MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
February 24, 2025 at 08:41 PM
*`SHAMBA LA HELA`* Yake; *Godlove Kabati* WhatsApp; 0763204351 --------------------------------- SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA. *Unapoamua kusaini mkataba wowote ule na shetani..basi usitegemee uaminifu wa aina yoyote ile kutoka kwake...* *Shetani sio lazima awe na pembe na wala sio lazima awe na mkia...* *Naweza kuwa mimi, unaweza kuwa wewe, anaweza kuwa yeye.* *Shetani sio jina, ni cheo.* Tafsiri kadri ya uelewa wako.... Na hii ni sehemu ya 26. Mwanzo haikujulikana kama mlipuko ule uliondoka na roho ya mtu ama ulisababisha kilema cha maisha kwa kila kilichokuwa na uhai eneo hilo. Haikujulikana mpaka pale Mtemi Moringo alipouhisi mwili wake uko kwenye mapambano na maumivu, huku ushindi wake ukionekana kuwa mbali sana. Alitambua kuwa mwili wake umeketi ardhini ukiigemia kitu kama kisiki au shina la mti na mgongo ukimuuma sana. Akayafinya macho yake kwa uchungu na kugundua kuwa nayo yanamuwasha kutokana na vumbi kali. Hapa akakumbuka kuwa ana mikono. Alipojaribu kuinyanyua akagundua kuwa hata nayo imezuiliwa baada ya kufungwa kwa kamba ngumu na kukazwa barabara. "Tumetekwa tena!" Wazo hili likapita kwa kasi akilini mwake. Wakati huu hakutaka kuwa steringi wa tamthilia mpya, maana hakuwa na maelekezo kutoka kwa director. Akachagua kuwa mtulivu, akiyavumilia maumivu. Kwa mbali sanaa akayasikia majibizano ya risasi na baada ya muda kidogo akaweza kuyafungua macho yake taratibu. Yakakutana na sura inayotetemeka kwa hasira, akatumia sekunde kumi kuitambua sura ile....alikuwa Don Franko! "Sh...shkamooo!" Hofu yake ikamlubuni na kumfanya atoe salamu ya heshima. "Mpumbavu mkubwa wewe!" Midomo ya Don Franko ikamtetemeka na akatamka kwa jazba. Akaukunjua mguu wake uliovikwa buti imara na akasukuma teke kali juu ya kifua cha Mtemi Moringo. Ilikuwa ni kama anataka kukikanyaga mpaka akipasue. Mtemi akaoiga ukelele wa kilio. "Ulidhani utanidanganya kiwepesi namna hiyo eh?! Boga wewe..." Mbavu zilizochoka za Mtemi zikakutana uso kwa uso na buti lilelile,.lililozikanyaga bila huruma. Don Franko akabonyea ardhini na kukukamata kichwa cha Mtemi akimtazama usoni. Akaachia cheko la dhiaka kabla hajatamka, "Bado najiuliza sijui nikuue kwa kifo gani...maana nikikikanyaga kichwa chako mpaka kisagike nitakua nimekupendelea sana. Nikisema niyachomoe matumbo yako yote, mwembamba na mpana halafu niwape ndege wa angani, nitakuwa nimekupa nafasi ya kujitetea..tena hapo utanishukuru sana. Labda nikulipue kwa bomu....au we unaonaje?" Akaacha kauli yake ielee hewani kisha akaendelea, "Sikia bwana mdogo, sitaki niukate uzi wako wa maisha hapa duniani. Bado hujala chumvi nyingi wewe. Umekula raha gani wewe mpaka ufe mapema namna hii? Sasa sikia, nipeleke kwa huyo Dario. Halafu mimi na wewe biashara yetu itakuwa imeishia hapo. Japokuwa safari hii kama ukiniweka kwenye mtego, tambua tu kuwa mtu wa kwanza kufa atakuwa ni wewe!" Akatamka kwa sauti ya taratibu na upole. "Feruzi yuko wapi?!" Jibu lake likawa swali. "Umekubaliana na shauri langu?" Na yeye akajibiwa kwa swali. "Sifanyi chochote kile mpaka nimuone Feruzi." Kwa mara nyinngine tena Mtemi Moringo akatamka kwa ujasiri huku akitazamana na Don Franko macho kwa macho. Ujasiri huu ni kama ulimrudisha nyuma Don Franko kwa sentimita kadhaa. Haya macho aliyokuwa anatazamana nayo hayakuwa ya kawaida. Kwa mara ya mwisho aliyaona kwa vijana wahuni wavuta bangi wa mitaani. Macho mekundu yanayosubiri