MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
February 12, 2025 at 05:23 PM
*`SHAMBA LA HELA`* Yake; *Godlove Kabati* WhatsApp; 0763204351 ------------------------------- SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA *`NABII TITO`* ----------------------------- Uso kwa uso, Konstebo Tito Ngeze alikuwa kwenye dawati la mahojiano na Abednego ambaye alihitaji kumueleza yote aliyoyashuhudia, yeye peke yake na sio askari mwingine. Tito alimpa sikio na akasimulia mambo yote yaliyotokea mpaka Feruzi anatekwa. Alisimulia yote, isipokuwa machache ambayo yalimhusisha yule bwana mwenye kovu na hakumsimulia juu ya mkasa uliomkuta Feruzi mpaka anajiingiza mwenyewe kwenye masaibu haya. Tito alimsikiliza kwa makini bila kumkatisha mpaka akamaliza. "Ndivyo ilivyokuwa kaka!" Ikawa sentensi ya mwisho kutoka kinywani mwa Abednego Kagoye. "Duh!" Ilimtoka Tito. Akashusha pumzi ndefu na kubaki kimya akiyasanifu yote aliyoelezwa. Ukimya ukachukua nafasi, wakati vichwa vya wanaume hawa vikitazama chini. Kila mmoja alizama kwenye fikra kwa namna yake. Tito Ngeze akiguswa na mkasa huu na Abednego akijaribu kutengenza mkanda wa picha akilini mwake kwa aliyoyaona. "Hili ni jambo kubwa!" Akatamka Tito akitikisa kichwa chake kwa masikitiko. "Kwani huyo rafiki yako hakuwahi kukuambia kuwa ana ugomvi na kundi lolote lile la uhalifu labda?" Akamuhoji. Abednego akajiumauma na kujikuta akiropoka, "Nadhani ndo hao hao waliokuwa wanamuwinda! Itakuwa ni hao hao..." alitamka bila kufikiri. "Kina nani waliokuwa wanamuwinda?" Swali la ghafla likatupwa kwake. Akashtuka, akagundua kuwa amechoma kibanda. Akabaki kimya bila jibu akiwa amemtolea macho Tito. Tito akagundua mara moja kuwa kuna taarifa ya siri ambayo ilichujwa na mdomo wake. Akamsogelea kisha akamnong'oneza, "Oa bro! Sasa kama umeniamini mimi mzee...halafu bado unanificha unadhani ni askari au afisa gani mwingine atakayekusevu? Sikia bro, mimi siwezi kukuchoma. Niambie kila kitu halafu nakuondoa hapa upesi. Kwani mi na we tumepiga mishe ngapi tena hatarishi? Sembuse hili la kuzurura usiku?.." akaweka kituo na kumsubiri Abednego ambaye alionekana waziwazi kuwa ameanza kutetemeka kwa hofu. "Poa kaka...nitakueleza kila kitu. Japo kwa usalama wako, libidi usiyajue haya mengine." Akamsimulia mambo yote aliyoyafahamu bila kuruka nukta wala alama za mshangao. Alipomaliza akategemea kuwa labda Tito atashtuka na kusisimka kwa hadithi yake, ambayo kwake yeye aliiona kuwa ya kuogofya na kutisha. Lakini haikuwa hivyo,badala yake akamshuhudia Tito akiinuka na kupiga hatua kuelekea lilipokuwa begi lake dogo la mgongoni. Akalipekua na kurejea na kitu kama karatasi ndogo kiganjani mwake. Akatazama kulia na kushoto kisha akamuonesha karatasi ile huku akimng'oneza kwa sauti ya chini zaidi ya awali. "Huyo jamaa yako ndiye huyu hapa?!" Hamadi! Ilikuwa ni picha ndogo iliyokuwa na sura ya Feruzi akiwa juu ya pikipiki. Abednego