Frenki sijui Franko Daaario ni nani huyo?!" Mtemi akamsogelea kwa karibu zaidi huku akichechemea na kabla hajamfikia akaganda kwa sekunde mbili akiwa ameshikilia tumbo lake, akakunja uso akiashiria maumivu makali. Kisha akamtazama Feruzi, "Hatuna muda mrefu sana wa kuzungumza bro...mimi nimeletwa hapa kama ulivyoletwa wewe. Na hawa watu tutakaokutana nao leo hapa ni watu makini sana ambao hawashangai kuona damu inavuja. Kwao kuua ni ibada!" Maneno yake yakazidi kumchanganya sana Feruzi. "Oyae! Hebu sikia...ina maana na wewe umeletwa hapa na huyo jamaa mwenye kovu usoni au?" Kwa sauti yenye jazba kidogo akalalamika. Mtemi akiwa bado ameshikilia tumbo lake akatikisa kichwa chake kwa huzuni kwa mara nyingine kisha akamtazama Feruzi, akamuinamia na kutamka kwa sauti ya kunong'ona, "Sikia bro....hapa tumetekwa. Na waliotuteka sio huyo jamaa unayemuongelea wewe. Hawa ni watu wengine tofauti kabisa!" Akamjibu. Feruzi akahisi kama mwili wake unaanza kuchemka, joto likampanda na picha za kumbukumbu zikaanza kujijenga kwenye ufahamu wake. Akakumbuka namna alivyokuwa anatafutwa na watu wasiojulikana huko mtaani kwake na sasa huenda ndio hawa hawa wamempata. "Hawa ni kina nani?! Askari au?" Akamuuliza vilevile kwa sauti ya kunong'ona. "Ni heri basi hata wangekuwa ni askari! Hao watakusumbuasumbua..halafu wakusweke rumande, ukiwapa shilingi kadhaa wanakuachia. Lakini hawa ni watu wa kikundi hatari! Nimeambiwa machache tu kati ya mengi yao, na nikaridhika kuwa naenda kukutana na changamoto mpya!" Akamjibu. "Nani amekwambia huyo?..." Feruzi akazidi kuuliza. Maswali yake mengi bado hayajajibiwa. "Franko Dario!" "Ni nani huyo?" "Yule jamaa uliyekutana naye porini yule...akakuachia uende bila kukuhangaisha! Mshukuru sana, alikufanyia upendeleo wa hali ya juu." Mtemi akamjibu na kisha akaongezea, "Ilaaniwe sana ile siku ambayo nilikupatia pikipiki yangu ukaenda kumpakiza yule kiumbe...kama ningekuwa na uwezo hata ile tarehe ningeifuta kabisa kwenye kalenda! Nisikilize rafiki yangu... Nimekutana na watu wa ajabu sana. Sijui ni lugha gani ile wanazungumza. Ni kama wamejitungia lugha yao huko porini. Wanaijua wao! Tamaa yangu ilinisindikiza kwenye mdomo wa mauti, halafu ikaniacha niangamie kabla hata sijamezwa na mdomo huo wa kutisha. Ulifika muda ambao mimi mwenyewe nilikiomba kifo, nikakitamani kifo kwa uchu mkubwa sana. Sikujua kama haya yote yatatokea asilani. Bro..nimepigwa kila aina ya kofi...sikuwahi kuzimia tangu nizaliwe lakini kule porini nimezimia zaidi ya mara kumi. Nimelazimishwa kula ugali mkavu bila mboga wala maji ya kunywa na nilipogoma nikalazimshwa kutafuna ulimi wangu kama mboga." Feruzi akaonekana bado ni mwingi wa maswali na hofu. Akatazama huku na huko kisha akamtazama Mtemi tena, "Enhe kulikoni tena imekuaje uko hapa kama alikuwa bado amekushikilia?" Kabla hajajibiwa, wakakurupushwa baada ya mlango wa chumba kile kilichofanania na ukumbi mdogo kufunguliwa. Kikaingia kikosi cha watu saba ambao walivaa suti nyeusi na wengine wakaongezea makoti makubwa juu ya suti hizo. Miongoni mwao walikuwepo wanne ambao mikono yao ilimiliki fimbo zilizogusa sakafu baada ya kila hatua wanayopiga. Walionekana kuwa ni kikundi maalumu chenye utaratibu wa pamoja au ni chama fulani. Waliingia moja kwa moja huku wakiwatupia macho Feruzi na Mtemi waliokuwa wamesimama. Bila kuuliza chochote wakachukua nafasi zao kwenye viti vilivyokuwepo ndani ya chumba kile. "Jamani karibuni mketi...miguu yenu isije kuingia tumboni aisee, mmesimama muda mrefu sana!" Mmoja kati ya watu wale akawasogezea viti viwili Feruzi na Mtemi ili waketi. Wakatii na kisha kwa kusita wakaketi huku wakiwa na hofu ya ni nini kitafuata baadaye. Feruzi akaamua kuwakagua hawa watu waliowazunguka, yeye na Mtemi wakiwa katikati ya ukumbi huu mdogo. Ni watu wasiowafahamu, watu waliovaa mavazi meusi kuanzia juu mpaka chini, nguo mpaka viatu. Ilionekana kama dhambi kuvaa vazi lolote lenye rangi tofauti na nyeusi. 