
IslamicForum
February 28, 2025 at 06:50 PM
MAKHATIBU WA IJUMAA LEO WAELEZENI WAISLAMU MAMBO HAYA
Leo inshaAllah ndio Ijumaa ya mwisho wa mwezi wa Shaaban, ambapo siku yoyote kuanzia kesho inshaAllah tutaingia katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Katika hali kama hiyo tunawasihi na kuwaomba kwa dhati kabisa makhatibu kesho katika mimbar zao wawaeleze Waislamu yafuatayo:
1. Swaumu ya Ramadhani imeletwa kwa lengo la kumcha Allah Taala. Na asili uchamungu ni jambo la muda wote. Maana yake ni kuwa Waislamu waubebe uchamungu ndio dira ya kila siku ya maisha yao.
2. Kwa sababu Swaumu inatuhimiza uchamungu, na kwa sababu uchamungu wa kweli hauwezi kufikiwa ila pawe na utawala wenye mamlaka kamili ya kuulinda. Ina maana kuwa Ramadhani inatuhamasisha tutawaliwe chini ya mfumo wa Kiislamu kwa kuwa ukamilifu wa taqwa hutegemea utawala wa Kiislamu (Khilafah) na si kinginecho.
3. Swaumu ni ibada ya Waislamu tu, na ndio maana amri yake ikaanza na mwito wa: ‘Enyi Mlioamini’. Hivyo, masuala ya kujumuika na wasiokuwa Waislamu katika mchakato wa ibada hii kama kuwaalika katika futari, (na asili si futari kwao kwa kuwa hawafungi) ni jambo la haramu, na ni kuucheza shere Uislamu. Kwa kuwa hii si ibada kwao. Wao wana dini yao na sisi tuna dini yetu. Tunasema huko ni kucheza shere wazi wazi, kwa kuwa lau wanaupenda Uislamu basi wangesilimu.
4. Suala la kuwepo rai mbili katika kufunga, kamwe si suala la mgogoro. Jambo hili limekuzwa kufikia kiwango cha farka na baadhi ya wasiojua, na baadhi kwa makusudi, na mara nyingi hukuzwa kwa msaada wa makafiri kamwe ! ili kuwagonganisha vichwa Waislamu na kukuza mifarakano isiyokuwa na msingi baina ya Ummah. Suala hili limezuka kuwa na rai mbili kwa kuwa tu leo Ummah hautawaliwi na Uislamu. Lakini lau kuna utawala (Khilafah) rai itakayosimamama ni rai ya mtawala pekee juu ya kufunga na kufungua. Katika hili hakuna mwenye haki ya kulazimisha rai yake ila mtawala pekee (Khalifah). Na asili suala hili limo ndani ya milki ya utawala wa Kiislamu na sio watu binafsi wala taasisi. Suluhisho ya suala hili sio mijadala, wala kutuhumiana bali ni kusimamisha Khilafah na kumkabidhi mwenye mamlaka jukumu lake, na hapo kubwatika rai zote ila yake pekee.
5. Ramadhani ni mwezi wa uchamungu. Umehimiza kujifunga na kila kitendo cha kujikurubisha zaidi kwa Muumba ili kuongeza uchamungu wetu. Vitendo kama kuswali usiku, kukithirisha kusoma Quran, kutoa sadaka, kuzidisha ihsani kwa wazazi, maskini, wajane nk. Kwa hivyo, ni kilele cha uovu na ni dalili mbaya isiyo na mfano kuitumia Ramadhani katika kumakinisha vitendo vya kifasiki kama dini mseto (ukuruba baina ya Uislamu na ukafiri), vitendo ambavyo lau si ujahili wa mtendaji huwa vinakurubia ukafiri.
Ramadhani kamwe isifungamanishwe kuwa ni chombo cha kuleta ukuruba na makafiri au na watawala wanaotawala kwa mfumo kinyume na Uislamu ambao ni wakala wa kuwapiga vita Waislamu na Uislamu. Kufanya hivyo, ni kuitumia Ramadhani kinyume na makusudio, na kimsingi ni dalili ya kubobea kwa uovu wa mtendaji, kwa kuwa kashindwa kujizuiya katika uovu wake hata ndani ya mwezi wenye hadhi na utukufu.
