
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
February 26, 2025 at 08:47 PM
Riwaya, *`SHAMBA LA HELA`*
Yake, *Godlove Kabati*
WhatsApp 0763204351.
SEHEMU YA MWISHO.
*Karma ni kweli...*
*Chochote kile unachokifanya leo...kiwe kiovu au chema...*
*Kitakurudia katika namna hiyohiyo*
*Na hii ni sehemu ya mwisho...*
Boss Mzito alifanikisha suala la kutega kifaa cha kutraki kwenye koti la Don Franko. Hiki kiliweza kuonyesha mwendo wake wote kwenye ramani maalumu.
Alijua fika kuwa yeye hatahusishwa moja kwa moja kwenye vita hii. Akaenda kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa ili mradi tu na yeye aonekane yumo.
Ni dakika chache tu baada ya wao kuondoka. Na yeye akafuatia nyuma yao, akawatoa Tito na Abednego kutoka kwenye buti ya gari lake na kuwapa maelekezo na silaha walizozihitaji.
Tito alitamani vita hii iwe ya kimya kimya, lakini baada ya kupima na kung'amua hatari itakayokuwepo akamwambia Abednego awahi upesi kufungua jalada la kesi hii ya ujambazi na utekaji ili hata watakapohitaji msaada waupate kwa urahisi.
Kisha haooo wakaenda kule msituni kama walivyosoma rada ya kifaa walichopewa.
Wakiwa na tahadhari kubwa wakaingia msituni wakisikia majibizano ya risasi yaliyokoma baada ya dakika kadhaa.
Wakaamua kufuatilia kwa uangalifu uelekeo wa kifaa kile...mpaka walipofika eneo hili.
Wakawaona kwa mbali kila tukio lililoendelea, tangu Viktoria anauawa kikatili na Dubu.
Wakafatilia na kugundua kuwa hapa wanaenda kukutana na watu hatari sana.
Wakachagua kuwamaliza wakiwa mbali.
Kwa njia ya kudungua.
Tito akaanza na tumbo la Dario, kisha akafuatisha kichwa cha Don Franko.
**********
Feruzi alizinduka na kujikuta eneo ambalo alilikumbuka kwa kiasi fulani.
Akajaribu kuvuta kumbukumbu..
Ni eneo hilihili ambalo aliwahi kuletwa na yule abiria mzee. Akapagawa na kusimama kwa fujo.
"Tulia Adam tulia!.."
Akamuona Dario amejilaza kwenye mti akiwa ameshikilia tumbo lake linalovuja damu.
"Najua kuwa unajuta sana kunifahamu. Lakini mimi kamwe sijuti kukufahamu, Adam Feruzi Adam!
Nisikilize...sina muda mrefu wa kuishi hapa. Na watanifikia kabla sijakuambia ninachotaka nikuambie.
Ukitoka hapa, nenda kijijini...nyumbani kwetu kwa mzee Kapongo kaniombee msamaha.
Mwambie kuwa nilitoka nyumbani kuja huku kutafuta na nimepata japo kwa njia haramu sana.
Mwambie hivyo ataelewa!"
Kutajwa kwa jina la mzee Kapongo. Kukamshtua sana Feruzi.
"Una...unamjuaje mzee baba yangu wewe.!" Akauliza akiwa mwingi wa wasiwasi.
Dario akatabasamu kidogo...tabasamu la nadra lakini linalosikitisha.
"Isaka... mdogo wangu Isaka. Hivi ni nani alikupa hilo jina la Feruzi? Ni jina la mjini huku au?"
Kutajwa kwa jina hili la Isaka...kukamfanya Feruzi akaribie kuanguka chini kabisa.
Hapa akapigia mstari kuwa yule Dario pale chini ni shetani haswaaa.
Kajuaje vitu vyote hivi mpka jina lake la kuzaliwa? Lakini neno mdogo wangu likampa tumaini tena.
"Mi mi mi mdogo wako? Kivipi tena?"
Dario akakohoa damu na kutamka na safari hii akawa analia machozi ya rangi tofauti. Nadhanj haoa hakuna haja ya kuelezea analiaje kila jicho.
"Ni mimi kaka yako Darius...ni mimi.
Nilitoroka kijijini kuja huku mikoani kutafuta maisha. Na haya nd'o maisha niliyokuwa nayaishi muda wote huo mdogo wangu!
Nimekuwa mtu mbaya sana mdogo wangu..."
Alipofikia hapo, Feruzi hakuamininkile alichokuwa anakisikia ,akachomoka upesi na kumkimbilia. Alipofika akamkumbatia kwa nguvu na kujaribu kumganga ili damu isivuje zaidi.
"Inabidi nikusaidie...unavuja damu nyingi sana kaka Darius" machozi yakichukua nafasi upya kwenye macho yake.
"Aah hapana dogo. Mimi inabidi nife leo hiihii. Niende kufanyiabkazi dhambi zangu zote. Enhe ulifuata nini huku mjini..Vipi na wewe ulikimbia kijijini?" Akamuuliza kwa upole...sasa yakawa ni kama mazungumzo ya kaka na mdogo wake.