akapata mgawanyiko wa hisia. Akawa mwenye kushtuka na kushangaa na kuogopa kwa wakati mmoja. "We..ume-umemjuaje huyu? Kwanza umeitoa wapi hii picha?" Akauliza kwa kigugumizi akiangaza shingo yake huku na huko kwa tahadhari. "Ni yeye au sio yeye?" Akarudia swali lake. "Nd'o yeye huyu Feri...Feruzi eeh. Nd'o yeye!" Akajibu tena kwa mashaka. Tito Ngeze akashusha pumzi zake kwa mara nyingine. Kisha taratibu akarejea kwenye begi lake na kurudisha picha ile. Akarudi pale mezani na kuketi akimtazama Abednego kwa udadisi uliopakwa rangi ya matumaini. "Kama kweli ni yeye basi Mungu amsaidie sana huko aliko!" Tito akanong'ona. "Una-unamaanisha nini?" Abednego akadakia bado ametoa macho kwa hofu. "Kama sasa hivi jamaa yako hapitii mateso makali ili ajibu baadhi ya maswali magumu, basi ni aidha wameshamuharakisha kumpeleka mbinguni au wameshazipondaponda korodani zake huku wakimcheka namna anavyolia kama mtoto mdogo!" Akaweka pumziko na kushusha pumzi kwa mara nyingine. "Ataiona rangi ya kifo kabla hajakikumbatia. Atateswa sana ili atoe majibu ya msingi. Na kama sikosei, sidhani kama utapata bahati ya kuishuhudia maiti yake. Sidhani!" Safari hii kijasho chembamba kilianza kuota juu ya paji la uso wake kama umande. Akajipangusa kwa leso kisha akaendelea, "Braza!" "Naam..." Abednego akaitikia kwa nidhamu ya hali ya juu. Ni kama ambaye anamuona Tito Ngeze kama mkombozi wake wa mwisho. "Hakuna skauti, mgambo, askari wala chombo chochote kile cha dola kilichoagizwa kumuwinda Feruzi. Hakuna! Lakini hawa ni watu walioagizwa na kigogo mmoja kwa shughuli maalumu. Na wanamuona Feruzi kama mtu hatari sana, wanamuweka kwenye daraja la uharamia na uhaini!" Akasita baada askari mwenye cheo cha juu kukatiza eneo lile na akasimama na kupiga saluti akitoa salamu kwa ukakamavu. Akajibiwa bila kutazamwa. Halafu akarejea kuketi. "Nadhani tutoke nje. Hapa sio mahali sahihi tena kwa ajili ya mahojiano!" Akamshurutisha. Wakatoka nje. Huko akamnyooshea maelezo juu ya alichokihisi kuhusu Feruzi na akajaribu kuunganisha nukta kutoka kwenye maelezo ya Abednego. Akapata mchoro wa ramani nzima, "Hii kesi hakuna askari yeyote anayeifahamu. Hata mimi nimeifatilia kwa siri sana." Akatamka akiwa amekunja ndita zake, bado amezama kwenye fikra. Wakati huu wote Abednego alikuwa kapigwa na butwaa. Simulizi za namna Feruzi alivyokuwa akiwindwa alizichukulia juu juu. Lakini sasa akagundua kuwa mchezo haukuwa mdogo. "Kwa hiyo tunafanyaje sasa hapo kaka!" Akauliza kwa unyonge. Mwili wake ni mkubwa kulinganisha na ule wa Tito Ngeze ambaye alionekana mwembamba kiumbo. "Ramani nzima tunayo tayari lakini haijakamilika bado. Tuna kichwa, mstari wa pambizo, dira na skeli lakini hatuna ufunguo. Ramani bila ufunguo haieleweki. Na mimi nitataka kushirikiana na wewe mpaka tuupate ufunguo!" Akatamka kwa sauti ya kujiamini. Abednego akamtazama kwa jicho la kumpima. Hakuamini kama huyu askari mgeni kazini