MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
February 22, 2025 at 07:41 PM
*`SHAMBA LA HELA`* Yake; *Godlove Kabati* WhatsApp; 0763204351 ------------------------------- SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO *Uwapo kwenye uwanja wa vita, hakikisha unatangulia kumuona adui yako kabla yeye hajakuona...* *Na hii ni sehemu ya ishirini na tano...* Ile hali ya hewa waliyoikuta katika hali ya utulivu, ikachafuliwa mara moja kwa kukubali kuruhusu milio ya risasi na hekaheka za hapa na pale. Bila kutegemea Don Franko na wenzie walijikuta wamewekwa katikati ya bonde na kutokea kwenye miinuko miwili iliyokuwa mbele na nyuma yao, iliwanyeshea mvua ya risasi ambazo hazikuwa na salamu kwa kitu chochote kile kilichozizuia zisiendeleze mwendo wake. Kabla hajatoa amri, Don Franko alikishuhuhudia kichwa cha kijana mmoja aliyekuwa kulia kwake kikifumuka na kupasuka kwa ghafla sana baada ya kuchanwa na risasi. Ile anageuka nyuma tu, akahisi kitu kama jiwe dogo lililo kasi limekatiza karibu kabisa na sikio lake kabla halijagota kwenye shina la mti uliokuwa mbele yake na kuuchana! Alikuwa amekoswa koswa na risasi. "Ingieni mitini haraka!" Akiwa ameinama akatoa amri na kukimbilia mitini, wachache waliobaki walimfuata maana wengine walishakimbia zamani kuziokoa nafsi zao. Ni nani angekubali kubaki afe akinyeshewa mvua kama hii kisa tu amri haijatolewa? Hiki hakikuwa kikosi cha jeshi kusubiria amri, kilikuwa kikundi cha magaidi na mahaini. Zaidi kuna mmoja kati ya vijana wale wakunja ndita aliendelea kuzubaa, ni kama ambaye hakuwahi kusikia mlio wa risasi hapo kabla. Huyu hakufanikiwa kukimbia, mwili wake ulipata bahati mbaya ya kutobolewa kwa risasi za kutosha kabla hajaiaga dunia. Wakiwa ndani ya mkusanyiko mkubwa wa miti, bado washambuliaji waliendelea kumimina risasi bila stahi. Walipiga risasi ovyoovyo ili mradi tu wabahatishe kuua walau kiumbe chochote kile hai ambacho kimo ndani msitu ule mzito wa miti na hawakioni. Jambo lililopelekea shabaha zao nyingi zipotelee kwenye matawi ya miti na popote pale pasipolengwa. Kosa la washambuliaji hawa likawa nafuu kwa Don Franko na kikosi chake, wakapata mwanya wa kutafuta uelekeo wa eneo salama zaidi na kupanga mbinu mpya ili walijibu shambulio hili la ghafla. Ashukuliwe sana yule fundi aliyetengeneza haya mavazi ya kuzuia risasi kupenya. Muda huu walimpa maua yake bila kujua kama yuko hai au tayari alishawekewa vishada vya maua kwenye kaburi lake. "Imekuwa ghafla sana, sikutegemea kama tungekutana na shambulio la ghafla namna hii!" Don Franko akiwa amejibanza nyuma ya kichuguu kikubwa yeye na wenzie wanne, akatamka huku akihema. "Itakuwa huyu fala alijua mapema kuwa tunakuja...au labda ana walinzi wake huku muda mrefu." Akaongezea huku akizitazama nyuso za wenzie ambazo nazo zilikuwa zimesawijika tayari kwa uoga na hofu ya kukipokea kifo kwa lazima. Wengine wakiwa wameshika vifua vyao wakihema kwa hofu. Ni wazi kuwa masikio yao yalikuwa yamepitisha miaka mingi kabla ya kusikia milio ya risasi mubashara labda kwenye filamu. "Nilikuambia mapema Don Bosco, kuwa wale vijana wawili wale wanatupeleka motoni. Niliziona nyuso zao kuwa hazina wasiwasi hata kidogo!" Viktoria akachangia kwa sauti ya chini inayohema pumzi yenye hofu na kukata tamaa. Wakati huu hakulitaja jina la mkuu wake kwa kutanguliza cheo mbele, kwenye hatari ya kufa wote walikuwa na vyeo sawa. Hata hivyo ile fimbo