
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
February 20, 2025 at 07:16 PM
*`SHAMBA LA HELA`*
Yake; *Godlove Kabati*
WhatsApp; 0763204351
-------------------------------
Sehemu ya ishirini na nne
*HEKAHEA MSITUNI*
-----------------------------------
Utulivu uliotawala kwenye maficho yao, uliwazawadia hisia kali mno ambayo ingeweza kumuona hata mdudu mdogo anayetambaa ardhini, kama tu angesababisha kelele isiyohitajika.
Walitulia huku wakilitazama jua linavyozidi kufanya safari yake ya siku zote, muda ukipotea na saa zao zikazidi kuwajulisha kuwa hata hii jioni inakaribia kuwaaga ili kulipisha giza la usiku.
"Mkuu! Una uhakika kuwa watanasa kweli?" Dubu akaitangaza wasiwasi yake ambayo alishindwa kuivumilia kwa wakati mrefu. Na sasa alikiwa anaelekea kutumbukia kwenye shimo la kukata tamaa.
Franko Dario hakumjibu. Aliendelea kuinamisha kichwa chake akiitazama ardhi.
Kofia yake pana ikificha sehemu kubwa ya kichwa chake. Alionekana kama mtu aliyelala tayari.
"Mkuu! Mkuu!..." Dubu akajaribu kumshtua.
"Watafika hapa muda wowote kuanzia sasa hivi wakiongozwa na yule chambo wetu." Kwa sauti yake kavu akamjibu bila kuinua kichwa chake.
Wamejificha eneo lile tangu saa kumi na moja alfajiri na sasa ikiwa ni saa kumi na mbili jioni. Bado hakuna dalili yoyote ile ya mjongeo au harufu ya wageni kwenye eneo hili. Duba na Dubu ndio walikuwa karibu zaidi na Franko Dario. Huku vikosi vya wapiganaji wale wa msituni vikiwa vimejipanga mafichoni, wakisubiria amri tu ili wazitumie silaha zao za moto.
Taratibu Dario akainua uso wake na haukuwa wa kawaida. Ile hali yake ya siku zote ambayo ilimtokea kama tu amekasirika au ana maumivu ilikuwa imemteka upya.
Chozi la damu lilikuwa linatiririka kutoka kwenye jicho lake la kulia. Jicho lililopata mkosi wa kupitiwa na ufa uliosababisha kovu kubwa usoni kwake.
Akalifuta chozi lile kwa kiganja cha mkono wake kisha kwa kukakamaza misuli ya shingo lake akavuta kamasi puani mwake na makohozi yote yaliyokuwa yamejikita kwenye njia zake zote za hewa.
Akatema kusanyiko kubwa la kohozi lililochanganyikana na damu.
Akakohoa tena kwa nguvu mara tatu, akakusanya tena na kutema makohozi yenye damu kando. Akachukua kibuyu cha maji na kusukutua kinywa chake.
"Hali yangu inazidi kuwa mbaya. Nimebakiwa na muda mchache sana wa kuishi lakini nilijihaidi kuwa sitakufa mpaka nitakaposahihisha kosa langu la tatu.
Nikisahihisha hilo usiku huu wa leo, nitakuwa nimesahihisha makosa yote ambayo niliwahi kuyafanya." Dario akatamka kwa sauti ya kinyonge kana kwamba anatoa wosia.
"Vipi mkuu kwani unaumwa?!...maana sio mara kwanza kuona unatema damu, kama unajihisi vibaya nadhani utulie tu sisi tutamaliza kila kitu hapa."
Duba akamtamka huku mkono wake mmoja ukiwa begani kwa Dario akimfariji na kumtuliza kwa pamoja.
Dario akamtazama kwa sekunde mbili kisha akaachia tabasamu jepesi, hajazoea kutabasamu na kama akitabasamu basi humaanisha.
Akabadilisha mkao wake na kutamka,
"Umepita mwaka mmoja na nusu tangu nikutane na nyinyi. Yalianza kama mahusiano baina ya mwajiri na waajiriwa tu lakini mahusiano yetu yakaota mizizi mpaka tukawa kama ndugu.
Siku ambayo niliacha kuwachukulia kama mabaunsa wangu ni ile ambayo mliniaminisha kuwa mtakuwa pamoja nami kwenye kila shida na raha. Na kweli mpaka sasa tumeishi wote humu ndani ya huu msitu pamoja.
Miezi sita ya kupambana na baridi na wanyama wakali, mmekuwa nami.
