
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
February 26, 2025 at 08:46 PM
Riwaya ya *`SHAMBA LA HELA`*
Yake; *Godlove Kabati*
WhatsApp; 0763204351
-------------------
SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA
*Ni rahisi sana kushinda vita endapo tu unapigana na adui unayemuona.*
*Ni vigumu sana kushindana na adui usiyemuona...*
*Omba sana adui yako asiwe yule unayekula naye sahani moja*
*Ni sehemu ya Ishirini na saba....*
Kilichoonekana pale mbele ya macho yao ni mwili wa mtu uliopasuliwa kwa mapigo mawili huru. Pigo la kwanza likikipasua kifua chake kwa panga na la pili likajaribu kutumia shoka kukitengenisha kichwa kwenye vipande vya nusu mbili, haikuwezekana baada ya shoka kugota katikati ya fuvu la mmiliki wa kichwa hiki. Ambaye ni Viktoria.
Kila pigo lilikuwa la kushtukiza sana japo Viktoria aliendelea kuwa mbishi dhidi ya kifo. Akajitutumua na kuitumia bastola yake kuwapiga risasi Dubu na Duba.
Kwa bahati mbaya sana, ubongo wake ulikuwa umepata hitilafu, asingeweza kufanya maamuzi sawasawa, hivyo akawa amekosea kulenga shabaha zake vizuri.
Badala ya kuvilenga vichwa vyao wote wawili, akajikuta ameupiga mguu wa Dubu na amefanikiwa kumwadhibu Duba kwa shabaha ya kichwa. Duba akaachwa ardhini, damu zikimvuja kwa wingi na kichwa chake kikiwa kimetobolewa kwenye paji la uso. Risasi ikaacha shimo pana kiasi lililofanana na chemchemi ndogo ya damu.
Kwa mara ya kwanza Feruzi na Mtemi wakamuona mtu aliyepigwa risasi namna anavyokata roho taratibu. Wakatishika sana japo hawakuwa na pa kukimbilia.
Dubu aliinuka kwa ghafla akiwa amegadhibika. Akapiga kelele ya kutisha kwa hasira. Dubu akawa kama mnyama mwitu,
Ndevu zake ndefu zikaitii hasira yake na zikamtetemeka kuendana na muungurumo alioutoa.
"Huyu jamaa nd'o maana walimwita Dubu!" Kwa mara ya kwanza Feruzi akaelewa maana ya jina lake kwa vitendo. Dubu aligeuka na kuwa dubu kwelikweli.
Akijipihapiga kifua chake kibabe akachachamaa na kumchota Viktoria ambaye alikuwa bado anayumba kama mlevi.
Akambwaga chini kama gunia zito. Akachomoa lile shoka lililogota kwenye safari yake ya kuutafuta ubongo wa kati na kulitupa chini kisha akaunganisha viganja vikubwa vya mikono yake na akakibana kichwa cha Viktoria katikati yake, akawa mwenye kukibonyeza kwa nguvu kama anayetaka kukipasua hivi.
Hapa Feruzi na Mtemi wakafumba macho yao kwa pamoja hawakutaka kushuhudia unyama kama huu.
Vijana wa Don Franko walipotaka kuingilia tu, akawanyooshe mkono na kuwatuliza. Alifahamu anachokifanya. Alichagua kuwa mtazamaji tu.
Utulivu huohuo ulikuwa pia kwa Dario...japo yeye alikuwa wa tofauti kidogo, hakuwa mtazamaji. Aliendelea kuinamisha kichwa chake ardhini, kofia yake pana ikificha uso wake.
Dubu alikibana kwa nguvu zaidi kichwa cha Viktoria ambaye alikuwa hajiwezi kwa lolote lile. Akaendelea kubana kwa nguvu sana, misuli yake mipana ikitanuka na kujichora ramani na michirizi kadhaa kama mizizi mpaka ukasikika mpasuko,
Paaaaa!
Kama nyanya mbivu inavyokanyagwa na unyayo wa mtu aliyevaa buti. Ukawa ni mwisho wa Franko Viktoria!
Dubu akarudi kinyume nyume huku anachechemea bado anaipangusa damu iliyochanganyikana na ute mweupe kwenye jinzi lake chafu.
"Nimemuua nyoka mkuu!" Akatamka maneno haya alipomfikia Dario aliyekuwa amesimama tuli.
"Umeikumbuka kanuni?" Dario akamuuliza kwa sauti kavu.
"Aah mkuu...nitasahauje tena?" Kwa sauti nzito Dubu akajibu.
