MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
February 19, 2025 at 05:22 PM
*`SHAMBA LA HELA`* Yake; *Godlove Kabati* WhatsApp; 0763204351 ------------------------------- SEHEMU YA ISHIRINI NA TATU *`BADO MASAA MAWILI...`* --------------------------------- Franko Don Bosco, ama Don Franko; Alikuwa ndani ya chumba chake kidogo ambacho yeye alikiazima imani yake yote na kukichukulia kama ofisi. Akiwa amesimama anazunguka zunguka huku na kule, kichwa chake kikipanga mawazo na kuyapima kisha kingeyapindua na kuyakataa. Halafu angepanga mengine na kuyaona yako sawa akayakubali. Mara likaingia wazo jipya lililomsogeza moja kwa moja mpaka juu ya ukuta ambapo alikuwa ametundika picha moja kubwa. Akaisogelea taratibu na kuikazia macho. Ilikuwa picha ya mtu ambaye kwake daima alikuwa ni adui namba moja. Kila alipoiona picha yake, aliitukana na kuinuzia laana na maneno yote mabaya aliyoyafikiria. Alimchukia mno! Na hii nd'o sababu akaitundika picha ile pale ukutani akaifanya kama kumbukumbu itakayoweza kumkumbusha jukumu la muhimu mno ambalo anadaiwa yeye kama kiongozi wa chama hiki cha siri. Akaitungua picha ile kutoka pale ukutani akaiweka mezani. Akaiinamia huku akiitazama upya kwa jicho makini zaidi. "Dario!!" Akalitaja jina la taswira aliyoina pale juu ya picha. Akiwa mwingi wa hasira na uchungu, akayafumba macho yake na kukumbuka kila tukio ambalo Dario alifanya na likamuumiza huko nyuma. Yeye akiwa bado hana cheo chochote kile ndani ya hiki chama, japo ana uzoefu na utumishi wa muda mrefu. Akaikumbuka ile siku ambayo wanampokea rasmi Dario kama kijana mdogo tu, akakaribishwa na kula viapo vyote. Kwa wakati huo, Dokta Albert Simfukwe ndiye alikuwa mkuu wa chama. Akakumbuka jukumu walilopewa yeye na Dario, kwenda kuuondoa uhai wa aliyekuwa Raisi wa nchi kwa wakati huo, ambaye alikuwa amejenga vizingiti vilivyowazuia kufanikisha biashara zao. Akaukumbuka uzembe ambao yeye aliufanya mpaka akakamatwa huku Dario akigeuka shujaa baada ya kutumia mbinu yakinifu na kufanikisha mauaji hayo. Kwa mara ya kwanza kabisa, Dario akakwezwa na kukaa kiti cha juu kuliko yeye. Kisha baada ya muda mfupi tu, akaaminiwa na kupewa fimbo ya mamlaka iliyomvesha cheo cha uFranko. Cheo kikubwa ambacho kinamilikiwa na watu watano tu ndani ya chama. Eti na yeye akakinyakua cheo hicho kiulaini kabisa. Ikawa ni kwamba DonBosco anapokea amri ma maagizo kutoka kijana kama huyu, ambaye amemtangulia idadi ya vikao vya chama. Kwake huu ulikuwa uonevu mkubwa. Akakumbuka namna ambavyo, huyuhuyu Dario alimuua mkuu wa chama, Dokta Simfukwe kisha akatoroka na kujificha pasipojulikana akiwa na faili lenye siri kubwa ya utajiri wa chama hiki. Akaondoka na kuliacha ghala lao likiwa jeupe. Akafumbua macho yake baada ya kugundua kuwa ni leo wanaenda kumtia mbaroni na kurejesha nguvu ya chama chao ambacho kilikuwa kimeanza kuipoteza nguvu yake baada ya kukosa nishati ya fedha na utajiri. "Mpumbavu wewe...fidhuli mkubwa! Mjaa laana na