Licha ya ulemavu wangu na roho mbaya niliyo nayo bado hakuna siku yoyote ile ambayo mlininyima heshima.
Tumepata kila tulichokitafuta huku...na kama Mungu akipenda nadhani leo nd'o siku ya kuondoka huku rasmi.
Dubu, Duba!
Mpaka tunamaliza hii vita, tambueni kuwa mimi sina ninachowadai. Bali nyinyi ndio mnaonidai.
Sioni kitu chochote kile cha thamani kinachoweza kulinganishwa na uaminifu wenu kwangu. Kama ni hela tulizozichimba nadhani mmeziona za kutosha.
Lakini nina ombi moja tu kutoka kwenu. Ombi moja tu!
Nataka mnihaidi kuwa mtalitimiza...
Niahidini!"
Hapa Dario akanyoosha mkono wake na kuvikamata viganja vya Dubu na Duba kwa nguvu. Kwa pamoja wakatamka wakiwa na wasiwasi,
"Tunakuahidi"
"Hakikisheni kuwa kaka yangu anabaki salama. Najua kuwa mimi nitakufa lakini sitakufa kizembe. Kwanza ni dhambi kufa kizembe.
Ila kama nikifa nataka nyie mhakikishe kuwa ndugu yangu niliyeshiriki naye kunyonya titi la mama mmoja anabaki salama! Nadhani mpaka hapo mmenielewa"
Wakatazamana kwa sekunde moja kisha kwa pamoja wakatikisa vichwa na kutamka,
"Sawa tunakuahidi!"
Na kabla hawajakaa sawa wakashuhudia shina la mti uliokuwa kando yao ukichanika na kupasuka kwa nguvu, tukio lililofuatiwa na mlio wa kutisha wa risasi.
Kitendo hicho hakikuwashtua, walikitegemea na ilionekana ni kama walikisubiri kwa muda mrefu.
Ilikuwa ni ishara ambayo waliitegemea kutoka kwa mmoja kati ya walinzi kuwa kama tu kutakuwa na ugeni wowote ule basi apige risasi shina lile la mti na wao wataelewa.
"Wamefika!" Dario akanong'ona.
Wakamsaidia kusimama, akaiokota fimbo yake na kwa pamoja wakaeleka kujipanga kwenyeeneo walilolokuwa wameliandaa wao.
*******
Magari sita yalisimama kwa fujo na kutimua vumbi kwenye eneo ambalo lilionekana kushindwa kumiliki upana wa kutosha kuruhusu magari haya kupita.
Kutoka kwenye magari matatu, wakachupa vijana kumi upesi. Wamebeba silaha za moto na wamekunja ndita kwenye nyuso zao kuonesha wako pale kwa ajili ya kazi ambayo haihitaji kutabasamu wala kucheka bali inataka uwe na hasira, roho mbaya na makasiriko ndipo utaimudu.
Walikuwa vijana kumi waliovaa mavazi ya maalumu wa ajili ya mapigano. Miili yao imevimba kwa mazoezi ikifunikwa na makoti maalumu ya kuzuia risasi kupenya yaani bulletproof. Silaha kadhaa zilizokosa nafasi kwenye mikanda na vifua vyao, zikafungwa mapajani.
Upesi wakafungua milango ya magari mengine na wakashuka wale maafisa saba wakiwa na mavazi yao yaleyale meusi.
Kisha wakatolewa Feruzi na Mtemi kutoka kwenye gari moja wapo huku midomo kadha ya bunduki ikiwa imewanyookea kana kwamba wao ni watu hatari zaidi ambao wanaweza kuleta balaa muda wowote.
"Sikieni vijana!"
Sauti ya kike ya Viktoria ikasikika huku akiwaelekea Feruzi na Mtemi.
"Kwa mwendo wa taratibu...bila papara. Mtatuongoza mbele na sisi tutakuwa nyuma.
Kama tulivyokubaliana, mnatupeleka kwanza lilipo shamba halafu tunamalizia kwa..."
Sentensi yake ilikatishwa kwa sauti ya hasira iliyokuwa inatetemeka kwa gadhabu..
"Hapana Franko!..hapana! Shamba lipo na tutalikuta tu. Hapa tunataka kwnaza tuanze na huyo Dario. Kazi za kutafuta shamba zitafuata baada ya kukipata kichwa chake hivyo tu basi. Hakuna jingine!"
Alikuwa ni Don Franko. Alifoka kwa nguvu mpaka akawa akitoa matone ya mate kinywani.