"Itaje!"
"Ukitaka kumuua nyoka sharti ukisage kichwa chake!"
"Very simple...very?"
"Simple!" Dubu akamjibu kwa sauti ya ushindi.
Baada ya hapo Dario akakiinua kichwa chake taratibu na kumtazama Don Franko.
"Sijawahi kuzisahau kanuni Franko Don Bosco! Nimemuacha Franko Viktoria apigane mwenyewe vita yake." Sauti yake kavu ikasikika.
"Nimeona!" Don Franko akajibu kwa ufupi.
Hapa walikuwa wakiitimiza sheria ya chama chao ambayo iliwazuia kuingilia mapigano ya aina yoyote ile yanayomuhusu kiongozi mwenye cheo cha uFranko. Akilianzisha alimalize mwenyewe.
Kimya kirefu kikachukua nafasi.
Viumbe hai nane vikawa vinatazamana...wakati huo mamlaka yalikuwa kwa watu wawili tu.
Dario na Don Franko. Ambao nao waliendelea kutazama macho kwa macho.
Feruzi na Mtemi waliendelea kubaki kwenye migogoro ya nafsi zao. Hawajui ni nani haswa atakayeutetea uhai wao katika vita kama hii inayohusisha kila silaha inayoweza kuua.
Dubu akainama chini na kuokota panga lile lenye kutu na sasa hivi likiwa na rangi ya damu. Akawatazama Feruzi na Mtemi kwa jicho la kikatili huku akililamba panga hilo.
Ni hapo ambapo Feruzi na Mtemi walishindwa kuyazuia machozi yao. Walianza kuliona giza ndani ya makaburi yao likiwaita kwa umbali wa futi sita chini ardhini.
"Dubu!" Dario akamuita bila kumtazama.
"Naam mkuu..." Akaitika akiwa anahema juujuu.
"Mtoto wa nyoka?."
"Ni nyoka mkuu..."
"Kuna haja ya kumsubiria akue aote meno nd'o auawe kweli?"
"Hapana mkuu...hilo ni kosa kubwa sana!" Akaanza kuliandaa panga lake mkononi tayari kuanzisha shari la pili.
"Unasubiri nini sasa..." Darioa akaendelea kutoa amri na wakati huu akainamisha tena kichwa chake chini.
Dubu akachomoka kwa kasi akipiga kelele za hasira kuelekea walikokuwa Don Franko na vijana wake watatu.
Hawakusubiri amri. Wakazikoki silaha zao na kummiminia Dubu risasi za kutosha.
Ni mahala hapa pekee ambapo Dubu alionyesha utofauti wake.
Licha ya kujeruhiwa na risasi zile, ilionekana ni kama hajali kuhusu maumivu yake. Yeye aliendelea kuwasogelea vijana wale mpaka alopowafikia.
Wakiwa hawaamini kama wanapigana na binadamu au jitu la kwenye hadithi, yeye hakuwapa huo muda wa kujifikiria.
Aliwakamata shingo zao mbili kwa nyuma na kuwakusanya kwa nguvu akivigonganisha vichwa vyao kwa pamoja.
Alifanya hivi akiwa na hasira sana mpaka alipohakikisha navyo vimepasuka.
Ilikuwa baada ya kumaliza tukio hili. Ndipo akakumbuka kuwa na yeye ni mwanadamu na amejeruhiwa sana kwa risasi. Akaanguka chini na kuvuta pumzi ndefu mara ya kwanza, ya pili, ya tatu kisha ya nne.
Hapo hakuvuta pumzi tena. Dubu akaifuata njia ya safari kama ya mwenzie Duba!
Sijui kama watakutana huko...asma la foleni imeshajaza watu wengine.
"Kama leo nitatoka hapa nikiwa hai...tena bila kilema chochote kile. Basi kwa namna yoyote ile sitakuja kufa daima!" Feruzi akaapa nafsini mwake.
Hizi mbinu za mauaji alizoziona zikitumika hapa zilikuwa zinazidi kumtisha. Wanapigana kwa kanuni maalumu ambazo zinawaongoza wenyewe.
Vita kama sio vita, uhasama kama sio uhasama. Na wala usingesema kuwa wana chuki hawa. Chuki gani wakati nyuso zao zimetulia tu na tangu wamesimama mahali hapo hawajabadili mkao?
Hakika, Feruzi na Mtemi walikuwa wanaangalia sinema ya kutisha sana...sinema ya mubashara kabisa!