ya mamlaka haikuwepo tena kwenye himaya ya mikono yake. Maneno yake yakajibiwa kwa tusi kali la lugha ya kigeni kutoka kinywani mwa Don Franko akiwatukana Feruzi na Mtemi kwa pamoja. Kisha akashusha pumzi kwa nguvu na akaikamata barabara bastola yake kubwa iliyokuwa imehamishia makazi kwenye mikono yake miwili. Akanyanyua shingo yake na kuangaza huku na kule kisha akainama chini taratibu kisha akanong'ona, "Hawa ni wapiganaji wa msituni...lakini inaonekana hawana mazoezi ya kutumia silaha za moto kwa ustadi. Hapa tupo sita na hatujui wengine wako wapi, ila ninajua fika kuwa watatumia ujuzi na weledi wao kujiokoa. Tutakachokifanya sasa hivi, ni kujigawa kwenye makundi mawili ya watu watatuwatatu. Halafu tutapanda juu kwa tahadhari kubwa iwe kwa kutambaa kwa matumbo, kuviringika au kunyata. Jamco! Una mabomu mangapi ya mkono hapo?!" Akatupa swali kwa kijana mmoja aliyekuwa amekakamaa. "Manne mkuu!" Akajibu kwa nidhamu. "Safi...na wewe Jofu?!" "Manne mkuu!" "Sasa nyie mtatugawia hayo mabomu kwenye makundi mawili, kila mtu apate sawa sawia . Tutawashtua nayo hayo kabla hatujawashambulia na kuwapunguza. Msisahau kuzingatia uchumi wa silaha tulizo nazo. Hatujui wao wamejipanga vipi hawa!" Akaweka kituo na wakajigawa kama walivyokubaliana. Don Franko alitambaa kwa tumbo mpaka alipofika kwenye eneo ambalo lilimlazimisha kuchutama na kunyata kutokana na mkusanyiko wa mizizi mikubwa. Akafanikiwa kuwaona watu sita waliokuwa makini kuzishindilia bunduki zao kwa risasi. Upesi akawawahi na kuwadungua mmoja baada ya mwingine na akamuacha mmoja kama mateka. Huyu akawa kama masihi aliyezibeba dhambi za wengine. Kwanza akateguliwa mguu wake ili asikimbie kisha vidole vyake vya mkono wa kulia vikavunjwa kimoja baada ya kingine. Anajaribu kujitetea lakini lugha yake haieleweki. Mwanzoni alidhaniwa kuwa anaigiza tu na lugha yake isiyoeleweka ikawa kama chumvi iliyoongeza ladha ya mateso yake. Lakini baada ya vidole vyote vya mkono wake kuvunjwa pingili kwa pingili ikaonekana kuwa ni wazi hii ni lugha yake. Labda lugha ya msituni au lugha ya siri, lugha ya kigaidi. Akawa anaulizwa swali moja tu lenye maneno mawili, "Franko Dario?!" Na ilimbidi ajiongeze kuwa hawa watesi wake wanataka awapeleke alipo Dario. Hapa ikaonekana sura mpya ya huyu mateka asiyeeleweka. Alikuwa na moyo mgumu mno licha ya machozi kuchukua nafasi kwenye madirisha ya macho yake. Hakutoa ushirikiano wowote ule. "Huyu ni gaidi! Wanapitiaga mafunzo maalumu ya kugoma kutoboa siri hawa!" Vikitoria akang'aka kwa jazba huku akiachia kofi kali juu ya uso wa mateka huyu. Ambaye alionekana kama kutekenywa tu na kofi lile. Akatoa cheko la kifedhuli huku akimtazama Viktoria, akafungua kinywa chake na meno yake yaliyosalimu amri na kuamua kuwa meusi moja kwa moja baada ya weupe wake kushindwa kutunzwa, yakaonekana. Akatamka maneno yaleyale yasiyoeleweka na kabla hajamaliza tu, Paaaaa! Akaanguka chini akivuja damu nyingi kichwani kwake. Don Franko alishindwa kuvumilia zaidi, akaamua amuwahishe kwenye foleni ya watu wanaoifuata hukumu yao ahera. "Tuendelee kupandisha na huu mwinuko tutamfikia tu Dario!" Ikawa kauli yake ya mwisho. Giza likaanza kuumeza msitu na kutengeneza vivuli vya kutisha. ******* Mbio walizokimbia Feruzi na Mtemi Moringo, zingewawezesha kushinda medali ya dhahabu kwenye michuano yoyote ile ya riadha ambayo wangeshiriki jioni hii. Miguu niponye... Ndio aina ya mbio ambayo