'Kina nani hawa?' Alijihoji. "Naitwa Franko Don Bosco ama ukipenda waweza kuniita Don Franko, nitafurahi pia. Na hawa ni wenzangu kazini, sitaki kupoteza muda kuwatambulisha mmoja mmoja. Lakini sisi ni wanachama wa chama kimoja. Mwanga wa giza!" Akatamka na kuweka kituo, akaacha maneno haya yazame kwenye akili zao. Kisha akaendelea, "Uuum sisi ni watu wema sana, japo tuna tabia moja mbaya ambayo hata sisi inatushangaza pia. Tunabadilika haraka sana, yaani hasira zetu huwa tunakaa nazo jirani tu. Zinakuja bila kualikwa! Lakini ni kama tu tukivurugwa." Sauti yake nzito iliorindima ndani ya chumba kile chenye ukimya, ikamfanya Feruzi ameze mate kwa woga. Mtemi alikuwa bado amelipakata tumbo lake na ametazama ardhini. Ni kama ambaye hana habari na kinachoendelea. Hata wale wanachama wengine walikuwa watulivu na hawatikisiki ni kama ambao wanaimba wimbo wa taifa. Wengine waliovaa miwani nyeusi kuficha macho yao ndio kabisaaa walifanana na sanamu. 'Mwanga wa Giza!' Ndio neno lililoendelea kupiga honi kwa nguvu masikioni mwa Feruzi. "Mnataka nini kutoka kwetu? Na tumewakosea nini..." Feruzi akajitutumua na kuuliza swali. "Umeuliza swali sahihi sana kijana...lakini haujaliuliza kwenye wakati sahihi." Akaweka pumziko kisha akaendelea, "Waungwana tunatambulishana kwanza bwana...mimi mmenifahamu lakini nyie siwafahamu." Donge kubwa la hasira likajikita kwenye kifua cha Feruzi. Kutekwa na watu ambao hawamfahamu jina lake lilikuwa ni zaidi ya tusi! "Naitwa Feri!" Akajibu kwa kifupi akiwa mwingi wa jazba. "Mtemi" huyu alijibu kinyonge. "Safi sana! Enhe...sasa nadhani tuwekane sawa hapa. Bwana Feri na Mtemi. Sisi tubahaidi kuwa rafiki wema sana kwenu kama tu mkitujibu tunachokitaka na mkatoa ushirikiano wa asilimia mia moja!" Huyu bwana akatamka uso wake ukikusanya hisia mchanganyiko za hasira na chuki. Kisha akasimama na kuwasogelea taratibu, "Ni wapi alipojificha Franko Dario?! Na shamba lake la hela liko wapi. Mkituambia haya mtatoka hapa kama raia huru wa nchi yenu huru, Tanzania!" Mtemi akanyanyua uso wake taratibu na kumtazama Feruzi. Akakutana na macho yanayouliza 'tuseme au tusiseme?'. Kimya kifupi kikapita... ******* Unyevu nyevu uliobeba ubaridi vikashirikiana kwa pamoja kumzindua baada ya kuzirai kwa muda ambao hakuweza kuukadiria. Ngozi ikaitika baada ya kugundua kuwa sehemu aliyopo ni kama amelowekwa ndani ya maji. "Ebooh nini tena!" Akashangaa. Macho yakaungana na ngozi yake iliyopigwa na upeo wa usiku unaokera. Akagundua kuwa amelala kwenye ufukwe na mawimbi ya maji yanayokuja na kuondoka yalikuwa yakifurahia kumlowanisha. "Ayaaa!" Akasimama upesi. Akaangaza huku na kule kama kuna mtu karibu, hakumuona. "Ina maana nimelala hapa ziwani au?" Akajishika paji lake la uso na mara moja akayakumbuka matukio yaliyomkuta mpaka akakutana na kiumbe cha kutisha. "Jini!" Akatamka. Anga la usiku huu lilinyimwa nuru ya mbalamwezi. Na kwa makadirio yake akapima kuwa ule