Na sasa wakawa wamebaki wao wawili tu. Don Franko na Franko Dario ambaye alikuwa amekikataa cheo chake na akataka aitwe Dario.
"Nadhani hata hapa unaikumbuka kanuni...au nikukumbushe?" Kwa sauti ileile nzito na ya tulivu Don Franko akamuuliza Dario.
"Wakutanapo wakuu wawili wanaomiliki fimbo ya mamlaka, fimbo ya giza. Watapigana bila silaha mpaka kifo. Na hakuna mtu anayeruhusiwa kuingilia!" Dario akanukuu maneno hayo kutoka akilini mwake kisha akainua kichwa chake kumtazama Don Franko,
"Nimekosea?" Akatafuta udhibitisho wa nukuu yake.
Don Franko akacheka kidogo kisha akabonyea chini na kuiweka bastola yake ardhini. Akaipiga teke na kuisogeza mbali naye,
"Hapana hujakosea...una kumbukumbu sana we hayawani. Na sidhani kama inahitajika silaha yoyote ile ili tumalizane mimi na wewe."
Akiwa anavua koti lake kubwa, Don Franko akatamka kwa dharau huku anamtazama Dario usoni akawa anajiandaa kwa mapambano ya ana kwa ana, tabasamu la kifo likaonekana usoni mwake lakini Dario akaendelea kubaki kwenye utulivu uleule.
"Na kabla hujaenda mbali sana Franko Don Bosco..." akamtuliza na wakati huu kikohozi kikamchukua, akakohoa kwa nguvu na alipotema chini ilikuwa damu nyeusi. Hakujali, akajipangusa na kuendelea...
"Nadhani umeanza kutengua kanuni wewe mwenyewe...na hapa mimi ndie mkuu wako!" Akatamka kwa kujiamini sana.
Don Franko akapigwa na butwaa. "Unamaanisha nini?"
"Fimbo yako ya giza iko wapi?!" Hili swali likaufanya tumbo la Don Franko litetemeke na akaanza kuhisi mjongeo kama wa vipepeo kwenye tumbo lake.
Ni kweli...alikuwa ameipoteza fimbo yake tangu zamani. Na hapa Dario alikuwa kwenye mamlaka.
"Naweza kukuua kwa namna ninayopenda mimi mwenyewe na usinifanye lolote. Nitakuwa nipo kwenye sheria na kanuni za chama kama zinavyodai!" Akapigilia msumari kwenye usahihi wake. Bado ni mtulivu, mikono yake akiibebanisha juu ya fimbo yake iliojikita ardhini.
"Huoni kuwa nimezitii sheria za chama?" Akamuuliza.
"Sheria gani mpumbavu wewe!" Akafoka kwa hasira sana Don Franko.
"Umevunja kanuni nyingi sana za chama chetu! Ulimuua Dokta Simfukwe, halafu ukatutumia kichwa chake tu eti tukizike.
Yaani mtu aliyekutoa kwenye umaskini akakuleta kwetu na kukupandisha cheo ukamlipa kifo.
Unaona ulivyo mnyama wewe?!
Hebu fikiria...ulimuua kiongozi wetu halafu bado ukatutumia kichwa chake tu tukizike.
Yaani kichwa tu nd'o kilizikwa. Hebu ifikirie familia yake ilijisikiaje?
Au kwa vile wewe huna familia...ugumba wako huo na sura yako mbaya nd'o vinakufanya uishi kwa hasira.
Bado hukupoa, eti ukakimbia na siri za hazina ya chama. Ukatufanya wapumbavu kwa kututumia barua pepe na jumbe za sauti ukitutisha. Unadhani nani aliyekuwa anakuogopa?
Umejificha huku maporini kama mnyama, umefukua hazina yote na kuondoka nayo. Halafu unasema kuwa we ni mnyoofu, unazitii sheria zetu?
Fedhuli mkubwa wewe...!
Na haya yote niliyatabiri kuwa yatatokea tu. Tangu unaletwa pale nilikuona kuwa ulikuwa unapika bomu ambalo ungelipakua muda wowote ule na kulililipua.
Wewe ni mbaya sana...una roho ya ajabu! Shetani mweusi wewe!!"
Don Franko alifoka kwa hasira, kwa maneno na vitendo mikono yake ikienda huku na huko kwa msisitizo. Mate pia yalikuwa yanakitoroka kinywa chake kwa kuruka kila alipotamka maneno yenye konsonanti zilizohitaji mkazo kuzitamka.
Akamaliza kumwaga yaliyokuwa moyoni mwake na kubaki akihema kwa nguvu.