amri kutoka kwenye ubongo wenye hitilafu. Yakiamrishwa kuwa hicho yanachokiona ni adui, Piga! Anapiga. Akakohoa kidogo kisha akatamka, "Uum ninachoweza kukuhaidi ni kuwa utamuona huyo rafiki yako. Lakini kuhusu usalama wake, itategemeana na nidhamu yako. Haya simama upesi!" Akamnyanyua kutoka pale ardhinibkwa mkono mmoja kisha bila kumfungua kamba zile kwenye mikono yake akamuamuru atembee uelekeo ambao alimwelekeza. Mtemi akiwa mbele na nyuma yake akiwepo Don Franko na bastola mkononi mwake ikikitazama kichwa cha Mtemi. Hawakutembea hatua nyingi sana kabla hawajakutana na Feruzi akiwa kapiga magoti ameweka mikono yake kichwani. Alionekana hoi na mavazi yake yamechafuka kuonesha kuwa amekula suluba za kutosha. Mwanadada Viktoria alikuwa akimtazama kwa jicho lenye kila aina ya chuki na makasiriko. Na vijana wengine wawili wamemuelekezea midomo ya bunduki zao. Wakaungana pamoja kuifuata njia anayoiongoza Mtemi Moringo. Safari hawakutaka kufanya makosa ya kuwaweka pamoja kama awali. Badala yake Feruzi aliendelea kubonyezwa kwenye mwili wake kwa mapigo kadhaa na maumivu yake ndiyo yaliyomsurutisha Mtemi kuongeza mwendo, mikono yake ikielea hewani na kisogo chake kikilindwa na silaha kadhaa nyuma yake. ******* Kwa umbali wa takribani mita mia moja. Haya yote yalikuwa yakifuatiliwa kwa umakini sana na kiumbe aliyejificha kwenye tawi la mti mkubwa. Mkononi mwake alishika darubini iliyomwonesha msafara huu mdogo ambao ulitaka kufanana na ile misafara ya enzi za utumwa. Akatikisa kichwa chake kwa huzuni kisha upesi akashuka kutoka kwenye mti huu. Akawahi kupeleka taarifa upesi. "Mkuu, wanakuja ila hawako peke yao!" Duba akaiacha sentensi yake hewani. "Wako na nani? Au bado wamewekwa mateka?" Kwa sauti ya utulivu, Dario akauliza. "Ni mateka...lakini waliowateka ni watu wanne tu...nadhani tunaweza kuwazuia haraka kama tu ukituruhusu!" Akatamka kibabe huku akiikoki silaha yake kujiweka tayari kwa vita. Sura yake ikabadilika na kukakamaa kwa mara nyingine. Dario akasimama na kupiga hatua mbili mbele kwa taabu huku akichechemea, daima fimbo yake iliendelea kumpa uaminifu kwa kukubali kutumika kama mguu wa tatu. "Miongoni mwa hao watekaji kuna watu waliovaa makoti makubwa meusi na wameshika fimbo kama hii ya kwangu?" Akauliza swali akionekana kulisubiria jibu lake kwa hamu kubwa. "Aah hapana mkuu...hawana fimbo japo kuna mwanamke mmoja ambay.." "Viktoria huyo...Franko Viktoria. Dada yake shetani!" Akamkatisha sentensi yake huku akionekana kunung'unika akilitaja jina la Viktoria na akalisindikiza kwa kashfa ya kumpa undugu na shetani. "Mwingine nani?!" Akauliza huku akiusanifu uso wa Duba. "Wengine ni mayanki tu...vijana barobaro wale..wamevimba tu miili hawana jipya. Labda na mwanaume mrefu hivi..nadhani huyo ndiye Don Franko!" Akamaliza sentensi yake kwa dhahania. Dario akabaki kimya akiwa ameitazama ardhi kwa muda wa dakika moja nzima. "Kama amenifata mpaka huku...sidhani kama vijana wetu huko wameweza kuwazuia. Sidhani. Amekuja kuninyanganya kilicho changu na amekuja kulipiza kisasi chake cha muda mrefu alichokuwa amekitunza. Mimi sikubali nifie kwenye mikono yake na wala sitakubali afie kwenye mikono yenu. Huyo nitamuua mwenyewe. Kuweni makini sana na Viktoria, yule ni kama dume la nyani lililojificha kwenye umbile la kike." Akaweka kituo kisha akawatazama Duba na Dubu tena kwa mara ya pili. Akawashika mabegani kwa taabu kwa maana walimzidi urefu kidogo. "Askari wangu waaminifu... Huenda nisiwaone tena lakini tambueni