akiwa hana cheo chochote kile. Kama anaweza kweli kukabiliana na watu hatarishi kama hawa. Lakini akayatukana mawazo yake baada ya kukumbuka matukio kadhaa ya kishujaa aliyowahi kuyashuhudia yakifanywa na askari huyuhuyu mwenye umbo dogo. "Ona sasa, unaanza kuongelea masuala ya ramani sijui funguo, sasa funguo gani tena?" Akalalamika akiwa amechanganyikiwa. "Ndio ipo funguo, hii itatusaidia kuelewa ramani yetu yote. Brown Kizito, muite Boss Mzito!" Akatamka huku tabasamu jepesi likiupamba uso wake. ****** Unabii wa Tito Ngeze, ulitimia. Ni kama alipewa aandike hadithi ya ufunuo juu ya mambo yajayo kwenye maisha ya Feruzi. Feruzi alikuwa uchi wa mnyama akiwa ndani ya chumba kilichomezwa na giza zito, kikifukuta kwa joto kali. Mwili wake hauna nguvu tena baada ya kupitia suluba ya kutosha. Ameshaonja ladha ya kukaa juu ya kiti cha chuma na kuzawadiwa shoti ya umeme, iliyomchachafya bila kumuua. Ameshashuhudia kucha zake mbili za vidole gumba vya mguuni zikichomolewa katika namna ya kutisha. Ameshachapwa bakora za kutosha akiwa uchi wa mnyama, kisha chumvi ikapakwa juu ya majeraha yale akiambiwa kuwa ni tiba itakayo yakausha upesi kabla hawajarejea kumchukua tena. Sasa wamemtelekeza ndani ya chumba hiki cha giza chenye joto kali ambalo lilizua ubishi kati ya chumvi na majeraha yake. Aliwashwa sana lakini asingeweza kujikuna. Kila alipojikuna alikuwa ni kama anachochea maumivu yake. Akaamua achague utulivu wenye mateso. Akajikuta anakitamani sana cheo cha kuitwa marehemu. Kwa mara ya kwanza maishani mwake, kifo akakiona kama moja kati ya starehe kubwa mno juu ya uso wa dunia. Akakitamani sana kifo, lakini muda huu kikamuepuka na kukaa mbali naye. Akiwa ameikumbatia sakafu ile yenye joto akalia kwa uchungu mkubwa. Akatukana kila aina ya tusi alilolikumbuka kisha akatunga na mengine mapya. Lakini akajikuta yupo peke yake na matusi yake yakakosa maana. Maswali yao yalikuwa mawili tu, Ni wapi alipo Franko Dario na liko wapi shamba la hela?! Kila alipojaribu kujitetea kuwa hakumbuki kitu chochote alionekana kama analeta utani. Na wakaamua kumsulubu akiwa yeye peke yake. Upande wa pili hakujua kinachoendelea kwa Mtemi Moringo. "Sijui wamemuua? Au nd'o wamemsaga miguu yake kama walivyotaka kipindi kile? Dah! Nakufa mie... Eeh Mungu wangu. Naomba unichukue, na kama ni kweli yule malaika mtoa roho huwa yupo, mtume haraka sana anifuate!" Akatamka kwa uchungu. Ghafla mlango ule mkubwa wa chumba hiki ukafunguliwa na mwanga mkali wa kurunzi ukammulika kwa ghafla. Whaaaaaa! Ulimuumiza macho yake akashindwa kutazama vizuri. "We sogea hukuu!" Sauti iliyovimbiwa hasira na kisirani ikamuita. Akajiburuza kwa taabu akijitahidi kusimama. Lakini hakusubiriwa apoteze huu muda. Akashtukia anaburutwa mzobemzobe na kuvishwa nguo zake kwa pupa. Aliumia na hakuna aliyejali juu ya maumivu yake. Aliposita na kugoma baada ya kutoneshwa kwenye miguu yake. Akazabwa kofi kali ambalo