Feruzi akiwa bado amepigwa na butwaa akakosa cha kutamka.
"Sikia sogea karibu.... usiogope na wala usishangae ni kwa nini nilikuficha muda wote huo. Nilitaka nikuambie yote haya kwa wakati sahihi ambao ni huu.
Yule rafiki yako ni rafiki bora sana. Ni rafiki wa kweli. Aliniambia kila kitu kuhusu wewe na hapo nikagundua kuwa wewe ni ndugu yangu wa damu kabisa.
Kutokana na mambo yalivyokuwa nisingekueleza kila kitu maana wewe una moyo mwepesi sana. Nimefanya kila jitihada mpaka uletwe huku na nikakuepusha kutoka kwenye midomo ya kifo cha hao wanachama wa mwanga wa giza.
Wale ni mashetani. Wanaua watu na kufanya kila dhambi ya mauti ili tu wapate fedha na nguvu.
Na kweli walikuwa na nguvu sana...sidhani kama chama chao kitaendelea.
Alaaniwe sana Dokta Simfukwe!" Dario akatamka akiwa na kila dalili ya uchovu na maumivu. Ilionekana wazi kuwa muda wowote ule anaenda kujinyakulia wadhifa mpya wa kuitwa marehemu.
"Kwa nini lakini Darius? Eeh kwa nini? Ulifanya nini mpaka ukajichukia wewe mwenyewe? Niambie bro...niambie!"
Bado Feruzi ameung'ang'ania ukosi wa koti lake akimlaumu na kumuonea huruma kwa pamoja.
"Ooh mdogo wangu
Nimefanya ukatili mwingi sana. Nina roho mbaya sana dogo. Nina roho mbaya sana, namchukia kila mtu ila sana sana najichukia mimi mwenyewe!
Wewe nenda fuatisha hio ramani hapo kuna mashamba mengine matatu ya hela za kukusaidia. Achana na lile uliloliona lilikuwa la mtego lile. Ni hela nyingi sana japokuwa ni za mauti. Ni juu yako kuzitumia au kuziacha. Sikuchagulii njia ya kwenda. Haya toka hapa!"
Akabadilika tena na kuanza kukasirika.
"Lakini bro..."
"Tokaaaaa!" Akakasirika mara dufu na akapaliwa mate. Akaanza kukohoa kwa nguvh akakohoa damu, jicho lake la kulia linavuja damu na jeraha tumboni nalo linavuja damu nyingi sana.
"Nenda..niache nife kwa amani.
Nimemwaga damu za watu wengi, acha yangu imwagike."
Akavaa kofia yake na kusimama...akapiga mwayo mrefu na kuinamisha kichwa chake ardhini akatulia.
"Adam Feruzi Adam!" Akaita.
Feruzi aliyekuwa kwenye fikra mchanganyiko muda huu, akajibu kwa woga...
"Naam..kaka Darius!"
"Ooh usiniite hilo jina...we lako si ulibadilisha? Na mimi nilibadilisha niite Dario nitaitika!" Sauti yake kavu ikasikika kwa utulivu sana.
"Adam Feruzi Adam!" Akamuita lakini hakusubiri jibu lake.
Akaanguka chini ghafla na kukoroma kwa nguvu kisha akatulia.
Punde wakafika watu watatu .Feruzi aliwafahamu wawili pekee na mmoja aliyeshika silaha hakumfahamu.
"Oya Feri! Nini kimetokea?!" Alikuwa ni Abednego akiutazama mwili wa Dario pale chini.
Feruzi alikosa jibu, alikuwa akitetemeka tu.
Angeanza vipi kuwanyooshea maelezo yake?
Akachagua kubaki kimya.
Kimya, akilia na moyo wake.
*********
(Baada ya miezi 6)
Boss Mzito akiwa ndani ya ofisi yake, akili yake imechotwa na kupekuwa mafaili kadhaa ya biashara zake. Akaona jina la Don Franko kwenye moja kati ya madeni aliyokuwa anadaiwa.
Akacheka kwa dharau. Na kulipuuza jina hilo. Lakini akasita na kulitazama tena kwa mara ya pili.
"Wajinga sana nyie. Yaani mmenipa maisha mazuri halafu mkataka kuyachukua tena. Nani wa kunitikisa mimi sasa hivi? Nani huyo?! Mimi ndio Mzito mwenyewe..." akatoa tena cheko la dharau.
Mara simu yake ikaita.
Akaipokea kwa madaha na aliyempigia alikuwa karani wake akimjulisha kuwa kuna wageni wake.
Akataka kuwajua zaidi akaambiwa kuwa ni wafanyabiashara. Bila kusita akaruhusu waruhusiwe kuingia ofisini mwake.
Wakaingia vijana watatu waliovaa suti nyeusi maridadi sana na miwani nyeusi nyusoni mwao.
