
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
February 11, 2025 at 06:19 PM
*`SHAMBA LA HELA`*
Yake; *Godlove Kabati*
WhatsApp; 0763204351
-------------------------------
SEHEMU YA ISHIRINI
*SHAMBA LA HELA*
--------------------------
Wingu zito liliudhibiti mwangaza hafifu wa mbalamwezi, na kuinyima ardhi ya haki yake ya kupata nuru wakati huu wa usiku.
Muunganiko wa vivuli vikubwa vya miti na sauti za vilio vya wanyama mwitu, vikaendelea kukoleza hali ya kutisha na kufanya msitu huu kuwa mahali pa kuogopeka zaidi.
Katikati ya giza hili hili, jumla ya miguu nane ya wanadamu, ilijongea kwa kutoa sauti za kelele baada ya kukanyaga majani makavu ya miti. Watatu wakiwa mbele na kumuacha mmoja nyuma kwa umbali wa hatua tano. Huyu wa nyuma alikuwa na mguu wa ziada, fimbo ambayo ilimsaidia kupata mhimili kwa maana alionekana kutembea kwa kuchechemea kidogo. Akaamua kubaki nyuma akiwafuata hawa watatu waliokuwa mbele yake.
Mwendo wao ulikuwa wa tahadhari kubwa. Ni kama ambao walichelea kumkurupua mtu au mnyama pori yeyote asiwadhuru kwenye giza hili.
Wakafika mahali ambapo palionekana kumchanganya Mtemi Moringo. Akiwa mmoja kati ya wale waliokuwa mbele, akabaa na kusimama asijue la kufanya. Wawili wengine wakachangamka na kuelekea kwenye magogo makubwa ya mti yaliyojilaza na wakaibuka na vifaa vya kufanyia kazi, majembe na patasi. Kisha wakarudi pale na wakatazama nyuma kwa huyu aliyekuwa wa mwisho. Huyu wa nyuma aliwapatia ishara kwa kuwaelekeza uelekeo na wakaufuata hima.
"Tangulieni mimi nakuja!" Kwa sauti kavu akawaamuru na wakamtii. Yeye akakata kona na kuelekea upande wa kushoto.
Baada ya dakika tano walifika kwenye eneo ambalo lilifunikwa kwa vichaka vingi vya miiba. Wakajitoma ndani yake na kutulia kimya kusubiri maelekezo maalumu.
Kilikuwa kichaka ndani ya msitu, ambacho kilikuwa na ajabu moja tu. Ukiingia, hautaweza kutoka kwa urahisi kwa maana hata mlango ulioingilia hautaweza kuugundua.
Mtemi akaangaza huku na kule akaisikia sauti za mbwamwitu na milio ya bundi. Akameza funda la mate kwa woga akikumbuka baadhi ya visa na hadithi za wachawi na mizuka. Akatetemeka na kupiga hatua nyuma ili tu asimame karibu na wenzie. Akashtuka baada ya kujikuta amekanyaga kitu kisichoeleweka kama ni jiwe linaloteleza au kipande cha mzizi. Akayumba kidogo na kurejea kwenye mhimili wake. Akatukana tusi kali la nguoni na akainama ili ashuhudie ni nini kimemtaka asalimie ardhi.
Akainama na kupapasa ardhini. Mwanzo akadhani labda ameshika jiwe laini lenye umbo lililopangiliwa vyema lakini alipotazama alichokishika na kukaza macho yake gizani, akakutana na fuvu la mtu likimkodolea macho. Hakuamini kama alikuwa anaota au la, akakaza macho yake zaidi na kutazama juu ya ardhi ile akagundua kuwa kuna runso la mifupa ya wafu imetapakaa. Akapiga yowe na kulitupa lile fuvu alililoshika huku akilitaja jina la Mungu wake.
"Oa dogo! Acha utoto..." sauti nzito kutoka kwa mmoja kati ya wale wawili ikamuamuru.
'Utoto?!' Akajiuliza.
Inawezekanaje aambiwe kuwa aache utoto wakati sekunde zilizopita alikuwa uso kwa uso na fuvu la mtu kiganjani kwake?.
"Hapana Duba...ina maana huoni kuwa hapa kuna mifupa ya watu? Eeh? Jamani hili ni eneo hatari sana. Kuna simba mla watu hapa jama." Akalalamika akiwa mwingi wa hofu.
Malalamiko yake hayakuwashtua wawili hawa hata kidogo. Ilionekana kama wanalijua wanalolifanya, wakabaki kimya.
Na hapa akazidi kuchanganyikiwa zaidi. Akateta na nafsi yake bila kufungua kinywa,
"Ina maana hilo shamba la hela linahusisha kafara za maisha ya watu?..Au kila anaesogea huko ni lazima aangukie pua ya mauti?"