walichagua kuitumia. Walikimbia kana kwamba hawatakuja kukimbia tena maishani mwao. Mwanzoni Mtemi alikuwa mbele na Feruzi nyuma yake lakini ajabu na kweli, baada ya dakika kadhaa Feruzi alikuwa mita sita mbele ya Mtemi. "Oa Ferii..Feri weeee!" Mtemi aliita kwa sauti huku akipambana na uwezo wake wa kuhema. Feruzi hakumsikia mpaka aple alipomuita tea kwa mara ya pili na ya tatu. Hakusimama badala yake alishtuka na kujikuta akigaragara chini huku akipiga mayowe, "Nisamehe..nisameheni! Sijui alipo...simjui mie." Mayowe yake yakamshusha kwenye daraja la watu waliochanganyikiwa. Mtemi Moringo akamzaba kofi kali la uso ambalo lilimrudisha kwenye daraja la utimamu wa akili. Wote wakajipa dakika nyingi za kutulia na kuhema kwa nguvu mpaka pale walipopata nguvu na uhuru wa kuongea tena. "Oya mzee hujakoswakoswa kweli na zile njugu?!" Mtemi akamsanifu rafiki yake ambaye alionekana wazi kuwa bado yupo kwenye hamaniko. Feruzi akatikisa kichwa kuashiria kuwa yuko sawa. "Afadhali! Mambo yameenda kama ilivyopangwa. Sasaaa..." akaangaza huku na huko kama anayetafuta njia anayoifahamu. "Nifuate Feri..." Akasimama na kujikung'uta uchafu iliokuwa umeng'ang'ana kwenye mavazi yake. Feruzi bado hakumuelewa... "Nikufate twende wapi?" Akamuuliza akiwa mwingi wa wasiwasi. Tangu amekutana na Mtemi Moringo kwa mara nyingine, aligundua kuwa huyu hakuwa sawa na yule rafiki yake wa zamani aliyemzoea. Huyu alikuwa na ujasiri wa ajabu tena mbele ya watu hatarishi. Akiwa tayari akili yake imeshamzika na kumpa heshima zote wanazopewa marehemu, akawa na wasiwasi kuwa huenda mbele yake umesimama mzimu wa Mtemi Moringo na sio Mtemi kama Mtemi halisi. "Hebu subiri kwanza..." Feruzi akatamka akisita na kuinama chini, akaokota jiwe na kumkabili Mtemi akijitahidi sana kukaa mbali yake kwa mita kadhaa. Mtemi akabaki akishangaa tu. "Wewe ni nani...na unataka kunipeleka wapi?" Likawa swali lililobeba ujasiri. Mtemi akashusha pumzi na kutikisa kichwa chake kwa masikitiko. "Basi bro...basi,inatosha! Nitakueleza kila kitu unachotaka kujua. Kaa chini!" Akajaribu kumtuliza na kumketisha Feruzi ambaye alionekana kuwa atalitumia jiwe lile muda na saa yoyote ile. Mtemi akamsimulia: "Nilipopotea kutoka nyumbani, Niliingiliwa na pepo la tamaa ambalo lilinishawishi kufika moja kwa moja mpaka hapa ili tu kulishuhudia hilo shamba la hela ambalo ulilinadi. Mwanzo sikuwa na matarajio ya kuzihitaji hizo fedha. Lakini kila nilipoufikiria utajiri. Nikajiona kabisaaa, nakaribia kuupiga teke umasikini. Na kujenga kiota cha fedha kwenye maisha yangu. Sikuwaza kuhusu hatari wala yale majitu majabari ya kutisha uliyonisimulia. Nilichokiwaza ni fedha na utajiri pekee. Nilichokutana nacho ni zaidi ya ulichonisimulia. Kumbe kuna mambo ambayo wewe hukuyaona kaka. Nimeshuhudia kwa mara ya kwanza mbwamwitu na mbweha wakifugwa na kupewa majukumu kama ya mbwa tunaowafuga huko uraiani. Nikaonjeshwa ladha ya mateso makali mpaka mimi huyu Mtemi mwana wa Moringo nikatamani nitume barua za maombi ya urafiki kwa malaika mtoa roho..walau basi aje aichomoe roho yangu niondokane na mateso hayo niliyokuwa nayapitia. Ulipopigiwa simu muda ule, ulitishiwa sana ili tu wapate uhakika wa utambulisho wangu. Na kweli ikaonekana unanifahamu. Hilo kidoogo likanipunguzia dhahama na taabu. Nikawa kama nimeajiriwa kufanya kazi za hapa na pale kwenye kambi ya huyo Franko Dario. Akanihoji maswali mengi sana kukuhusu