MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
February 18, 2025 at 05:50 PM
*`SHAMBA LA HELA`* Yake; *Godlove Kabati* WhatsApp; 0763204351 ------------------------------- SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI *MAKOSA MATATU* --------------------------------- Hakukuwa na namna... Baada ya kutishiwa uhai juu ya kufichuliwa kwa siri ya utajiri wake, Boss Mzito alitamka kila alichokifahamu bila kuacha kitu chochote kile. Aliwafunulia kila kurasa ya kitabu cha historia ya maisha yake kuanzia nchini Uganda mpaka alipoletwa hapa nchini Tanzania kama mfungwa aliyetoroshwa. Akawafunulia kurasa zilizotaja ufanisi wake wa kazi kwenye mafaili kadhaa ya uhalifu yaliyomilikiwa na watu wa chama hiki cha siri. Akawaambia kila kazi chafu alizoagizwa kuzifanya zikija kwake kama amri na sio ombi. Na yeye akazitekeleza bila kuibua mijadala au hoja ya aina yoyote ile. "Nimemaliza yote...tafadhali! Ninachokiomba kwenu ni usafi wa jina langu. Hilo tu! Sitaki jina langu lichafuliwe." Akasisitiza tena kwa mara ya mwisho. Uso wake umelowa kwa machozi ambayo yamechanganyikana na jasho. "Aiseee..." Tito aliguna huku akisikitika baada ya kila kitu alichokisikia. "Ina maana hawa watu wameshiriki mpaka kwenye mauaji ya viongozi wakubwa wa kiserikali? Wana nguvu kiasi gani hawa?" Akamswalika. Boss Mzito akashusha pumzi zake kisha akatamka kwa sauti tulivu ya kunong'ona, "Mwanga wa giza! Wana nguvu sana kuliko hata serikali yenyewe. Wao ni zaidi ya serikali. Kila mwaka wanahakikisha kuwa zaidi ya asilimia sitini ya viongozi walioko madarakani ni wanachama wa hiki chama chao cha giza! Tena wale viongozi wa sekta za juu kabisa. Hawashindwi lolote..." akatia nukta. "Unaweza kutueleza ni sababu gani haswa imewafanya wamuwinde huyu kijana Feruzi?!" Abednego aliyekuwa kimya muda wote huu, akajitutumua na kumuuliza swali. "Kwa kweli sijui...na hata kama ningetaka kujua, hiyo haki nisingepewa. Lakini ninachokifahamu ni kuwa kuna mwanachama wao mmoja ameasi na amekimbilia kusikojulikana. Nadhani huyu kijana anahusika naye kwa namna moja au nyingine." Mzito akajibu. Ukimya wa ghafla ukapita, macho manne yakimtazama Boss Mzito yakiwa yamejaa udadisi kana kwamba bado kuna vitu anawaficha. Na yeye akaligundua hilo, akawahi kujitetea, "Siwaongopei...hakuna ninachokijua zaidi ya hapo. Kama nilivyokuambieni, mimi ni mtu wa nje ya mfumo. Na ninafanya kazi kama maagizo ya nje ya mfumo. Nimeshiriki vikao vyao vichache tu na hivi karibuni nimeshiriki kikao kimoja pekee ambacho walinitaka nishiriki. Kwenye hicho kikao wamemtaja huyo muasi." Akawasanifu usoni ili kugundua kama maneno yake yamewaaminisha au la! "Kijana ametekwa tayari!" Tito akaunguruma. "Wewe kama mtu wa nje ya mfumo, unatusaidiaje sisi kumuokoa huko aliko?" Swali lake likawa kama tonge kubwa la nyama lililokwama kooni mwa Boss Mzito na kumfanya ashindwe kutoa sauti yoyote ile. Akabaki kuhangaika. "Sikiliza Mzito...kama nilivyokueleza hapo awali. Hii