hayawani! Hivi ilikuwaje mpaka ukaingia kwenye chama chetu?" Ilikuwa ni kama anazungumza na ile picha moja kwa moja. Anaitukana lakini haionekani kuumizwa kwa matusi yale, anaiuliza swali lakini hajibiwi. Badala yake ikabaki kumtazama tu, tena miongoni mwa macho yaliyomtazama lilikuwepo lile jicho bovu lililokuwa na kovu kubwa lililotengeneza mpasuko katikati yake. Tabasamu kavu likiuvaa uso huu na kuifanya sura ile kufanana kwa ukaribu zaidi na sura ya shetani asiyeuogopa moto wa jehanamu. Ni tabasamu hilo lililomfanya Don Franko atishike kidogo na akaitupa mbali picha ile ikadondoka sakafuni. Na ikapata mpasuko kwenye kioo ambao ulitengeneza ufa uliokatiza pale pale kwenye kovu la sura ile! "Huwezi kufa hata kwenye picha?!" Don Franko akaunguruma kwa hasira. Akakusanya nguvu zake zote na kutungua kisu kikubwa cha kijeshi kilichokuwepo palepale ukutani. Kisha akakikita kwa hasira juu ya ile picha. Akarudia rudia kuchoma picha ile kwa kisu mara kadhaa mpaka alipotosheka kuwa kioo kimesagika na picha imeharibika barabara. Akatoa tusi kali mno, akiukashifu uchi wa mama aliyemzaa Dario. Akiwa bado hajazinduka kwenye wazimu wake, mlango wa chumba chake ukafunguliwa na akaingia mwanamke aliyevaa mavazi yaliyoshabihiana na ya kwake, Franko Viktoria. Hakumpa muda wa kushangaa au kuhoji ni kitu gani kinaendelea pale ndani, "Kila kitu kiko tayari?!" Kwa sauti inayotetemeka Don Franko akamuuliza. "Ndio...nimeshakamilisha kila kitu." Akajibiwa kwa sauti ya kike iliyokuwa na kila dalili ya kujiamini japo usoni alionekana mwingi wa maswali. "Vizuri. Nadhani mkae sawa,leo saa kumi na mbili jioni tutaanza safari" akatoa amri kisha akageuka na kuketi juu ya kiti huku jasho likimtiririka. "Mkuu una uhakika uko sawa kweli?.." Viktoria akamuuliza huku akitupa macho yake kwenye sakafu iliochafuliwa kwa vipande vya vioo. Hakujibiwa mpaka alipouliza swali hili mara mbili. "Ni muda mrefu sana tangu nilipopania kumkamata huyu hayawani. Na sidhani kama kuna kitu chochote kile ambacho kitanizuia kumharibu!" Akauma meno yake kwa hasira. Kisha akatazama saa yake ya mkononi, "Tumebakiwa na masaa nane tu!" Kauli yake ilieleweka na ikamuondoa Viktoria kutoka pale chumbani. ******* Mnamo majira ya saa kumi jioni, ugeni mpya ambao haukutatajiwa uliwasiri mbele ya jumba hili kubwa lililofanana na kasri. Gari aina ya VX lilizuiliwa na walinzi ambao daima walikuwa makini kuchambua magari yanayoingia na kutoka kwenye uzio huu. Na yeye wakazuia gari lake lisipenye katika geti la jumba hili. Aliyekuwemo ndani yake akafoka na kulalamika kama ambavyo alizoea kufanya hivi siku zote. "Namna gani bwana! Kijana...mimi ninaweza kukufanya uachishwe kazi hapa! Usiniletee upuuzi wako!" Alifoka kwa sauti kubwa. Walinzi wale ambao walisimamia kauli yao kuwa hakuna mtu yeyote yule aliyealikwa siku hii na hawana maelekezo ya kumruhusu yeyote wakazidi kutanua vifua vyao kumzuia asipite. Akatoka nje kwa hasira akiwa amechachamaa! Akatoa simu yake