ni usiku wa manane. Aende wapi? Akajipekua na hakuwa na simu zake zote. "Leo nimepatikana!" Akajisemea. Kwa mbali akaona umbo kubwa kiasi la mtu aliyekaa akichezea kitu kama mwangaza wa simu ndogo . Akatulia na kukaza macho yake kwenye giza lile. Akagundua kuwa huenda yule ni mvuvi au mlinzi wa eneo hili la beach akaamua kumsogelea ili aombe msaada wa haraka. Lahaula! Mtu yule alifanana kila kitu na yule kiumbe jini mtu aliyekutana naye usiku huu. Kabla hajachukua maamuzi yoyote yale ya kukimbia au kupiga mayowe mtu akammulika na tochi ya simu ile kisha akapaza sauti, "Njoo uchukue vitu vyako bwana! Mie sina kazi navyo." Hofu ikampotea ghafla na akasogea kwa unyonge. "Kaa hapa!" Akaamrishwa. "Uzembe ulioufanya tuliutarajia...na kwa bahati nzuri sana wewe sio mmoja wao hao waliomteka. Ama sivyo ningekufanya chakula cha samaki leo." Sauti yake nzito ikakoroma. "Sitaki ujue mambo mengi...uliyoyajua yanakutosha kama ukiongeza mengine utaingia matatani. Haya chukua simu zako na yote yaliyotendeka hapa yabaki kuwa siri. Ukiyapeleka kwingine utapotea!" Akamaliza na kusimama, Umbo lake kubwa lilimtisha sana Abednego. "Kaka samahani...kwani we ndiye uliagizwa kuja kumchukua Feruzi au?" Aliuliza swali kwa woga. "Naitwa Dubu! Feruzi ametekwa na mshukuru Mungu wako nimekuacha unaishi!" Mtu huyu akaondoka na kupotea eneo hili. Majibu magumu dhidi ya swali jepesi. Abednego hakuona usalama kuendelea kukaa eneo lile. Akaamua kuichangamsha miguu yake kukimbia kadri ilivyoweza kumbeba. Akakatiza barabarani kwa kasi nguo zake nzito zilizolowana zikamfanya mzito, akawaza kuzivua. Akaanza kwanza kutelekeza koti lake, kisha akatoa suruali ile kwa kuondoa mguu mmoja tu, Mara paap! Gari la doria hili hapa. Akamulikwa na taa zenye macho makali yanayotema mwanga mkali mno. Kwa woga akaanza kukimbia huku mguu mmoja wa suruali uko nje na mwingine umevaliwa. "Aisee yule nani yule?! Sio Kagoye yule?" Askari mmoja akauliza kwa shari. "Ni yeye aisee...halafu mbona kama kalowana, hebu tumkamate haraka!" Mwingine akadakia kwa ushabiki. Mbio za miguu ya mwanadamu hazijawahi kufua dafu mbele ya matairi ya gari. Abednego akiwa kama kichekesho akaangukia kwenye mikono ya wabaya wake kwa mara nyingine. Akiwa vilevile anayetetemeka kwa baridi na unyonge, wakampeleka moja kwa moja mpaka kwenye chumba alichokizoea, chumba chenye giza na harufu za ajabu ajabu ambazo ziliwafukuza mpaka nzi na mende. Rumande! Wakamkebehi huku wakimcheka kuwa hawataacha kumuandama mpaka aache uhalifu na biashara za magendo. Maswali aliyoulizwa hakuweza kujibu hata moja, Kwa nini anazurua usiku tena kwenye maeneo yaliyokatazwa? Kwa nini amelowana namna ile? Na kama hana makosa ni kwa nini amekimbia haraka baada ya kumulikwa na gari la doria maarufu kama tenga?! Wakaenda mbali na kumuuliza ile simu ya pili kaitoa wapi na wakati wamemzoea kuwa na simu ile moja tu wanayoifahamu? Ni Abednego Kagoye dhidi ya watesi wake wa siku zote. Hii vita yao, sisi hatuingilii. Usiku huu amekamatwa muda mbovu, muda wa majini, muda wa Dubu! ---------------------------- Mambo ni moto! Utamu kolea.... Huku wakisondekwa kwenyw kumbi za mahojiano. Kule wanasondekwa rumande. Umewahi kwenda rumande? Nyie kazi yenu ni ileile, Kuacha reaction zenu na kutoa maoni kwenye 0763204351. Maoni ni muhimu sana kwa mwandishi....kukosoa, kupongeza au kutoa zawadi 😃. Tungeendelea KESHO...kama reaction zikifika 10. Kazi kwenu!
❤️ 👍 👏 😢 🙏 🥰 11

Comments