kesi bado ni mbichi sana. Kwanza sio kesi hii...tuseme ni mgogoro tu. Maana hakuna chombo chochote kila cha dola kinachoufahamu huu mgogoro. Itakuwa kesi kama tu ikiripotiwa..." akaweka pumziko kisja akaendelea. "Ni mimi pekee ninashughulika nayo hii...na sijataka kuwaiwasilisha kwenye uongozi maana najua kuwa naimudu. Kwa maana hiyo ni sisi hapa watatu tunaohusika nayo moja kwa moja!" Akatulia kuyaruhusu maneno yake yazame na kumuingia Boss Mzito kisha akaendelea, "Hapa una machaguzi mawili tu. Moja, ulete ugumu halafu niipeleke hii kesi juu ili iwe kubwa halafu hilo jina lako unalolilinda kwa nguvu zote lichafuke... Mbili, utusaidie kumuokoa huyo raia mmoja asiye na hatia halafu wewe uendelee na huu ubosi wako. Unachagua nini hapo." "None of the above!" Akatamka Boss Mzito akimaanisha kuwa hakuna jibu ambalo angechagua kutokana na machaguo ambayo angepewa. "Hapo uongezee na machaguo haya hapa.. Tatu, uipeleke hii kesi juu halafu hao hao wakuu wako wakufute kazi na ikibidi wasuke njama za kukuangamiza kabisa. Kwa sababu na wao wanategemea malisho kutoka kwenye chama chetu. Nne, nikubali kuwasaidia kwenda kuokoa roho moja halafu roho zenu mbili ziunganishwe kwenye mateso makubwa ya kuiona rangi ya kifo kabla hamjazikwa mkiwa hai. Maana hakuna askari au jeshi lolote linaloweza kuwafikia hawa viumbe." Akaweka pumziko na kumtazama usoni konstebo Tito Ngeze. Macho yao yakapimana na ya kwake yakaonekana kumaanisha kile alichokisema. "Ningechagua haya majibu mawili ya mwisho. Ni majibu yenye uhalisia na ukweli zaidi kuliko hayo ya kwako." Akamalizia sentensi yake. Tito akageuka na kuzungukazunguka ndani ya ile ofisi, mikono yake ikiwa nyuma, kichwa chake kimeinama chini akiwa mwingi wa mawazo. Mara akainuka na kuitazama picha kubwa iliyokuwa imetundikwa ukutani pale. Ilikuwa picha ya Raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania. Akatumia sekunde kadhaa kuitazama na kuisanifu, "Vipi na mheshimiwa ana kadi ya uanachama wa chama chenu?" Swali lile likamtoka kimasihara. "Nani? Raisi au?...Huyo ni mmoja kati ya mawindo ambayo yanatazamwa kwa jicho la makini zaidi. Sijui wamepanga kumfanyia nini. Lakini hawampendi na wanamchukia!" Boss Mzito akajibu. Jibu lake likamfanya Tito aachie cheko jepesi. Cheko lake likawashangaza sana wenzie, hawakujua sababu ya yeye kucheka katikati ya sintofahamu kama hii. "Vipi kuhusu makamu na waziri mkuu?" Akauliza huku akijihangaisha kukunja mikono ya shati lake katika namna ya kujiandaa na kazi fulani ya ghafla. "Hao wako safi...isipokuwa huyo waziri mkuu. Huyo nadhani ni mmoja wetu!" Tito akatikisa kichwa akasogea kurudi juu ya kiti chake taratibu kisha ghafla akakunjuka na kuachia teke kali lililotua juu ya kifua cha Boss Mzito. Boss Mzito akapepesuka na kurushwa nyuma, kiti chake kikabinuka na kichwa chake kikaisalimia sakafu na kujikuta kikijibiwa kwa maumivu makali. Kabla hajaamua ajitetee vipi, tayari Tito Ngeze alikuwa juu ya kifua chake. Akashtukia