Bado tu Dario anamtazama akiwa ametulia tuli bila kutikisika.
Ilikuwa ni kama ameyapuuza maneno yake.
Mwili wake ulitulia lakini jicho lake la kulia halikutulia katu. Lilikuwa likimchezacheza sana na kama kawaida yake, likawa linavuja chozi la damu. Na yeye muda huu hakulifuta akaliacha liendelee kuvuja tu.
"Piga magoti chini..." Kwa sauti ndogo ya utulivu isiyokuwa na kinyongo, Dario akamuamuru Don Franko ambaye alipigwa na butwaa na hakuamini kuwa ni yeye anapeqa amri kama hii kutoka kwenhe kinywa cha kijana kama huyu.
"Unasema?" Akatafuta udhibitisho wa amri ile.
Dario akasonya kisha akampiga risasi ya mguu Don Franko. Ilikua ghafla sana, na hakuna aliyetarajia.
Don Franko akabonyea chini kwa lazima huku akisikilizia maumivu kwenye mguu wake mmoja.
"Nasema piga magoti sio goti!" Akamuongezea na risasi nyingine kwenye ule mguu uliokuwa bado unasubiria amri ya ubongo wa Don Franko.
"Aaaargh!" Dom Franko akawa amelala chini ameikumbatia miguu yake yote akigaragara kwa maumivu.
"Niko kwenye mamlaka sa'hivi inabidi utiii!"
Hapo hapo Dario akaanza kupiga hatua kwa kuchechemea akimfuata palepale chini alipo.
Sura yake sasa imebadilika. Haina ule umakini na utulivu tena bali ametoa macho akiwa tayari kuua.
Feruzi na Mtemi wote walikuwa tayari wamewahi kuwa wahanga wa hasira na roho mbaya ya Dario. Wakaamua kubaki kimya kushuhudia hii sinema ya bure ya kutisha. Wakitamani ni heri hata isingekuwa ya bure, wasingejisumbua kuitazama.
Don Franko akafurukuta na kuisogelea bastola yake iliyokuwa kando kwa pupa. Akaikota kwa kasi na kuilenga kwa Dario ambaye aliendelea kusogea huku akitumia mhimili wa fimbo yake.
"Kiwete wewe!" Alipojaribu kuachia risasi, akashtukia kuwa bastola ile haina risasi hata moja. Hapo akagundua kuwa amepatikana.
Dario akamfikia na kuudaka ukosi wa shati lake kisha wakatazamana uso kwa uso.
"Nisikilize Don Bosco...
Kama tu ungejua hadithi ya kifo cha Simfukwe kilivyokuwa. Sidhani kama mngenishutumu.
Na laiti kama mngeijua ile siri ya ile hazina, msingenilaumj kwa kile nilichokifanya.
Kama tu chama kilikuwa kinafanya kila aina ya dhambi, dhambi mbaya zinazotisha...roho nyingi sana zimenyimwa haki ya kuendelea kuishi kwenye miili yake. Na hawa watu walikuwa na familia, angalau basi mngewaza kuhusu hilo.
Lakini nyie mkawa wabinafsi na wauaji wakubwa.
Nishukuru sana niliwatumia kichwa chake...maana alitaka yeye mwenyewe kiwafikie ili mkizike.
Nyie ni lini mliwahi kutuma mwili wa watu waliouawa kule kwenye maabara zenu ili wakazikwe?
Nijibu Don Bosco..." akamuuliza swali akiwa anamtazama usoni. Akameza funda la mate kisha akaendelea...
"Utazame uso wangu...
Achana nao...hebu litazame hilo jicho langu la kulia. Angalia namna linavyolia....angalia hilo chozi la damu.
Nataka nikueleze kitu DonBosco...hilo jicho lilishuhudia ukatili mkubwa uliofanywa na mikono yangu mimi mwenyewe... mpaka liko hivi.
Limeunganishwa moja kwa moja na mapigo ya moyo wangu. Ninapoumizwa na moyo nalo linatoa chozi la damu.
Ni mshahara wa dhambi nilizozifanya nikiwa chini ya mwavuli wa chama cha giza.
Nilipata kilema cha maisha....nikapata na jeraha baya sana kwenye jicho langu la kulia. Unamjua aliyenishambulia nikiwa natimiza majukumu ya chama?
Unamjua?...humjui.
Laiti kama ungemjua..." akaweka pumziko na kukohoa tena kwa mara nyingine...