wewe, na akanitaka nimueleze ukweli wote bila kumficha kitu. Ndugu yangu, hapo utanisamehe bure kaka. Hebu fikiria mtu unashuhudia waziwazi mzoga wa mwanadamu aliyeuawa baada ya kukatiza tu kimakosa kwenye huu msitu, unatupwa kama chakula kwa mbwamwitu na mbweha waugombee. Mimi sio mnafiki bro, Nilitaja kila taarifa yako ili mradi tu ninaifahamu. Kuanzia unakozaliwa, elimu yako, kazi yako, timu yako unayoshabikia mpaka demu wako nilimtaja pale." Alipofika hapa akaweka pumziko na kumtazama Feruzi kidogo. Feruzi akashtuka lakini hakusema neno. Mtemi akaendelea, "Baadaye sana, ikagundulika kuwa kikundi fulani ambacho kina kisasi na Franko Dario kimegundua kuwa wewe ulifika huku. Kikaamua kukuwinda kwa udi na uvumba mpaka kikupate na uwapeleke moja kwa moja mpaka alipo yeye. Lakini wewe hukujua lolote lile kumuhusu na ilikuwa kama bahati mbaya tu ukaingia kwenye anga zisizokuwa zako. Yaani kama malaika aliyekosea njia akajikuta Jehanam. Huruma ikaushinda ukatili wa moyo wake, akaunganisha na maelezo niliyompatia kukuhusu. Akaamua kukusaidia! Na hapo akanitumia mimi kama chambo akinihaidi kutusaidia na kufuta kila kivuli cha ubaya kitakachojaribu kutufuatilia hapo baadaye. Kiufupi alitaka kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Akuokoe wewe halafu awaangamize hao watu wa chama cha giza, kinajiita Mwanga wa giza. Akanipatia ujumbe maalumu na kunipa maelekezo ya namna nitakavyoondoka mpaka nitakapofika na kukutana na hawa watu. Nikawapa mchoro mzima wa mahala ninakotoka mpaka mahala ulipo wewe. Nadhani nd'o ule usiku ambao uliambiwa uende kwenye viwanja vya Gymkana usiku? Unakumbuka bro? Enhee sasa huo ulikuwa mchoro mzima kaka. Mimi niliamua kuwa muigizaji, nikaigiza vizuri sana hii tamthilia. Nikaigiza mbele yao nikijifanya sielewi kitu nikichelea sana uzima wako na wangu. Mpaka tulipofika hapa msituni nikajua tayari tamthiliya ninayoiigiza inakaribia mwishoni. Na kama kawaida sterling huwa hafi... Nd'o nimekuleta mpaka huku mzee. Mimi na wewe nd'o masterling wa mchezo mzima. Hatujafa!" Akatia nukta na kumeza funda la mate. Simulizi yake ikamuacha Feruzi kinywa wazi. Hakujua ajibu nini. Akabaki kumuangalia Mtemi Moringo akimvika vyeo vipya vya kila aina. "Sasa kilichopo hapa bro..." Mtemi Moringo akaendelea. "Kabla sijaondoka huku kuja kuigiza hiyo tamthiliya, niliapa kwa jina na nikaokota udongo nikihusisha mifupa ya babu yangu kuwa nitakaporudi nikulete wewe ukiwa hai. Tena nikupeleke moja kwa moja mpaka kwa huyo, Franko Dario!" Akamaliza akiwa kwenye kilele cha tabasamu na ushindi moyoni mwake. Mara ghafla, Vuuuuuuuum! PAAAAH! Ukasikika mvumo wa kutisha kisha mlipuko mkubwa ukatokea eneo hili. -------------------------------- Mama ee🙆‍♂️... Msitake tuamini kuwa kuna roho za watu zimerudisha jezi hapa aisee... Ni kipi kitaendelea baada ya Mtemi Moringo kuuweka ukweli wote nje nje? Share link ya chaneli... Acha reaction yako.. Na toa maoni kwenye 0763204351. Tutaendelea JUMATATU. ---------------------------------- Simulizi ya *'KIKAO CHA HAKI'* itatoka rasmi siku ya kesho. Itagawiwa bure kabisa kwa kila mwanafamilia wa chaneli hii kwa mfululizo wa siku tatu kuanzia kesho. Yaani kuanzia kesho mpaka siku ya Jumanne. Kuipata simulizi hii, ni rahisi sana... Tuma neno *KIKAO CHA HAKI* kwenda namba 0763204351. Na utaunganishwa moja kwa moja kwenye orodha ya wataogawiwa bure kabisa kazi hii. Asante! 🙏🙏🙏
👍 ❤️ 🔥 🙏 5

Comments