anapigwa na kitu chenye uzito wa kawaida lakini kilichomuumiza kwenye shavu lake la kushoto. Hakupewa muda wa kufikiria zaidi kuwa ile ni ngumi. Kitu kile kile chenye uzani sawa na cha awali kikatua kwenye shavu lake la kulia. Na ukawa ni muendelezo mpaka zilipohesabika jumla ya ngumi nane. "Utatupeleka alipo Feruzi au hutatupeleka?!" Ulikuwa ni mfululizo wa maswali ambayo angeweza kuyasikia kila ilipotua ngumi. "Sawaaa nitakupelekeni! Nitakupelekeni!" Akajibu baada ya kuhitimu ngumi ya nane. Akaamua asalimu amri na akaachiliwa. Tito akasimama akihema juu juu kwa jazba huku akikunjua upya mikono ya shati lake nadhifu. Abednego alikuwa amesimama wima huku mikono yake ikiwa kiunoni akishuhudia sinema ya bure kabisa. Hekaheka kama hizi yeye asingeziweza licha ya ubabe wake. Na hapa kwa mara ya kwanza akaishuhudia rangi sahihi ya Tito Ngeze. Huyu alikuwa mwingine kabisa tofauti na yule wa zamani. Yeye hakujua ilikuwaje kuwaje ila alishtukia tu purukushani halafu mtu yuko juu ya Boss Mzito anashusha mapigo. Boss Mzito akahangaika kusimama huku akijizoazoa pale sakafuni. Akapapasa taya lake na kugundua kuwa sio damu tu bali tayari meno mawili ya juu yameshaliaga taya na kuacha mapengo mawili. Akatazama huku na huko na kuyona meno yale, akayaokota. "Nitawapeleka....lakini kumbukeni kuwa hawa watu ni hatari sana!" Akaweka msisitizo kwa mara ya mwisho. ******** "Mkuu una uhakika kuwa watanasa kwa urahisi kweli hawa watu?" Sauti nzito ilielea hewani na ikajirudia tena kwa mwangwi uliodumu kwa sekunde chache kabla haijajibiwa na yule aliyeulizwa swali. "Tangu nimejitambua hapa duniani nimewahi kufanya makosa matatu tu. Na sitegemei kama nitafanya kosa la nne kabla sijaondoka hapa duniani!" Sauti kavu ikamjibu. "Unamaanisha nini?!" Akaulizwa tena. Lakini mara hii aliulizwa na sauti mpya tofauti na ile ya awali. Akakohoa kidogo kisha akatema chini makohozi yake. Na akatamka, "Duba..Dubu!" Akawaita kisha akatamka, "Kosa la kwanza nililolifanya ni kutoroka nyumbani kwa baba na mama yangu, nikaja mjini kutafuta mali. Kosa hilo la kwanza likazaa kosa la pili, ambalo nililifanya baada ya kumuamini dokta Simfukwe. Nikawa kama mbwa muaminifu kwake nikimsaidia kila dhambi ambayo aliitenda. Halafu kosa la tatu n'do hili ambalo linatufanya tuviache vitanda vyetu usiku huu tusilale... halafu twende kuutega huu mtego!" Akawajibu kwa utulivu. Jibu lake bado likazaa swali jipya, "Kosa la tatu? Tusilale?...nd'o kosa gani hilo?" "Kosa la tatu ni pale nilipoivunja sheria yangu mimi mwenyewe, nikamruhusu Adam Feruzi aondoke akiwa hai siku ile ambayo alimleta yule msaliti." Baada ya maneno haya akasimama. "Ni heri ningemchinja na kumuua kabisa. Au ningempiga hata risasi moja tu ya kichwa akafa. Sijui shetani aliye ndani yangu aliazima wapi hii huruma. Eti nikamruhusu yule dogo aondoke, tena akiwa na kitita cha fedha. Ni heri basi ningemuacha aende mikono mitupu. Mimi na upumbavu wangu nikampa mpaka hela aende nazo. Yeye kazaa