lilimtuliza na akatulia. "Haya tembea mbele! Haraka!" Sauti ile ikamuamuru. Akang'amua kuwa amesimamiwa na wanaume watatu waliovimba miili yao kwa mazoezi. Nyuso zao zimekasirika kwa kukunja ndita na zaidi ya yote walikuwa na hasira sana dhidi yake. Hakujua kawakosea nini maana yeye ana inda na muajiri wao na sio wao. Labda wanaichukia kazi yao wanayoifanya, labda wanalipwa kiduchu, labda wamehaidiwa kuwa watalipwa zaidi kama wakimleta akiwa amechakaa. Labda, labda... Wakaikamata mikono yake na kuikunja nyuma ya mgongo wake kisha wakaifunga kwa kamba ngumu na kuikaza sana kana kwamba Feruzi angeweza kuipasua kwa urahisi. Wakamtoa chumbani mle wakimlinda kwa umakini mkubwa kama vile yeye ni mtu hatarishi sana anayeweza kufanya ubaya muda wowote. Wakatembea na kupinda kona nyingi, wakajikuta wamerejea kwenye ukumbi uleule wa awali. Feruzi akaweza kumuona Mtemi katikati ya ukumbi amesimama mikono yake ikifungwa nyuma kwa kamba ngumu, akiwa amechakaa vibaya kwa uchovu na maumivu. Huenda na yeye alikuwa anapitia hatua za mateso makali kabla hajaliona kaburi. Na wale watu walioonekana kuwa makini sana ndani ya mavazi yao meusi wallikuwa wamesimama wima kwa utulivu. Feruzi akaungana na Mtemi mahala pale. Kisha wanaume waliomleta wakainamisha vichwa vyao kwa heshima na kuondoka. "Unaendeleaje Feruzi?" Kauli iliyobebwa na sauti nzito tulivu ya upole ikatua kwenye masikio ya Feruzi kama sumu kali ya unafiki. Akaporomosha matusi bila kutarajia. Lakini matusi yake yalipuuzwa. Akamgeukia Mtemi na kumtamkia "Eer..nadhani hatuna muda wa kupoteza. Kesho utatupeleka huko shambani. Na kama mambo yakienda kama tunavyotarajia basi mtapata uhuru wenu. Mkafurahie matunda ya uhuru wa nchi yenu!" Akatamka Don Franko. Akaagiza wafunguliwe kamba zile na wapelekwe kwenye vyumba tofauti kila mmoja. Kisha wapatiwe huduma nzuri za chakula na malazi kadri wanavyotaka wao. Hili likawa ajabu jingine! Baada ya kusulubiwa, sasa wanahudumiwa kama wageni rasmi. Ikawa kama ilivyoagizwa... Ikisubiriwa siku mpya ya kesho yake. Siku yenye safari kuelekea alipo Franko Dario na shamba lake la hela! ******** Alikuwa nusu mwehu nusu timamu baada ya kusoma jina hili juu ya kioo cha simu yake. Lilikuwa jina liloliogopa na kuliheshimu sana. Hakuona usalama wowote wa kuipokea ofisini mwake akatoka nje ya ofisi bila kumuaga karani wake akaenda kutafuta pembe aliyoiamini ili azungumze na simu yake. "Tumempata kijana...tena kiulaini kabisa. Lakini tunaanza kuwa na mashaka na utendaji kazi wako." Kitendo cha kusikia neno, 'tumempata kijana!' Kikasababisha mijongeo ya viumbe kama vipepeo tumboni mwake. Kabla hajajitetea sauti ile nzito ikaendelea, "Chunga sana Karoli, maisha yako ndani ya chama chetu hayana muda mrefu. Unazijua kanuni halafu unaleta utani kazini!" Sauti nzito ikaunguruma. Muungurumo huo ukalitetemesha mpaka tumbo lake kwa woga. "Hapana mkuu...vijana wangu walikuwa bado