tu kuwa kuna mpuuzi mmoja aliyekuwa anaitwa Dario. Huyu anawashukuru sana kwa kila jambo mlilomtendea. Hana anachowadai!" Akamaliza huku chozi la damu likivuja kwenye jicho lake la kulia. Akalipangusa kama kawaida na kisha akatembea mbele kuongoza njia. Mwendo wake ni ule ule wa kuchechemea. Dubu na Duba wakatazama wakimshangaa Dario. Atawezaje kupambana na watu wenye mafunzo halafu wana silaha za moto. Ni kweli walikuwa wanauelewa sana ukatili wake na ujasiri. Lakini mwendo wake wa kuchechemea ulimfanya aonekane kama asiyeweza mapigano ya ana kwa ana. "Mkuu, nadhani ungebaki tu siye tutamaliza kila kitu. Hali yako sidhani kama inakuruhusu kupigana sidhani..." Dubu akatoa maoni yake akiwa na sauti iliyojaa nidhamu na ushawishi. Dario akapunguza kasi ya mwendo wake. "Mimi na wale wote wanaomiliki fimbo kama hizi tuna undugu wa damu kabisa na shetani. Yule Don Franko ni kaka mkubwa, yule Viktoria ni dada 'ake shetani...halafu mimi ni kaka mdogo wa shetani!" Akaweka kituo nna kusimama ghafla. Kipindi ubongo wa Dubu una meng'enya maana ya sentensi zile. Ghafla Dario akajikunja na kuzunguka hewani...akachia mateke mawili ya mfululizo juu ya kifua cha Dubu. Dubu akapagawa na kujikuta yuko ardhini. Hakuna aliyetegemea kitendo kama hiki muda huu. Akiwa bado yuko kwenye mshangao, akaona Dario amempa mkono ili amuinue. Akaupokea lakini hakuinuliwa badala yake mkono wake ukabonyezwa kwa nguvu manusura uteguliwe licha ya ukubwa wake. "Dubu una muda gani tangu umenifahamu?" Hili lilikuwa swali ambalo lilibebwa kwa sauti yenye amri ndani yake. "Mwaka mmoja...mmoja na nusu mkuu!" Akajibu huku akigugumia maumivu. Hakuwahi kubonyezwa mkono na kiumbe mwenye nguvu namna hii. "Yeah ni mwaka mmoja na nusu sio? Kwanaza hata hio nusu haifiki vizuri. Sasa sikia...mimi ni shetani. Na ukikutana na shetani usijifanye tayari umeshamzoea. Shetani hazoeleki ndugu yangu!" Akalegeza mkono wake na kumnyanyua juu. Bado hawakuamini kama ni huyuhuyu Dario ambaye walizoea kuishi naye hapo mwanzo wakiwa kama walinzi wake binafsi, kabla hawajatorokea msituni kukamilisha hii misheni yao. Dario akarejea kwenye kuchechemea na wakati huo lile chozi la damu lilikuwa limeanza kuvuja upya. Akalipangusa kwa kiganja chake na wakaendelea mbele. Zikiwa ni hatua kama ishirini tu mbele yao. Wakawaona kwa mbali viwiliwili vya watu wawili wanaokuja upande wao taratibu. Wakatulia na kusimama kwa sekunde kadhaa kabla hawajawatambua watu wale kuwa ni Feruzi na Mtemi wakiwa peke yao. Ajabu nyingine ikazaliwa hapa! Wako wapi wale watekaji walioonwa na Duba? Wote wakapigwa na butwaa. Wote isipokuwa Dario. Yeye akajipekua taratibu kwenye koti lake kwa mkono wa kushoto, mpaka kwenye mkanda na aliporudisha mkono wake alikuwa tayari ana bastola mkononi. "Tulieni wapo hapa karibu...hawapo mbali." Akanong'ona kisha ghafla akanyoosha mkono wake na kuwalenga walipokuwa Feruzi na Mtemi. Upesi akahamisha ulekeo na kulenga juu yao. "Njooni huku haraka!" Akafoka. Akapiga pigo moja la risasi...ambayo ni kama ilienda kuwadhuru Mtemi na Feruzi. Lakini haikuwa hivyo badala yake ikapaa hewani mpaka kwenye tawi la mti uliokuwa juu yao na risasi ile ikalipasua tawi lile katikati. Feruzi na Mtemi wakawa tayari wamefika karibu yao japo nyuso zao zilisawajika kuonesha kuwa wana jambo la kusema lakini wanazuiliwa kwa namna fulani. "Baada ya kupotea kwa muda mrefu hatimaye leo uko hapa!" Sauti ilitokea nyuma yao. Walipogeuka walikutana na Don Franko. Kabla hawajajua wafanye nini tayari wakawa