mfukoni na kuipekua upesiupesi huku akiendelea kutukana. "Mnajifanya mnajua sana sheria eh?! Sasa ngojeni!" Akainyanyua mpaka sikioni mwake ikiwa inaita. "Halooo! Naam Franko!...kama nilivyokueleza. Naona hawa mburukenge wananizuia nisipite hapa!" Akafoka! Kelele zake zikawachangamsha mpaka mbwa ambao walikuwa wakishikiliwa siku zote kusaidia ulinzi na kukosa kazi maalumu maana hapakuwa na hatari yoyote ambayo wangeishuku. Leo hii wakaona fursa ya kuonesha umuhimu wao na ili waonekane kuwa hawali nyama za bure, wakaanza kubweka kwa fujo. Mara moja simu ikapigwa na maelekezo mapya yakatolewa. Ishara zikatembea baina ya hawa walinzi na wakachungulia ndani ya gari lake kuhakikisha kuwa alikuwa ni yeye peke yake kisha geti likafunguliwa kumruhusu mgeni huyu aingie. Akarudi ndani ya gari mara moja huku akisonya kisha akavurumisha gari lake kwa fujo na kuzama ndani ya uzio huu mkubwa. Nyuma yake geti likafungwa na ukimya ukarejea upyaa. ******* "Unataka kuniambia kuhusu nini?" Don Franko akamuuliza Brown Kizito, Boss Mzito! Mgeni ambaye ni nusu saa tu iliyopita tangu wawasiliane na kumruhusu afike mahala pale kabla hajakutana na rabsha za walinzi kumzuia getini. Akakohoa kidogo na kutamka, "Najua kuwa leo nd'o siku iliyopangwa kwenda kumuwinda huyo mbaya wetu hukohuko alikojificha na mimi kama mtu wa karibu nisingekubali kuliruhusu hili lipite bila kuweka walau thumuni ya jitihada zangu kukisaidia chama chetu!" Akaweka pumziko kisha akaendelea. "Nimekuja hapa ili kukupa dondoo kadhaa juu ya huyo mtu mnayeenda kumtafuta leo hii. Kwanza kabisa naomba unipe ruhusa yako...kabla sijaendelea!" Akainamisha kichwa chake kwa nidhamu. Don Franko akarekebisha mkao wake juu ya kiti akapumua pumzi ndefu kisha, "Endelea Kizito...endelea!" "Naam, ujue mtu tunayeenda kumtafuta huko hatujui ni namna gani amejipanga! Na isitoshe sisi hatuna ramani ya ule msitu. Naogopa sana kudhania kuwa tunaenda kupigana vita kwenye uwanja wa ugenini. Tena tunaingia kichwakichwa tu bila ya kuwa na uelewa mzuri wa mitego ambayo tumetegewa huko!" Akaweka kituo akimtazama Don Franko, akiwa na matarajio kuwa maneno yake huenda yatamfurahisha ama yatampa sifa kubwa. Badala yake Don Franko akaangukia kwenye kicheko cha kifidhuli ambacho kilimfanya apaliwe na kukohoa kwa taabu kwa sekunde kadhaa. "Sikutegemea kama utafikia hatua ya kutudharau namna hii Brown, sikutegemea kabisa! Yaani ni heri maneno uliyoyasema nimeyasikia mimi peke yangu. Maana nina uhakika kama timu yangu yote ingeyasikia basi muda huu wewe ungekuwa umepasuliwa vipande vipande halafu mbwa wa kule getini wangeachiwa nyama yako wakufaidi! Yaani unadhani sisi ni wapumbavu kiasi hicho? Kweli Brown?" Akabadilika sura yake na akavaa uso ulioiva wenye macho yenye gadhabu. Brown Kizito, a.k.a Boss Mzito akajichekesha na kutamka, "Aaah hapana mkuu kwani kuna jambo ambalo sijalijua? Au nipo nyuma ya muda kidogo" Don Franko akasikitika kisha akanyanyua kichwa chake na kumtazama upya