wanalifuatilia hili suala!" Akajitetea huku jasho likianza kutota kwenye makwapa yake. "Ongeza sana umakini! Hauna maisha marefu sana kwenye chama chetu!" Simu ile ikakatwa. Akitetemeka akajikuta akijilaumu mwenyewe . Japo alichelea wafanyakazi wake wasimgundue. Akachonga tabasamu bandia usoni mwake na kurejea ofisini mwake. Karani wake ambaye daima tabasamu liliupamba uso wake, akamueleza kuwa kuna wageni walioingia ndani ya ofisi wakidai kuwa yeye ndiye kawambia waingie moja kwa moja. Akashangaa na bila kutaka maelezo zaidi akanyooka mpaka ndani. Akawakuta vijana wawili nadhifu walioketi wakimsubiri kwa utulivu. "Aisee...nyie ni kina nani bwana. Mbona mnavamia tu ofisi bila ridhaa yangu na mnaongopa kuwa nimewaruhusu?" Akawauliza kwa hasira. "Samahani sana Boss Mzito. Hatukuwa na lengo baya!" Mmoja wao akajibu kwa upole. "Samahani nd'o nini kwa Kiswahili? Haya nje! Haraka! Mpaka niwaite!" Kwa hasira na kiburi akawafukuza huku akiwaonyesha mlango wa kutokea. Alikuwa mjivuni sana. Hawakusimama wote., akasimama yule mwingine aliyekuwa kimya. Huyu akaenda akaufunga mlango kwa ufunguo na ufunguo akauweka kwenye umiliki wake. Brown Kizito akashangaa sana. Kisha akagundua mara moja kuwa hawa hawakuwa wageni wema. Akakurupuka upesi mpaka kwenye droo ya meza yake na kutoa bastola akawanyooshea kuwatisha. Hawakutishika! "Nitawapasua vichwa vyenu! Nyie ni kina nani eeh?" Hakujibiwa. Akabonyeza kitufe ili afyatue risasi lakini sauti ya 'kochooo! kochooo!' Ikamuumbua. Hakukuwa na risasi hata moja ndani ya bastola ile. Yule aliyebaki pale mezani akatoa rasasi sita na kuzipanga mbele yake kwa utulivu na umakini mkubwa akimuangalia Boss Kizito usoni. "Sekunde mbili zilizopita ungetuua kama tu nisingekuwa na unabii wa kutabiri ni wapi unaficha silaha yako na nikaondoa hizi risasi sita. Sa hivi ningekuwa nasomewa vitabu vya hukumu aiseee!" Akatamka katika hali ya utulivu kisha akamkazia macho kwa ukakamavu kama anayempima. "Naitwa Konstebo Tito Ngeze ama unaweza kuniita nabii Tito. Na huyu ni mwenzangu anaitwa Abednego Kagoye a.k.a King Nego!" Akaweka kituo na kumtazama usoni Boss Mzito. Ambaye matukio kama haya kazoea kuyaona kwenye filamu za kijasusi. Akakaa juu ya kiti chake huku akivuja jasho na kutetemeka zaidi. "Mnataka nini kwangu?" ---------------------------------- Aiseeee 🥱, Kuisoma riwaya kama hii tena bure kabisa ni upendeleo wa hali ya juu. Tunazidi kuunganisha nukta na kukutana na hekaheka za hapa na pale. Tito Ngeze a.k.a nabii Tito anafanya utabiri ambao unatimia akilenga kuikamilisha ramani yake.Lakini bado hatujajua ana lengo gani na Boss Mzito. Hatujajua itakuweje kule kwingine waliko Feruzi na Mtemi Moringo na safari yao ya kuelekea alipo Franko Dario na *shamba* lake *la hela*. Tatizo lenu hamtaki kusambaza link ya chaneli. Ingeendelea hata kesho hii! Haya bwana mi nawadai reaction na maoni kwenye namba 0763204351. Itaendelea!
❤️ 🔥 👍 8

Comments