Akiwa mwingi wa maswali haya. Ghafla yule kiongozi wao aliyekuwa amepotea kwa muda akarejea akiwa na sanduku dogo na kurunzi.
Akajongea kwa taabu akichechemea na kuwafikia, akampatia Mtemi sanduku lile kisha akatangulia na kurunzi. Sasa yeye akawa mbele na wao nyuma.
Ajabu nyingine ikaisulubu akili ya Mtemi kama radi. Kwa macho yake alishuhudia kabisa kuwa huyo kiongozi hakuwa na silaha yoyote ile zaidi ya fimbo aliyotumia kutembelea tu, tena kwa kuchechemea. Na hawa watu wawili nyuma yake walikuwa wamebeba mapanga na majembe kwa ushupavu. Ni kwa nini wasingemfyeka kama wanamchukia kwa udhalimu wake kwao?
Likawa swali gumu ambalo hata yeye hakuwa na majibu ya uhakika.
Alikuwa amekaa na watu hawa msituni kwa takribani siku tatu na aliweza kuzifahamu hulka zao. Na huyu kiongozi alionekana kuwa shetani ambaye adhabu ya moto wa milele wa jehanamu ilikuwa ni upendeleo mkubwa mno kwake.
Akamlaani kimoyomoyo na kujazilizia laana ile kwa matusi mengi ya mtaani aliyoyakumbuka.
Njia waliyopita ikaonekana kudidimia kama wanaoingia shimoni, lakini ghafla wakaibuka mbele ya kiwanja kilichojitenga na kutengeneza uwazi ambao ulifanana na machimbo ya udongo. Mashimo makubwa yalionekana na makasha kadhaa yaliyochakaa yalirundikwa pembezoni mwa ardhi hii.
"Nikikuambia urudi ulikotoka bila kusindikizwa unaweza?" Kiongozi yule akatamka kwa sauti nzito akimtazama Mtemi usoni.
"Nani mimi?...nitarudije sasa na njia zenyewe nd'o zinachanganya kama hivi?!" Akajibu.
Yule bwana akarekebisha mkao wa kofia yake kubwa ambayo ilimfanya asionekane sura yake.
"Ina maana haya machimbo ya udongo ndilo shamba la hela lenyewe ama? Au wametuleta hapa ili tuchimbe udongo wa ujenzi?" Mtemi akajiuliza yeye mwenyewe na nafsi yake.
"Naitwa Dario!" Akatamka kwa ufupi na kisha akakohoa kidogo. Akatema chini na kugundua kuwa ametema kohozi lililochanganyikana na damu. Akatikisa kichwa chake kwa masikitiko huku mshangao ukazivaa nyuso za hawa aliokuja nao. Hasahasa kwa Mtemi ambaye kwake yeye kila kitu kilikuwa kigeni.
"Hapana sitakufa sa'hivi muda wangu bado..." akajitamkia mwenyewe. Kisha akainua uso wake na kumtazama Mtemi.
"Naitwa Dario...na kwa vile umeshalifahamu jina langu. Wewe ni mmoja kati ya wakulima wangu ambao kama watashiriki vyema kwenye huu mradi wa kilimo changu, basi watakula mema ya nchi!" Akaweka kituo na kukohoa tena lakini wakati huu akainama akilishikilia tumbo lake kwa maumivu kiasi. Ilionekana kama anayeumia.
"Nisikilize! Umetoka huko kulitafuta hili eneo sivyo? Basi hili nd'o shamba la hela lenyewe. Na sisi ni wakulima wenye nia moja tu. Kuvuna mpaka mazao yote yaishe shambani! Haya shime..." akatoa ishara kuwaamuru wale vijana waanze kazi.
Wakachupa na kuanza kulima ardhi ya eneo lile...wakatifua na kuchimba. Mtemi akabaki akishangaa namna vipande vile vya wanaume wa miraba minne vinavyopambana na ardhi kwa majembe na makoleo. Akatambua kuwa hata kipimo cha ugali mkubwa na nyama za kutosha walizokuwa wanakula watu hawa, havikwenda bure.
"Unasubiri nini?!" Akaamrishwa akashirikiane nao. Kwa pamoja wakatifua ardhi na kuchimba eneo kubwa mno. Mtemi alichimba akidhani kuwa hapo wanatifua udongo ili waukusanye wakauze, na ndio maana halisi ya kuitwa shamba la hela.
Lakini akashangaa sana kuwaona Dubu na Duba wakichimba ardhi kwa vipande vipande vya mashimo na kuhamahama kama ambao wanataka kuzika au kugundua kitu kwenye ardhi hii.