tatizo, na najua tu hata hela nazo zitazaa matatizo. Hela nilizompa, sio za halali. Zimejaa machozi na damu za watu waliouawa bila hatia. Nawakumbuka, walikufa huku wakinilaani mimi na dokta Simfukwe. Wakatutakia maisha mabaya sana na wakatutakia roho ya kifo ituandame kila tutakapokuwa. Zile hela zimejaa laana. Halafu mimi mjaa laana nikazigawa kwa asiye na laana. Ni kosa langu la mwisho ambalo nataka kulisahihisha... Kijana Feruzi abaki salama! Na nikifute moja kwa moja hicho chama chenye wajaa laana. Mwanga wa giza!" Dario akamaliza maneno yake yaliyojaa ahadi nyingi za visasi. Akapiga hatua kwa kuchechemea huku akiungwa mkono na fimbo yake ambayo siku zote ilikubali kutumika kama mguu wake wa tatu. Wakaendelea kupiga hatua wakiwa kimya mpaka walipofika kwenye mdomo wa pango kubwa. Lilikuwa na ukubwa wa kutisha, kama tu ungepewa jukumu la kusimama mbele yake usiku kama huu uliopakwa rangi nyeusi ya giza kama hili. Dario akapiga mbinja mara tatu kwa nguvu mbele ya pango hilo. Vikasikika vishindo kwa mbali kama jeshi dogo la watu wanaotembea kwa tahadhari kutoka ndani yake. Mara wakatokea watu waliokuwa wamejitanda mavazi yasiyoeleweka. Mararu sio mararu, magunia sio magunia, masurupwenye sio masurupwenye. Wengine walivalia magome ya miti na kujifunga majani kwenye vichwa vyao. Ili mradi tu waonekane kuwa ni magaidi au kikundi cha waasi wenye weledi kwenye vita vya msituni. "Haruuu haruuuu! Wimba gwisaaaa!" Dario akapaza sauti ya kishujaa huku akinyanyua fimbo yake juu kibabe. "Haruuu! Wimba gwisaaaa!" Kikundi kile cha wanaume wapatao hamsini wakamjibu kwa kunyanyua silaha zao wakiwa na morali ya hali ya juu. Salamu ile ikarudiwa mara tatu. Na kadri ilivyorudiwa ndivyo hali ya hewa ilivyozidi kuchangamka na morali ikaongezeka zaidi. Wanaume kadhaa wakapiga risasi hewani kwa furaha. Dario akatumia dakika kadhaa kuwahutubia kwa lugha ileile ambayo ilionekana kujulikana baina yao pekee. Mimi na wewe hatuijuii, kama wewe unaijua inabidi utujibu uliijuaje na mlipanga kufanya nini usiku huo. Baada ya hotuba yake fupi, wakatawanyika kila mmoja akaelekea eneo aliloonelana kulifahamu tena akiwa na furaha maradufu. Ilikuwa ni kama watoto wa chekechea wenye furaha baada ya kuruhusiwa kurudi nyumbani mapema. Walionekana kama wana uchu na vita ambayo wamejiandaa nayo kwa muda mrefu. --------------------------------- Kosa la tatu litasahihishwa namna gani? Na ni kitu gani ambacho Tito Ngeze na wenzie watakifanya ili kumuokoa Feruzi... Kwani wanajua kuwa hata Mtemi yupo hai? Haya yote tutayajua hapa hapa... *ITAENDELEA KESHO* -------------------------------- Simulizi ya *'KIKAO CHA HAKI'* sasa inatarajiwa kutoka rasmi tarehe 23 ya mwezi huu na itagawiwa bure kabisa kwa kila mwanafamilia wa chaneli hii. Kuipata simulizi hii, ni rahisi sana... Tuma neno *KIKAO CHA HAKI* kwenda namba 0763204351. Na utaunganishwa moja kwa moja kwenye orodha ya wataogawiwa bure kabisa kazi hii. Asante! 🙏🏻
❤️ 👍 🔥 🙏 4

Comments