*(NDUGU MSOMAJI, MKASA WA MAISHA YA DARIO UNAPATIKANA KWENYE RIWAYA YA *`NAITWA DARIO`* ITAKAYOKUJIA HIVI PUNDE...)*
Safari hii akazidiwa na ukali kikohozi chake, akakohoa sana huku akiwa amekishika kifua chake. Akatema damu za kutosha.
"Ni nani aliyekushambulia?" Don Franko akamuuliza kwa udadisi.
Dario akasimama kwa taabu na kuirejea fimbo yake.
"Alisababisha mpaka mapafu yangu yakapata hitilafu. Nadhani sina muda mrefu sana wa kuishi... Aliyemuua Dokta Simfukwe huyo....ooh masikini Dokta Simfukwe!" Dario akalalamika kwa sauti ya kinyonge.
"Una bahati sana siku hii ya leo...DonBosco. Ningekuua kwa ukatili sana, tena kwa roho mbaya sanaaaa. Pengine kuliko hata nilivyoshuhudia dokta Simfukwe alivyouawa.
Lakini mimi siko hapa kwa ajili yako.
Japo utakufa...na huenda isiwe mikononi mwangu. Ila utakufa hakika!
Utakufa kifo cha kawaida sana. Kifo cha upendeleo."
Ghafla ikasikika milio ya risasi kwa mbali.
"Vijana wangu hao wanamalizia kazi...sidhani kama baada ya hapa , chama chetu kitazidi kusimama. Sidhani!"
Akasimama na kumuacha Don Franko pale ardhini anaumgugumia maumivu ya miguu yake.
Akapiga hatua kuelekea walipokuwa Feruzi na Mtemi. Akawaamuru wasimame, maana muda wote huu walikuwa ni kama wamewekwa kwenye jokofu. Na hata walipoamuriwa wasimame walikuwa bado hawaamini kama wameamriwa kweli wasimame.
Dario aliwatisha sana...walidhani wanaongea na shetani mubashara katika umbo la mwanadamu.
"Nifuateni!!" Akawaamuru.
Wakamfuata huku wakijitahidi sana kutomkaribia.
"Adam Feruzi Adam!"
"Na..na.naaam!" Kigugumizi cha ghafla kikamkumba Feruzi.
Dario akakurupuka na kuidaka shingo ya Feruzi, katika hii kukurukakara Dario akatuliza ngumi ya kawaida kwenye shingo yake na Feruzi akazirai na kuanguka chini.
Mtemi akapigwa na butwaa, akaganda kama sanamu.
"Lala chini!! Haraka!" Dario akapaza sauti na akampiga mtama Mtemi na kumfanya aanguke chini kama mzigo.
Alikuwa amemshuhudia Don Franko akijikongoja kuwahi kuiokota bunduki ya mmoja kati ya wale vijana wake.
Upesi sana akaiwahi bastola yake iliyokuwa kiunoni akajaribu kuwa wa kwanza kumshambulia haraka lakini akawa kachelewa tayari.
Tayari risasi moja ilikuwa imeshatua kwenye tumbo lake lakini hii haikuwa risasi ya kawaida. Ilitokea kusikojulikana!
Nani huyu? Akajiuliza.
Damu nyingi sana zikaanza kuvuja.
Akawahi haraka sana kulala chini baada ya kumuona adui mpya kwenye huu uwanja wa mapambano.
Mdunguaji aliyesimama kwenye jiwe kubwa mbali.
Mlengaji huyu akaanza na kichwa cha Don Franko. Akakifumua kwa pigo moja tu la risasi kikasalimu amri, kikapasuliwa na kusambaratika.
Dario akawahi haraka sana kuubeba mwili wa Feruzi aliyekuwa hajitambui. Akajitahidi haraka sana kwa kuchechemea.
Sasa mdunguaji alikuwa ameipata shabaha ya kichwa chake lakini akasita.
"Mh! Oyah Nego! Mbona kambeba sasa?..."
Ilikuwa sauti ya Tito Ngeze. Akishangaa baada ya kumuona Dario, akimuweka Feruzi mabegani na kuanza kutokomea naye kusikojulikana.
"Hebu nione.." Abednego Kagoye akatumia darubini kuangalia kilichoko huko.
"Ebooo! Hebu muwahi huyo kaka...ataenda kumuua. Yule pale chini ni nani sijui!"
Tito akajaribu kulenga upya lakini akawa amechelewa sana. Tayari Dario ameshatokomea kwenye vichaka.
Wakashuka upesi kuwahi mawindo yao.
Inaendelea
🔥
😢
🙏
3