Baada ya kazi ngumu ya muda mrefu, Dubu akagonga kitu kama sanduku la mbao ambalo lilisikika na wote. Hapa akatazamana na Duba na wote wakatoa tabasamu jepesi.
Kwa mara ya kwanza kabisa, Mtemi akaliona tabasamu kwenye nyuso za hawa watu. Ambao alikuwa amewapa vyeo vya ukatili na ugaidi.
Wakatumia nguvu zao kwa pamoja kushirikiana kunyanyua sanduku lile kubwa kutoka shimoni na kulitua juu ya ardhi.
Dario akasogea kwa kuchechemea na mkwaju wake mpaka mbele ya lile sanduku. Likafunguliwa...na noti nyingi sana kwa mabunda zilipangiliwa ndani yake.
Baadhi ya noti hizo zilianza kuvunda tayari.
Akazipapasa kwa upole na kutamka maneno kwa sauti ya chini ambayo aliyafahamu mwenyewe.
"Dola za kimarekani!" Akatamka kwa sauti na kisha akamuita Mtemi asogee karibu.
"Hizi noti sijaiba! Ni mali yangu ya halali kabisaa. Lakini wewe ulikuja hapa ili uibe kisichokuwa halali yako...
Hili eneo lote unaloona hapa limezika makasha kama haya mengi sana. Kuna hela za mataifa mbalimbali chini ya huu udongo. Huu ni mgodi ambao uko hai lakini kuna mashetani huko duniani ambao hawalali. Wanakesha kuutafuta kwa hamu kubwa ili wajitajirishe wao!
Na mimi sina roho mbaya...nitawapatia huu wote."
Mtemi akashuhudia ujazo wa kasha lile liliokuwa na ukubwa wa kutosha kupimwa kwa zaidi ya kilo mia za noti zile. Akapigwa na butwaa. Akaupima wendawazimu aliokuwa nao Dario akaona kuwa umezidi kilo kwa nyingi. Ilimuhitaji punguani pekee ambaye atasusa utajiri kama huu na kuacha uende kwenye mikono ya watu wengine ambao amewapa vyeo vya kishetani.
"Najua unanihisi kama nimechanganyikiwa...au labda nimerukwa na akili. Kwamba nimekuleta hapa ili nikuoneshe shehena ya mali yangu, burebure tu.
Halafu mara eti niigawe ghafla! Haya naona una maswali mengi sana. Hakuna wa kukujibu badala yangu. Niulize swali unalotaka kuniuliza." Akampa uwanja wa maoni. Na kweli Mtemi akamuuliza kwa hamu kubwa sana kutaka kufahamu ni nini kilichopo nyuma ya haya yote.
Majibu aliyoyapata yalimuogopesha sana na kumfanya atambue kuwa bado hapa duniani kuna watu makatili ambao bado wana chembe za utu wema. Aliielewa zaidi sentensi ya mwisho iliyotoka kinywani mwa Dario,
"Nimemuingiza Adam Feruzi kwenye matatizo. Nataka nimsaidie, kisha nisawazishe kabisa kila tuta nililoliweka maishani mwenu!"
*********
Ni asubuhi ya siku ya pili, akiwa nyuma ya mlango mkubwa wa mahabusu ambao ulimzuia asiyaone yanayoendelea nje, Abednego Kagoye aliendelea kuweka ngumu kutoa maelezo juu ya uhalifu alioufanya.
Mbele yake alisimama askari mmoja aliyekuwa amechachuka kwa ukali akifoka!
"Yaani mura! Utasema urikuwa wapi, na unashirikiana na kina nani. Mimi sio kama hao wanaokuonea huruma kira siku muraa. Usiposema reo basi mimi Chacha Mariba, nitakuwa sio mtu wa Kasikazini!"
Askari huyu alifoka bila ustaarabu kiasi kwamba kila alipotamka neno 'mura' ulimi wake ulikosa namna ya kudhibiti wingi wa mate yake na ukayachota kama yalivyo na kuyarusha nje. Hali ilikuwa hivihivi kila alipochanganya silabi 'ra' badala ya 'la'. Alinyesha mvua ya mate kila alipopayuka kwa sauti ili tu aonekane ana hasira.
Abednego akafanya kosa moja kubwa ambalo mahabusu wenzie walijaribu sana kulivumilia na kutomkosoa askari huyu. Akasema,
"Aah afande! Taratibu bwana unanyesha!".
Askari yule mrefu ambaye alikuwa na cheo cha ukopro akachachamaa na kumrukia Abednego pale alipokuwa ameketi sakafuni.
Akamvaa mzimamzima na kuudaka ukosi wa fulana yake, akamburuta na kumbwaga sakafuni kwa mtindo wa kumlaza.