Na kweli, amri yake ikasikilizwa na mpango ukabadilika.
Lakini Mtemi akawasubirisha,
"Eer samahani wakuu...nataka kuwataarifu tu kuwa njia inayotupeleka kwa Dario inapitia kwanza shambani halafu inanyooka kuelekea kwake. Hivyi msije kushangaa!" Akatamka akiwa na utulivu.
Wakamtazama na kuyapima maneno yake.
"Tambua tu kuwa kama unayoyatamka ni uongo au njia ya kutulaghai basi kifo chako kitapitia njia ngumu sana!" Viktoria akamuonya.
"Sawa twen'zetu!" Wakaondoka.
Feruzi ambaye alikuwa bado amebaa, akashtukia kichwa chake kinashtuliwa kwa pigo la kadri kwa kitako cha bunduki,
"Tembeaaa!"
Yeye na Mtemi wakaongoza kundi huku mikono yao ikielea juu na nyuma yao wakiwa chini ya ulinzi mkali wa midomo ya silaha za moto.
Feruzi akazidi kutetemeka akilalamika kuwa hajui lolote lile. Na kweli, alikuwa hana kumbukumbu ya aina yoyote ile kuhusu Dario wala shamba linaloongelewa.
Zaidi zaidi yeye alikumbuka tu kuwa alijikuta katikati ya msitu wa kutisha na waliomzunguka hawakuwa watu wa kawaida.
Walimtishia kwa kumuonesha rangi halisi ya damu ya mwanadamu namna inavyofanana ikiwa tu itavuja kwa wingi.
Wakamtishia uhai wa maisha yake na kumpa zawadi ya hela kisha wakamuachia tena kwa kumfunga kitambaa usoni ili asiione njia.
Hakika alostahili kulalamika kiwa anaonewa.
Lakini hali ilikuwa tofauti kwa Mtemi Moringo. Yeye hakuwa na wasiwasi wala hofu. Alionekana kujiamini sana. Na hapo ndipo Feruzi akazidi kuchanganyikiwa,
"Oya Mtemi! Unaenda wapi mzee? " kamuuliza kwa kunong'ona.
"Tulia dogo tulia!" Akamjibu kwa kunong'ona pia.
Baada ya dakika kumi na tano wakafika sehemu yenye mteremko wa wastani na kichaka kikazidi kuongezeka. Wakaanza kupata taabu kukwepa miiba na miti iliyowazuia kupita kwa urahisi.
Mmoja wa wale vijana aliyekuwa amekunja ndita zake usoni kwa makasiriko akajisahau na koti lake likakwama kwenye miiba alipohangaika kujinasua akajikuta amechana koti lake.
Hapo Mtemi akawageukia,
"Aisee jama..nilisahau kuwapa angalizo hii njia tunayopita ni sehemu yenye ugumu kidogo . Sasa wale mliojifungafunga mabomu na makombora mjipange aisee sijui kama mtapaweza!"
Akatamka Mtemi akiwa na sauti iliyoonesha waziwazi kuwa haogopi kitu chochote kile. Zaidi zaidi anataka kufanya mizaha.
Sentensi yake ikamkasirisha kijana yule aliyechana koti lake. Hasira yake ikaonhezeka maradufu baada ya kuitafsiri kauli hii kama dharau akamsogelea Mtemi na kumtandika mkwaju wa nguvu kwenye mguu wake wa kushoto,
"Ongoza njiaaa!! Acha mizaha!"
Bila kujibu wala kulipiza Mtemi akazidi kuongoza njia.
Kwa kuhangaika wakafanikiwa kukatisha kona kadhaa ndani ya kichaka hiki kilichobebwa na ardhi yenye mteremko. Mara wakaibukia kwenye ardhi iliyotengeneza bonde kubwa.
Lahaula!
Macho yao hayakuamini walipokutana na eneo hili. Palifanana na mgodi wenye madini ya fedha.
Makasha mengi kwa idadi yaliyojaa noti za fedha yalitulia tuli. Yalikuwa mengi mno,
Hakuna mashine yoyote ile duniani ambayo ingemudu kuhesabu noti zote hizi bila kupata hitilafu.
Labda wingi wake ungepimwa kwa mizani.
Wakachukua dakika kadhaa kushangaa. Hata wale wakunja ndita wakazikunjua kwa dakika chache kwanza.
"Tupite huku wakuu...hapa tuachane napo kwanza. Dario yuko huku!" Sauti ya Mtemi ikawashtua na kuwatoa kwenye kilindi cha mawazo.