wamezungukwa na watu wengine watatu wenye silaha. "Dario...weka silaha yako chini!" Viktoria akang'aka kwa hasira akiwa amemnyooshea Dario bastola. Dario hakuonyesha kushtuka... Badala yake akatabasamu. Na kwa mara ya kwanza mbele ya Don Franko na Viktoria, wakawa wameiona rangi ya tabasamu la Dario namna inavyofanana. "Naona ngedere wa msituni wamekufundisha kuwa kuna kitu kinaitwa tabasamu aisee..!" Don Franko akamkebehi. "Aah ni kweli...na ndio maana nimetaka mlione tabasamu langu kwa mara ya kwanza, msije mkaenda huko hukumuni mkamsimulia mtoa hukumu eti kuna mtu huku hajawahi kutabasamu. Wakati kukasirika tu ni dhambi." Na yeye akajibu kwa kebehi, sawasawa na alivyoulizwa. "Nimesema weka silaha yako chini Dario! Na nyie makubwa jinga, fanya fasta!" Viktoria akiwa nahema akazidi kuhimiza amri yake. Dubu na Duba wakatazamana, kisha wakazitazama silaha zao. Ni zile zile za siku zote. Mapanga yenye kutu lakini yasiyo butu, yanaweza kukata na kufyeka. Halafu mashoka yaliyonyimwa haki ya kuwa na mpini mrefu lakini yakajaliwa chuma kizito chenyw makali. "Oya we demu sikia!" Kwa sauti nzito iliyojaa kiburi Dubu akamgeukia Viktoria, "Unaviona hivi vyuma...havijawahi kugusa udongo hata siku moja. Na kama vikigusa udongo baai vitaulowanisha kwa damu iliyo juu yake. Sasa chagua moja viendelee kukaa mikononi mwetu au viguse udongo ndio..lakini vikiwa na damu yako!" Akaweka pumziko akilisubiria jibu lake. Hapo akafanya kosa kubwa sana, kosa la kusahau ni kiumbe gani aliyemwambia maneno kama haya. Huyu Franko Viktoria hakuwa kiumbe wa kutaka maelezo mengi bali vitendo. "Dubu..Dubu.." Dario akatamka akitikisa kichwa chake kwa masikitiko. "Unazidi kuharibu Dubu...unazidi kuhari-" kabla hata Dario hajamalizia sentensi yake, Viktoria akafyatua risasi kwenye miguu ya Dubu na Duba mara moja bika hata kufikiria. Pyaaaa! Pyaaaa! Wakiwa bado wanaugulia maumivu, akawasogelea kwa kasi na kusimama mbele yao bila kumhofia Dario. Mwanamke akaweka mikono yake kiunoni na kusimama kwa ujasiri mbela ya wanaume wawili waliobonyea chini wakishikilia majeraha kwenye miguu yao. "Mmeniitaje? Demu...ndivyo mnavyowaita mama zenu hivyo eh?!" Akawauliza akihema kwa nguvu. Hasira zimemjaa. "Mmempa kidole awang'ate....ameshawang'ata tayari. Haya mbondeni kichwa chake!" Dario akatamka kwa sauti ya chini lakini iliyosikika kwa wote, huku kichwa chake kikiwa kimetazama chini. Mara ghafla, damu ziliruka kwa fujo. Kama bomba kubwa lililopasuliwa ghafla. Kila mtu alibaki anakodoa macho yake. Hakuna aliyeamini kinachotokea. Halafu milio ya risasi ikafuatia. Paaa! Paaa! -------------------------------- Ni mwendo wa minyukano tu na mipasuano. Don Franko amefanikiwa kukutana na hasimu wake, Franko Dario. Akiwa na kikosi chake... Tayari Viktoria ameanza kuonesha ustadi wake kwenyw medani za ndondi..tena dhidi ya kombinesheni matata ya majitu Dubu na Duba. Vipi kuhusi Feruzi na Mtemi? Wao ni watazamaji au niaje? Wako wapi nabii Tito, King Nego na Boss Mzito? Share link ya chaneli... Acha reaction yako.. Na toa maoni kwenye 0763204351. Tutaikamilisha riwaya yetu rasmi siku ya Kesho kutwa, *JUMATANO* ---------------------------------- Simulizi ya *'KIKAO CHA HAKI'* bado ipo kwenye kilinge cha zile siku tatu za ofa. Inagawiwa bure kabisa, Na mwisho wake ni siku ya kesho. Kuipata simulizi hii, ni rahisi sana... Tuma neno *KIKAO CHA HAKI* kwenda namba 0763204351. Na utaunganishwa moja kwa moja kwenye orodha ya wataogawiwa bure kabisa kazi hii. Asante! 🙏🙏🙏
🔥 😮 2

Comments