Haikujulikana aliitoa wapi fimbo yake ambayo daima hutembea nayo akiificha ili kudili na mahabusu wenye kiburi kama hawa. Lakini iliibuka kutoka pasipojulikana na sasa iko mkononi mwake.
Askari huyu akashusha mguu wake kwa nguvu juu ya miguu ya Abednego halafu kama anayepiga kwata, akaikanyaga na kuibana kwa nguvu kama anataka kuchinja kuku.
Halafu akaanza kumshushia Abednego bakora za nguvu kama mtu anayepiga nyoka. Hakujali fimbo ile inasulubu macho, pua au shingo. Yeye aliteremsha henzirani tu.
Kama tu asingezuiliwa na askari wenzake basi Abednego angekuwa mwanadamu anayepigwa kipigo cha kuuwa nyoka.
Mahabusu wengine walitishika sana kwa tukio hili wakaamua kuifyata mikia yao na kutulia kando. Hasira za watu wa kabila la askari huyu aliyejiita Chacha Maraba zilijulikana, ni nani ambaye angetaka zijaribiwe juu ya mwili wake? Wakanywea.
Abednego akaachwa palepale akiwa ameikumbatia sakafu ya baridi. Alikuwa akiona vimulimuli vikimweka kisha akaona giza, ghafla hakujua kinachoendelea. Akapitiwa na usingizi.
*******
Baada ya muda akashituliwa kwa teke jepesi la mguu ambalo lilimwamsha. Akaamka na kugundua kuwa kichwa chake kilikuwa kizito sana na bado maumivu ya mikwaju iliendelea kufanya ziara kwenye mwili wake. Akaketi kwa taabu na mbelenyake kulikuwa na sahani ya chuma iliyokusanya ugali na maji yenye mchanganyiko wa mbegu za maharage na wadudu kadhaa wanaoelea juu ya maji haya yasiyofaa kuitwa mchuzi.
Akasikitika sana kisha akakumbuka kitu kwa ghafla. Akapepesa kulia na kushoto na akamuona askari aliyeleta chakula kile. Akamuomba kuwa anahitaji kuzungumza na askari anayemfahamu kwa jina la Tito Ngeze.
Askari yule hakumjibu kitu badala yake akaondoka kwa dharau. Jambo lililoibua hali ya vicheko vya fedhea kutoka kwa mahabusu wengine dhidi yake.
Baada ya muda kidogo mlango ukafunguliwa na akaingia askari mmoja aliyevalia sare yake kwenye hali ya unadhifu. Huyu aliangaza chumba kile kwa utaratibu kisha akawasalimia mahabusu.
Ajabu!
Huyu alikuwa askari wa kwanza kutambua kuwa hawa viumbe ndani ya chumba hiki ni binadamu na wanahitaji kujuliwa hali.
Macho yake yakagota juu ya sura aliyoonekana kufahamiana nayo.
"Tito Ngeze!" Abednego akatamka akilazimisha tabasamu usoni mwake, ambalo lilitokeza kwa taabu mno.
Alikuwa ni askari aliyemfahamu na aliyemuamini siku zote. Waliwahi kukutana kwenye harakati kadhaa wa kadhaa miaka ya nyuma kabla hata mtu huyu hajaamua kupokea gwanda la jeshi la polisi na kuapa kuwalinda raia na mali zao.
Ma wakakutana tena kwenye matukio kadhaa ya uhalifu yaliyomuhusisha Abednego na huyuhuyu Tito akiwa kama askari.
Naam alikuwa ni Tito Ngeze akitazamana naye uso kwa uso.
"Kaka Kagoye!" Ngeze alimjibu uso wake ukichora tabasamu jepesi.
Mahabusu wengine wakabaki kwenye ulimwengu wa kushangaa ni namna gani watu hawa wanafahamiana.
"Kitu gani kimekukuta tena wewe nyang'au!" Akauliza katika hali ya utani japo alikuwa makini sana usoni mwake.
"Dah kaka! Nimekutana na mambo ya ajabu sana. Nadhani kwenye maisha yangu yote ya kukusumbueni sijawahi kukutana na mabalaa kama hayo ya jana!" Akatamka na kusita baada ya kugundua kuwa masikio yote ya mahabus yalikuwa yametegwa ili kupata habari kemkem juu ya hayo mambo ya ajabu yaliyomkuta Abednego Kagoye.
Hata Tito alilitambua hilo mara moja. Akamchukua Abednego na kutoka naye nje ya chumba kile.
Huku nyuma akaacha miguno isiyoeleweka. Ni hasira baada ya kukatishwa kupata umbea huu au ni kwa kuwa ametolewa mtu na wao wamebakizwa?
Walijua wao...
----------------------------
Itaendelea Kesho Jumatano.
❤️
👍
🔥
4