Kizito, "Ni nani aliyekuroga? Ulianza vizuri sana lakini naona unazidi kupungukiwa na akili siku baada ya siku. Hivi unadhani sisi tunaweza kwenda vitani bila kujua tunapigana na nani?! Nakusikitikia sana ndugu yangu, mchawi aliyekuroga siku hizi hajaondoka na akili tu, amekokoroa mpaka ufahamu wa kawaida ambao kila mtu anao. Hata hivyo sishangai... Ni upumbavu wako huohuo uliotufelisha kumkamata huyu kijana upesi, eti ukakodisha vijana wa mtaani licha ya ukwasi ulionao. Ni upumbavu huohuo unaokufanya ugombane na walinzi getini. Kamuombe msamaha huyo mchawi aliyekuroga! Mwambie akurudishie walau robi ya ufahamu wa kawaida!" Akamaliza. Boss Mzito akakohoa kidogo kisha kwa sauti iliyojaa nidhamu akajititumua na kutamka, "Uum mkuu! Sio kwamba nina hofu juu ya utendaji wenu na mipango mlioiandaa. La hasha! Nilichokitaka mimi ni kushiriki bega kwa bega na nyinyi kwenye hii shughuli. Nataka nipigane pamoja nanyi ubavu kwa ubavu. Mpaka tufufue kila kitu ambacho chama chetu kimepoteza. Hilo tu!" Akanyanyua mikono yake kama ishara ya kusihi na kujiondoa kwenye upande wenye makosa. Boss Mzito akatazama saa yake ya mkononi kisha akasimama na kuondoka bila kumtazama Boss Kizito huku akisema, "Tuna masaa mawili tu! Kaa tayari..." Akamuacha Mzito pale juu ya kiti. Na alipotoweka usoni mwake, Boss Mzito akakagua pembe za chumba hiki kikubwa na akang'amua kuwa hakukuwa na kamera wala rwkoda zozote zile zilizokiwa zikimtamzama. Akavuta kifaa kidogo kilichokuwa kwenye kifungo chake cha shati akakibofya na kutamka... "Nadhani mmesikia kila kitu....saa kumi na mbili kamili wataondoka hapa rasmi. Kaeni tayari!" Kisha akakibofya kukizima. Akasimama na kuondoka eneo lile kimya kimya. ******* Ndani ya buti ya gari lililoingia punde tu ndani ya uzio wa jengo hili, kulikuwa na viumbe wawili ambao jasho liliendelea kuwavuja huku joto likifukuta kwa fujo. Taarifa ya kuendelea kusubiri kwa masaa mawili zaidi, ikawafanya wajutie mpango huu waliousuka wao wenyewe. 'Tutakuwa kwenye buti ya gari yako na usifanye upuuzi wa aina yoyote ile tutawashtua wenzetu ambao wanatufuatilia kila hatua ambayo tunapiga na wewe! Wewe fika huko na hakikisha tunafika mpaka eneo la tukio!' Yalikuwa maelekezo maalumu yaliyotolewa na Konstebo Tito Ngeze ambaye muda huu alitaka ajulikane kama nabii Tito kwenye hii misheni. Boss Mzito akatii na kuhaidi uaminifu wake endapo tu ataokoka na mikono yake ibaki safi. Abednego Kagoye akaongezea kitisho kuwa kama akiwachomea utambi kwa hawa matajiri wake basi na yeye ataweka wazi kila siri aliyoitoa. Huyu akataka kujulikana kama Kingi Nego kwenye hii misheni ya kumuokoa swahiba wake Feruzi. Wakala dili na sasa yamebaki masaa machache tu. ---------------------------------- Naam bado masaa mawili.... Timu mbili zimejiandaa kwa ajili ya mapigano.. Don Franko dhidi ya Franko Dario. Kitajiri nini tena huko msituni? Haya yote tutayajua hapa hapa... Muhimu share link ya chaneli *`ITAENDELEA KESHO`*
👍 💪 2

Comments