"Mhm..mhm..subiri kwanza!" Don Franko akamtuliza.
"Ulisema kuwa yeye yuko mbele halafu hili nd'o shamba lenyewe eh?" Akamuuliza kwa mara nyingine.
Mtemi akatikisa kichwa kukubali.
"Aiseee!" Don Franko akaweka mikono yake kiunoni akishangaa eneo lile kubwa lenye mita za mraba za kutosha.
Wakasogea wale wenye suti nyeusi ambazo hivi sasa hazikuwa na ule unadhifu wake tena shauri ya vumbi na utomvu wa mimea ya msituni.
"Mkuu! Nataka nikushauri kitu....ujue hapa ni kama tunacheza kamari. Sawa...tutaenda kule kwa Franko Dario, lakini hatujui kama tutarudi sote tukiwa hai.
Ni kwanini tusijigawe hapa...wengine wasimamie hii hazina iondoke, halafu wengine wakamsake huyo mtu?" Yalikuwa maoni ya mwanaume mmoja wao.
"Unategemea tutapita vipi na hii shehena yote kwenye njia kama hizo zenye miiba?" Don Franko akamuuliza swali gumu ambalo alishindwa kulijibu.
Viktoria akarudi nyuma na kumnong'oneza Don Franko,
"Nina wasiwasi na huyu kijana ambaye ametuongoza hii njia. Inawezekanaje asione hofu yoyote licha ya hatari kubwa aliyonayo Dario?
Halafu bado anatufanyia mizaha tu.."
Don Franko akamtazama Viktoria na kuyapima maelezo yake. Akagundu kitu ambacho alikuwa amechelewa sana kukigundua.
Walipotoka ni mbali, wanakokwenda hawakujui. Ubongo mmoja tu ndio unaowaongoza njia. Nao unaonekana umekaa kwenye mfumo ambao unaweza kuwasababishia hatari muda wowote ule.
"Tuongeze umakini tu basi...kama hajatudanganya kuhusu shamba, sitegemei atudanganye kuhusu Franko Dario!" Akahitimisha.
Wakachagua kuendelea mbele zaidi.
Feruzi akazidi kuchanganyikiwa maradufu akamnong'oneza Mtemi,
"Kaka..kaka. Mbona ni shamba tofauti hili? Mimi nilipokuwa hapakufanana hivi. Au ni nini umepanga kufanya?"
Mtemi akamsogelea karibu zaidi na kumwambia,
"Sikia...sogea hapa. Ukisikia mlio wa kwanza wa risasi lala chini haraka halafu viringika kushoto kwako sawa?"
Hakueleweka.
"Unasema?" Feruzi akamuuliza akiwa na kitete.
"Acha ufala! Nimesema ukisikia mlio wa kwanza wa risasi. Lala chini upesi halafu viringika kushoto!"
Sauti yake ilikiwa ya chini mno.
Wakiwa kwenye muinuko wa kadri mara ghafla ukasikika mlio wa risasi hewani.
Paaaa!
Wote wakashtuka na kusimama.
Wakiwa bado hawajafanya upembuzi yakinifu, ikamwagika mvua ya risasi kuelekea walipokuwa wao.
Upesi Feruzi na Mtemi walikuwa wameikumbatia ardhi na kuviringika kila mmoja kwenye upande wake.
Kila mmoja akashikiria silaha yake mkononi na kuanza kutetea uhai wake. Aidha kwa kutafuta yalipo maficho. Au kwa kujibizana na walengaji waliokuwa dhidi yao.
----------------------------------
Minyukano na mitafutano imeanza.
Kikosi cha Don Franko kimeanza rasmi kumuwinda Franko Dario.
Ni nini kitajiri?
Je wako wapi nabii Tito na King Nego?
Tutayajua haya yote siku ya *JUMAMOSI*
--------------------------------
Simulizi ya *'KIKAO CHA HAKI'* sasa inatarajiwa kutoka rasmi tarehe 23 ya mwezi huu.
Itagawiwa bure kabisa kwa kila mwanafamilia wa chaneli hii.
Kuipata simulizi hii, ni rahisi sana...
Tuma neno *KIKAO CHA HAKI* kwenda namba 0763204351.
Na utaunganishwa moja kwa moja kwenye orodha ya wataogawiwa bure kabisa kazi hii.
Kumbuka ni ofa ya siku tatu tu kuanzia Jumapili hii.
Asante! 🙏🙏🙏
🙏
❤️
👍
🔥
5