6. Wakumbusheni Waislamu namna Ramadhani ilivyokuwa chini ya kivuli cha utawala wa Kiislamu (Khilafah) ilivyolindwa katika upeo wa kulindwa, walivyokuwa wakisaidiwa wanyonge, madhaifu na mafukara na kufanyiwa usahali katika majukumu mbalimbali wakaweza kufunga kwa usahali. Wakumbusheni hili ili waone tofauti baina ya ramadhani leo chini ya mfumo batil na thaqil wa kidemokrasia/kibepari na ilivyokuwa chini ya utawala wa Kiislamu.
7. Waonesheni Waislamu namna leo Waislamu wanavyofunga wakiwa katika hali duni katika kila hali, kukosekana utulivu na usalama kitaifa, kama Waislamu wanavyonyanyaswa kwa mateso na mauaji huku wengine kwa mamia kama sio maelfu wakiwa ndani, na kesi zao zikibakia kuwa ni tamthiliya zisizomalizika. Pia waonesheni Waislamu hali ya kimataifa ilivyo kuanzia Afghanistan, Syria, Iraq, Somalia, Yemen, Libya, Turkistan Mashariki nk. Bila ya kusahau kupanda kwa gharama ya maisha hususan mfumuko wa bei za vyakula nk. kwa sababu tu ya uroho wa wa mfumo wa kibepari na sera mbovu za kiuchumi. Haya yote yanawahimiza Waislamu kufanya kazi ya ulinganizi wa Uislamu ili kuweka suluhisho la Kiislamu kwa kuanzia katika nchi kubwa za Kiislamu ili kutatua matatizo ya kiuchumi, kisiasa nk. na kuwarejeshea furaha na utengamano Waislamu na wanadamu kwa jumla.
8. Wahamasisheni Waislamu wapatilize fursa adhimu ya mwezi huu kwa kujifunga na kila aina ya ibada na kuhimiza familia zao nk. Aidha, wahimizeni kuzidisha kutenda wema kwa wazazi na jamaa kuwasaidia katika usahali wa ibada hii. Wakumbusheni Waislamu kuwa mwezi huu una neema nyingi sio tu kula vyakula vizuri. Aidha, wakumbusheni kutumia muda wao vyema na sio katika mambo yasio na maana kama kucheza karata, kuangalia vedio za kipuuzi na kulala ovyo.
9. Watanabahisheni Waislamu wasiburuzwe na ujanja wa watawala wa kidemokrasia ati kuhimiza wafanyabiashara wapunguze bei za bidhaa ili Waislamu wapate usahali wa kufunga. Watawala hao hawana huruma na Waislamu wala Uislamu, na kimsingi hawana huruma na raia kamwe kwa ujumla, kwa kuwa wafanyabiashara wamefikia hatua ya kupandisha bei bidhaa zao kutokana na kubanwa kwa makodi, taratibu na sera za kidhulma za watawala katika biashara.
10. Wakumbusheni Waislamu kama ambavyo wana ghera, hamu, heshima na taadhima kwa faradhi hii ya Ramadhani, ndio hivyo hivyo wawe na hamu kubwa katika kuzitekeleza na kuzihifadhi faradhi nyengine zote bila ya kubagua. Kwa kuwa Aliyeleta Ramadhani ambaye ni Allah SWT ndiye aliyeleta faradhi nyengine zote. Na faradhi zote hustahiki kupewa haki sawa. Ni jambo la huzuni kubwa leo kuna baadhi ya Waislamu wanaipokea Ramadhani kwa taadhima, lakini wakati huo huo wanabeza ibada nyengine ikiwemo kutawaliwa kwa mujibu wa Uislamu.
11. Mwisho, wahimizeni wenye uwezo na wanaowaajiri Waislamu wafanye usahali/ uwepesi katika kuwasaidia na kuwapunguzia majukumu mazito Waislamu ili waweze kufunga kwa usahali. Pia kwa Waislamu wenye uwezo kuwasaidia wanyonge na madhaifu. Japo kuwa Muislamu hufunga katika hali yoyote kikazi na katika kipato, na jukumu la moja kwa moja la kuwasaidia kwa kuwapatia futari kwa wasio na uwezo na ndugu ni la dola ya Khilafah. Lakini katika hali ya sasa ya Waislamu kukosa dola hiyo na katika mlango wa khairat na uchamungu wenye uwezo wasiache kuchukuwa fursa hiyo kwa kutoa msaada.