
WATANI WA JADI
May 18, 2025 at 07:50 AM
UONGOZI wa Simba baada ya kupata taarifa ya kubadilishwa ghafla kwa uwanja ambao utatumika kwa mechi yao ya nyumbani ya hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane, ulifanya kikao kizito Morocco kujadili jambo hilo.
.
Kikao hicho kilimalizika kwa azimio la kuandika barua nzito kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa lengo la kuona kama itaweza kulishawishi kurudisha mechi uwanja ambao ulipangwa ichezwe awali. Katika barua hiyo ambayo tayari imeshatua CAF, Simba imeandika ikihoji uamuzi wa shirikisho hilo kuhamisha mechi ya marudiano ya fainali kutoka Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam hadi New Amaan Complex, Zanzibar. Simba imetoa hoja tatu nzito za kuionyesha CAF kuwa uamuzi wa kubadili uwanja haukuwa sahihi.
.
Hoja ya kwanza ambayo Simba imeitumia katika barua yake ya kuonyesha mashaka kwa uamuzi wa CAF ni kukiukwa kwa kanuni ya 9(3) ya mashindano hayo juu ya utaratibu wa kufuatwa katika kufanya mabadiliko ya uwanja. Kanuni hiyo inafafanua hivi: “Eneo, tarehe na muda wa kuanza mchezo wa mechi za makundi, robo fainali, nusu fainali na fainali unapangwa na kamati ya mashindano ya klabu ya CAF baada ya kushauriana na shirikisho mwenyeji.
Simba imejiridhisha kuwa hakukuwa na mashauriano yoyote ambayo yalifanyika kabla ya uamuzi huo na badala yake kamati ya mashindano ya klabu ya CAF iliamua yenyewe kuipeleka mechi hiyo Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan Complex bila kufanya mashauriano na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
.
“Tumejiridhisha kuwa uamuzi ulifanyika bila kufanyika mashauriano. Kwa vile kabla ya hapo hakukuwa na angalizo lolote kutoka CAF kuhusu uwanja na hata TFF yenyewe haikufanya mawasiliano na CAF juu ya suala la uwanja maana ni lazima pia yahusishe klabu mwenyeji na serikali,” amefichua mmoja wa vigogo wa Simba.
.
Hoja ya pili ambayo Simba imeiweka kwenye barua yake kwa CAF ni kwamba tayari ilishaanza mchakato wa kuuza tiketi za mchezo huo ambapo hadi sasa imeuza zaidi ya 20,000, namba ambayo ni kubwa zaidi ya idadi rasmi ya mashabiki wanaopaswa kuingia katika Uwanja wa New Amaan ambao unaingiza mashabiki 15,000 tu hivyo Simba inahoji ipi itakuwa hatima ya zaidi ya mashabiki 5,000 ambao tayari wameshakata tiketi zao na watashindwa kuwepo uwanjani kwa vile New Amaan Complex haitoshi kuingiza idadi hiyo ya mashabiki.
Hoja ya tatu ambayo Simba imeiweka mezani wasiwasi wa mazingira ya uamuzi huo kufanyika kwa upendeleo na mgongano wa kimaslahi, kinyume na ibara ya 2(3) ya katiba ya CAF inayolazimisha uadilifu na maadili kwa wanachama wa CAF na wanafamilia wa mpira wa miguu Afrika.
.
Simba imeambatanisha ushahidi wa taarifa ya RS Berkane kuwataarifu mashabiki wao kuwa mechi hiyo itachezwa Zanzibar kabla hata mabadiliko hayo ya uwanja hayajatangazwa jambo ambalo kiutaratibu halikuwa sahihi na ikiamini tayari timu hiyo ya Morocco ilishafahamu hilo mapema kutokana na kuwa na kigogo mmoja mzito ndani ya CAF.
.
Pamoja na hilo, Simba imeambatanisha ushahidi wa RS Berkane kuweka oda ya hoteli ambayo itafikia Zanzibar kabla hata barua ya CAF ya mabadiliko ya uwanja haijatolewa.
#uto ngoja tuwafundishe taratibu za kuandika barua za migomo