"Karibuni jamani!" Akawakaribisha kwa bashasha. Hakujibiwa.
Bashasha lake likafifia punde tu baada ya kukutana na sura moja kati ya zile tatu ambayo ni kama aliifahamu.
Vijana wawili wakaketi moja kwa moja kwenye viti vilivyokuwepo ofisini pale na mmoja akasimama. Wote wakazivua miwani zao kwa pamoja. Sura zao zimekauka bila kujulikana kama wamekasirika au wana bifu na tabasamu.
Hapo Boss Mzito akataka kukimbia baada ya kumtazama yule akiyekuwa amesimama. Ni sura ambayo alishaanza kuisahau kwa takribani miezi 6 iliyopita.
"Mzee Karoli Sande!!"
Kutajwa kwa jina hili tu kukamfanya airuhusu haja ndogo ianze kugonga hodi. Jina lake la zamani sana akiwa mfungwa huko nchini Uganda. Sasa linatajwa na vijana wageni kabisa machoni kwake.
"Nadhani unanikumbuka...naitwa Abednego! Na hawa ni wenzangu huyo anaitwa Feruzi na huyu anaitwa Mtemi." Akaweka nukta.
"Hatujaja hapa kwa shari...labda kama utalitaka wewe mwenyewe. Tuko hapa kufanya biashara na wewe mzee.."
Mtemi akatamka kwa sauti ya upole.
"Na kama ukituzingua tu...bas hii inakuhusu" Feruzi akamuelekezea Boss Mzito mdomo wa bastola. Mzito akatetemeka kuuona mdomo ule. Haukuwa na tabasamu na wala haikujulikana utatapika risasi muda gani.
"Jamani tusifikishane huko jamani...mnataka nini tena sa hivi? Si...si nimeshawapa Don Franko jamani?"
"Tuko hapa kibiashara tu mzee Karoli. Tunataka tufanye kazi na wewe..yaani tuhusike moja kwa moja kwenye biashara zako." Abednego akatamka kwa sauti ya kujiamini.
"Biashara zangu? Kivipi tena..halafu hilo jina wanangu...msilitaje kwa sauti. Tafadhali sana!" Mzito akasihi.
Feruzi akashusha pumzi na kuweka briefcase lake mezani pale. Akafungua na kutoa nyaraka kadhaa.
"Tunataka kutakatisha fedha zetu kupitia biashara zako mzee. Wewe ni tajiri mkubwa sana hapa mkoani na unatufaa sana kwenye hili maana unahusika moja kwa moja na maafa yote yaliyowahi kutokea!" Akaweka pumziko na kumtazama Mzito.
"Sielewi aiseee.." akajitetea.
"Tuna jumla ya dola bilioni kumi pointi sita. Na hiki ni kiasi kikubwa mno cha fedha. Tunachotaka sisi ni kuzitakatisha kupitia biashara zako bwana Karoli Sande!
Unasemaje?!"
Akamsogezea nyaraka zile na akazisoma kwa kutetemeka. Akawarejea na kuwatazama mmoja baada ya mwingine kisha akautazama na mdomo wa bastola ile.
Akatikisa kichwa kukubali.
"Sa...sawa lakini mnaniahidi nini?!" Akahoji.
"Tunakuhaidi kila kitu...utajiri, usalama na uhai! Haya saini hapo." Abednego akamsurutisha kusaini.
Boss Mzito akamwaga wino wake upesi.
Kisha vijana wale wakaondoka ofisini pale kimyakimya.
Walipotoka nje kila mmoja akaangua kicheko cha nguvu. Ilikuwa ni kama walikuwa wamekibana kifuani kwa muda mrefu na sasa wanakilipua kama bomu.
"Aaah ila nyie mfala nyie..." Feruzi akatamka kwa kicheko.
"Deal done hapa ni kula maisha tu. Kesho inabidi nikaoge India, chai ninywe Oman, halfu mchana nikazurure Dubai. Usiku naenda kuangalia mechi ya basketball Marekani!" Mtemi Moringo kwenye moja na mbili zake.
"Aaah we naye...hapa mi sa hivi ni mwendo wa kubadilisha totoz kwenye mashuka ya hoteli za nyota tano tu! Hahaha" Akatoa kicheko Abednego. Kabla kila mmoja hajaingia kwenye gari lake,
"Enhe na wewe Feri utafanya nini sasa?!" Mtemi akamuuliza.
Feruzi akatabasamu na kutamka,
"Mimi nataka nianze kilimo!"
Kilimo? Wakamshangaa...
"Ee niwe mkulima. Niwe na shamba kubwa, shamba la hela!"
TAMATI
-----------------------------------
Ilianza moja ,mbili ,.tatu na sasa tumeikamilisha safari ya kuisoma riwaya yetu ya *SHAMBA LA HELA*.
Ni matarajio ya mwandishi kuwa umejifunza mengi, na una maoni yako.
Karibu sana 0763204351,
Uache maoni yako.
Mnajua maana ya kutakatisha fedha? 😃
🙏
❤️
😂
8